Tuesday, January 03, 2012

Babu Wa Loliondo Janga La Kitaifa 2011 - Maggid Mjengwa


Mh. Lukuvi na Binti yake Mwalimu Nyerere wakipata 'kikombe' kutoka kwa Babu
Imeandikwa na Maggid Mjengwa

Babu Wa Loliondo Janga La Kitaifa 2011

 “Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote”,ni wimbo unaovutia ni wimbo; unaelezea wasifu wetu wasifu wa nchi yetu Tanzania kweli jina lako ni tamu tulalapo tunakuota wewe, Ndoto wakati mwingine uashiria kitu kijacho !

Naam ndugu zangu Watanzania, tukiwa tunakaribia kumaliza mwaka nchi yetu imekumbwa na majanga kadhaa likiwepo hili la mafuriko napenda kuchukua nafasi hii kuwapa pole wote  waliofikwa na mafuriko najua Mungu atasimama upande wao, janga hili ni  muendelezo wa majanga mengi yaliyoikuta Tanzania yetu tunayoiota utalalapo, Ambikile Mwaisapile maarufu kama babu wa loliondo ni moja ya majanga hayo .

Inayodaiwa kuwa tiba ya Babu wa Loliondo, badala ya kuwa msaada kwa taifa, imeonyesha madhara zaidi ya kiafya, kijamii na kiuchumi. Tuliandika kutahadharisha na kushauri. Tumepuuzwa; maana, kwa wengine, tiba ya Babu ilikuwa ni mradi, na kwa kweli kugeuzwa kuwa mradi wa kitaifa.

Na kilichojikita katika kuwaacha watu wetu wakitaabika ni unafiki wetu. Tuna maradhi mabaya, na ni sugu. Ndio, miongoni mwetu kuna wenye kusumbuliwa na maradhi ya unafiki. Nitatoa mfano nilipata kukaa na wasomi wawili, tena wana digrii zao. Tukazungumzia ya Babu wa Loliondo.

Mimi na wasomi wale tulikuwa na misimamo ya kufanana, tulipinga upotoshaji unaoendelea katika jamii kuwa Babu wa Loliondo, Ambilikile Mwasapile, anatibu ukimwi, kansa, kisukari na mengineyo. Na kwa vile wote tumekwenda shule, hoja kuu ilikuwa hii; kuwa hadi sasa hakuna hata wagonjwa watatu wa ukimwi waliothibitishwa kitaalamu kuwa wamepona ukimwi kwa dawa ya Babu.

Badala yake, kuna wengi wamekufa baada ya kuacha kutumia madawa waliyoelekezwa na madaktari watalaamu waliosomea tiba.

Wakati tukiendelea kuzungumza, mara akatokea mheshimiwa fulani, naye akaingia moja kwa moja kwenye mjadala. Alimtetea Babu na kusisitiza kuwa. Babu ni lulu ya taifa, lazima aenziwe. Wasomi wale afadhali wangekaa kimya, hapana, walianza kumuunga mkono mheshimiwa kwa hoja nyepesi.

Hawakuwa wapumbavu, walijifanya tu wapumbavu wakiniacha mimi nikipambana peke yangu kuziponda hoja za mheshimiwa yule. Kwa kiasi fulani, niliogopa kuona hulka hii ya wasomi wetu. Wasomi ambao, kwa unafiki, wanashindwa kutetea na kusimamia katika hoja zao za msingi. Na hii, bila shaka, ni moja ya majibu ya swali la kwa nini Tanzania ni masikini?

Hakika, ya Babu wa Loliondo ni aibu yetu kitaifa. Katika karne hii ya 21 nchi yetu inatumia raslimali zake kufanya promosheni ya ndoto ya Mtanzania mmoja kati ya Watanzania milioni 42! Ndio, tunafanya promosheni ya jambo lisilo na uthibitisho wa kisayansi. Si tuliona, haikupita siku bila kusikia  habari za Babu wa Loliondo?

Kwa sasa, tunaweza kabisa kusema, kuwa habari za huduma za Babu wa Loliondo zilitangazwa na kuufikia umma kuliko habari za Wizara yeyote ile katika  Serikali ya Awamu ya Nne. Babu wa Loliondo si mchezo bwana, alikuwa na ‘maafisa habari wake’ wanaowafunika hata maafisa habari wa Wizara za Serikali.

Na katika mzaha huu wa mambo ya msingi kitaifa, tuna maelfu kwa maelfu ya Watanzania wanaotaabika na hata baadhi kufa kwa kuamini kuwa Loliondo kuna tiba, na iko Loliondo tu! , kuna Watanzania walioweka rehani mavuno yao ya  mwaka mzima ili wapate nauli ya kwenda kwa Babu. Si wameambiwa, kuwa hata mawaziri wanapanga foleni ya kwenda kupata kikombe cha Babu!

Na wakishapata kikombe wanapiga picha ya ukumbusho, au labda ya kisiasa.  Asubuhi yake ’maafisa habari’ wa Babu wameshatundika picha ya waziri ukurasa wa kwanza gazetini! Jimboni kwa mheshimiwa wapiga kura wake watamwona au  kusikia kuwa Mheshimiwa naye anaumwa kama sisi, na amepata kikombe cha Babu!

Kikombe cha Babu ni abrakadabra, nilipata kuandika hilo. Na Watanzania, baadhi, kwa hiyari yetu, tumekubali kujifanya, wajinga na hivyo kuwapumbaza wengi wengine. Kwanini? Tulitafute jibu kwa kufikiri kwa bidii.

Hebu jiulize; wakati Shirika la Afya Duniani (WHO), Juni mwaka huu, liliadhimisha miaka 30 ya mapambano dhidi ya ukimwi, je, Tanzania, kama nchi, tulikuwa na banda la maonyesho likielezea ugunduzi wa tiba ya ukimwi  iliyotokana na ndoto ya Babu?!

Labda ndio maana, magazeti yetu ya lugha ya Kiingereza hayakufanya sana promosheni ya tiba ya Babu. Maana, kama habari za Babu zingepewa uzito kama  ilivyo kwenye magazeti yetu ya lugha ya Kiswahili, basi, wana jumuiya ya  Kimataifa, wakiwamo wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, huenda  wangeshindwa kuamini wanachokisoma.

Maana, wawakilishi wa mashirika kama PSI na FHI yenye miradi ya kupambana na ukimwi nchini na mengineyo wangejiuliza; nini hasa wanachokifanya katika  nchi yetu. Na pengine wameshatafsiriwa tunachooandika juu ya Babu kwa Kiswahili chetu!

Si ajabu basi, Ubalozi wa Marekani ulikuja na tamko lake Mei 5 mwaka huu.  Wamarekani hawa, kwa kuwaonea huruma Watanzania, wameshauri watu wanaotumia  tiba mbadala wasiache kutumia dawa walizopewa na madakatri na vile vile  waendelee kujikinga na maambukizi.

Na wakaweka msisitizo kuwa, kuacha kutumia dawa hizo za madaktari watalaamu kunafanya dawa hizo zinapotumiwa tena kushindwa kufanya kazi ipasavyo (drug resistance). Na ajabu ya habari ya tamko lile la Wamarekani ilichapishwa katika gazeti moja tu kwa lugha ya Kiingereza - The Citizen, jina la gazeti  hilo lina maana ya Mwananchi; ingawa wananchi wengi hawakupata habari hiyo kwa lugha yao!

Kwa hakika, hatuhitaji kuambiwa na Wamarekani juu ya ukweli huu na wajibu wetu. Huu ni wakati kwa wizara inayohusika kufanya jitihada za dhati kutoa tamko litakaloweka bayana kuwa tiba inayodaiwa kutolewa na Babu bado haijathibitika kitalaamu kama inaponya maradhi sugu kama vile ukimwi, kansa; na kisukari.

Wakati utafiti huo ukiendelea, umma ukumbushwe kuwa, dawa zinazotambulika kitalaamu kwa sasa ni zile zinazotolewa na madaktari wetu watalaamu. Kwamba  wanaokwenda kwa Babu wana ruhusa ya kufanya hivyo, lakini, kikombe cha Babu  kinaweza kunywewa pamoja na dawa za hospitalini.

Tufanye hivyo sasa, na ujumbe huo usambazwe kwa nguvu zote na maafisa wa  habari wa wizara husika. Ndio, maofisa habari wa Wizara ya Afya nao  washindane na ‘maafisa habari’ wa kujitolea wa Babu wa Loliondo!

Watanzania tunapita kwenye kipindi kigumu sana. Na huu ni wakati wa  kutafakari kwa kina. Na nimepata kumwuliza jamaa yangu swali hili; mwanadamu ; unafanyaje unapoamka na kukuta dunia unayoishi ardhi yake imeanza kumegeka na kuchotwa na bahari? Naye akanijibu; ” Huo ndio utakuwa mwisho wa dunia!”

 Aliyenijibu alikuwa amechoka kufikiri. Nilidhani angetamka kuwa, angeanza kujifunza kuogelea. Maana, kwa kuogelea majini angeweza kukutana na kisiwa, au nchi kavu.

Wanadamu tumejaliwa akili ili tuweze kufikiri. Na kufikiri ndio njia  mojawapo ya kuiteka kweli. Kufikiri kunahamisha milima na hata kuiweka kando  kuruhusu mwanga upite. Inakuwaje basi mwanadamu anapoacha kufikiri?

Haya ya kwa ‘Babu wa Loliondo’ ni kielelezo cha Watanzania kuamua kuacha kufikiri. Kuna umma uliojifunika vilemba vya ujinga. Umma uko gizani, ; unahitaji mwanga.

Yumkini wakatokea Watanzania wenzetu wakaoteshwa na Mungu juu ya  dawa za tiba kwa mwanadamu. Na hapo wakaingiza suala la imani. Lakini, jambo hilo halituzuii wanadamu kuhoji na kudadisi. Ndio, kuuliza maswali. Na kwa Serikali, jambo hilo haliizuii kufuata taratibu zake za kawaida ikiwamo kufanyia utafiti jambo hilo na kutoa msimamo wa kiserikali.

Hata kama Watanzania watakuwa na uhuru wa kwenda kwenye tiba za imani, lakini msimamo wa Serikali uwepo. Na kwa wengi utabaki kuwa ndio mwongozo;  maana, watakuwa wameufanyia utafiti. Nahitimisha.

Niwatakieni Heri ya Mwaka Mpya.

Maggid Mjengwa.

http://mjengwablog.com/

*************************

 SOMA HABARI ZAIDI ZA VIFO LOLIONDO GLOBAL PUBLISHERS:

http://www.globalpublishers.info/profiles/blogs/loliondo-1

8 comments:

Anonymous said...

maggid mjengwa acha kuandika. fanya kazi zingine. uandishi haukutaki wewe.

Anonymous said...

Kaka Maggid, mjadala ulio mbele yetu kuhusu KIKOMBE cha Babu ni mpana sana na hivyo si vema kuanza kufanya hitimisho kabla ya kujibu maswali muhimu. Hata na wewe unakiri hivyo katika hoja zako. Hata michango mingine kuhusu hoja hii inaonesha kuwa madala ni mpana. Mchango wangu ulihusiana na hitimisho lako kwamba Babu ni janga la taifa.Sikukubaliana na hitimisho lako. Sasa umefanya hitimisho lingine kwamba wasomi wamepumbazwa. Sikubaliani na hitimisho hili pia. Hata kama wapo wasomi waliopumbazwa, lakini wapo pia wasomi ambao wanatimiza wajibu wao wa kushauri namna bora ya kujitawala kama nchi ingawa ushauri wao unapuuzwa.Hili la nafasi ya wasomi katika kusababisha au kukabiliana na 'majanga ya kitaifa' pia linahitaji nafasi ya kutosha kujadiliwa.

Kwa maoni yangu, Kikombe cha Babu ni kiashiria cha mwenendo wetu mbaya wa kujitawala na ukosefu wa muafaka wa kitaifa juu ya siasa uchumi yetu- ni kiashiria cha ubovu wa mfumo wetu wa sekta ya afya na hata sekta ya uongozi wa kisiasa. Kila sekta inaviashiria vyake vinavyoonesha ubovu wa mfumo wetu na kila mwanabidii anaweza kwa nafasi aliyonayo katika jamii kuvitaja viashiria vya ubovu wa mfumo wetu wa siasa uchumi. Nafikiri tuanze sasa kujadili namna ya kujenga muafaka wa kitaifa na matuko kama hili la Loliondo yatusaidie kudadisi kwa kina madhila yanayotusibu kama taifa na namna ya kukabiliana nayo kwa pamoja. Kila mwananchi atakuwa na mchango wake katika zoezi hili-hili litakuwa zoezo la kitaifa siyo zoezi la kisomi.

n said...

Mimi pia siamini kwenye kikombe cha babu,ingawa pia sikubali kuwa Babu ni janga la kitaifa,uwezekano wa kuwepo waliopona kutokana na kikombe cha Babu ni mkubwa sana,hadi mwezi Mei mwaka 2011,watu milioni 3,walikuwa wamepata kikombe cha Babu,hii ni takwimu ya idara ya takwimu ya mkoa wa Arusha.

Anonymous said...

Mimi si mmoja wa watumiaji wa dawa za Babu au dawa nyinginezo zenye msingi wa imani kuliko uhalisia lakini sifurahishwi na style ya uandishi wa huyu Mjengwa kwa kuwa siku zote anakuwa hatendi haki kama mwandishi wa uchambuzi atakiwavyo. Mjengwa hutoa hitimisho kwa upeo au maono yake bila kufanya tafiti au kujumuisha maoni ya watu wengine ikiwamo huyo anayemshutumu ili kupata hitimisho lililo na uwiano kamili.
Sote twajua huyu Mjengwa alianza kumpinga huyo Babu wa loliondo tangu mwanzo na hakufanya jitihada yoyote kutafuta ukweli haswa kama wasomi wengi wafanyavyo. Sasa anapoamua kutoa hitimisho ni wazi hilo halimshtui yeyote kwa kuwa ni kama marudio ya yale aliyotaka yawe au aliyoyaandika kabla.
Hilo moja, la pili tukiangalia kwa ujumla watu wa aina ya Babu wapo weni na wamekuwapo miaka nenda rudi si Tanzania tu bali hata Nchi kubwa zilizoendelea. Mfano kuna fortune tellers hawa wamejazana kila mahali na tiba au utatuzi wa matizo ya wateja wao hautofautiani na Babu wa loliondo kwa kuwa wote wamejikita kaitika imani. Pia kuna wale viongozi wa dini ambao kama jinsi ilivyo kwa Babu wamekuwa wakitoa huduma za uponyaji hata kabla mjengwa hajazaliwa.Naam ni dini zote maana tunaambiwa kuna maji ya zamzam kwa wale waumini wa dini ya kiislam sasa mjengwa usitake tuamnini kwamba haya hujayasikia na kuyaweka katika janga la Taifa. Kuna maji ya uhai ya mhubiri anayejiita Mzee wa upako, kuna maji ya baraka kwa wale wakatoliki kuna maji ya kila aina na yanahusihwa na imani katika uponyaji wake lakini huyu jamaa hakuwahi kuyaita janga. Kwa wenzetu wa nchi za nje kuna therapists, psychologists, psychics mediums na wengineo wote wakitoa tiba mbadala ambayo zaidi sana hujikita katika imani ya yule anayetibiwa au wale wenye mgonjwa. matokeo ya tiba hizi bado hayana grounds nzito za kisayansi zenye kuonesha kwamba hizi tiba zinafanya kazi(scientific proof) lakini watu hawa wana leseni za huduma zao na hawajawekwa katika category ya janga. Well, unaweza kusema watu wengi hawaendi kupata tiba hizi lakini utakuwa unajidanganya, asilimia 86 ya watu wa nchi ya Mexico wanatumia tiba hizi sasa tusiguse takwimu za Asia, Eastern Europe na zaidi sana Africa. Ni nani ambaye hajawahi kusikia habari za waganga wa jadi achilia mbali kupata huduma zao au kuwa na ndugu aliyewahi kuwatembelea watu hawa? Sasa tunaweza kusema hii kitu haijaanzia kwa babu wa loliondo bali ipo katika utamaduni wetu na njia mojawapo ya kuonesha tarajio la mwanadamu kuwa na afya njema kwa njia yeyote itakayojitokeza. Ukimshambulia Babu utakuwa unakosea sana huyu ni mmojawapo wa mamilioni ya watoa tiba wanaokwenda kwa majina tofauti yakiwemo ya kisansi,kidini, kiganga, kiimani, au kitamaduni weather tiba zao zina matokeo sahihi au ni imani zao tu. Mjengwa anza na maji ya zamzam, maji ya baraka, maji ya upako, maji ya roho mtakatifu, maji ya mkunazi, maji ya muarobaini, na yote yafananayo na hayo hapo utakuwa unapambana na janga lakini hii ya kushutumu mtu mmoja ni kama kupambana na mbu mmoja katika kutokomeza malaria.

Anonymous said...

Ilikuwa ajabu kuona viongozi wanapewa kipaumbele katika kupata hiyo dawa kuliko mwananchi wa kawaida. Watu wamefariki wakingonjea hiyo dawa. Wangapi wamepona maradhi yao?

Anonymous said...

Watanzania wana mihela sana! yani huyo babu anachukua sh.500 tu! lakini mpaka kumfikia hapo alipo si chini ya laki 3 tena kwa yule maskini ukizingatia matajiri wanakwenda hadi na helkopta atakua ametumia shilingi ngapi, Mtu kama huyo? Halafu wakiambiwa watoe michango kusaidia watoto yatima na wale ambao ni masikini, wanakwambia hawana hela. je? Hiyo mihela yote ya kwenda kwa huyo babu wamezipata wapi? Ukizingatia hizo hela zilizotumika kwenda huko Loliondo kwa hesabu yake mpaka sasa zimeshazidi ile hela tunayodaiwa na kampuni feki ya Dowans. Wa TZ, Tusiwe na roho mbaya tuwe tunasaidia ( Yatima na masikini ) Na Allah! atatulinda na marazi makubwa kama hayo waliyonayo ndugizetu..

Anonymous said...

Kaka,natamani ningekuwa na muda wa kuandika yote niliyoniyo...sina.Ila pongezi kwa kusema lililo moyoni kwa ujasiri.Leta takwimu za mexico,Insia ,Asia.....wanatangaza tiba zao za asili kama Babu alivyotangazwa?If only Tanzanians na serikali yake wangetangaza rasilimali na habari zote za kitalii na wakajumuika pamoja tungekuwa wapi????Kaka...andeleza kazi nzuri unayoifanya ya kusema lilinalokukera bila woga!!!

Anonymous said...

sioni haja ya kumsakama babu, watu walioenda walienda kwa imani yao haikuwa ni lazima, kama watu walioenda wanakaribia milioni tatu wangekufa wote hapo ingeitwa janga la taifa, wapo waliopona nina uthibitisho wa dada mmoja aliekuwa na pumu hata ongea yake ilikua ya mkato karibu kila siku,karudi kwa babu miezi imepita bila kushikwa na pumu, sasa huyo utasema babu ni janga la taifa atakuelewa? kuna wanaolazwa hospitali watoto kwa wakubwa na ugonjwa wa malaria na tunaambiwa malaria yanatibiwa hospitali tusitumie mitishamba na bado hao wanaotumia hizo dawa kuna ambao hawaponi, wanakufa,sasa madakitari na wizara ni janga la taifa kuwaambia kuwa watu waende tibiwa malaria hospital?