Tuesday, February 14, 2006

Kumbuka Mpenzi Wako!

Leo ni Valentine’s Day yaani sikukuu ya Wapenzi. Ni siku ya kukumbuka wapenzi wetu. Na huko Tanzania nakumbuka tulikuwa tunakesherekea kwa kupeana kadi na zawadi ndogo ndogo. Mwanamke anaweza kukuta ana zawadi ya kanga mpya, perfume, vitambaa, nk.

Na hapa Marekani unaona watu wana haha kununua maua, machocolate, kadi, na hata chupi nyekundu na nguo za ndani zingine zenye theme ya Valentines Day. Basi bei ya maua, na hivyo vitu vimepanda kweli kweli. Yaani dozen roses leo ni zaidi ya dola mia! Hata yule mChina anayeuza maua kwenye kituo cha subway kapandishwa bei. Maua sita anauza dola thelathini, wakati juzi zilikuwa dola sita tu. Na watu wananunua kusudi wasionekane kama hawapendi wapenzi wao.

Pia, leo ni siku ya wapenzi kuonyesha mapenzi yao huko faragha yaani chumbani. Basi bidhaa za mapenzi zinauzwa kwa kasi, na hata condoms zinatolewa bure sehemu nyingi.
Watu wananunua mishumaa, mafuta, na manukato mengine, na vitu vya kufanya mapenzi iwe ya ajabu. Huko CVS na Walgreens ile sehemu ‘nyeti’ inapata biashara kweli!

Lakini nilikuwa naangalia hao wanaume wanamnunulia nani hizo zawadi. Utakuta mke kamnunulia kachocolate kidogo na kimada kamnunulia Chocolate boxi kubwa!

Basi leo nikakumbuka maongezi na wanaume kadhaa Tanzania na Marekani. Ni maongezi ya kawaida tu na wala msidhania kuwa mimi nilikuwa mpenzi wao. Utasikia mwanaume anasema mke wangu nampenda lakini zile feelings nilizokuwa napata wakati ndo yetu bado changa sisikii tena.

Niliwahi kumwuliza baba fulani, ofisa katika wizara fulani huko Tanzania kwa nini anapenda kutembea na wanawake wanaofanya kazi ofisini kwake. Nilishangaa jamaa alivyokuwa muwazi kwangu kasema “Mke wangu kachoka!” Nikamwuliza mke kachoka kwa vipi? Jamaa kasema eti matiti yake yamenyauka, kanenepa, siyo kama alivyokuwa nilivyomwoa. Nikamwuliza amebarikiwa watoto wangapi na huyo mke wake, kaniambia kuwa wana watoto sita.

Nikamkumbusha kuwa huyo mke wake ndiye mama watoto wake. Mwili wake ameutoa kama sadaka kwa ajili yake na hao watoto. Jamaa kafikiria halafu kaniambia, ni kweli, na kakumbuka kuwa alivyomwoa alikuwa mzuri kweli. Nikamshauri aende akambusu mke wake huko kwenye tumbo yake kuonyesha mapenzi na kuwa anashukuru kuwa kamzalia hao watoto.

Mwingine kaniambia kuwa eti matiti ya mke wake yamelala na yeye anapenda matiti saa sita. Anasema anapenda matiti yakimchoma kifuani akiwa anafanya mapenzi. Basi nikamwuliza kama mke wake alikuwa na matiti saa sita wakati anamwoa, kasema Ndiyo. Basi nikamkumbusha kuwa na huyo kimada wake 'spring chicken' akizaa na matiti wake yataanguka pia.

Mwingine kaniambia kuwa eti anamwona mke wake kama dada yake, hata hawezi kusimamisha hata mke wake akilala uchi kitandani! Hapo nilipigwa butwaa! Nikaona huyo kweli ana matatizo na mke wake, maana wanaume wangi wakipata nafasi ya kufanya ngono wanasimamisha bila shida! Huyo jamaa ana vimada kibao, na nadhani ana ugonjwa wa akili!

Na mwingine kaniambia kuwa anapenda kutembea na 'spring chicken' kwa vile huko chini pana bana. Nikamwambia kuwa akimzalisha mke wake kila mwaka chensi ya kuelegea huko chini ni kubwa maana uke haupati nafasi ya kurudi katika hali yake ya awali. Lakini jamani navyoona wanawake wengi pana bana ila basi tu, wanaume mnakuwa na fikra kuwa mwanamke kazaa basi tena panalegea!

Mwanaume mwingine anasema hataki kutoka na mke wake kwenye party kwa vile eti, ‘kazeeka’ au eti hajui kuvaa vizuri. Kwanza kama ni housewife ulimpa hela ya kununua nguo na viatu kusudi avae vizuri? Huko utakuta kimada katoka vizuri na nguo latest, tena kamnunulia mwanume huyo huyo. Na kama mke hana msaada huko nyumbani kweli atakuwa kachoka maana kulea watoto na kufanya house chores inachosha.

Lakini kinachoniudhi zaidi ni wanaume ambao wanasahau kutunza familia zao na badala yake wanatunza vimada au nyumba ndogo. Unakuta mke na watoto wanaishi kwa dagaa, nguo zao zimechakaa, na girlfriend anakula nyama fillet na ana nguo mpya! Wanaume mna laana kweli!

Lakini pamoja na kuwa mnasema mwanamke kachoka, na nyie wanaume mnachoka pia! Badala ya six pack mnakuwa na vitambi, full head ya nywele kichwani mnakuwa vipara, na hata huo ubarikio wenu hauwi mgumu kama ilivyokuwa awali.

Kumbukeni kuwa kila mtu atazeeka na kuonekana kuchoka. Na ule mwili uliyokuwa nayo ukiwa na miaka 20, hutakuwa nayo ukiwa na miaka 50! Lakini cha muhimu leo tuonyeshe mapenzi na heshima kwa wapenzi wetu.

Friday, February 10, 2006

Wanaume Mkienda ‘Abroad’ Mzoee Kufanya Mambo ya Kike Kike

Leo ngoja niongee kuhusu tatizo wanaume wa kiBongo wanaopata wakija hapa Marekani au Ulaya Hasa wakienda sehemu enye baridi sana.

Ni kweli huko Tanzania tumezoea kukaa kwenye joto na kutoka jasho kila wakati. Lakini ukienda sehemu wakati wa winter mbona utakoma ha huo ubaridi.

Na kama ulikwishafika Ulaya/Marekani wakati wa winter unajua kuna tatizo kubwa sana na ni ngozi kukauka. Utaona mtu mweusi mikono meupe kama vile kaziingiza kwenye poda vile. Kumbe ngozi umekauka shauri ya hali ya hewa. Ukiwa ndani ukiwa nje ngozi utakauka tu! Tena bila kupaka mafuta kwenye ngozi mtu anajikuta anajikuna kila saa. Wakati mwingine sehemu anajikuna hata sehemu nyeti kama matakoni, mwasho unazidi. Halafu ukicheki mdomo, umekuwa mweupe kama vile katoka kubusu kopo la poda. Ubaya zaidi ukikuna ngozi hiyo utaona kama unatoka unga kwa vila ngozi umekauka.

WaMarekani weusi wanaita hiyo tatizo ‘ashy’. Ukiambiwa ngozi yako ni ‘ashy’ basi ni kama vile umetukanwa. Wataalum wanasema kuwa ngozi nyeusi haupendi baridi. Of course, haupendi baridi asili yetu ni Afrika.

Kumbe watu wangejiepusha na huo balaa kwa kupaka mafuta au lotion mwilini. Lakini wanaume ambao ndo kwanza wameshuka kwenye ndege kutoka Bongo wanasema, “Ah siwezi kupaka mafuta mwilini kama mwanamke!’ Heh! Mteseke eti kwa vile hutaki kufanya mambo ya kike kike. Basi utaendelea kuchekwa kwa vile unaonekana kama umedumbukia kwenye poda.

Lakini nimeona kuwa baada ya kukaa siku kadhaa na udume wake, mwenyewe anaenda kununua hiyo lotion, mafuta, na kuanza kujisikia vizuri. Kwani hakuna haja ya kujikuna kila saa na ngozi unapendeza. Na hata wanawake wanaanza kumsalimia.

Hakuna ubaya kukaa na kopo au stiki ya Lip Moisturizer au tube ya lotion na kujipaka. Kila mtu anafanya hivyo wakati wa baridi, kwa hiyo watu hawakuona kinyago. Watashangaa zaidi kuona unapenda kutoka hadharani ukiwa 'ashy'.

Kumbe kuna mambo ya kike mazuri yanayofaa hata kwa wanaume.