Thursday, February 02, 2012

Tarifa ya TPN Kuhusu Migogoro/Migomo Iliyopo Hususani Sekta Afya

Kwa muda mrefu sasa jamii yetu imekumbwa na migogoro na migomo ya mara
kwa mara katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu n.k.Na inaonekana
kwamba hali hii inataka kuzoeleka na kuonekana ni hali ya kawaida, na
kama haitathibitiwa kwa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu basi inaweza
ikalifikisha Taifa letu mahali pabaya na kupunguza kasi ya ukuaji wa
uchumi na hivyo kuathiri mikakati ya kupunguza umasikini.

Kwa sasa dunia nzima iko katika hali tete kutokana na kudorora kwa
uchumi na baadhi ya nchi ukuaji wa uchumi umesimama au umeshuka sana
hivyo kwa namna moja au nyingine nchi zetu pia zinaathirika na hali
hii kwa njia moja au nyingine.

Kwa kuzingatia hali hiyo sisi wanataaluma tunaona kwamba kwa sasa
rasilimali tulizonazo ikiwemo watu, ardhi, maliasili n.k tuzitumie
vizuri ili zitusaidie kupambana na janga hilo.
Kwa hali hiyo ni dhahiri uwezo wa serikali kugharamia baadhi ya huduma
utapungua hivyo basi tunaomba kwa sasa wananchi waelewe hali hivyo na
ni jukumu letu sote sasa kushirikiana kupambana na changamoto hizo.

Chanzo kimojawapo cha migomo na migogoro hiyo ni kupungua kwa
mawasiliano miongoni mwa wadau husika hivyo kusababisha upande mmoja
kutojua au kutohusishwa katika kututua tatizo husika.

Hivyo basi tunashauri wadau wote yaani serikali, viongozi, watendaji
wa wizara na taasisi mbalimbali wakae na washirikishane katika sehemu
zao za kazi na kupashana habari kwa muda muafaka.

Kuhusu tatizo linaloendelea kwa sasa katika sekta ya afya tunawapa
pole nyingi sana watanzania wote waliopoteza maisha na waliaothirika
kwa namna moja au nyingine kutokana na athari za mgomo huu.

Baadhi wa waliaothirika yaani wagonjwa na baadhi ya madaktari ni
wanachama wetu.
Sisi kama wanataaluma tunaipongeza serikali kwa hatua zilizochokuliwa
hadi sasa za kupunguza athari za tatizo hili japokuwa bado sehemu
nyingine hali bado haijatengemaa lakini ni matumani yetu kila mtu
atatimiza wajibu wake kwa mujibu wa taaluma zao.

Tunaiomba Serikali iharakishe mazungumzo na madaktari na itoe ahadi ya
kutekeleza madai ya madaktari kadri uwezo utakavyoruhusu Tunaiomba
Serikali ifikire upya uamuzi wake wa awali wa kuwafukuza kazi wale
madaktari ambao walikuwa bado hawajaripoti kazini kama agizo la Mh.
Waziri Mkuu lilivyoelekeza badala yake tunashauri hatua nyingine za
kinidhamu zichukuliwe badala ya kuwafukuza kazi, kwa sasa bado nchi
ina upungufu mkubwa wa wataalamu katika sekta hii.

Tunawashauri madaktari wote nchini wakati madai yao yakishughulikiwa
warejee katika maeneo yao ya kazi na wafanye kazi kwa bidii na maarifa
yao yote, waonyeshe uzalendo kwa nchi yao.

Wale wote walitajwa katika taarifa mbalimbali kwa tuhuma mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kushindwa kuwajibika kwa kutoa kauli zilizochochea
au kukuza mgogoro huu basi waombe radhi mara moja na kama wakishindwa
basi hatua za kinidhamu zichukuliwe haraka dhidi yao.
Tunaomba watanzania wote, viongozi, watendaji wa Taasisi za umma na
binafsi tuwe waadilifu tuzingatie dhana ya utawala na uongozi bora,
tuwe wazalendo wa kweli na tuweke mbele Utaifa na maslahi ya walio
wengi.

Phares Magesa
Rais- TPN

No comments: