Thursday, March 30, 2006

Mandisa aka Mandiva

Kama mnaangalia mashindano ya American Idol, mtaona mwaka huu kuwa kuna dada fulani anaitwa Mandisa. Huyo Mandisa ana miaka 29, ni Mmarekani Mweusi na pia ni kibonge cha dada. Pia ana matako makubwa kweli kweli.

Kwa kweli waMarekani hawapendi kuona watu wanene kwenye TV, na hasa wenye matako makubwa, lakini huyo dada amebarikiwa na sauti nzuri sana. Ana kipaji cha kuimba. Ningependa kuona anashinda na kuwa American Idol wa Season 5, lakini sidhani kama WaMarekani watampa nafasi hiyo.

Kwa msiofahamu, American Idol ni mchezo wa kuchagua mwimbaji mzuri. Mshindi anapata ‘contract’ ya kutengeza santuri, dola millioni moja, gari, na zawadi zingine tele.
Maelefu ya watu kati ya miaka 16 hadi 28, wanajaa kwenye auditions, wakiwa na ndoto ya kuchaguliwa kushiriki kwenye show. Majaji wanapita miji mingi USA wakitafuta washiriki. Halafu watu wanapunguzwa na majaji mpaka kufikia watu 24. Wakifika hapo ndo watazamaji wanapewa nafasi ya kumpigia kura mtu ambaye wanadhania anastahili kashinda.

Basi huyo Mandisa, alipoaudition mara ya kwanza mbele ya majaji na kupita kuendelea Hollywood, Simon Cowell alisema, “We’re going to need a Bigger Stage this year” Yaani watahitaji jukwaa kubwa zaidi kwa ajili ya huyo Mandisa.

Maskini Mandisa wa watu hakujua huyo Simon kasema nini, basi ikaonyeshwa kwenye National TV na dada wa watu alilia. Anasema alikuwa anatazama na marafiki zake na kwa kweli aliona kama kashfa. Baadaye baada ya kupita kuendelea akamwambia Simon kuwa amemsamehe na hata Simon mwenyewe alionekana kuwa na haya kwa alichosema.

Nimekuwa nikisikiliza redio na kusoma kwenye magazeti na Talk Shows. Anapendwa lakini watu wanasema hata pita kwa vile ni mnene. Basi kuna mzungu moja alisema eti paja moja la Mandisa ni kikubwa kuliko kiuno cha dada wa kizungu, Melissa ambaye alishatolewa wiki kadhaa ziizopita. Mara waseme hayo matako, maana wazungu hawapendi kabisa matako makubwa. Na bila kujali maneno ya watu kila wiki Dada Mandisa anatoa wimbo kali. Anaimba hasa, mpaka sauti yake inakuingia. Anapanda kwenye jukwaa anapendeza na anajiamini!

Kuona watu bado wanampenda na unene wake wengine wakamkashifu kwa kuimba wimbo wa dini wiki hii. Kwanza hiyo ‘Christian’ ni genre ya muziki kama Jazz , R& B na Classical. Wazoee! Na mbona yule mzungu Carrie Underwood ambaye alishinda mwaka jana alivyoimba wimbo wa dini kwenye show hawakusema kitu!

Kwa kweli roho inaniuma, nikifikiria kuwa huyo dada hatafika katika TOP 3 ya hayo mashindano kwa sababu ya unene. Mshindi wa zamani, Ruben Studdard alikuwa Mnene karibu paundi 400, naye alikuwa na sauti tamu kweli kama Luther Vandross. Watu wanasema, ilikuwa ‘okay’ kwa Ruben kushinda na unene wake kwa sababu ni mwanaume. Lakini eti Mandisa hawezi kupita kwa vile ni mnene na ni mwanamke. Duh, hata kwenye unene hakuna usawa.

Kama mnaangalia American Idol nawaomba umpigie kura huyo dada Mandisa.. Sauti anayo tena nzuri kuliko akina dada wote kwenye show. Matako Makubwa na unene yasiye sababu ya kukosa U-American Idol.

Na natabiri asiposhinda atakuwa Star kama akina Mo’Nique. Tutamwona kwenye commercials na sinema na concerts maana. American Idol ndo mwanzo wa kujlikana kwake.

Na baadaye nitaongea juu ya siasa za American Idol.

Kwa habari zaidi za America Idol nenda http://www.americanidol.com

Tuesday, March 28, 2006

Ulafi wa Bia Haipendezi Marekani

Ulafi wa Bia Haipendezi Marekani!

Hivi majuzi nilienda kwenye ‘Party’ ya waBongo hapa Boston. Party ilifanyika kwenye basement ya nyumba. Na kama kawaida waBongo walijaa. Na kama kawaida chakula kilikuwa kingi na vinywaji tele. Kwa ‘Party’ waBongo ndo wenyewe maana wanachanga bia na chakula bia shida. Huyo anakuja na kesi ya bia, yule anakuja na kesi, yule anakuja na tray ya mapochopocho, mambo swafi kabisa!

Basi kuna MBongo kashuka kwenye ndege juzi juzi, alikuwa kalala kwenye Lawn Chair ndefu anastarehe huko akipunga upepo wa USA. Jamaa kalala kwenye hiyo lawn chair tena bila wasiwasi wowote, huko anaongea na watu. Nikamcheki, jamaa kalegea kabisa na kikofia kichwani anakula maisha ya USA. Basi chini ya hiyo Lawn Chair alikusanya kama chupa kumi za Heineken.

Nikasogea kwa huyo jamaa kumcheki, kama ni mzima au taira au nini, au labda mtu hajiwezi, ndo maana kalala hivyo. Kuongea na jamaa nikakukuta ni mzima kabisa. Basi nikamwuliza sababu ya kulundika mabia chini ya kiti wakati ziko tele jikoni. Na nikamwuliza kama hapendi bia baridi maana kuziweka chini ya kiti zinapata joto. Nikamwambia jamaa kuwa ni mshamba na anajiaibisha. Jamaa kabisha kasema yeye ana bia tele chini ya kiti atakuwaje mshamba na hawezi kujiaibisha. Hakuwa na habari kabisa kuwa wageni waliokuwepo walikuwa wanamsema chini chini. Lakini jamaa hakujali maana kajiona kafika! Tena kafika USA.

Nadhani watu wangemwona kafika kama hizo bia kununua yeye, na hiyo nyumba ilikuwa yake.

Kwa kweli tabia zingine za Bongo tunaweza kuziacha Bongo. Maana nakumbuka kwenda kwenye shughuli mbalimbali Bongo, na kuona watu wanakusanya bia chini ya kiti. Hiyo kukusanya bia chini ya kiti watu walikuwa wanafanya wakidhania bia zitaisha. At least walikuwa na akiba na rafiki akija wana kitu cha kumpa. Halafu ilikuwa ni sifa kuonyesha kuwa una hela ya kununua bia zote hizo.

Lakini hapa USA bia ziko tele! Kila mahala kuna liquor store na kuna bia tele. Hela yako tu. Na kwenye party za waBongo hata siku moja sijawahi kusikia bia zimeisha, au zikiisha basi watu wanaenda kununua zingine.

Jamani eh, tabisa zingine zinafaa ziachwe huko Bongo. Mnasemaje?

Friday, March 24, 2006

Nilikuwa 'Busy' Kidogo

Habari zenu wasomaji wapendwa. Kwanza naomba mnisamehe kwa kutokubandika posti mpya hapa siku nyingi. Nilikuwa busy kidogo, na mambo ya uigizaji (acting). Kuna kujitayarisha kwa ajaili ya auditions, na mengine.

Wiki hii nilienda New York City kwa ajili ya Casting Call ya Mo'nique's Fat Chance.
Mnaweza kusoma Blog yangu hapa lakini ni kimombo. Nilikuwa najiona kibonge kumbe hamna kitu, pale nilionekana mwembamba! Nilirudi zangu Boston bila hata kufika raundi ya pili.

http://chemiche.blogspot.com/2006/03/my-experience-at-fat-chance-casting.html


Pia najiandaa kwa ajili ya auditions za sinema kadhaa zitakazo kuwa filmed hapa Massachusetts wakati wa summer. Auditions zina kazi jamani na ni lazima kila mara kufanya mazoezi ya monologues.

Wapendwa Wasomaji, asanteni kwa uvumilivu wenu na naahidi mapya yanakuja!