Thursday, August 24, 2006

Kajambanani?

Kila siku asubuhi nikiamka nafungua TV kuangalia taarifa ya habari kwenye Fox 25. Kuna mzungu mwanaume mnene ndo anchor wa Beacon Hill studio (Dowtown Boston) na anapendwa na wengi, anaitwa VB. Na huko kwneye studio yao Dedham kunakuwa na akina Dada Anquenette (mweusi), Gene Levanchy na Kim Carrigan. Leo nikafungua na nikasikia sauti ya ajabu. VB kajamba tena kwa sauti. Nikajiuliza kama VB kaweka microphone matakoni kusudi tumsikie. Nikasema sijui kala nini jioni yake. Kwanza nikamwonea huruma maana najua hawezi kuamka kukimbia chooni mpaka break ikaja. Bora yuko nje maana studio utajaa harufu ya mishuzi. Basi kila baada ya sekunde chache anaachia. Nikasema huyo mzungu kala maharagwe na hajayazoea nini! Cha kushangaza kawa anaongea bila kujali kitu.

Kukaa kidogo huko kwenye studio kuu, anchor Gene Levanchy naye kajamba. Kim Carrigan kamtazama kwa dharau kubwa na kushika pua lake. Gene na VB wakamwuliza kama yeye hajambi na kawa kama kasirika kuuliza hivyo. Kim kajifanya hayumo kwenye mambo ya kujamba. Basi kwenye break aliamka kwenye kiti halafu tukasikia mjambo pwaaaach. Tukasikia kila mtu studio anacheka. Kumbe wenzake walimwekea ‘Whoopee cushion’ (Kimpira kinachotoa mlio kama mtu kajamba). Ukikalia inatoa mlio kama vila mtu kajamba. Kima katoka haraka uso mwekendu!

Basi ndo VB kaelezea kisa cha yeye kuwa anajamba jamba. Kumbe kwenye magazeti waliandika habari ya intern huko White House kusema kuwa rais Bush anapenda kujamba ofisini. Heh! Rais mzima anjamba! Tena mbele za watu. Lakini kwa nini watu washangae, ni bindamu na vayakula anavyopenda ni vya kiMexico ma nacho, refried beans, na maburrito na bia. Lazima zitafanya tumbo ijae gesi. Sijui kama yuko na Rais mgeni kutoka nchi nyingine anaachia mishuzi. Tumekwisha jua kuwa anapataga ashki.

Haya sasa fikiria uko kwenye basi au subway (treni). Watu wanajamba huko hasa kama umejaa, tena vile vya kimya kimya vya kuniuka hasa! Bora hizo zenye milio mikubwa. Cha kuchekesha mtu anabanwa gesi, anaachia kimya kimya inanuka halafu watu wanalalamika na huyo aliyetoa analamika. Huwezi kujua nani kajamba.

Wazungu wengine hawana haya, wanajamba, halafu wanasema, “Oh Excuse me” Utajibu kweli? Kama unamjua labda utasema, “You’re excused”. Wamarekeni weui wana usemi, “You smelt it, you dealt it!” (Umesikia ushuzi hivyo wewe ndo umejamba), Ukiwa na weusi ni bora kunyamaza na ubane pua.

Na hapa Marekani watu wanatajirika kwa kuuza vidonge vya kuzuia watu kujamba. Phazyme, Beano, Papaya pills, vina soko kubwa.

Kabla sijamaliza lazima nikumbuke Bongo na usafiri wa treni Third Class Bongo (Central Line). Watu walikuwa wanabanana safari ndefu, watu wana jamba jamba, na huwezi kuwalaumu maana choo hakuingiliki na inabidi usubiri mpaka treni isimame kwenye kituo halafu ushuke haraka na kujisaidia pembeni. Basi Thedi ikapewa jina, KAJAMBANANI! Unasafiri daraja gani, Nasafiri, KAJAMBANANI bwana hela sina ya First!

Lakini baada ya maajabu niliyoona leo nangojea kusikia kama kutakuwa na Official Fart Day! Siku ya kujamba. Kumbe kujamba ni sifa, wazungu bwana!

Wednesday, August 23, 2006

Kusogoa Chooni


Jamani Marekani watu maofisini wananishangaza sana. Kuna mtindo wa watu kusogoa na kupiga gumzo chooni. Tena kwa muda mrefu.

Yaani mtu anajisaidia, huko mwenzake yuko nje anamsemesha. Au unaingia chooni na kukuta watu wamepiga kambi kwenye masinki ya kunawia mikono na kupiga soga, huko watu wanajisadia kwenye stalls. Wanasikia mtu anakojoa, hao wanaongea bila kujali. Kwa kweli nashangaa sana. Labda mtu akiwa anajisaidia haja kubwa ndo wakimbie kwa ajili ya mishuzi.

Kwa kweli Restrooms/Bathrooms za Marekani maofisini ni safi sana, yaani unakuta toilet bowl cheupe kama vile bado kipya. Zinasafishwa mara kwa mara kwa siku. Nakumbuka Mbongo fulani aliwahi kusema vyoo vingine visafi mpaka unaweza kula huko, (mhhh sijui, mimi siwezi kula huko)! Usafi chooni ni muhimu sana hapa, na hao wanaosafisha wakizembea wanashutukia kazi hawana wanaletwa wengine. Lakini bado sijaona kama chooni ni sehemu ya kupiga gumzo.

Unaingia kwenye stall (kichumba chenye choo), mwenzako yuko nje kaona unaingia anaanza kupiga mastori. Aisei umesikia, hivi na hivi, je, unaonaje hivi na vile. Kwa kweli naona mkojo unataka kwa shida huko unajisaidia, huko unajaribu kuongea.

Lakini kuna kitu niligundua. Kisheria Marekani, mwajiri anarushisiwa kuweka recording devices kila mahala ofisini na Mfanyakazi asijue. Wanaweza kuwa na makamera na ma-audio device na usijue. Ila ni mwiko kuweka hizo devices chooni! Je, ni sababu ya watu kupiga gumzo chooni kwa vile wanajua hawawezi kunaswa kwa ajili ya kupoteza muda kazini.

Mnaonaje kuhusu suala hii?

Monday, August 21, 2006

Idi Amin Hajambo?Sisi waTanzania hatutasahau ushenzi wa aliyekuwa Dikteta wa Uganda marehemu Idi Amin Dada. Lazima yuko motoni kwa mauaji aliyofanya akiwa kiongozi wa nchi hiyo. Lakini alivamia nchi yetu Tanzania na kusema eti Kagera ni sehemu ya Uganda. Ndipo Mwalimu Nyerere kaja juu na kutuma Jeshi la Wananchi na Mgambo kumtoa nduli Idi Amin! Na hatutasahau ile miezi kumi na nane ya shida baada ya hapo ambayo karibu iwe miaka kumi na nane ya shida. Enzi za kukosa sabuni, sukari, na vyakula na bidhaa mbali mbali madukani na sokoni! Lakini asante Nyerere huyo kichaa kafukuzwa Uganda maana maiti zilikuwa zinajaa Ziwa Victoria mpaka watu walikataa kula samaki kutoka pale!

Leo nimepata habari kuwa kuna sinema itatoka mwezi ujao (Septemba) kuhusu Dikteta Idi Amin wa Uganda. Sinema hiyo inaitwa, ‘The Last King of Scotland’.

Sinema ilipigwa Uganda na mcheza sinema maarufu hapa Marekani, Forrest Whittaker, ndiye anaigiza kama Idi Amin. Mcheza sinema mrembo, Kerry Washington anaigiza kama mmoja wa wake za Amin. Sinema hiyo inasubiriwa kwa hamu na wengi na tayari wanazungumzia habari za ma Oscar kwa ajili ya Forrest Whittaker na Kerry Washington.

Uzuri sinema ilipigwa Uganda kwa ruksa ya Rais Yoweri Museveni. Alitoa msamaha ya kodi mbali mbali kwa ajili ya watengeneza sinema waliokuwa na bajeti ndogo ya kutengeneza hiyo filamu. La sivyo wasingweza kuitengeneza. Alikubali kuwa hatimaye sinema hiyo inaweza kusaidia kuongeza utalii Uganda.

‘The Last King of Sctoland’ inatoka tarehe 26 Septemba. Kwa habari zaidi someni hapa.

Bonyeza hapa kuona Trailer ya sinema: THE LAST KING OF SCOTLAND

Monday, August 14, 2006

Kitabu kuhusu Utengenezaji wa filamu Maangamizi


Bi Queenae Mulvihill ametoa kitabu kuhusu sinema Maangamizi the Ancient One. Hiyo sinema ilipigwa Bagamoyo, Kilimanjaro na Morogoro kati ya 1994 na 1997. Mimi niliigiza kwenye hiyo sinema kama Nurse Malika. Sinema hiyo ilikuwa ni ya kwanza kutoka Tanzania kuwa katika mashindano ya Academy Awards Hollywood yaani Oscars.

Kwa kweli kuna mengi yalitokea na yalitendeka. Kulikuwa na majonzi mengi, ukosefu wa fedha, ugomzi, hasira, vifo, ahadi za uongo, wizi na mengine. Pia hao akina Mulvihill bado wanadaiwa karibu $150,000 kutokana na hiyo sinema. Lakini sinema ilitoka. Jamani kutengeza sinema siyo rahisi. Kinahitaji utaalamu, uvumilivu na pesa!

Kitabu kinaitwa 'Warriors: Spritually engaged - The Making of Maangamizi the Ancient One.'

Linki ya kitabu ni hii....

http://calendars.lulu.com/content/265217

Kitabu kina ukurasa 379. Siku nyingi sijasoma kitabu kizuri lakini wikiendi hii niliacha kila kitu na kukisoma. Kilikuwa kizuri na sijui nilipenda kwa vile nafahamu watu wengi waliotajwa mle, au vipi, lakini ni kizuri. Dada Queenae ana kipaji cha kuandika and amedika kutoka moyoni na anaongea kwa uwazi na bila aibu. Mambo yaliyoomo ni karibu kuvunjika kwa ndoa yake na mapenzi. Moyo wangu ulijaa huzuni, majonzi na raha nilivyosoma.

TWO THUMBS UP!

Kwa habari zaidi kuhusu sinema ya Maangamizi bonyeza hapa...

http://www.grisgrisfilms.com/

Wednesday, August 09, 2006

Meli ya M.V. LiembaKuna sinema ambayo itatoka hivi karibuni kuhusu meli ya MV Liemba. Hiyo meli iko Ziwa Tanganyika. Nilishangaa sana kusikia kuwa baada ya miaka yote hii bado inafanya kazi. Yaani imefanya kazi karibu miaka 100!

Kumbe ndo meli iliyotumika kwenye sinema ya The African Queen. Kwa hiyo wacheza sinema wa enzi zile Humphrey Bogart na Katherine Hepburn walipanda.

Kwa habari zaidi someni hapa:

http://www.liemba.org/

Mimi sijawahi kufika Ziwa Tanganyika. Kama umewahi kusafiri na hiyo meli tupeni story basi.

Thursday, August 03, 2006

Wapenzi na Wivu

Mara nyingi tunasikia habari ya mtu kumpiga mpenzi wake kwa ajili ya wivu. Mwanamke kasalimiwa na mwanaume mwingine, kibao! Mwanamke anapiga simu nyumbani kumwulizia mume wa mtu, mke anampiga na sufuria na mengine. Lakini wakati mwingine wivu unazidi mpaka watu wanafanya maajabu.

Nimesikitika sana kusikia habari ya jamaa kujinyonga Gesti huko Tandika eti kwa vile mpenzi wake wa miaka 19 alikuwa na wapenzi wengi. Kitu gani kilimwingia marehemu Said Libonge mpaka kaamua kumchoma mpenzi wake kisu na yeye mwenyewe kujinyonga. Ni wivu au ugonjwa wa akili?

Mimi sikuwepo bali nimesoma tu hiyo habari ya kusikitisha. (Soma Hapa) Na huyo dada lazima atajiuliza mara mbili tatu kabla ya kuingia gesti na mwanaume au kuwa na mpenzi mwingine.

Lakini nikikumbuka vituko wanavyofanya wapenzi kwa jina la wivu, nasikitika na nacheka. Haya tuchukue kesi ya mama fulani aliyemkuta mume wake yuko kwenye shughuli ndani ya gari eneo ya Mbuyuni Dar es Salaam miaka ya tisini. Yule mama alidai kuwa alifungua mlango wa gari kamkuta mume wake yuko juu ya howara wake anapampu na alidai kuwa mambo yao yalikolea kiasi kuwa alikuwa anampiga mume wake aliyekuwa ameshusha suruali matakoni na hakusikia kitu. Kwanza mtu wa kawaida angebakia anashangaa mdomo wazi, au angekimbia kwa aibu. Lakini hapa huyo mama na wivu zake kaweza kufungua mlango wa gari na kuanza kumpiga mtu shughulini.

Haya nakumbuka kisa cha mama mwingine miaka ya themanini. Mume wake alienda na howara wake kwenye gesti Manzese. Yule mama alijua yuko chumba gani. Kitanda kilikuwa chini ya dirisha. Basi yule mama alikesha pale kwenye dirisha na walipoanza mambo yao, yule mama kafungua dirisha na kuwamwagia chupa ya tindi kali. Kwa vile walikuwa uchi wote waliungua vibaya! Wivu jamani!

Nilivyokuwa nasoma Tabora Girls kuna dada fulani aliuliwa na mume wake. Sitamsahau yule dada. Alikuwa anakaa National Housing na mume wake, ndoa yao bado changa. Dada mwenyewe alikuwa mzuri kweli kweli. Mume wake alikuwa ni mwanajeshi mwenye cheo cha Kepiteni. Alikuwa mwembamba mwenye kipara. Kuna wenzangu walimuwa wanamvizia yule baba. Basi kuna siku yule baba alishikwa na wivu, kamfunga kamba mke wake na kumtia matambara mdomoni mwake kusudi asiweze kupiga kelele. Wanasema kuwa yule baba alimpiga raundi ya kwanza, kampiga raundi ya pili, kampiga raundi ya tatu mpaka yule dada kafa. Eti kapusuliwa bandama! Kisa cha kumpiga mke wake mpaka kafa kilikuwa eti alimwona anaongea na mwanume mwingine. Yule baba alihukumiwa kifo.

Niendelee? Kuna visa vingi, vya watu kuua au kuumiza wapenzi wao kwa jina la wivu.

Mimi mwenyewe nimeshikwa na wivu mara kadhaa lakini siyo kiasi cha kuua au kumwumiza mtu! Niwasimulimie kisa kimoja. Kuna jamaa nilikuwa nampenda sana. Lakini yeye hakunijali wala nini zaidi ya kusalimiana. Basi kuna siku nilimwona anakwenda kwenye deti mjini DSM na dada fulani! DUH! Nilijikuta naona kizunguzungu, Siwezi kusema, hasira zimejaa na nikaanza kulia! Watu waliniuliza nalia nini, nikashindwa kusema! Baadaye nikasema basi Mungu hakupanga niwe naye. Yaani nikikumbuka nacheka.

Mnasemaje kuhusu wapenzi na wivu?