Al
Shaabab Ni Nani? ( Makala Raia Mwema)
Na Maggid Mjengwa,
ULIMWENGU umepatwa na mshtuko mkubwa kwa kuona picha za tukio kubwa la
kigaidi kwenye moja ya maduka makubwa jijini Nairobi. Hili ni shambulio kubwa
la kigaidi kupata kutokea Afrika Mashariki tangu lile la mwaka 1998. Na ajabu
ya kihitoria ni kuwa matukio mengi ya kigaidi yametokea katika mwezi wa
Septemba.
La Nairobi ni shambulizi la kigaidi la kulaaniwa vikali na wapenda amani
wote ulimwenguni. Hata hivyo, moja ya tafsiri ya vitendo vya kigaidi
tunavyovishuhudia Nairobi ni kuwepo kwa hali ya vita vya kigaidi vyenye
kuendeshwa kwenye maeneo ya mijini (Urban terrorism).
Ni shambulizi lenye athari mbaya kiuchumi si tu kwa nchi ya Kenya, bali hata
majirani zake ikiwemo Tanzania. Ni shambulizi lililowaogopesha wageni wengi
wakiwamo wawekezaji pia. Kwamba Al Shabaab inalenga pia nchi za Magharibi.
Hivyo basi, hata raia wake. Kunahitajika jitihada za pamoja kuwaondoa hofu watu wa
mataifa ya nje, kuwa kilichotokea Nairobi kitadhibitiwa kwa njia zote,
kisitokee tena.
Na hakika, aina hii ya ugaidi ni ngumu sana kudhibitika hatakama nchi ina
jeshi kubwa na lenye vifaa vya kisasa. Inahitaji ushiriki wa raia wema katika
kutoa taarifa za wahalifu hata kabla hawajafanya matendo yao maovu. Inahitaji
pia maandalizi makini, ya kuwa na vikosi vilivyo tayari wakati wote kukabiliana
na matukio kama haya.
Ni dhahiri, kuwa mbinu inazotumika kikundi cha kigaidi cha Al Shaabab ambacho
maana hasa ya jina hilo ni ' Vijana', ni moja ya changamoto kubwa katika
mapambano dhidi ya ugaidi.
Al Shabaab iliundwa mwaka 2006. Kinasemekana kuwa na wapiganaji wenye silaha
wapatao 10,000. Al Shabaab katika miaka ya karibuni wamepoteza maeneo mengi ya
mijini waliyokuwa wakiyadhibiti, ikiwamo mji wa Kismayu ambao majeshi ya Kenya
yaliudhibiti baada ya kuwasambaratisha Al Shabaab. Kwa sasa Al Shabaab bado
wana nguvu maeneo ya vijijini katika Somalia.
Kufuatia Kenya kujiingisha kijeshi kupanbana na Al Shaabab, kikundi hicho
kimeifanya Kenya kuwa adui na kutangaza wazi azma yake ya kuishambulia Kenya.
Mwezi Aprili mwaka huu watu watano walipoteza maisha nchini Kenya baada ya
wapiganaji wa Al Shabaab kuingia kwa nguvu wakiwa na silaha kwenye mgahawa mmoja
kwenye mji wa Garissa nchini Kenya.
Mwaka 2012 ndipo Al Shabaab walipojiunga rasmi na mtandao wa kigaidi wa Al
qaida chini ya kiongozi wa Al qiada, Ayman al- Zawahiri.
Hakika, hapa duniani matukio ya kigaidi yameongezeka.
Kwa faida ya wasomaji, nitaanza kwa kuangalia chimbuko la ugaidi kihistoria. Ni
rahisi kusema kwamba ulimwengu umebadilika baada ya ugaidi wa Septemba 11 mwaka
2001 kule Marekani. Kwamba ugaidi umesogea karibu zaidi katika fikra zetu.
Watanzania bado tunakumbuka tukio la shambulizi la kigaidi dhidi ya jengo la
Ubalozi wa Marekani jijini Dar Es Salaam Agosti 7, 1998.
Sura ya ugaidi imeonekana vema zaidi miongoni mwa walimwengu. Bila shaka,
picha ya filamu ya televisheni yenye kuonesha majengo mawili ya World Trade
Centre kule Marekani yakitunguliwa na kuanguka, zimeonwa na takribani asilimia
75 ya watu wa ulimwengu huu. Katika hili la kuchambua ugaidi, hebu
basi tuanze na kujiuliza;
Ugaidi ni nini?
Itakumbukwa wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano walipokutana Dodoma
mwaka 2002 walipitisha Muswaada wa Ugaidi. Wabunge wetu walitumia muda mwingi
sana kujadili tafsiri ya neno "ugaidi".
Kwa kifupi, ugaidi ukitafsiri kutoka neno la Kiingereza
"Terrorism" tunapata maana ya "hofu". Neno la Kiingereza
"Terror" lina maana ya hali ya "kutisha".
Vitendo vya kigaidi hutumiwa na mtu au makundi ya watu ili kuwaingizia watu
hofu ndani ya mioyo yao na pengine hata kuchukua madaraka ya kisiasa. Ugaidi ni
njia ya mnyonge na hata mwenye nguvu kutimiza malengo yake. Hili litafafanulika
zaidi kadri utakapofuatilia maandiko haya.
Kihistoria tunaona kuwa, vitendo vingi vya kigaidi humu duniani vimefanywa
pia na dola zilizo madarakani kwa minajili ya kuendelea kushika hatamu za dola.
Mathalan, msemo wa " Utawala dhalimu" kwa tafsiri ya Kiingereza
"Terror regime" hutumika tunapoielezea dola yenye kutumia mabavu na
nguvu nyingi kupita kiasi. Dola au mtawala asiyezingatia sheria wala haki za
kibinadamu.
Msamiati huu wa utawala dhalimu unatokana na lugha ya Kifaransa na una
chimbuko la Mapinduzi ya Wananchi kule Ufaransa kati ya mwaka 1789 hadi 1799.
Utawala dhalimu wenye kutisha" la terreur" ulikuwepo kule Ufaransa
kunako miaka ya kati ya 1792 hadi 1794. Katika kipindi hicho watu takribani
40,000, wengi wao wakiwa wakulima na wahunzi waliuawa.
Mifano ya tawala dhalimu na za kutisha katika sehemu nyingine za dunia ni
kama Urusi ya zamani chini ya dikteta Stalin, utawala wa Kinazi wa Ujerumani
kati ya 1933-1945 chini ya Fashisti Hittler.
Katika Afrika, tuna pia mifano kadhaa ya tawala dhalimu na za kutisha ambazo
kimsingi ni tawala za kigaidi. Uganda ya Idd Amin, Afrika ya Kati ya Bokassa,
Zaire ya Mobutu, na nchi nyingine nyingi. Hizi zilikuwa tawala dhalimu.
Ugaidi kimsingi ni ile hali ya mtu, kikundi au dola, kwa maana ya
taifa,kutumia nguvu nje ya wigo wa sheria ili kufikia malengo yao. Mwenye
kuendesha vitendo vya kigaidi huchagua watu wake watakaoathirika na vitendo
hivyo. Si lazima mtu au watu hao watakaoathirika wawe ni wahusika wa moja kwa
moja wa mgogoro husika, isipokuwa, waathirika mara nyingi huchaguliwa na huonekana
kama wawakilishi wa malengo ambayo magaidi wanataka kuyafikia.
Malengo au sababu za ugaidi zaweza kuwa ni za kidini, kijamii na kisiasa.
Ugaidi huwa wa kimataifa pale tukio la kigaidi linapofanywa nje ya mipakaya
yule anayatenda tendo la kigaidi, au raia wa nchi moja wanapokuwawalengwa na
kauthirika na tendo la kigaidi katika nchi ya tatu, mathalan,magaidi kutoka
Colombia wanapofanya tendo la kigaidi dhidi ya raia waUingereza katika nchi ya
Zambia.
0754 678 252,
http://mjengwablog.com