Showing posts with label Prof. Ibrahim Lipumba. Show all posts
Showing posts with label Prof. Ibrahim Lipumba. Show all posts

Saturday, January 08, 2011

TAMKO LA CUF KUHUSU MAANDAMANO YA CHADEMA ARUSHA

THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi)

VYOMBO VYA DOLA VINAHATARISHA AMANI YA NCHI.

CUF - Chama Cha Wananchi kimeumizwa sana na kitendo cha kinyama kilichofanywa na jeshi la polisi na serikali ya chama cha mapinduzi kuwapiga na kuwaumiza viongozi, wanachama na wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) na wananchi mbalimbali wapenda demokrasia na haki ndani ya nchi yetu waliokuwa wakiandamana kwa amani jijini Arusha jana tarehe 05 Januari 2011. Tunalaani vikali kukamatwa na kwenda kuhojiwa kwa Wabunge wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa Taifa Mhe. Freeman Mbowe, Mbunge wa Hai , Mhe. Godbless Lema Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Joseph Selasini Mbunge wa Rombo na Mhe. Philemon Ndesamburo, Mbunge wa Moshi Mjini.

CUF inaamini kuwa CHADEMA kama chama cha siasa kilichosajiliwa kihalali ndani ya nchi yetu kilikuwa na haki ya kikatiba na kisheria ya kufanya maandamano yao ya amani ambayo mwanzoni tayari jeshi la polisi jijini Arusha kupitia kwa kamanda wa polisi wa mkoa lilishaahidi kutoa ulinzi wa kuyaweka maandamano hayo salama.

Jeshi la Polisi na Serikali ndiyo wanaostahili kulaumiwa kwa uvunjifu wa amani uliotokea Arusha. Ushahidi wa kimazingira unaonyesha wazi kuwa amri ya kusitisha maandamano iliyotolewa na IGP saa chache kabla hayajafanyika ilitokana na shinikizo za kisiasa. Hoja iliyotolewa kuwa taarifa za kiintelijensia zinaonyesha kutakuwa na uvunjifu wa amani na ndiyo maana maandamano yanazuiliwa ni usanii mtupu. Kama kweli polisi wana taarifa za kiintelijensia kuwa kuna watu watavunja amani basi wazitumie taarifa hizo kuwadhibiti watu hao na siyo kuyasitisha maandamano na kuwanyima wananchi uhuru wa kisheria wa kufanya maandamano.

Nchi hii inapaswa kuongozwa na katiba na sheria na Watanzania tusikubali Serikali iliyoko madarakani kutumia vyombo vya dola kuua uhuru na demokrasia ya nchi yetu.

Hivi sasa jeshi la polisi limekuwa mstari wa mbele kuzuia kila aina ya madai yanayotolewa na vyama ili mwisho wa siku jeshi lifanye kazi yake kuu ya kulinda CCM na utawala wao kijeuri na kisanii. Haiwezekani kila watu wakitaka kuandamana jeshi la polisi lianzishe hoja ati “kwa sababu za ki-intelijensia” maandamano hayo yanafutwa. Hizi taarifa za ki-intelijensia ni zipi?

CUF inaamini kuwa polisi na serikali ya CCM wanataka kutumia kitisho cha ugaidi kilichozikumba Kenya na Uganda kama sababu ya kupinga mikusanyiko mikubwa ya kisiasa kwa lengo la kuitetea Serikali. Lazima tujiulize,hivi magaidi wakitaka kulipua Tanzania mbona kuna sehemu nyingi sana ambazo wanaweza kufanya hivyo bila kusubiri maandamano ya CHADEMA au CUF au vyama vingine?

Hivi tujiulize kama kweli pana tishio la ugaidi iweje mechi za mpira ziendelee bila kuzuiwa na polisi? Mikusanyiko yote inafanyika isipokuwa maandamano ya vyama vya siasa tu? Hawa magaidi walio tishio kwa jeshi la polisi wanaotaka kulipua maandamano peke yake wametokea wapi? Kwa nini nchi hii iendeshwe kisanii na kiujanja ujanja namna hii? Kwa nini serikali inaogopa maandamano?

CUF inalaani ukatili waliofanyiwa wakazi wa Arusha katika maandamano ya CHADEMA na kuwa ukatili huo hauvumiliki na unahatarisha amani na utulivu wa kweli wa nchi yetu.

Ukatili huu hauna tofauti na ule tuliofanyiwa CUF – Chama cha Wananchi tarehe 28/12/2010 ambapo maandamano ya amani yaliyokuwa yaongozwe na Kaimu naibu katibu mkuu Julius Mtatiro yalipigwa marufuku ghafla na kisha mamia na mamia ya polisi wakisheheni silaha za kila aina wakaanza kuwapiga na kuwakamata wafuasi wa CUF na wananchi wengine walioshiriki katika maandamano yale. Kitendo kile ambacho polisi walikifanya kimetia doa kubwa sana jeshi la polisi linaloongozwa na kiongozi tunayemheshimu IGP Said Mwema.

Kitendo hiki cha pili kilichofanyika Arusha kinazidi kuharibu kabisa sifa na uaminifu ambao vyama vya siasa vilikuwa nao juu ya IGP Mwema. Ni muhimu sana kwa taifa letu kwa IGP Said Mwema kulinda heshima yake na asikubali kutumiwa kisiasa kukandamiza demokrasia ndani ya nchi.

Chama cha wananchi CUF kinaamini kuwa ustawi wa demokrasia, utawala bora, usawa, maendeleo ya nchi yetu na amani ya nchi havitaletwa kwa mtutu wa bunduki wala mabomu wala kila aina ya nguvu, hata kama CCM wataendelea na mbinu zao za kuwadhibiti wapinzani hatutokaa kimya na wala hatutoacha kutumia fursa za kikatiba kutoa maoni yetu kwa njia ya amani kama walivyofanya CHADEMA tarehe 05/01/2011 na CUF tarehe 28/12/2011.

Tunaamini walichokuwa wakipigania CHADEMA jijini Arusha ni kitu cha msingi sana,walikuwa wakipinga kitendo cha kukiuka demokrasia katika uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha. CHADEMA hawakuwa na budi kutumia njia za kidemokrasia kuonyesha kutokukubali na kutotambua utaratibu huo wa kinyemela ulioendeshwa na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kwa manufaa ya CCM.

CUF inawapa pole wahanga wote waliopigwa na kuumizwa na mabomu, risasi, maji ya kuwasha n.k katika tukio hilo la kihistoria la kudai haki ya wanyonge jijini Arusha. CUF iko pamoja nao katika kuendelea kupigania haki. CUF inawapa pole viongozi wote wa CHADEMA waliokamatwa katika maandamano ya Arusha na tunawataka waendelee na juhudi za kupigania ukombozi kama inavyofanya CUF.

CUF inamtaka Rais Jakaya kikwete kutumia busara za hali ya juu sana katika kuendesha nchi katika kipindi hiki ambacho anamalizia miaka yake mitano ya mwisho. Rais Kikwete ana fursa ya kujenga misingi imara ya demokrasia ili akitoka madarakani akumbukwe kwa mambo ya heri na siyo kwa mambo ya shari.

Kukaa kimya kwa Rais wakati polisi wanatumia nguvu kubwa kuua demokrasia ndani ya nchi kunaashiria kuwa wanatimiza amri ya Rais.

Pamoja na mambo yote hayo CUF inawataka Watanzania kuendelea kutuunga mkono ili tuweze kuendeleza mapambano ya kudai demokrasia na maendeleo ya kweli ya nchi yetu kama chama mbadala kitakachomkomboa Mtanzania.

Mwisho tunawataka wakazi wote wa Arusha, Dar es salaam na mikoa mingine wazidi kuungana na CUF na wadau wengine wote muhimu katika madai mazito ya kudai katiba mpya.

CUF inaamini suluhisho la sehemu kubwa ya ukatili unaofanywa sasa ni kukosekana kwa katiba mpya itakayotoa mwongozo sahihi wa taifa letu. Tofauti na sasa ambapo jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola vinaweza kufanya lolote wanalotaka juu ya maisha ya watanzania huku katiba ikiwalinda au wanaivunja na hakuna mwenye mamlaka ya kuwauliza.

Tanzania inahitaji Katiba Mpya ya Wananchi wenyewe na Tume Huru ya Uchaguzi. Tamko la Rais la kuunda Tume Maalum ya Katiba na ishara nzuri ukilinganisha na matamko ya awali ya Waziri wa Sheria na Katiba. Hata hivyo ni muhimu Rais akawafafanulia Watanzania kuwa lengo la mchakato mzima ni kupata Katiba Mpya yenye misingi imara ya demokrasia itakayotokana na ushiriki wa wadau wote. CUF inawaomba na kuwasisitiza Watanzania watuunge mkono sana ili tuhakikishe kwa pamoja tunapata katiba itakayoandikwa upya na kubeba matumaini ya Watanzania na siyo kuwekwa viraka kwa katiba iliyopo.

Imetolewa na

Prof Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti - CUF.
06 Januari 2011.
Dar es salaam.

Tuesday, August 26, 2008

Kongamano la CUF

CUF waandaa kongamano la ukosefu wa uongozi na hatma ya Tanzania

Chama Cha Wananchi
Office of The Secretary General
P.O. Box 10979
Dar Es Salaam, Tanzania
www.cuftz.info
www.hakinaumma.wordpress.blog

TAREHE: 26/08/2008

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUHUSU: KONGAMANO LA KITAIFA KUJADILI
UKOSEFU WA UONGOZI NA HATIMA YA TANZANIA

Imetolewa na Mbaralah Maharagande,
Mkurugenzi Haki za Binadamu na Mahusiano ya Umma.

Nchi yetu inapita katika moja ya kipindi kigumu katika historia yake tokea ilipopata Uhuru mwaka 1961. Hali ya uchumi ni ngumu sana huku gharama za maisha zikipanda kwa kasi ya ajabu chini ya falsafa ya ari, nguvu, na kasi mpya. Tofauti za kipato na kiwango cha maisha kati ya matajiri wachache na walalahoi walio wengi inazidi kuongezeka. Migomo ya wafanyakazi na wanafunzi imekuwa ni jambo la kawaida hivi sasa.

Nyufa katika Muungano wetu zinazidi kukua na hata kutishia uhai wa Muungano wenyewe. Migawanyiko ya kidini inaonekana kuzidi kujikita. Mpasuko wa Kisiasa Zanzibar umeshindwa kupatiwa jibu huku uchaguzi mkuu wa 2010 ukiwa unakaribia. Serikali inaonekana kuzidiwa nguvu katika mapambano dhidi ya ufisadi na sasa mafisadi wanaonekana kutamba. Taifa linakwenda bila ya Dira wala Mwelekeo unaoeleweka. Wananchi wanaonekana kukata tamaa.

Matatizo haya kwa kiasi kikubwa yanaonekana kusababishwa na ukosefu wa uongozi thabiti, makini na adilifu. Hii si hali nzuri na tusipokuwa makini Taifa litayumba sana. Wazalendo wakweli wa Tanzania hawapaswi kukaa kimya na kusubiri matokeo ambayo kwa vyovyote vile hayawezi kuwa mazuri.

The Civic United Front (Chama Cha Wananchi-CUF) kikiwa chama makini kikuu cha upinzani nchini, kinachotegemewa na Watanzania walio wengi, kimeandaa kongamano maalum kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu hali hii ya ukosefu wa uongozi na athari zake kwa hatima ya Tanzania. Kongamano hilo litafanyika siku ya Alhamis, tarehe 28 Agosti, 2008, kuanzia saa 3.30 asubuhi katika ukumbi wa Diamond Jubilee, mjini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Mhe. Prof. Ibrahim Lipumba, atawasilisha mada kuhusu UKOSEFU WA UONGOZI NA HATIMA YA TANZANIA na baadaye washiriki watapata nafasi ya kuichambua mada hiyo na kutoa maoni na mtazamo wao.

CUF imewaalika watu mbali mbali kushiriki katika kongamano hilo wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa, wahariri na waandishi wa vyombo vya habari, taasisi za kiraia na kijamii, viongozi wa kidini, wasomi na wataalamu, maofisa wa kibalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania, wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

HAKI SAWA KWA WOTE
Mbaralah Maharagande,
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano ya Umma.

0773 062 577

Monday, August 04, 2008

Vigogo Wahaha! - Kifo cha Wangwe

Naona hata mwandishi wa hii stori kahofia maisha yake, wameandika 'mwandishi wetu' . Sasa kilichobaki ni kuita Scotland Yard wachunguze.

*******************************************************

Kutoka ippmedia.com

Kifo cha Wangwe: Vigogo BP juu!

2008-08-04

Na Mwandishi Wetu, Jijini

Mazingira tata ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime, Mhe. Chacha Wangwe (CHADEMA), yamewafanya baadhi ya vigogo kuingiwa na hofu kubwa ya maisha yao na sasa wengine wamedai kuwa wana data ambazo hata kuzianika hadharani wanaogopa kwa sababu za kiusalama.

``Uchunguzi umethibitisha wazi kuwa Wangwe hakuuawa kwa risasi... lakini pamoja na ukweli huo, bado baadhi ya vigogo katika siasa, hasa wale wa upinzani, wamekuwa na hofu kutokana na mazingira tata ya ajali yenyewe na kile kilichomtokea (Wangwe) hadi kufa,`` kimesema chanzo chetu kimoja kilicho jirani na vigogo maarufu wa upinzani nchini.

``Hivi sasa kuna data nyingi zilizopatikana na kuibua maswali mengi kuhusiana na kile kilichotokea. Kijana aliyekuwa na Wangwe wakati wa ajali ndiye anayeelekezewa kidole zaidi kutokana na maelezo yake kila alipohojiwa... hili limeongeza hofu zaidi kwa vigogo hao, wakiamini kuwa wao wako hatarini na taifa pia liko hatarini,`` kimeongeza chanzo hicho.

Taarifa hizo za kuwepo kwa hofu miongoni mwa baadhi ya vigogo zimetiwa nguvu na yale yaliyosemwa jana Wenyeviti wa Umoja wa Vyama vinne vya upinzani nchini jana na kunukuliwa na vyombo vya habari leo asubuhi, kuhusiana na shaka iliyopo katika ajali iliyomuua Mheshimiwa Wangwe.

Wakizungumza hiyo jana, wenyeviti wa vyama hivyo vya CUF, CHADEMA, TLP na NCCR, wamesema wanazo taarifa zinazoibua maswali mengi kuhusiana na kifo cha Wangwe, hasa juu ya kijana anayedaiwa kuwa naye ndani ya gari, Bw. Deus Mallya.

Wakasema maelezo ya kijana huyo juu ya tukio hilo, namna Wangwe alivyopata majeraha yaliyomuua na ziada ya taarifa walizopata toka kwa watu wanaomfahamu kijana huyo (Mallya), ni baadhi ya mambo yanayowafanya wawe na hofu kuwa kuna ujasusi umefanyika.

Wakasema viongozi hao ambao ni Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF, Augustino Mrema (TLP) na James Mbatia (CHADEMA), kuwa kwa taarifa walizo nazo, wanaamini vilevile kuwa upo mtandao hatari unaotishia usalama wa taifa.

Akizungumzia hofu hiyo, Prof. Lipumba akasema waliyemuona Mallya kabla ya tukio, wanasema alikuwa ni mtaalam wa kompyuta, alikuwa na vitambulisho vingi na vingine vimeandikwa kiarabu na pia, wanahisi kuwa amepata mafunzo ya kijasusi nchini Libya.

``Imekuwaje akawa karibu na marehemu kwa muda mfupi?`` Akahoji Profesa Lipumba wakati wakizungumza na waandishi wa habari. Akautaja utata mmojawapo juu ya kifo cha Wangwe kuwa ni kuonekana kuwa kichwa cha marehemu kimepondeka na hakuna maelezo dhahiri ya suala hilo. ``...mle ndani ya gari hakuna hakukuwa na vyuma wala mabati yaliyopondeka.

Kweli hakufa kwa kupigwa risasi... lakini ile ajali ilitokeaje mpaka lochwa kikapondeka?`` akasema Prof. Lipumba. Aidha, Mbatia naye akasema.

Aidha, Mbatia naye akasema kutokana na utata mwingi juu ya kifo hicho ikiwa ni pamoja na maelezo ya kujikanyaga ya kijana Mallya, wao wameamua kumuona IGP Said Mwema ili wampe taarifa za siri kuhusiana na ukweli wa kifo hicho, kwa maslahi ya taifa.

``Inaonekana kuna mtandao unaohatarisha usalama wa nchi.... kijana huyo (Mallya) ana mafunzo ya Kimafia,`` akasema Mbatia.

SOURCE: Alasiri