Tuesday, August 11, 2009

Da Flora Aongelea Suala la Mahausegeli

Wadau, hii suala la mahausegeli kugeuza nyumba danguro lipo siku nyingi. Pia mahausgeli kupata mimba za baba mwenye nyumba au vijana wa kiume kwenye nyumba ni jambo la kawaida. Tufanye nini ili kutokomeza hiyo tabia chafu?

***********************************************************************
Na Flora Wingia
9th August 2009

Mpenzi msomaji, lipo jambo moja nimesimuliwa nikaona ni vema nawe nikumegee pengine huna habari kama hata hayo yanatendeka nyumbani kwako bila kujua.

Ndani ya familia zetu nyingi, hazikosi mtumishi wa nyumbani awe ni hausigeli au shambaboi. Katika nyumba hizi, zipo zenye watoto wadogo au zingine zina wazee ambao wanatunzwa na mahausigeli hao.

Pia zipo ambazo hazina wazee wala watoto bali ni mahausigeli pekee ambao hubakia nyumbani baada ya matajiri zao kwenda kazini. Hizi ndizo nitakazozungumzia leo, nikigusia kidogo zile zenye watoto wadogo.

Ipo familia moja jirani na kwa rafiki yangu pale Makonde, Mbezi Beach inafanyiwa shere na hausigeli wao lakini hawajui kwa kuwa wote ni wafanyakazi.

Rafiki huyu akanisimulia kwamba binti huyo ambaye anaishi na familia moja yenye watoto ambao wote wanasoma shule za bweni, amekuwa akialika rafiki zake wa kiume pale nyumbani bila woga.

Majirani zake wamekuwa wakimtizama kwa jicho moja na hata walipomtaarifu mama mwenye nyumba kuhusu tabia hiyo, yeye alipinga kwa maelezo kuwa huenda wanamuonea gere kwa kumpata hausigeli mzuri na mchapakazi. Kumbe anasahau msemo kuwa ‘kikulacho kiko nguoni mwako’

Msichana huyu toka moja ya mikoa ya Kusini mwa nchi, anachofanya ni kuamka alfajiri na kuhakikisha kuwa anawaandalia matajiri zake kila kitu wanachohitaji ili wanapoondoka tu majira ya saa 12 asubuhi aweze kurudi kulala kwa saa kadhaa.

Hiyo ndiyo imekuwa ratiba ya bibie huyo kila siku isipokuwa Jumamosi na Jumapili ambapo wenye nyumba wanakuwa nyumbani. Lakini katika siku zingine yeye ndiyo hujipangia ratiba ya kujirusha na yule ampendaye.

Jirani huyu anasema kuwa yupo baba mmoja wa makamo ambaye amekuwa akionekana karibu kila siku nyumbani kwa familia hiyo kuanzia majira ya saa moja asubuhi hadi baada ya mlo wa mchana.

Swali ni je, baba huyu anayedhihirisha kuwa ameoa na anao watoto, haoni aibu kuzoea nyumba hiyo yenye wenyewe? Isitoshe, umri wa binti anayemmendea ni mdogo ikilinganishwa na ule alionao. Na wenyewe wakiibuka ghafla atajitetea vipi? Au ndio amekolewa na ule msemo kuwa inzi kufia kidondani ni halali yake’?

Hicho ni moja ya vimbwanga vya mahausigeli. Tena wengine, huthubutu hata kuleta wanaume zao ndani ya nyumba kama huyo niliyemzungumzia na kudiriki kujirusha juu ya kitanda cha bosi wake.

Eti naye aone raha kama ile aipatayo bosi akiwa na mamsapu wake. Na ukiona hivyo, binti wa aina hiyo huenda analala chumba cha ovyo ovyo, hivyo kujiongezea thamani anaamua kujiliwaza katika mandhari wanayofurahia matajiri zake.

Mahausigeli wengine bila aibu, hujipitishapitisha mbele za mabosi wao wa kiume ili waweze kunasa kwenye ulimbo. Ushawishi huu ni ushetani usiokubalika lakini unazitesa sana baadhi ya familia zetu. Ukweli ndio huo.

Matokeo yake, wanawavuruga vichwa baadhi ya kinababa na hivyo kutamani bila kupenda. Ndio hao unaosikia kuwa mama kamfumania mumewe na hausigeli.

Au mama anamtilia shaka hausigeli kuwa ana mahusiano na mumewe hivyo anamtimua. Wapo kina mama waliowafukuza mahausigeli kibao, kisa macho hayatulii wanapokuwa nyumbani na hasa akiwepo baba mwenye nyumba. Maisha Ndivyo Yalivyo! Au siyo? Kwamba purkushani za aina hii hazikosekani.

Mahausigeli wengine wanapoibukia kwenye nyumba zenye mashambaboi au wengine huwaita mahausiboi, inakuwa kama wamefungishwa ndoa za mikeka. Mabosi wakiondoka kwenda kazini wao ndiyo huanzisha nyumba zao za muda. Wapo waliobebeshana mimba kwa mtindo huo.

Bila kusahau wale wanaotoroka usiku kwenda kujirusha na washikaji wao na kisha kurejea alfajiri bila matajiri wao kung’amua. Hii ni hatari kwani wanaweza kutoa mwanya kwa wezi na kuiba.

Naam. Mpenzi msomaji, hapa nilitaka kuonyesha kuwa pamoja na umuhimu wa watumishi hawa katika kuhudumia familia zetu, lakini wengi wana madhaifu yao kama binadamu. Yapo yanayovumilika lakini mengine hakika hayakubaliki.

Kwa mfano kwa zile familia zenye watoto, wapo baadhi ya mahausigeli wameharibu watoto. Kwa mfano atamleta mshikaji wake nyumbani halafu kwa raha zao wanapigana mabusu huku watoto wakishuhudia. Haya sio malezi mazuri kwani badala ya kuwajengea watoto nidhamu nzuri anawaharibu kwani wataiga matendo yake

Mpenzi msomaji, kwa kifupi nilitaka kuwatahadharisha wazazi wenzangu kuhusu hawa wafanyakazi wetu wa majumbani. Pamoja na umhimu wao, lakini wanahitaji uangalizi wa karibu ili mabosi wanapokuwa makazini, na nyumbani nako kuwe na heshima yake badala ya kugeuzwa nyumba za wageni au sehemu za kufanyia maasi ya kimya kimya.

Tusiwape uhuru wa moja kwa moja. Ikiwezekana katika nyakati fulani mmoja wao, awe baba au mama afanye ziara ya kushtukiza. Yapo mambo mengi yanayoweza kubainishwa na ikiwezekana kuzimwa mapema badala ya kuachwa na hatimaye yakatokea madhara.

Wanapogundua kuwa zipo ziara za kushtukiza, sidhani kama wale waliozoea kuleta washikaji mara tu mabosi wanapoondoka watathubutu kufanya hivyo tena. Pia taarifa za majirani zisipuuzwe kwani wao ndio walioko karibu na wanaona mengi yanayotendeka wakati wenye nyumba hawapo. Au siyo? Huo ni ushauri wa bure, waweza kukubalika au kukataliwa lakini ukweli unabakia pale pale kwamba, lisemwalo lipo na kama halipo linakuja.

Msomaji wangu, kama unayo maoni au mchango wowote nikandamizie kupitia

flora.wingia@guardian.co.tz

4 comments:

Anonymous said...

Aliyosema Da Flora ni kweli tupu ingawa pia kuna mahasigeli ambao wametulia. Ziara za kushitukiza ni ushauri mzuri. Taarifa za majirani ni vizuri kuzikiliza na kutafiti ukweli wake kabla ya kuchukua hatua.

Anonymous said...

Hao hausegeli wanajipeleka wenyewe. Wanataka wapate mimba ili watunze na hao vigogo. wengi wanaishiha kutupwa!

Anonymous said...

Hayo aliyosema Da Flora ni kweli lakini tuangalie upande mwingine wa shilingi. Hawa wengi wao wanatafuta maisha mazuri, wameondoka kwao kutauta maisha wengine wanateswa au kubakwa na familia mpya ( baba tajiri au watoto wa kiume au mimama bosi) wanawalazimisha mapenzi wakikataa wanafukuzwa kazi. Wengi wanafanyishwa kazi nyingi lakini malipo madogo.

Anonymous said...

Yote yaliyoongelewa ni sawa kabisa. Ila tatizo la housegirl, ukimuweka karibu na wewe, umfanye kama mmoja wa ndugu zako nayo inakuwa tatizo. Hasa sisi waafrika, huwa tunawachukulia kama watoto/ndugu zetu, tunakula pamoja, atalala chumba kimoja na watoto wetu, yaani kunakuwa hakuna ubaguzi, lakini cha kushangaza, atajisahau kama yeye amekuja kufanya kazi pale, atabishana na watoto mle ndani kuhusu kufanya kazi za ndani wakati yeye ndo analipwa, atakuwa jeuri, yaani vituko tu. Lakini housegirl huyo huyo akienda kufanya kazi kwa mhindi, mbali ya kubaguliwa, kula makombo, kutukanwa, atadumu mahala hapo. Hapo ndipo huwa nashangaa hivi hawa wanataka kuwa treated namna gani? Kwa kweli sijapata formula ya jinsi ya kum-treat housegirl huyu!!!