Friday, August 19, 2016

Benki ya Dunia Kuendelea Kusaidia Sekta ya Maji Nchini

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge akifungua  kikao cha pamoja na ujumbe wa Benki ya dunia, Wizara ya Maji ,Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (Dawasco ) na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (Dawasa) namna ya kutatua changamoto za usambaza Maji kwenye Jiji la Dar es Salaam yakiwamo Mivujo na Miundombinu chavu , kilichofanyika Jijini Dar es salaam.

Dar es Salaam.
KATIKA kuhakikisha sekta ya Maji inakua kwa kasi na inatosheleza mahitaji ya sasa ya huduma ya maji, Benki ya Dunia imejitolea kulisaidia Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es salaam (DAWASCO), ili kusaidia katika upatikanaji wa huduma ya Majisafi na Majitaka katika maeneo mbalimbali ya wakazi wa jiji la Dar es salaam pamoja na Miji ya Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani.

Hayo yamezungumzwa na Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini, Bi. Bella Bird, ambaye alikuwa ameambatana na wajumbe wake katika kikao cha pamoja na Waziri wa Maji, Mhandisi Gerson Lwenge, pamoja na Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO). 

Kikao ambacho kililenga uboreshaji na upatikanaji wa huduma ya Maji katika maeneo kadhaa ya jijini Dar es Salaam hasa maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo.

Aidha, Mwakilishi huyo wa Benki ya Dunia, ameridhishwa na juhudi za makusudi zinazofanywa na Dawasco katika kuwapatia wananchi huduma ya Majisafi, pamoja na kupambana na kiwango cha Maji kinachopotea bila sababu ya msingi. 

Ameeleza kuwa Benki ya dunia imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Majisafi na Majitaka ili kuimarisha uendeshaji wa utoaji wa huduma ya Maji kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kutekeleza kikamilifu kampeni ya “Mama Tua Ndoo Kichwani” ili kuwapunguzia akina mama wengi tatizo la Maji, kwani ndio wanaoonekana kuwa wahanga wakuu wa tatizo hilo.

Nimeridhishwa na utendaji wenu wa kazi, jinsi ambavyo mmejipanga katika kufanya kazi, hasa juhudi zenu mnazoziweka katika kupambana na upotevu wa Maji na kuwapatia wananchi huduma ya Maji alisema Bi. Bird

Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano mzuri waliouonesha, na kwamba kiasi cha fedha kilichotengwa na Benki ya Dunia kitatumika katika kuboresha na kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili shirika katika utoaji wa huduma ya Maji.

Changamoto ni nyingi katika utoaji wa huduma ya Maji, naamini kuwa kiasi cha fedha kilichotengwa kitasaidia kuondoa changamoto hizo alisema Mhandisi Luhemeja.

Benki ya dunia imekuwa ikifadhili miradi mingi ya maendeleo hapa nchini ikiwamo miradi mbalimbali katika sekta ya Maji, Nishati na Madini, Kilimo na Mifugo, pamoja na Uchumi na Biashara.


No comments: