Showing posts with label Dr. Remmy Ongalla. Show all posts
Showing posts with label Dr. Remmy Ongalla. Show all posts

Thursday, September 22, 2011

Tamasha la Kumuenzi Hayati Remmy Ongala



Aziza Machozi Ongala na mumewe Miael McGeachy, mzawa wa Jamaika, wakiongea na Urban Pulse na Freddy Macha kuhusu shughuli zao kuimarisha kumbukumbu na kazi za mwanamuziki Remmy Ongala aliyefariki Desemba 2010, mjini Dar es Salaam.
Mahojiano yalifanywa  katika Ubalozi wa Tanzania, London.


Asanteni,

URBAN PULSE CREATIVE Wakishirikiana na Freddy Macha

Monday, December 20, 2010

KUMBUKUMBU ZA REMMY ONGALA


Pichani : Marehemu Remmy Ongala (1947-2010)


KUMBUKUMBU ZA REMMY ONGALA

Na Freddy Macha

Miaka yake ya mwisho ya Remmy Ongala alikuwa Mlokole, tuseme akimsifu Yesu Kikristo. Kutokana na hali hiyo huenda baadhi ya vijana waliozaliwa karibuni wakashindwa kumjua vizuri. Mbali na kubadili dini marehemu alikata nywele zake ndefu na kuacha kuimba nyimbo maarufu tulizozoea mathalan Siku ya Kufa, Nalilia Mwana, Samaki na Mambo Kwa Soksi.

Mwaka 1997 televisheni ya Channel Four, Uingereza ilitoa kipindi (documentary) kilichotayarishwa na Mswidi, Jan Roed, kuhusu Remmy Ongala. Picha na mahojiano zilimwonyesha jijini Dar es Salaam, akifanya shoo zake sehemu kadhaa, akiongea na wananchi, vile vile akielezea dini yake asilia, Kibatala.

Nilifurahishwa sana na maelezo yake Mwanamuziki Ramazani Mtoro Ongala kuhusu imani zetu za jadi kabla ya kuja Wazungu. Leo ni wasanii au viongozi wachache sana bara Afrika wanaothubutu kusema hadharani Uislamu na Ukristo vililetwa na wageni. Mwanamuziki mwingine ni Fela Kuti wa Nigeria aliyekuwa akitambika na kusali kupitia imani za kabila lake la Kiyoruba. Fela Kuti alifariki mwaka 1997 ( kwa UKIMWI) pasina kugeuza imani zake za kijadi; kama alivyofanya marehemu Ongala.

Kimaudhui Waafrika hawa wawili mashuhuri wanatukumbusha kwamba iko haja ya kujichunguza zaidi tunatoka wapi, sisi ni nani na tunakwenda wapi, kiutamaduni.

Nilikuwa na mazoea ya karibu na mwanamuziki Remmy ambaye jina lake Ramazani lina maana “mizimu iko nami” toka nikiwa mwandishi wa habari Uhuru (1976-78). Wakati huo alipiga na bendi ya Mzee Makassy iliyokuwa ikiwika Afrika Mashariki nzima.

Remmy alianza kuitwa Dokta na waandishi wa habari wa Uhuru kutokana na alivyokuwa akivaa kama mchawi. Aliitwa pia mvuta bangi, kichaa hata muhuni. Mwaka 1983 nilianza kumwandika na kumhoji nikiwa na safu yangu ya Utamaduni (Cultural Images) gazeti la Sunday News, baada ya kuchoshwa na dharau kwa msanii huyu aliyekuwa akifungua uwanja mpya wa muziki Tanzania. Mathalan alioanisha muziki wa jadi na wa kisasa (pop) akishirikiana na wacheza ngoma wa Muungano wakiongozwa na Norbert Chenga, manju aliyecheza ngoma ya nyoka na Bugobogobo ya Kisukuma.

Ushirikiano huu ulifikia kilele wakati Remmy alipoanza kuunganisha ngoma maarufu ya “Mdundiko” (ya wenyeji asilia wa Dar es Salaam) na ile Sokous aliyoiimba kwa Kilingala, Kifaransa na Kiswahili. Nilitoa kitabu kuhusu maisha yake kilichochapishwa nikishirikiana na marehemu Stanley Mhando, mwaka 1985.

Kitabu cha Remmy kilifuatiliwa na msururu wa vitabu vingine kimojawapo cha hayati Ben Mtobwa aliyemlinganisha na Bob Marley.

Mwaka 1988 kuna Mzungu (Simon) aliyeituma kanda yake (Nalilia Mwana) kwa kampuni ya “Real World” iliyosajili na kuanza kutoa albam zake Uingereza. Awali Dk Remmy (kama wanamuziki wengine) alitolewa tu Redio Tanzania; hapakuwa na runinga au studio kama leo.

Kati ya 1988 hadi 1998 Remmy aliwaka dunia nzima. Alizunguka na Super Matimila akiimba nyimbo zilizoangalia maisha ya walala hoi, wasifu wa Mwalimu Nyerere (kwa kuondoa ukabila Tanzania) na kuchangia vita dhidi ya Ukimwi (“Mambo kwa Soksi”).

Mara kwa mara niliongea, nikamhoji na kumhoji Remmy alipokuja Uingereza.

Mara ya mwisho alipofanya shoo yake London mwisho wa mwaka wa 1996 katika klabu ya Mean Fiddler alinidokeza anao ugonjwa wa kisukari na kwamba waganga wamemweleza apunguze unene, aache pombe na sigara.

Tulizungumzia pia kuandika kitabu chake kipya katika lugha ya Kiingereza. Mara ya mwisho kuongea naye ilikuwa Oktoba 1997 nyumbani kwake. Wanawe niliowaacha wakiwa wadogo ( Kali, Jessica, Aziza) na Shema (aliyezaliwa karibuni) sasa walikuwa vijana wakakamavu. Mkewe Toni bado aliishi Bongo, akisema Kiswahili fasaha. Na nyumbani kwake palikuwa sasa “Kwa Remmy”, kituo cha basi.

Kifupi alinipa taswira ya mtu aliyeshajijenga; aliyechangia muziki wetu na kutukuza utamaduni wa Bongo ingawa hakuzaliwa hapa. Miaka yote alinisisitizia kuwa yeye ni Mwafrika na kwamba popote alipoishi au kutembea barani palikuwa nyumbani kwake. Mungu ailaze roho yake pema peponi, Amina.

http://www.freddymacha.com/

Wednesday, December 15, 2010

Rest in Peace Dr. Remmy Ongalla

Baadhi ya walombolezaji nje ya nyumba ya Dr. Remmy Sinza
Mama Yangu mzazi Rita Che-Mponda akimpa pole Mama Ongalla

Kali Ongalla akicheza na kasuku wao

Mjane wa Dr. Remmy, Toni Ongalla, wanae Tom na Kali masaa machache kabla Dr. Remmy kufariki dunia.


Wadau, siku ya jumapili 12/12/10, nilialikwa nyumbani kwa Dr. Remmy na mke wake Toni. Tunafahamiana na famila ya Ongalla tangu mwaka 1978. Hivi karibuni walikuwa wamehamia kwa muda nyumba huko maeneo ya Africana kwa vile nyumba ya Sinza inakarabatiwa.

Basi, nilifika huko kwenye saa 7 na nusu. Toni alinipeleka chumabni kumsalimia Dr. Remmy. Dr. Remmy alikuwa amelala kwenye kitanda na mwanae Tom. Mke wake alisema, "Chemi amekuja kukusalimia, unamkumbuka Chemi?"

Dr. Remmy aliwaambia anataka kwenda sebuleni kukaa. Walivyotoka kwenda kumchukua kiti cha kumsukuma kwenda huko (walikuwa wanatumia viwili vya palstiki kwa vile hawakuwa na wheelchair, Dr. Remmy aliinuka mwenyewe kitandani na nguvu zake. Alikaa akanitazama sana, ila hakusema kitu. Nilimwambia pole kwa kuumwa lakini atapata nafuu. Walileta kiti halafu walimpeleka sebuleni kwenye meza ya kulia chakula.

Chakula kililetwa na nilikula na familia huko natazamana na Dr. Remmy. Mara kadhaa alishika mke wake mkono kama vile anamwambia asiwe na wasiwasi mambo yote yatakuwa sawa. Dr. Remmy hakuweza kula lakini alikunywa soda kidogo na supu. Wanae Kali na Tom walimsihi baba yao ale chakula ili apate nguvu. Baada ya muda aliomba arudishwe chumbani, wanae walimpeleka.

Mimi na Toni tuliongea sana maana Dr. Remmy alikuwa na matatizo ya mafigo na marehemu mume wangu Rev. Whitlow alifariki kutokana na maradhi ya figo. Toni alisema kuwa Dr. Remmy alipata Stroke (kiharusi) tangu mwaka 2000. Toni aliniuliza kama ingekuwa vizuri awaite wanae walio nje kuja kumwona baba yao. Nikamshauri awaiite mara moja, maana niliona hali ya Dr. Remmy ilikuwa ya kutisha, lakini sikutegemea kama angefariki siku ile. Alikuwa bado ana mwili. Tuliaagana na familia ya Ongalla, halafu nilienda zangu.

Kesho yake nilitoka Muhimbili baba yangu alikolazwa kwenye saa nne na nusu kwenda kupanda daladala kwenda Kariakoo kwenye stendi pale Muhimbili. Nikiwa nimekaa kwenye basi walitangaza kwwenye redio kuwa Dr. Remmy amefariki dunia. Nilianza kupiga mayowe na kushgangaa kuwa mtu niliyemwona akiwa haia masaa machache kabla alikuwa amefariki. Si watu walinizunguka kusikia kuhusu ile last supper na Dr. Remmy.
Sikumpiga picha maana ningependa ktumukumbuke kama alivyokuwa. Mungu awape familia nguvu katika kipindi hiki kigumu.
REST IN PEACE DR. REMMY!