(pichani marehemu Mohamed Mpakanjia na mke wake marehemu Amina Chifupa)Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.
Kutoka Michuzi Blog:
HABARI ZIMEINGIA SASA HIVI ZINASEMA MOHAMED MPAKANJIA, ALIYEKUWA MUME WA MAREHEMU AMINA CHIFUPA, AMEFARIKI DUNIA MCHANA HUU KATIKA HOSPITALI YA LUGALO ALIKOKUWA ANAPATIWA MATIBABU, DURU ZA KARIBU NA MAREHEMU ZIMETHIBITISHA.
KWA SASA GLOBU YA JAMII INAWEZA KUTOA TAARIFA HIYO TU,
ZINGINE ZITAFUATIA BAADA YA KUHAKIKIWA.
*************************************************************************
Kutoka Lukwangule Blog:
MFANYABIASHARA maarufu na mdau mkubwa wa michezo na burudani nchini, Mohamed Mpakanjia(pichani) amefariki dunia leo katika hospitali ya jeshi la Lugalo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika hospitalini hiyo ambayo pia alifia aliyekuwa mkewe Amina Chifupa, Mpakanjia amefariki dunia katika hospitali hiyo majira ya saa saba mchana.
Chanzo chetu cha habari kilichopo katika hospitali hiyo kilisema kuwa mfanyabiashara huyo alifikishwa hopitalini hapo jumamosi iliyopita kutokana na kusumbuliwa na homa ya mapafu (PNEUMONIA).
"Aliletwa hospitalini hapa jumamosi akisumbuliwa na matatizo ya homa ya mapafu. Wakati analetwa alionekana mwenye afya njema lakini hali yake ilibadilika ghafla leo na mauti kumfika," kilisema chanzo hicho cha habari.
Katika uhai wake Mpakanjia alikuwa ni miongoni mwa watu waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya michezo na burudani hasa kutokana na kusaidia wasanii, wanamuziki na bendi nyingi za muziki hapa nchini.
Alikuwa mfadhili mkuu wa bendi ya DDC Mlimani Park 'Sikinde', Tanzania One Theater 'TOT Plus' na pia alidhamini albamu za pamoja za wanamuziki Ramadhani Masanja 'Banza Stone', Ally Choki na kiongozi wa Msondo iitwayo 'Sisi ndiyo Sisi' ya mwaka 2005.
Kwa upande wa sanaa alitoa mchango mkubwa kwa kuwasaidia wasanii wengi wa sanaa ya filamu na maigizo kwa kuwawezesha kifedha kukamilisha kazi zao hizo.
Mungu ailaze roho yake pema peponi. Amina.
Habari hii nimeletewa na Selemani Mkangara.

