Thursday, March 22, 2012

Dr. Mbele Asifia Tiba Aliyopata Dar

Wadau, Prof. Mbele yuko safarini Tanzania.  Ameugua na kwenda hospitalini. Anasema kuwa ameridhika na tiba aliyopata, hakuwa na haja ya kukimbilia nchi za nje kam India kutibiwa.

****************************************

Kutoka  Hapa Kwetu  Blog



Thursday, March 22, 2012

Nimeugua Dar es Salaam; Natibiwa Hapa Hapa, Sio India

Nimeugua Dar kuanzia siku chache zilizopita. Nimejikuta nikiwashwa hasa mikononi, miguuni, na mgongoni. Kwa siku mbili sikuweza kulala usiku. Katika kuulizia watu, nikaambiwa ni "allergy." Na mhudumu mmoja kwenye duka la madawa maeneo ya Sinza aliniambia niende Magomeni, kwenye hospitali ya Dr. Ole.

Nilienda hapo. Wakati wa kuchukuliwa damu ili ipimwe, mpimaji alinipiga mchapo kuwa isije ikawa nimewekewa sumu ya unga. Akazidi kutonya, huku akijifanya ananyunyizia unga mezani, kuwa kaunga kidogo tu kanatosha. Nami nilijibu kuwa mtu huwezi kujua, kwani Bongo haina dogo. Tukawa tunachkea.

Ni kweli daktari alipochunguza ripoti ya upimaji amegundua nina "allergy," na akanielezea sababu zake. Aliniandikia sindano na vidonge vya aina mbali mbali. Alisema kuwa hiyo dozi itafuta kabisa hili tatizo. Nimedundwa sindano jana na vidonge nikaanza. Tayari nimeshaanza kujisikia nafuu. Naendelea vizuri kabisa.

Nimeleta habari hii binafsi kwa sababu maalum. Kwanza, mimi kama m-Tanzania nina imani na madaktari wetu. Ninafundisha Marekani, na ninapougua kule natibiwa kule. Ninapougua Tanzania natibiwa hapa. Tena, miaka yote ya maisha yangu, kabla sijaenda Marekani nilikuwa natibiwa hapa Tanzania, bila matatizo.

Sioni kama kuna tofauti kati ya madaktari wa Marekani na wa kwetu. Kilichopo tu ni kuwa madaktari wa kwetu wapewe mahitaji yanayopasika katika kumshughulikia mgonjwa. Na hilo ni jukumu la serikali, wala isijaribu kukwepa, kwani Tanzania si nchi maskini. Nakerwa ninapowasikia viongozi wa nchi hii wakidai kuwa sisi ni nchi maskini. Juzi hapo nimemsikia waziri kwenye kipindi cha televisheni akitoa huo upupu kwamba Tanzania ni nchi maskini.

Nawashangaa wa-Tanzania waoendelea kuwapigia kura mbumbumbu wa aina hiyo, wasio na upeo kiuongozi, hawana fikra za kuijengea jamii ari ya maendeleo, badala yake wana upeo wa kudumaza na kukatisha tamaa. Nawashauri wajifunze kutoka kwa Rais Obama, ambaye katika mazingira yoyote yale, hawakatishi tamaa raia wake, bali anawahakikishai kuwa Taifa litapambana na litashinda, litafanikiwa. Lakini viongozi wa kwetu, kila kukicha ni vilio kuwa sisi ni nchi maskini!

Uwezo wa kuimarisha hali ya mahospitali yetu tunao, tukizingatia rasilimali nyingi tulizo nazo katika nchi hii. Pia, magonjwa mengi tunayopata hayahitaji daktari bingwa. Yanatibiwa vizuri, iwe ni Marekani au Tanzania. Tena yako magonjwa ambayo ni ya nchi kama zetu, ambayo wataalam wake ni hao madaktari wentu. Mifano ni malaria. Usidhani kuwa ukipata malaria, ukimbilie Marekani. Unaweza ukafia kule, kwa sababu sio madaktari wengi wanaijua malaria na namna ya kupambana nayo kama wanavyojua madaktari wa nchi kama Bongo. Hao madaktari wetu wanasomea magonjwa ya hapa kwetu. Ninavyofahamu, wanapoenda kusomea Ulaya, utakuwa wanasomea "tropical medicine" ambayo ndio uwanja wa mapambano katika nchi kama yetu.

Madaktari wetu wana ujuzi wa hali ya juu, utawakuta wako katika nchi mbali mbali. Ninawafahmu baadhi ambao wako Marekani, katika hospitali mbali mbali, kama vile Mayo Clinic, ambayo ni maarufu sana duniani. Yaani inashangaza kuwa ukienda hizo hospitali, unawakuta madaktari wengi wa kutoka Afrika, yaani madaktari kama hao wanaonyanyasika Tanzania kwa sababu ya viongozi wetu kutokuwa na upeo upasao.

Kwa hiyo, serikali yetu inachopaswa kufanya ni kuwekeza katika huduma za mahospitali yetu hapa hapa nchini. Iweke vifaa na miundombinu, ili madaktari wetu waweze kutumia ujuzi wao ipasavyo. Wakipata vifaa na miundombinu, na wakilipwa ipasavyo, watafanya yale yale ambayo baadhi ya watu nchini wanayatafuta India au ughaibuni. Tunapowapeleka watu nje eti kuchekiwa afya, wakati hizi ni taaluma za madaktari wetu pia, au tunawapeleka watu kutibiwa ugonjwa kama niliopata mimi wiki hii, ambao madaktari wetu wanajua namna ya kuutibu, ni kuwadhalilisha madaktari wetu, na mimi sitalilazia damu suala hilo.

Miezi michache iliyopita, nilipata fursa ya kumsikiliza Dr. Mark Jakobson, ambaye ni mwendeshaji wa hospitali ya Selian, Arusha. Alikuwa akitoa mhadhara Minnesota, kuhusu shughuli za hospitali hiyo. Siku moja nitaelezea katika hii blogu yangu. Jambo mmoja ninalokumbuka ni jinsi alivyowapigia debe madaktari wa ki-Tanzania wanaofanya naye kazi. Anatamani tu angekuwa na uwezo wa kulipa vizuri zaidi, ili wasipate vishawishi vya kwenda sehemu zingine.

Makala hii nimeiandika pia kwa sababu juzi hapo niliandika makala kuhusu mgomo wa madaktari nikaishutumu serikali kwa kudiriki kugombana na madaktari. Kwa hivi, nimejichukulia fursa hii kuelezea zaidi hisia zangu. Kati ya mambo niliyosema ni kuwa kisaikolojia, daktari anapaswa awe kazini akiwa amefurahi na moyo mkunjufu.

Huyu jamaa aliyenipima damu alitoa mchapo na tukacheka. Muuguzi au daktari anapokuwa na moyo mkunjufu na ucheshi, anapokuwa hana msongo wa mawazo, ni baraka kwa wagonjwa. Watafiti wa masuala ya saikolojia ya wagonjwa na matibabu wanathibitisha hilo. Ndio maana niliishutumu serikali kwa kutotambua umuhimu wa kuwaridhisha madaktari.

7 comments:

Anonymous said...

Profesa Mbele umefanya vizuri kuelezea suala hili.Ukweli Wamasiasa wanadharau sana Wanataaluma Madaktari,Maeinjinia n.k.Kitendo cha wao kukimbilia nje kutibiwa ni dharau kwa Madakitari wetu ambao wamesomea hapa USA na Ulaya.Labda ni kwavile tuu pesa hizo hazitoki mifukoni mwao[kodi za wananchi].Nakuhusu suala la pesa Nchi inazo na Rasilimali zipo ila tuu zinatumiwa vibaya.Mfano tuna Wabunge karibuni 400 nawengi wao ni wakuteuliwa na viti maaluum,kwanini tusiwe na wabunge 200 tuu wamajimbo.Mawaziri na Makatibu karibuni 120,swali Nchi yenyewe ina ukubwa gani kuwa na idadi kubwa ya viongozi wote hao.Mwisho wachiba Madini walipishwe Kodi ya Kisawasawa.Ukweli Katiba na mfumo wa Uongozi uliopo wauna Faida na umepitwa na Wakati,Viongozi nawakumbusha kuwa tupo KARNE ya 21 punguzeni Matumizi kwa kuwa na SERIKALI NDOGO.

Anonymous said...

Ninakubaliana 100% na mtoa mada. Kwenye hotuba yake na Wazee wa Dar es salaam, JK alisema fani ya udaktari ni muhimu sana kwani wakigoma mgonjwa anaweza akafa, na wanaporudi hawataweza kurudisha uhai wa marehemu. Hii ni kweli sasa Ilipaswa kwa kulijua hili serikali iwape madaktari kipaumbele kwa kuwapatia malipo mazuri,nyenzo na mazingira bora ya kazi.

Kwenye uchumi wa Soko Huria kila mtu anaangalia maslahi yake pia. Iweje Madaktari waachiwe jukumu la kubeba afya za wananchi wa kujitolea na kujiumiza wenyewe na familia zao.

If the government truly values the contribution from the Doctors as they claim to, then they (the government) must show their appreciation by paying them worthy salaries.

Mdau Dar es salaam

Anonymous said...

Bongo kuna huduma nzuri ya afya, kama una hela ya kwenda Private! Maskini walie tu. Na hao viongozi wantafuta shopping tu au hawataki tujue wanaumwa nini! Wengi wanaenda nje kutibiwa ugonjwa wa kisasa.

emuthree said...

Hebu fikiria hizo za kwenda kuwatibia huko nje, nafikiri zingesaidia hata kuongeza wodi za wajawazito huko hospitali za mikoani, lakini wapi, kila mtu anajijali yeye...haya katibiweni huko, lakini mjue hizo hela mnazotumia ni za walalahoi ambao hata tiba ndogo wanaambiwa dawa hakuna....lakini tunashukuru kuwa madocta wapo, ingawaje wanalipwa kiduchu ukilinganisha na wabunge wetu....

Nizar said...

Sawa bwana profesa mbele unayetushangaa sisi watanzania kuendelea kuwapigia kura wanasiasa wetu mbumbumbu. Jee, vipi wewe ambaye siyo mbumbumbu uachane na hiyo "pursuit of american dream" na uje ugombee uongozi hapa nyumbani ili ubadilishe hali halisi? Jee huoni kwamba mbumbumbu wanachaguliwa kwa sababu watu ambao siyo mbumbumbu kama wewe wanaogopa kushindana na mbumbumbu?

Na kama kweli unaridhika na huduma za afya za hapa nyumbani, kwanini umekwenda magomeni kwa dokta ole? kwanini hukwenda mwananyamala au amana hospitali kwenye hospitali zinamilikiwa na walipa kodi?

Nakuomba ukiumwa tena au mtoto wako akiumwa mpeleke hospitali za serikali, kisha uje hapa utueleze kwamba unaridhishwa na viwango vya huduma za afya.

Anonymous said...

Nizar Dokta Mbele yuko wright kwenda magomeni na siyo mwananyamala anachosema yeye Tanzania kuna huduma nzuri haijalishi umeipata wapi hata kama umeipata private bado ni Tanzania kwani hata huko ulaya kuna hospitali za serikali na private.Kuhusu kumwambia aje agombee uongozi yeye mwenyewe labda anaona hiyo siyo fani yake ingekuwa fani yake angegombea. Kwanza akigombea si mtaanza oo mara ana tamaa wabongo maneno mengi vitendo haba. Kwa mtaji huu CCM itatawala na kufanya inavyotaka mpaka mwisho wa Dunia kwani asilimia kubwa ya wabongo ni watumwa wa fikra na hawataki kuusumbua ubongo wao ndiyo maana wanaishi maisha ya karne ya 17 na hawana wasiwasi

Anonymous said...

Nami nakubaliana na Nizar Dr. Mbele angeenda mwananyamala au Hospitali ambazo watanzania wa ukweli wanatibiwa kwa kweli tungemuelewa kweli huduma zikoje? Hapo bado ni sawa na kwenda nje ya nchi.
Issue ni kuwa siyo madaktari wetu hawafanyi kazi bali wanazidiwa na kazi, hakuna dawa za kutosha na pia hospitali hziko kwenye viwango vinavyotakiwa na madaktari wapo wachache sana na la mwisho serikari haiwajali madaktari wake.