HALI ya upatikanaji sukari nchini, imeanza kuwa kwenye mwelekeo mzuri,
baada ya tani zaidi ya 10,000 kuingizwa kutoka nje. Nyingine 31,000
zinasubiriwa kuwasili huku viwanda vya bidhaa hiyo pia vikianza
uzalishaji wiki hii.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Charles Mwijage alitoa taarifa hiyo jana bungeni wakati mjadala wa
bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ukihitimishwa.
Akielezea sukari inayoingia kutoka nje, Mwijage aliwataka
wafanyabiashara wote wanaojishughulisha na bidhaa hiyo, kujitambulisha
kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ili wanayopewa Dar es Salaam,
waifikishe kwa viongozi hao waione.
Kuhusu viwanda ambavyo awali
vilitarajiwa kuanza uzalishaji Julai mwaka huu, Mwijage alisema, “Adha
ya sukari iliyokuwepo, sasa inakwenda kuisha. Kuna sukari ya
kutosha…kwani leo kiwanda cha Kagera Sugar kimeanza kuzalisha tani 250.”
Waziri Mwijage alisema pia Kiwanda cha Kilombero (K One), kimeanza
kuzalisha na kitazalisha tani 600 kwa siku. Wakati matumizi ya nchi ni
tani 1,200 za sukari kwa siku, Mwijage alisema tofauti iliyobaki ndiyo
imeagizwa kutoka nje.
Aliwataka wabunge kutambua kuwa uamuzi
uliochukuliwa na serikali, ulijenga imani na kuleta wawekezaji. Alisema
hivi sasa, Kiwanda cha Sukari Kagera kinapanua eneo la Kitegule na
kuzalisha tani nyingine 60,000 na pia kukiwa na mwekezaji kutoka Oman,
ambaye ataongeza uzalishaji katika kiwanda hicho na kufikia tani
300,000.
Alisema adha ya sukari ambayo nchi inapitia sasa ni kwa
ajili ya kudhibiti uingizaji sukari na kisha kuleta wawekezaji kwenye
uzalishaji wa sukari. Mwijage alisema hali ya sukari ni ya kutosha na
sasa wamechukua hatua ya kujenga kiwanda cha Kigoma Sugar katika eneo la
hekta 47,000.
Kutoka
1 comment:
Wakati Serikali ikisema hali ya upatikanaji wa sukari imeimarika bado kuna maeneo mbali mbali hapa nchini ambayo kuna uhaba wa bidhaa hiyo kwa mujibu wa vyombo mbali mbali vya habari. Wakati viwanda vya ndani vikianza uzalishaji wa sukari Serikali inatakiwa kuainisha mahitaji halisi ya sukari na kuhurusu kiasi kinachotakiwa kuagizwa kutoka nje ya nchi na kutoa vibali mapema kuruhusu uagizaji kwa muda unaotakiwa.
Post a Comment