Tuesday, January 16, 2007

Ndoto inaweza kutokea Kweli!
Mimi nimewahi kuota kuwa natuzwa Oscar. Nilivyoamka ilibidi nicheke. Nikasema haiwezekani nituzwe hiyo Oscar, kwanza weusi huwa hawatuzwi, na pili nani atanipa nafasi ya kuigiza kwenye sinema itakayonipa nafasi hiyo.

Lakini jana nimeamini kuwa ndoto huwa inaweza kutokea kweli. Baada ya kuona, Jennifer Hudson, kashinda Golden Globe Award kama Best Supporting Actress. Ijumaa alishinda Critics Choice Awards na sasa watu wanasema anastahili Oscar. Mwaka jana saa hizi nani alitegemea kuwa leo, Jennifer angekuwa Superstar? Ni sinema yake ya kwanza kuigiza, na pia mwaka 2004, alishindwa kwenye mashindano ya American Idol….kama utakumbuka Fantasia Barrino alishinda mwaka ule. Jaji Simon Cowell, alimwambia kuwa hata fika mbali na uimbaji. Kwa kweli nilisikitika sana siku hiyo alivyotolewa kwena AI, maana nilijua Jennifer ana kipaji.

Mungu ni mwema. Akifunga dirisha anafungua mlango. Jennifer kapata nafasi ya kuwa kwenye sinema ya Dreamgirls. Jennifer alichaguliwa kutoka kwenye waigizaji 781 waliofanya audition. Kama hujaiona Dreamgirls nakushauri ukaione. Nilienda kuiona juzi na kwa kweli ni sinema nzuri mno, yaani mno. Sijawahi kuona sinema nzuri kiasi hicho miaka mingi, tena waigizaji wakuu ni weusi. Na waMarekani wametokea kuipenda hiyo sinema. Soundtrack ya sinema ni namba one sasa hivi! Na kila mtu anamsifia Jennifer Hudson na kuigiza na kuimba kwake.

Kwa ufupi, Jennifer anaigiza kama Effie White, ambaye ni mwimbaji mkuu wa Kikundi cha The Dreams. Meneja wa Kikundi (Jamie Foxx) anamshusha na kumweka, Deena Jones, (Beyonce) kuwa mwimbaji mkuu kwa vile ni mzuri wa sura kuliko Effie. Effie anatupwa na kikundi cha chake na anasota na maisha. Sitaki kuwaeleza mengi lakini kuna mapenzi mle. Beyonce naye aliteuliwa kwa ajili ya tuzo ya Best Actress, lakini hakupata.

Eddie Murphy anaigiza kama James ‘Thunder’ Early, ambaye ni mwimbaji mwenye staili ya pekee ya kuimba. Anatokea kupendana na moja wa hao Dreams. Naye alituzwa Golden Globe kama Best Supporting actor. Kama hamkuona show, walivyomtangaza mshindi, alionekana kuwa na mshangao. Sishangai maana alishateuliwa mara kadhaa kwa ajili ya sinema kana The Nutty Professor, na hajashinda hata siku moja. Na huko kwenye Oscars ndo hawajamjua kabisa.

Kwa hiyo ndoto huwa zinatokea kweli. Jennifer Hudson, ametuonyesha kuwa inawezakana.

Tuesday, January 09, 2007

Oprah ajenga shule ya kifahari ya Wasichana Afrika Kusini

Bila shaka mmesikia habari ya Oprah Winfrey kufungua shule ya wasichana huko Afrika Kusini. Shule enyewe inaitwa ‘The Oprah Winfrey Leadership Academy’. Kwa kweli nampongeza kwa kitendo chake cha kukumbuka Afrika na kusaidia wasichana huko. Wanafunzi waliochaguliwa wanatoka kwenye familia zenye kipato cha chini. Na walichaguliwa kutoka kwa maelfu ya wasichana walioomba nafasi ya kuingia huko.

Oprah alijenga shule hiyo kwa gharama ya dola za kimarekani $40 milioni. Kwa sasa ina wanafunzi 145. Bila shaka tutasikia waliosoma hapo watapata mafanikio mazuri kimasomo na kwenda kusoma vyuo vikuu maarufu duniani kama Harvard, Stanford, Cambridge, Oxford etc.

Shule enyewe ni ya kifahari hasa. Hata wanaosoma shule za Ivy League na ma Prep school duniani wanaweza kuwaonea wivu has wasichana. Nikisema ni ya kifahari, nina maana ni ya kifahari hasa. Oprah mwenyewe ni bilionea na kazoea maisha ya kifahari na alitaka hao wasichana wajue ufahari manake nini. Mfano, shule ina saloni kwa ajili ya kutengeneza wasichana nywele, wanalalia mashuka enye nyuzi 200 count (Duh…kama wanalala hoteli ya Waldorf Astoria) sahani zilichaguliwa na Oprah na si ajabu sahani moja ina gharama ya dola mia, ina theatre za ndani na nje, ina ma fireplace tele (Afrika unahitaji fireplace ya nini?) na mengine mengi. Walimu wameletwa kutoka nchi za nje.

Je, wakirudi majumbani mwao kwa ajili ya likizo wataishi namna gani? Si wamezoea ufahari. Si uwongo kuna watu ambao baada ya kukosa maisha ya kifahari waliozoea, walirukwa na akili na wengine kujiua. Natumaini Oprah ana mpango wa kuhakikiisha hao wasichana wanaendelea kuishi maisha ya kifahari wakimaliza masomo yao.

Lakini najiuliza kama hizo pesa katumia vizuri kweli? Nakubali kuwa ni hela yake na anaweza kufanya anachoaka nazo. Lakini jamani hiyo hela ingeweza kusomesha maelfu ya wasichana huko Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla. Kuna faida gani ya mtu kula chakula kwenye sahani enye thamani ya dola mia, wakati huko nyumbani kwake huenda hakuna chakula. Pia watoto wengi Afrika wanashindwa kusoma vizuri shauri ya kukosa mlo wa kutosha. Na kisa cha kulalia shuka enye 200 thread count wakati huko majumbani mwao wanashukuru kuwa na sehemu safi ya kulala. Au wanalala wane kwenye Kitanda kimoja. Kuhusu hiyo saloni si bora wangekuwa wanasukana wenyewe kwa wenyewe, ili wajue sanaa ya kutengeneza nywele.

Samahani lakini navyoona kuna watoto Afrika ambao wangeshukuru kuwa na unifomu na viatu vya kuvaa kwenda shule. Wangeshukuru kuwa na vitabu, na madaftari. Wangeshukuru kama wanakuwa na uhakika wakulipwa ada ya shule, na kuwa na njia ya kufika shule bila bugudha, kama vile school buses. Yaani hiyo dola milioni $40 zingeweza kutumiwa kujenga hata shule kumi bora Afrika na kusaidia wengi zaidi.Hayo ni maoni yangu tu. Wapendwa wasomaji, mnaonaje?

Saturday, January 06, 2007

Hongera Dada Asha Rose Mtengeti-MigiroNachukua nafasi hii kumpongeza Dada Asha Rose Mtengeti-Migiro, kwa kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (United Nations). Kwa kweli ni jambo sisi WaTanzania lazima tujivunie.

Namfahamu Dada Asha Rose, tangu alivyokuwa anasoma UDSM. Mimi wakati huo bado nilikuwa nasoma Secondary School. Kwa kweli huwezi kujua Mungu amempangia mtu nini. Nikikumbuka enzi zile, yaani tusingeweza kutegemea kuwa atakuwa kiongozi anayeheshimika dunia nzima. Alikuwa hana makuu. Lakini miaka ilivyoenda tuliona alivyoonyesha meno kuwa anaweza kuongoza na kuongoza vizuri.

Pia kuteuliwa kwake unaonyesha jinsi Tanzania inavyoheshimika duniani. Hatujawa na migogoro mingi ya kisiasa kama nchi zingine barani Afrika. Na nasikia ilikuwa kila mkutano wa kimataifa akienda anapata washabiki kwa uongozi wake mzuri. Watu wengine wamekuwa wakishangaa alipataje kuteuliwa katika nafasi nzito hivyo. Nawambia ameteuliwa kwa sababu ameonyesha watu wengi Tanzania na nje ya Tanzania kuwa ni mtu mzuri mwenye moyo na kipaji cha uongozi.

Jambo lingine ni kuwa mwanamke kutoka Third World amekababidhiwa uongozi mzito. Lazima Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban Ki-Moon, kamwona Dada Asha Rose ni mwanamke jasiri atakayeweza hiyo kazi.

Dada Asha Rose amekuwa ni mfano mzuri kwa wasichana wote wa Tanzania na Afrika kwa ujumla!

Akina Mama Oyee!

Wednesday, January 03, 2007

Poleni Wafiwa


Kwanza naomba mnisamehe kwa kuongea kuhusu kifo. Najua si jambo la kufurahisha.

Leo nimekwenda kwenda 'Wake' (kilio) ya Mama Anastazia Rupia. Alifariki hapa Boston siku chache kabla ya Krismasi. Alikuwa amekuja kwenye mahafali ya mwanae, Septemba na kwa bahati mbaya alianza kuumwa muda mfupi baada ya hapo.

Kwa kweli waBongo walitokea wengi kuwafariji wenzao waliofiwa na mama yao. Mchungaji mzungu alisoma misa mzuri sana. Watu walikuwa na majonzi hasa mtoto wa marehemu John Rupia, alivyosimulia habari ya maisha ya mama yake na alivyougua. Alivyomaliza naye, John alianza kulia ndo hapo chumba chote tuliishia kulia.

Maiti anawasili Dar Jumamosi na ndege ya SwissAir, naomba muwepokea vyema huko. Poleni.

Lakini jamani ukweli uchungu wa kufiwa unaujua wewe uliyofiwa. Hata tukikupa pole ngapi, marehemu ni marehemu, hatarudi. Watu wataenda zao kwenye shughuli zao na wewe mfiwa utabakia na majonzi yako.

Watu wengi wanajua uchungu wa kufiwa na mtu wa karibu. Nilivyofiwa na mume wangu wa kwanza, mwaka 1995 hata sikumbuki nilifikaje Tanzania. Nilikuwa nasoma hapa Boston, nikapata taarifa, nikakatiwa tiketi na nikashutukiwa niko Dar uwanja wa ndege na wafanyakazi pale walinipa pole na kuniuliza kama nina mtu wa kunipokea. Ile safari yaani ilikuwa kama vile ndoto mbaya na niseme miezi kadhaa baada ya kufiwa si kuwa mzima maana nilijisikia kama sijui niko wapi. Wakati mwingine nilikuwa najiona kama niko kwenye wingu, mara naona mwili mzito kutembea shida. Mungu alinisaidia kipindi kile. Amini usiamini, miaka zaidi ya kumi imepita na bado nina omboleza ila siku hadi siku uchungu unapungua. Unapungua lakini haushi kabisa.

Lakini sisi tuliyobaki inabidi tuendelee kuishi na kujenga maisha yetu na kusimulia kwa wanaetu kuhusu ndugu zao waliowatangulia hapa dunia.

Kwa kila mtu aliyefiwa na ndugu au rafiki yake nasema, pole. Poleni wafiwa wote popote mlipo, na Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu. AMEN.