Saturday, December 31, 2005

Heri ya Mwaka Mpya!

Wapenzi wasomaji, nawatakia heri ya mwaka mpya. Naomba mwaka 2006 iwe wa amani na upendo na majalio tele kwa wote.

HERI YA MWAKA MPYA!

Wednesday, December 21, 2005

OmbaOmba

OmbaOmba


Hapa Boston kuna ombaomba kibao! Tena wengi ni wazungu. Hao ombaomba wengi wao ni walevi na watumia madawa y kulevya na wenye ugonjwa wa akili. Miaka nenda, miaka rudi, ombaomba ni hao hao!

Unapita njiani, unasikia “Spare Change”! Utaona mtu kasimama na kikombe chake anakitikisa. Kuna wengine usipowapa kitu wanakutukana matusi ya nguoni. Halafu kuna wale wakali wanakufuata mpaka ndani ya ATM. Basi watu kwa uoga wanatoa walichonacho na kuwapa kwa kuhofiwa kupigwa au kuibiwa.

Haya, lakini ni lazima niongelee kitu ambacho nimeona, na labda wengine hapa USA mmeona. Kuna ubaguzi katika kile watu wanachotoa kwa ombaomba. Tuseme mtoaji ni mzungu, na ombaomba ni mweusi, basi kama atampa kitu anampa vichenji. Huyo huyo mzungu atatoa noti kwa ombaomba mzungu. Nimeshuhudia mara nyingi tu. Nimeona ombaomba wa kizungu wakipewa noti za $1, $5, $10 na hata $20! Lakini mweusi atapewa vichenji, kwa nini? Je, ni kwa vile mzungu anajisikia vibaya kuona mzungu mwenzake katika hali hiyo, hivyo ni jitihada ya kumwinua? Je, ni kwa vile anaona kuwa mweusi ni hali ya kawaida kuwa maskini? Sijui kama tutaelewa sababu.

Halafu utaona weusi wako tayari kutoa kwa yeyote. Atampa mzungu, atampa mweusi lakini mara nyingi nimeona weusi wakisaidia weusi wenzao kuliko mzungu. Kisa, anajua kuwa yule mzungu anaweza kuishi maisha mazuri akitaka maana Marekani maana bado kuna ubaguzi Marekani.

Lakini nisiseme kuwa wazungu wote ni wabaguzi, maana mwaka juzi kuna ombaomba Cambridge, anaitwa Ramsey, alikuwa amesimima pale Memorial Drive. Basi Mzungu jike tajiri kapita ndani ya gari yake ya fahari na kampa noti ya $100. Ndiyo kampa dola mia moja! Halafu mzungu kamwambia Merry Christmas, maana ilikuwa Christmas Eve. Lakini jambo kama hiyo kutokea ni bahati nasibu.

Utaona wazungu wana jaribu kusaidia wazungu wenzao kupata public housing na huduma zingine. Lakini mweusi anaweza kupitwa. Kuna magari ya kuwasaidia zinapita mitaani, lakini hebu cheki, hao ‘volunteers’ wataenda kwa wazungu kwanza halafu mweusi ataambulia kilichobaki.

Ajabu na si kitu cha kushangaza sana ni kuwa hao ombaomba wa kizungu wakienda kuoga, ku-shave, kuchana nywele na kuvaa vizuri, anaweza kupata kazi kabla ya wewe mweusi na digrii zako!

Na kama hamniamini ukipita barbarani tazama mwenyewe. Ngoja niishie kwa leo, na kwa maksudi sijaongelea habari ya welfare, na shelters maana hii blogu ingekuwa ndefu mno!

Monday, December 12, 2005

Asante Civil Rights Movement!

Bibi Rosa Parks amefariki dunia jana 10/24/05 akiwa na umri wa miaka 92. Kwa kweli aliishi mpaka uzeeni kabisa, lakini alifanya mengi na alibarikiwa kuona matunda ya matendo yake.

Siku ya Desemba mosi, 1955, Bi Parks akiwa kwenye basi akielekea kurudi nyumbani alikataa kusimama kumpisha baba wa kizungu. Alikuwa amechoka baada ya kazi ngumu. Kwa nini ampishe mzungu tena mwanaume? Kumbuka, enzi hizo weusi Marekani hawakuwa na haki sawa na wazungu. Weusi Marekani walikuwa watumwa, na baada ya kupata uhuru wao 1864 walikuwa bado wanaishi katika nchi ya kibaguzi!

Kabla ya Civil Rights movement kafanikiwa, weusi walisoma shule duni, na kuishi sehemu zilizotengwa na wazungu. Ulikuwa huwezi kukaa na wazungu hata kama ulikuwa na pesa. Kazi walizokuwa wanafanya zilikuwa za kuhudumia wazungu, yaani maklina, mesenja, kubeba mizigo, kuzoa takataka. Walikuwa hawawezi kupata kazi ya maana shauri ya ubaguzi, hata kama angekuwa amesoma kiasi gani! Kulikuwa na mabomba ya maji ya kunywa, mzungu alikuwa na bomba safi na mweusi labda alikuwa na kabomba na maji yanatoka ovyo ovyo na iko sehemu chafu! Au unaenda restaurant kula lakini unawekewa meza jikoni au karibu na choo! Au unaambiwa uchukue chakula mlango wa nyuma! Vyoo (restrooms) vilitengwa kwa ajili ya wazungu na weusi. Weusi waliokuwa hawezi kuingilia mlango wa mbele ya majumba, ilikuwa lazima wapitie mlango wa nyuma. Walikuwa hawawezi kukaa hoteli za wazungu. Na mara nyingi ilikuwa kama wewe mweusi unasafiri unalala ndani ya gari au nyumbani kwa mweusi mwenzio. Enzi hizo weusi walikuwa wanasaidiana sana shauri ya huo ubaguzi.

Fikiria unaenda Airport halafu unaambiwa kwa vile mweusi ukalie sehemu duni. Yaani sehemu enyewe ina viti vya mbao, baridi na mavumbi, halafu unaona sehemu ya ‘White Only’ wamewekewa masofa mazuri kabisa, halafu pamepambwa vizuri. Au unasafiri, halafu wazungu wanaenda kwenye vyoo vya kisasa vya ku-flush, weusi mnaambiwa muende kutumia choo cha shimo! Ndivyo hali ilivyokuwa. Shule za weusi zilikuwa duni pia. Walikosa vitabu vya kutosha halafu majengo mabovu! Yaani! Na ilikuwa ukisema kitu, basi unaweza kuuwawa!

Unaweza kusema hali ya weusi Marekani ilikuwa ni sawa na apartheid ya Afrika Kusini. Lakini ilikuwa ni tofauti maana katiba ya Marekani inasema kuwa watu wote ni sawa. Eti “All Men Are Created Equal” Walikuwa sawa kwenye karatasi tu! Fikiria, ukienda kwenye historic archives, unakuta weusi waliorodhewa kama mali, sawa na wanyama, na! Wazungu hawakutuona sisi weusi kama binadamu, na eti ukimpiga mweusi hasikii maumivu! Loh!

Kweli WaMarekani weusi wametoka mbali toka enzi za Utumwa na Civil Rights. Waliopigania Civil Rights ni wengi, tusisahau akina Dr. Martin Luther King, Jr., Malcolm X, Frederick Douglas, W.B. DuBois, Medgar Evers, yaani watu wengi tu! Na watu walikufa wengi pia majina yao hatuyajui, na wamesahaulika.

Lakini ni lazima tushukuru, hao waliotangulia na kufanya weusi leo wawe na haki Marekani. Kutokana na juhudi zao na damu iliyomwagwa, si weusi tu, bali watu kutoka nchi mbalimbali na rangi mbalimbali wanaweza kuishi vizuri Marekani na kula matunda ya Civil Rights movement. Marekani sasa kweli wanaweza kusema, “All Men Are Created Equal”.

Saturday, December 03, 2005

Wapenzi wa Matako Makubwa

Wapenzi wasomaji, leo nimeamua kuzungumzia suala ya matako makubwa. Tafadhali msione kama ni matusi lakini hapa USA ni issue kubwa, maana watu wanayachukia! Nimeona nizungumzie suala ya matako makubwa kwa vile jana kazini, mzungu aliyekondeana mno kasema ni mnene na akila keki eti yote itaenda matakoni. Nilishangaa na kusikitika sana.

Uzuri kwa wazungu ni kuwa na matako fleti kama vile yamepigwa pasi. Sijui kwa nini. Mtu anashepu ya mbao, mwanamke hana hips kakaa kama dume vile eti ndo uzuri. Kumbe ni kwa sababu hao models na wacheza sinema wako hivyo! Basi wasichana ana akina mama wanajinyima chakula kusudi wakonde na eti wapendeze. Ndo maana magonjwa kama Bulimia na Anorexia zimeshamiri hapa. Lakini ukitazama sinema za miaka ya nyuma kama za 1930's na 1940's, wanawake walikuwa na shepu na walikuwa wamejaa na hata wanaume wa kizungu walikuwa wanasifia. Mpaka 1950's kulikuwa na mcheza sinema Marilyn Monroe, alikuwa na zinga la figure 8, na wanaume wote walikuwa wanampapatikia. Ama kweli mambo yanabadilika. Hivi sasa wanasema eti walikuwa ni obese yaani wanene!

Mbona mimi naona matako fleti kama chapati ni mabaya na hayapendezi? Au ni kwa sababu nimekulia Africa? Brothas (waMarekani Weusi) wanapenda mwanamke awe na matako ya maana! Akipita mwanamke mwenye mbarikio utasikia brothas wakisifia, "umm, umm umm!" Kuna siku nilisikia wanaume wa kizungu wakijadili sababu ya wanaume weusi kupenda matako makubwa, walisema ni "cultural thing". Kwa kweli ni culture yaani utamaduni! Kama umekulia katika mazingara ya kupenda kitu utakipenda. Na ndo maana kuna weusi USA wanataka kuwa na shepu iliyokondeana kama mzungu kumbe haiko katika 'genes' zake. Wajitahidi kupunguza mzigo lakini wapi, iko pale pale.

Sisi wanawake wenye asili ya Afrika tumebarikiwa huko nyuma. Yaani boxi, siha, wowowo, booty, na nasikia waGhana wanaita yokohama, matako makubwa yana majina mengi. Waafrika tunaona kama ni urembo, lakini wazungu na waliokulia uzunguni wanaona kinyaa. Wanasema eti ni dalili ya ulafi na uvivu! Lakini kama ni dalili ya ulafi mbona hata mwanamke mwembamba mwafrika anaweza kuwa na kamzigo huko nyuma? Ubaya mwenye matako makubwa anaweza kubaguliwa kwa vile bosi anaweza kuona kuwa ni 'ugly' na mwenye nacho anachafua mazingira ya ofisi. Kweli kabisa!

Hayo matako makubwa ni 'genes' za sisi waafrika. Lakini ajabu kuna siku nilisikia wazungu wakisema eti waafrika tuna matako makubwa kwa sababu ya utumwa. Eti mabibi zetu walinyimwa chakula hivyo matako ndo ilikuwa godown ya mafuta ya akiba. Nadhani ni uzushi kama ile ya ngamia kuweka maji kwenye nundu zake!

Mimi mara nyingi nimeambiwa nina matako makubwa, niyapunguze kwa kwenda gym kufanya mazoezi. Hayo mazoezi haisadii kitu ni makubwa vile vile! Lakini msione kama naona haya, wala! Mtu akiniambia nina matako makubwa namwambia mbona kama ni madogo, na ningependa yawe makubwa zaidi! Wanabakia kushangaa hasa nikiwaambia kuwa Afrika, matako makubwa ni uzuri.

Na amini usiamini kuna opresheni ya kuyapunguza inaitwa Liposuction. Wanawake wengi weusi na wazungu wamefanya hiyo liposuction ya matako, akiwemo mwimbaji Janet Jackson. Ubaya, ni kuwa ukishafanya hiyo liposuction, mafuta yataenda kwingine mwilini, hivyo utakuwa na shepu ya ajabu!

Sisi waafrika tunapenda kuringia huo mbarikio wa matako makubwa. Nilipokuwa nacheza ngoma shuleni na jeshini, tulikuwa tunatia nguo ndani ya bukta kusudi tuonekana na matako makubwa kweli kweli! Lakini, mara nyingi mitaani hapa USA, nimesikia akina dada wakifokewa, "You got a big a-s!" Kuna siku nilikuwa kwenye kituo cha Subway hapa Boston, kapita mama fualni Mganda, aisei alikuwa amejaliwa kweli huko nyuma, mpaka nikaona wivu. Basi ungeona wazungu walivyokuwa wanamtazama kwa mshangao ungecheka. Ila nilishuhudia baba fulani Mmarekani Mweusi akimtazama kwa furaha na kawa kama vile anamezea mate.

Nampenda sana mecheza sinema, Whoopi Goldberg. Nilikuwa nasoma jinsi akienda kwenye audition au akiwa kwenye movie shoot, wazungu wanamwambia kuwa ana matako makubwa au avae nguo ya kuzificha. Yeye alichoka, na mwishowe kusema, " Mimi ni mwanamke mweusi, nina matako makubwa niache kama nilivyo!" Wanawake wote tungedai heshima kama Whoopi nashani wazungu wangeheshimu matako yetu makubwa.

Tatizo linigine la kuwa na matako makubwa USA ni kupata nguo. Ukienda kununua sketi au gauni uanweza kukuta mbele refu nyuma umepanda. Au unavaa hiyo nguo lakini kwenye hips na matako haipiti! Hii ni kwa sababu nguo imeshonwa kwa ajili ya wazungu wenye matako fleti. Na kupata Jeans inayofiti ni vigumu. Mtu ambaye atatengeneza nguo 'molded for the black woman' atapata wateja kweli kweli, maana tunalilia nguo kama hizo.

Pamoja na yote haya sasa wazungu wameibuka na staili ya kuwa ka ka-butt. Yaani jeans inakuwa na pedi ndani kusudi mtu aonekana ana matako. Loh! Watu hawaridhiki! Sijui tuseme asante J-Lo (mwimbaji Jennfier Lopez) au nini. Kwanza walikuwa wanamcheka J-Lo na matako yake makubwa lakini naona watu wanaanza kuyapenda. Mpaka kuna opresheni sasa ya kuongeza matako. Wacha wafanye haitapendeza kama matako natural tulytozaliwa nayo waafrika.

Matako Makubwa Oyee!

Saturday, November 26, 2005

Ugonjwa wa Mafua ya Ndege (Bird Flu) – Disease of the Day!

Ugonjwa wa Mafua ya Ndege (Bird Flu) – Disease of the Day!

Haya jamani, kuna huo ugonjwa unaitwa Bird Flu ambayo wanasema iko hatarini kuingia bara Marekani na kuangamiza maelfu ya watu. Kila ukifungua TV unasikia mtu au ndege kapatikana na ugonjwa huo hatari huko China au bara Asia eti kapata kwa kula kuku mwenye huo ugonjwa. Basi watangazaji wanaanza kujadili na kutabiri lini utaingia Marekani.

Lakini nataka kuzungumzia hasa jinsi watu Marekani walivyo waoga wa magonjwa yanayotoka barani Asia na Africa. Miaka ya nyuma kulikuwa na tishio la ugonjwa wa Ebola. Basi waafrika waliotoka barani Afrika walikuwa wanachunguzwa kwa makini. Yaani mtu atoke Africa hasa Congo, aende kwa daktari hapa USA, basi kisirisiri daktari anajaza ile fomu ya CDC (Center for Disease Control) halafu mtu anashutukia anatembelewa na mtu wao! Mtu atasumbuliwa na simu, visits, halafu medical record yake itachunguzwa we! Nia yao ni kuwa huo ugonjwa usisambzwe kwa watu wengine.

Halafu ulitokea ugonjwa wa West Nile Virus. Huo ugonjwa unasambazwa na mbu. Iliingia na iliua watu wachache. Yaani huo uoga wa mbu ilikuwa balaa. Mpaka walichora katuni ikionyesha ndege ya jeshi inatumwa kuua mbu moja! Caption ilisema (West Nile Mosquito sited!) Walikuwa wanapuliza miji mizima na mapori dawa ya kuua mbu kusudi waue mbu. Wanadai uliletwa nchini Marekani na ndege iliyotoka Africa. Eti mbu mwenye West Nile alidandia lifti kwenye baggage compartment ya ndege kutoka Africa na alishukia Logan International Airport! Basi hata ndege zilizotoka Afrika zilikuwa zinapulizwa dawa mara wakifungua mlango wa baggage compartment!

Kutokana na huo uwoga waBongo ma waafrika wengi wamegunda ni bora kusema unaumwa UKIMWI kulikoni usema unaumwa Malaria! Kuna MBongo alifukuzwa kazi baada ya kutoka likizo Tanzania. Alirudi na malaria, kachukua off (sick days) siku mbili. Aliporudi kazini, na bosi kamwuliza alikuwa anumwa nini. Jamaa bila kusita alijibu kuwa alikuwa na Malaria! Loh! Yule bosi aliogopa nakumfukuza kazi mara moja eti alihofu ataambukiza watu wafanyakazi ofisini huo ugonjwa. Na hata mwafrika akienda hospitalini USA analalamika anaumwa malaria utaona wafanyakazi, manesi na hata madaktari wanamkwepa na kumtenga na wagonjwa wengine. Sijui wanadhania malaria ni ugonjwa wa aina gani! Wnagejua hiyo malaria ndio common cold ya waafrika!

Na tusisahau tishio la SARS mwaka juzi! Mbona waChina wenye Restaurants hapa USA walilia shauri ya kukosa wateja! Watu kwenye TV na magazetiu walidai ukienda Chinatown au kula Chinese food unaweza kupata SARS! Jamani! Na kweli watu hawakwenda huko!

Haya nimegusia hayo mgonjwa mengine, lakini leo hii naona watu hapa USA wanahofia hiyo Bird Flu. Halafu wanadai kuna chanjo lakini ni watu wachache wanaoipata, ni wenye hela ya kulipia na watu wakubwa yaani wenye vyeo. Wanasomba hiyo chanjo ya Tamiflu na kampuni mwenye patent haitaki makampuni mengine yaitengeneze generic version, ambayo inaweza kuuzwa kwa bei rahisi. Huo ndio ubepari hasa… kujali pesa mbele ya maisha ya binadamu! Kwa sasa hapa Marekani mtu wa kawaida akina kamchape class, tulie tu. Lakini hata hivyo najiuliza kama kuna haja ya kupata hiyo chanjo kweli, na je, Bird Flu ikiingia USA itakuwa hatari kama wanavyotabiri?

WaMarekani wako macho sana. Nyama ya kuku na bata kutoka bara Asia imepigwa marufuku kuingia USA kwa sasa. Kuku, bata, bata mzinga (turkey) wanapimwa kabla ya kwenda kwenye bucha. Na siku akipatikana kuku, bata, au bata mzinga mwenye huo ugonjwa mtasikia, nyama ya kuku hakuna madukani! Maana serikali wata- recall yote na kuichoma moto! Au hata ile nyama iliyo salama, watu wataogopa kununua. Heri tuliyozoea kula maharagwe na mchicha!

Halafu watu wanaotoka barani Asia/ China kwa sasa wanapimwa Airport wakishuka kwenye Ndege. Kama wana dalili ya ugonjwa wanawekwa quarantine. Nasikia hata marubani na ma-air hostess wa Ndege wamembiwa wawe macho kwa watu wanaokohoa au wenye dalili za mafua kwenye ndege halafu wawa ripoti! Juzi juzi hapa USA kuna Mzee wa Kichina alifariki baada ya kurudi kutoka likizo huko China. Walizuia familia yake wasimzike mpaka maiti ilifanyiwa uchunguzi. Lakini kumbe hakufa kwa Bird Flu bail Natural causes, yaani ilikuwa wakati wake.

Halafu hapa USA watu wanapenda kulisha ndege chakula yaani Birdfeeding kama hobby. Wengine wameacha eti kwa vile wanaogopa hao ndege wataleta bird flu kwenye balcony na yard zao. Serikali wamekwisha tangaza kuwa kulisha ndege ni salama, hivyo hakuna haja ya kuacha! Ndege wenyewe hasa ni wa porini na hapa USA kuna akina blue jay, sparrows, robins, njiwa, lark woodpecker, na aina mbalimbali. Wakati wa winter wanapendeza kweli.

Pamoja na yote hayo nashukuru kuwa watu wako macho kwa magonjwa tishio. Na ni bora huko Afrika watu wawe makini pia maana ukiingia huko itakuwa balaa. Kwa kweli ukiingia barani Afrika maelfu ya watu watakufa. Hivi waliopewa jukumu la kufuatulia masuala ya Public Health Afrika wanafuatilia kweli? Au wana tumia muda mwingi kwenye miradi kusudi wapate pesa za kutosheleza mahitaji ya familia ya mwezi?

Pamoja na uwoga kuna mengi ya kujifunza kuhusu jinsi wanavyoshughulikia magonjwa yanayohatarisha usalama wa jamii! Mko macho Lakini?

Tuesday, October 18, 2005

Acheni Ushamba

Acheni Ushamba!

Jamani, jamani, jamani! Siku hizi nikiona vijana waBongo hapa mitaani Boston nakimbia! Hao vijana siyo wale wa miaka ya nyuma waliokuwa tayari kufanya kazi mbili/tatu ili waweze kuishi vizuri na kupeleka zawadi nyumbani. Hapana vijana wa siku hizi wanataka vya dezo! Wamekuja Marekani wakidhania maisha USA ni kama vile kwenye video za Rap. Hapana vijana, maisha siyo hivyo kabisa.

Hapa USA kama hukuja na hela zako basi uwe tayari kuchapa hizo kazi mbili/tatu, utafanikiwa!

Lakini kinacho niudhi hasa ni hao vijana wanaoenda madukani na kuiba, yaani shoplifting! Yaani mtu anaingia dukani anasomba vitu, tia ma-cap kichwani halafu wanatoka nje ya duka. Wanakamatwa halafu unaombwa uwawekee dhamana! Si waliiba wao wacha wakome huko jela! Tena jela za Boston ni nzuri kuliko kupelekwa Keko!
Nasema hao vijana ni washamba maana ukiwauliza kwa nini waliiba, watasema, “Oh, sikujua kama wananiona!” Hawakuoni???? Heh!

Mjue mkifika kwenye mall tena parking lot, mnaanza kuchgunguzwa na makamera yaliofichawa kila mahala isipokuwa chooni! Yale mapambo na magololi yanayoing’inia si urembo tu, bali ni masecurity camera. Hivyo huwezi kusema, “Oh sikuiba!” huko store detective anakutolea kanda ya video ambacho wewe ndo star! Wanaona kwa vile mlango huko wazi hakuna security, au watu wengi basi ni free for all.

Kitu kingine hao vijana,utasikia wanaongea, sijui vitu gani, wakidhania English! Wanajaribu kuiga ma-slang wanaosikia kwenye movies. Nyie! Watu hawaongei hivyo! Ukitaka kazi ya maana ujfinze kuongea English! Yaani inatisha maana huwezi hata kuelewa ansemaje na Slang zake zenye Bongo accent!

Na acheni kuvaa kama gangsta! Kwanza ukikosea rangi utapigwa risasi na ma-gang au utasumbuliwa na polisi wakidhania wewe ni gang banga! Ngojea niishie hapo… maana!

Sinema Mpya - TUSAMEHE

Watu wanangojea kwa hamu sinema mpya iitwayo, TUSAMEHE. Hiyo sinema ni kitoto cha Ndugu Josiah Kibira wa Minneapolis, Minnesota. Sinema hiyo una husu janga la ukimwi kwa sisi waTanzania na Afrika kwa ujumla. Hadithi yake ni hivi, Ndugu Bilantanya kasoma USA na kafanikiwa kupata kazi nzuri, anaoa Mtanzania mwenzake. Lakini anatembea nje ya ndoa na kupata ugonjwa wa ukimwi na kumwambukiza mke wake. Lakini cha kusikitisha mke wake anapata mimba huko Bilantanya anazidi kuumwa. Anaomba aweze kuishi mpaka mtoto atakpozaliwa. Je, atafanikiwa! Kwa habari zaidi nenda kwenye site ya Kibira Films, http://www.kibrafilms.com/tusamehe.

Walioigiza hiyo sinema ni waTanzania waishio USA, na mimi nimo kama Mama Kurusumu. Nilifurahi sana kupewa nafasi ya kushiriki katika hiyo sinema, kwanza sinema kuhusu sisi waafrika hapa USA ni chache. Pia, mimi ni sawa na waTanzania wengine, nina Ndugu, marafiki, majirani na wafanyakazi wenzangu waliokufa shauri ya ukimwi. Kama huo ugonjwa utasaidia kupunguza kasi ya ukimwi au kusaidaia dawa zipelekwe Afrika kusaidia waathirika tutatkuwa tumefanya la maana.

Thursday, September 29, 2005

Barack Obama

Hii ni jambo la kujivinia sisi wana Afrika Mashariki kuwa huenda rais wa kwanza wa Marekani Mweusi huenda akawa Barack Obama ambaye ni Senator huko Illinois. Senator Obama ni hafukasti, mama yake ni Mzungu na baba yake ni Mkenya. Ajabu zaidi ni kuwa mama yake ni mtukuu wa Jefferson Davis ambaye alikuwa Kiongozi wa Confederates. Yaani enzi za utumwa Marekani, Davis alikuwa ni rais wa maConfederates waliochukia weusi na kutaka wabakie katika utumwa na kusababisha Civil War, vita vya wenyewe kwa wenyewe (1860’s). Watu wa Kaskazini hawakutaka utumwa na watu wa Kusini walitaka utumwa udumu. Huyo Jefferson Davis bila shaka anajigueza huko kaburini kwake.

Mwaka jana, Obama alipewa nafasi kuwa keynote speaker katika Democratic National Convention, wana Demokrat walivyomchagua bwana John Kerry kuwa mgombea wa rais katika uchaguzi uliyopita. Na nilishangaa jinsi alivyoweza kuongea na watu kumsikiliza kwa makini kama vile wanamsikiliza Martin Luther King au Mahatma Gandhi. Kila mtu alimpenda na wazungu ndo kabisa sikusikia neno baya juu yake isipokuwa kutoka kwa mpumbavu Alan Keyes (MRepublican) aliyekubaliwa kuwa toi.

Na hivi karibuni alitoa shutuma kali dhidi ya serikali ya Marekani kuhusu Jinsi walivyowasaidia walioathirika na Hurricane Katrina. Bila haya, alisema kuwa serikali ilikuwa legelege na response yao kwa vile walioathirika wengi walikuwa ni weusi na maskini. Katika siku zijazo tufuatilie kawa makini matendo na maneno ya Senator Barack Obama.

Wednesday, September 28, 2005

Any time is Swahili Time

Baada ya kuongo waBongo wenzangu wakiblogu wa Kiswahili na mimi nimeamua nianzishe blogu ya kutoa maoni kwa Kiswahili. Hii ni posti ya kwanza.