Showing posts with label EPA. Show all posts
Showing posts with label EPA. Show all posts

Friday, September 16, 2016

Matokeo ya Tanzania Kukataa EPA


KAMA mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na zile za Umoja wa Ulaya (EU) utaendelea kubaki kama ulivyo sasa, ni wazi kwamba Tanzania itabaki na msimamo wake.

Nimezungumza na baadhi ya mawaziri wa serikali ya Rais John Magufuli na nadhani msimamo huo utabaki ulivyo hata baada ya kupita kwa miezi mitatu kama ambavyo wakuu hao walitangaza wiki iliyopita.

Lakini, hivi kuna nini kibaya kwenye mikataba hiyo ya kiuchumi ambayo inafahamika kwa kifupi cha EPA (Economic Partnership Agreement)?

Kuna mengi lakini nitasema machache tu. Mikataba hiyo inataka Tanzania iondoe ushuru wa bidhaa kutoka nje zisizokuwa za kilimo kwa asilimia 90 na pia ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa za kilimo kutoka kwao. Hapa wanataka bidhaa zao zije kushindana na zetu wakati wao wameendelea zaidi kimtaji na kiteknolojia.

Nchi wanachama wa EAC watabaki kuwa masoko ya bidhaa za Ulaya. Wakati huohuo, kwa utaratibu huo wa bidhaa za kilimo, maana yake ni kuwa nchi hizi za Afrika zitabaki kutoa malighafi tu kwa ajili ya viwanda vya Ulaya kuzalisha bidhaa.

Kwa utaratibu huu wa EPA, Tanzania ya viwanda haitawezekana asilani. Hakuna namna ambayo viwanda vya Afrika vinaweza kushindana na vile vya Ulaya. Kuna kipengele pia katika mkataba huo ambacho kinataka nchi za Ulaya zipewe upendeleo uleule ambao watapewa wabia wengine wa kibiashara wa Afrika kama vile India na China.

Yaani, kwa mfano, kama tukisema India tutawapunguzia ushuru wa bidhaa hii kwa kiwango hiki, basi na Ulaya nao wafaidi kwa kiwango hichohicho. Cha ajabu, mkataba huo hausemi kwamba na wao wazungu wakiingia makubaliano ya namna hiyo na rafiki zao, nasi wa EAC tufaidi vilevile. Hakuna !

Ukiniuliza kwanini Kenya, Rwanda na Uganda wanataka kusaini mikataba hiyo, jibu langu litakuwa sijui. Lakini, ninachojua ni kitu kimoja pekee –kwamba wazungu hawataacha hili lipite hivihivi.

Jijini Dar es Salaam, Rais Yoweri Museveni alizungumza wiki iliyopita mbele ya wageni akiomba watu wa EU wasiiadhibu Kenya kwa kuwa imekubali kusubiri hiyo miezi mitatu.

Museveni anawajua wazungu. Anajua visasi vyao. Inawezekana mara moja au mbili kwenye utawala wake amewahi kukumbana na visanga vyao.

Kwenye kitabu chake Trade is War, Profesa Yash Tandon, ameandika kwamba inawezekana Uganda na Rwanda zimebanwa na wazungu kwamba wakikataa kusaini, wanaweza kukosa misaada mbalimbali mingine ambayo haihusiani na EPA kama vile silaha na vita dhidi ya ugaidi.

Tandon, mmoja wa wasomi mashuhuri barani Afrika, ameandika pia kwamba biashara ya maua; inayofanywa na matajiri wengi wa Kenya wakiwamo wanasiasa, itaathirika endapo viongozi wa EPA wasiposaini. Kwa kuishughulikia biashara hiyo, watu wa EU wanafahamu watakuwa wanafanya jambo ambalo linawaumiza wakubwa moja kwa moja.

Nchi za Ulaya, na mabeberu katika ujumla wao, hawapendi nchi masikini kujiamulia mambo yao. Wanafahamu kwamba Tanzania ikiwa na uchumi wa viwanda, itajikwamua kutoka kwenye makucha yao. Wanafahamu kwamba wao waliendeleza viwanda vyao kwa kuvilinda. Sisi wanataka tusivilinde.

Fidel Castro si kiongozi mbaya. Lakini mabeberu hawakupenda siasa zake za kutotaka kulamba miguu ya wakubwa. Matokeo yake ni kuwa nchi yake leo inachechemea. Hali iko hivyo kwa Venezuela ya Hugo Chavez na hata Chile ya Salvador Allende.

Patrice Lumumba alionyesha dalili mapema kwamba atakuwa mwiba kwa mabeberu, akapotezwa. Hapa kwetu, mtu kama hayati Abdulrahman Babu aliishia kuwekwa rumande na kupewa kazi za kutangatanga tu bila utulivu. Mabeberu wasingekubali apewe nafasi ambayo angeonyesha njia ya kweli ya maendeleo.

Hatua hii ya Magufuli na serikali yake si hatua ya mchezo. Endapo mwishowe atakataa kabisa kusaini mikataba hiyo, afahamu kwamba atatangazwa kuwa adui namba moja wa mabeberu.

Habari zake zote zitakuwa mbaya. Ataandikwa kwa aliyoyafanya na asiyoyafanya. Atapewa majina ya kila namna na uchumi wetu utaanza kufanyiwa hujuma. Na kwa sababu mabeberu ndiyo wameshika uchumi wa dunia, safari ya huko tuendako inaweza isiwe rahisi.

Kama ameamua kwa dhati kufuata njia hii, ni muhimu ajiandae na yanayokuja. Ingekuwa vema pia kama angeweza kushirikisha jamii pana ya Watanzania katika kufahamu kiini na sababu za kuchukua hatua anazochukua. Hii ni sawa na kusema anatakiwa pia kuwaandaa watu wake.

Kama serikali ya Magufuli ina nia ya dhati ya kuhakikisha Tanzania inajenga viwanda vyake na haibaki kuwa soko la malighafi kwa ajili ya viwanda vya mabeberu, ni muhimu ikashikilia msimamo wake wa kukataa kusaini EPA kama ilivyo sasa.

Cha msingi, ni kufahamu kwamba mabeberu hawatakaa kimya wala bwete wakati Tanzania ikichukua uamuzi mkubwa na muhimu kama huo.

Raia Mwema

Monday, September 22, 2008

Skandali nyingine Bank of Tanzania (BoT)






Kutoka kwa Mzee wa Sumo (Mpoki Bukuku) Blog:

" Hii ni kutoana nishaji jamani na ukiukwaji haki za wanawake yaani wengine wameamua kutoa wigi la urembo kujikinga na fedheha! Sijui wengine walikuwa na swaum? " - Mpoki Bukuku akizungumzia picha alizopiga.

TUHUMA za kuwepo kwa upendeleo wa watoto wa vigogo kwenye ajira za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zimesimamisha kizimbani wafanyakazi wanane ambao wameshtakiwa kwa kosa la kughushi vyeti.

Tuhuma dhidi ya watoto 16 wa vigogo ziliibuka wakati kashfa ya wizi wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), ikiwa imeshamiri kiasi cha kusababisha aliyekuwa gavana, Daud Ballali kusitishwa mkataba wake na kufanyika kwa mabadiliko kadhaa kwenye uongozi wa chombo hicho nyeti cha fedha.

Na Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, aliahidi kuzishughulikia tuhuma hizo wakati huo baada ya tuhuma hizo kushikiwa bango.

Jana, wafanyakazi wanane wa BoT, baadhi yao wakiwa wamejifunika nyuso kwa nguo na nywele za bandia, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakishtakiwa kwa tuhuma za kughushi vyeti na kutoa hati za uongo.

Wafanyakazi hao, wengi wao wakiwa wanawake, ni Justina J Mungai, ambaye imeelezwa kuwa ni mtoto wa Joseph Mungai, ambaye amewahi kushika wizara tofauti ikiwemo ya elimu, Christina G Ntemi, Siamini Eddie Kombakono, Janeth John Mahenge, Beatha Constantine Massawe, Jacquiline David Juma, Philimina Philibert Mutagurwa na Amina Mohamed Mwinchumu.

Wafanyakazi hao walifikishwa katika mahakama hiyo saa 4.00 asubuhi na kusomewa shtaka mbele ya Hakimu Neema Chusi. Wakili wa serikali, Edgar Luoga, akisaidiana na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Abubakar Msangi, ndio walioongoza mashtaka hayo.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kutoa hati za uongo kwa mwajiri wao, ambaye ni BoT.

Washtakiwa Mungai, Massawe na Mwinchumu, wanadaiwa kughushi vyeti hivyo mwaka 2001, wakati Ntemi, Kombakono, Mahenge na Mutagurwa wanadaiwa kughushi vyeti hivyo mwaka 2002. Wanadaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kutoa BoT hati za uongo, wakionyesha kuwa vimetolewa na Baraza la Mitihani la Taifa, wakati si kweli.

Ilidaiwa kuwa, Mutagurwa alighushi cheti hicho mwaka 2000.

Thursday, August 21, 2008

Kulikuwa hakuna Makuu!

Rais Kikwete akihutubia Bunge leo

Imeandikwa na Beda Msimbe

Gumzo la lukwangule:Nilichovuna saa 4 za kumsikiliza rais

JANA nilisema kwamba kutakuwa na makubwa leo. Naamini saa nne za kumsikiliza JK hazikuzaa hasara kama mtuma habari. Lakini kama mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi yapo makubwa yaliyoainishwa na kutolewa ufumbuzi ambao unaweza usiwe bora leo lakini miaka kadhaa ijayo.

Jambo la msingi ambalo mimi nimeliona ni kuwa masulaa niliyodhani atayagusa aliyagusa, sikutarajia mengi makubwa katika EPA kwa kuzingatia mfumo wa sheria wa nchi yetu, lakini kwa sasa wabunge waliokuwa hawaelewi nini EPA sasa watakuwa wameelewa.

Nilichotoa hai katika EPA ni kufilisiwa kwa watu, kunyimwa nafasi ya kusafiri na fedha hizo zinazorejeshwa kusaidia wakulima kwa kuanzisha ruzuku katika mbolea na pia katika kusaidia TIB yaani Tanzania Investment Bank kuwa na uwezo wa kukopesha wakulima kwa muda nrefu na riba nafuu.

Swali linalobaki je hawa wahuni waliotwaa fedha ambazo si za serikali lakini serikali inaweza kudaiwa watafanywa nini? Matajiri azimio la Arusha walishughulikiwa kwa kurejesha mali zao kwa umma je hawa hawastahili kweli kushtakiwa, wanasheria wanajua lakini la maana zaidi utawala wa sheria hauna maana ya kuachia wakwivi kutokomea hivi hivi tu lakini pia si kwa kuwafanya waingie mahakamani bila kigezo, hawa ni wevi au wajanja hilo ni swali kwanza kisha... waswahili wanasema habari ndio hiyo... lakini amesema kwamba Novemba Mosi kitaeleweka mahakamani.

Nilisema shauri la Zanzibar lakini kidiplomasia kabisa kasema watu wasikoroge mambo na kwamba ukiwa nje ni tanzania ukirejea hapa unazungumza zanzibar, alitumia akili sana kuhusu hili hasa aliposema wimbi hili nalo litapita walio watu wazima wasiwe wapuuzi, nadhani kimeeleweka.

Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Bunge hilo kwa mara ya pili tangu ashike madaraka mwishoni mwa mwaka 2005 nilichoona kama alivyowahi kusema katika hotuba yake ya kwanza alitumai tena fursa hiyo kuelezea mwelekeo wa uchumi wa taifa na masuala mbalimbali ambayo serikali yake imekuwa ikiyapa kipaumbele.

Na shida zote alisema tusigombee fito, tunajenga nyumba moja na hili siwezi kulikataa, lakini inakuwaje unapokuwa na watu ambao hawaelewi hasa nini wanatakiwa kukifanya, na watu hao wakiwa viongozi? Lipo tatizo la ufinyu wa sheria na utawala pengine Sitta yuko sahihi sheria zetu zinaruhusu mambo kuenenda kigoigoi zaidi.

Huu muungano nao aliuzungumzia vyema, alisema wazi ubaya wa uropokaji, alisema matamshi ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya viongozi yanaweza kuchangia kuwavuruga kama siyo kuwachochea wananchi.

Ilivyo ni kwamba kama ni kujadili suala la Muungano basi hapana budi mjadala ufanyike kwa hekima na busara na siyo jazba kama ambavyo imejitokeza katika siku za karibuni, hili siliendelezi sana.Na huu mpasuko wa Zenj kumbe ulishafikia hatua nzuri lakini jamaa hawa wa Unguja kama wanavyosema katika suala la U nchi na Usio nchi amesema wanashindwa kuaminiana.

Kitu ambacho nilikiona kuwa kidogo cha mgomo, kumbe sivyo, rais alizungumzia haki ya watu kugoma, lakini ndani ya sheria, ndani ya uelekezi wa kawaida uliokubalika, kama kweli ni mgomo unaostahiki. Hapa alifafanua vyema kuhusu mgomo unaokuja, hakuugusia wa walimu lakini huu wa TUCTA alisema mpaka kwa Kiingereza haukubaliki. Alikuwa na vigezo vyake.Alisema kwamba mfuko wa hazina baada ya makubaliano sio ATM ni lazima kuweka sawa baada ya bajeti na walizungumzia Agosti sasa watu watazame kama serikali haitalipa.

Kweli kabisa serikali kwa mgao wa kota si ATM lakini nini maana ya maneno yote hayo ambayo serikali inazungumza. Inamaananisha kwamba haipo tayari kuyumbishwa, makubaliano ni muhimu watu wa TUCTA wanajua wamevumilia kiasi gani lakini wachambuzi wa mambo wa naweza pia kuelewa kwa kina nini maana ya kauli ya serikali kuhusiana na njia zilizotumika kutangaza mgomo.

Shauri la mwisho ambalo mimi nilisema ni la kawaida ni matumizi mabaya ya uhuru wa kunadika na kusema, maandamano,kupiga domo, kupinga serikali,kushughulikia hasira na kutuliza munkari.kwa haraka haraka unaona kwamba alikuwa anachimba mkwara, lakini kama yeye aliwezesha upana wa mambo katika kucheua sumu mwilini alitaka watu wawe wastaarabu wasitapike bila mpangilio wakawavushia matapishi wenzao wakabaki wananuka bila sababu.

Hili halina ubishi kucheua sumu muhimu lakini utapike kwa mipangilio na uwe na sababu sio uachie tu mradi mdomo wa kutapikia unaoKimsingi mimi nasema rais saa zake nne hazikuwa mbaya sana ingawa haya mengine ni elekezi za kawaida za nini amefanikisha katika miaka miwili na miezi saba ya utawala wake, kilichobaki ni kuangalia ushauri wa spika kwamba kunahitajika kasi zaidi kushughulikia wanaohujumu uchumi kwa mtindo wa EPA.

Naam, kweli tunahitaji mabadiliko kwani hii ni salamu, kazi yenyewe bado iko kwa wananchi wenyewe, ni hotuba inayotakiwa kuchambuliwa, kuna mengi sana ambayo sikuyatia hapa kwani huenda yakasaidia miaka mitatu ijayo wakati wa uchaguzi: ni ukweli kuwa wanaobungua nchi hii ni viongozi wafanyabiashara kwa hiyo tunahitaji waamue ama kuwa na biashara au kuwa wanasiasa na viongozi, hata ughaibuni linajulikana.

Monday, August 18, 2008

Taarifa ya Ikulu - EPA

Taarifa ya Ikulu kuhusu EPA


DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail : press@ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120
DAR ES SALAAM.Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo (Jumatatu, Agosti 18, 2008) amepokea rasmi ripoti ya uchunguzi wa upotevu wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Nje (External Payments Accounts - EPA) katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Rais Kikwete amekabidhiwa ripoti hiyo na Mwenyekiti wa Timu iliyokuwa inafanya uchunguzi huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson P.M. Mwanyika.Mwanasheria Mkuu huyo alifuatana na wajumbe wengine wa Timu hiyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Saidi Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Edward Hosea.

Rais amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Timu hiyo kwa kazi kubwa na ngumu lakini nzuri.Rais, baada ya kuwa ameisoma na kuitafakari ripoti hiyo, ataitolea maamuzi katika siku chache zijazo, na taarifa rasmi ya maamuzi hayo ya Rais itatolewa kwa wananchi.

Timu hiyo iliundwa na Rais Kikwete Januari 9, mwaka huu, 2008 katika tangazo rasmi lililotolewa kwa waandishi wa habari na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.Wakati anaunda Timu hiyo, Rais aliipa muda wa miezi sita kukamilisha kazi yake, ambayo ilikuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa fedha zilizolipwa isivyo halali zinarudishwa.

Rais aliunda Timu hiyo baada ya kuwa amepitia Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Mwaka wa Fedha 2005/06 za EPA katika Benki Kuu Tanzania (BOT), uliofanywa na Wakaguzi wa Kampuni ya Ernst and Young, kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.Kampuni hiyo ya Ernst and Young iliombwa na Serikali kuifanya kazi hiyo.

Iliianza Septemba, 2007 na kumalizika Desemba, mwaka huo huo, 2007. Rais Kikwete alikabidhiwa Taarifa hiyo Januari 7, mwaka huu, 2008 na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Siku ya tatu, baada ya kuwa ameisoma na kuifanyia kazi, Rais aliitolea maamuzi Taarifa hiyo, ikiwa ni pamoja na kuunda Timu ya Mwanyika.

Imetolewa naKurugenzi ya Mawasilia ya Rais,

Ikulu,DAR ES SALAAM.

18 Agosti, 2008