Monday, December 12, 2005

Asante Civil Rights Movement!

Bibi Rosa Parks amefariki dunia jana 10/24/05 akiwa na umri wa miaka 92. Kwa kweli aliishi mpaka uzeeni kabisa, lakini alifanya mengi na alibarikiwa kuona matunda ya matendo yake.

Siku ya Desemba mosi, 1955, Bi Parks akiwa kwenye basi akielekea kurudi nyumbani alikataa kusimama kumpisha baba wa kizungu. Alikuwa amechoka baada ya kazi ngumu. Kwa nini ampishe mzungu tena mwanaume? Kumbuka, enzi hizo weusi Marekani hawakuwa na haki sawa na wazungu. Weusi Marekani walikuwa watumwa, na baada ya kupata uhuru wao 1864 walikuwa bado wanaishi katika nchi ya kibaguzi!

Kabla ya Civil Rights movement kafanikiwa, weusi walisoma shule duni, na kuishi sehemu zilizotengwa na wazungu. Ulikuwa huwezi kukaa na wazungu hata kama ulikuwa na pesa. Kazi walizokuwa wanafanya zilikuwa za kuhudumia wazungu, yaani maklina, mesenja, kubeba mizigo, kuzoa takataka. Walikuwa hawawezi kupata kazi ya maana shauri ya ubaguzi, hata kama angekuwa amesoma kiasi gani! Kulikuwa na mabomba ya maji ya kunywa, mzungu alikuwa na bomba safi na mweusi labda alikuwa na kabomba na maji yanatoka ovyo ovyo na iko sehemu chafu! Au unaenda restaurant kula lakini unawekewa meza jikoni au karibu na choo! Au unaambiwa uchukue chakula mlango wa nyuma! Vyoo (restrooms) vilitengwa kwa ajili ya wazungu na weusi. Weusi waliokuwa hawezi kuingilia mlango wa mbele ya majumba, ilikuwa lazima wapitie mlango wa nyuma. Walikuwa hawawezi kukaa hoteli za wazungu. Na mara nyingi ilikuwa kama wewe mweusi unasafiri unalala ndani ya gari au nyumbani kwa mweusi mwenzio. Enzi hizo weusi walikuwa wanasaidiana sana shauri ya huo ubaguzi.

Fikiria unaenda Airport halafu unaambiwa kwa vile mweusi ukalie sehemu duni. Yaani sehemu enyewe ina viti vya mbao, baridi na mavumbi, halafu unaona sehemu ya ‘White Only’ wamewekewa masofa mazuri kabisa, halafu pamepambwa vizuri. Au unasafiri, halafu wazungu wanaenda kwenye vyoo vya kisasa vya ku-flush, weusi mnaambiwa muende kutumia choo cha shimo! Ndivyo hali ilivyokuwa. Shule za weusi zilikuwa duni pia. Walikosa vitabu vya kutosha halafu majengo mabovu! Yaani! Na ilikuwa ukisema kitu, basi unaweza kuuwawa!

Unaweza kusema hali ya weusi Marekani ilikuwa ni sawa na apartheid ya Afrika Kusini. Lakini ilikuwa ni tofauti maana katiba ya Marekani inasema kuwa watu wote ni sawa. Eti “All Men Are Created Equal” Walikuwa sawa kwenye karatasi tu! Fikiria, ukienda kwenye historic archives, unakuta weusi waliorodhewa kama mali, sawa na wanyama, na! Wazungu hawakutuona sisi weusi kama binadamu, na eti ukimpiga mweusi hasikii maumivu! Loh!

Kweli WaMarekani weusi wametoka mbali toka enzi za Utumwa na Civil Rights. Waliopigania Civil Rights ni wengi, tusisahau akina Dr. Martin Luther King, Jr., Malcolm X, Frederick Douglas, W.B. DuBois, Medgar Evers, yaani watu wengi tu! Na watu walikufa wengi pia majina yao hatuyajui, na wamesahaulika.

Lakini ni lazima tushukuru, hao waliotangulia na kufanya weusi leo wawe na haki Marekani. Kutokana na juhudi zao na damu iliyomwagwa, si weusi tu, bali watu kutoka nchi mbalimbali na rangi mbalimbali wanaweza kuishi vizuri Marekani na kula matunda ya Civil Rights movement. Marekani sasa kweli wanaweza kusema, “All Men Are Created Equal”.

1 comment:

Ndesanjo Macha said...

Watu wote uliowataja hapa na wengine wengi, leo hii tumesimama juu ya mabega yao. Hatuna budi kuwakumbuka na kujifunza toka kwao kwamba haki huwa hupewi tu hivi hivi...UNAIDAI na KUITWAA!