**************************************************************
Mkapa Apigwa Kombora
VITA ya maneno, vijembe na kejeli kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na• Ahusishwa na kifo chenye utata cha Mwalimu Nyerere
na Mwandishi wetu, Arumeru
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika kampeni za
uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani
Arusha imeanza.
Baada ya juzi Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kufanya uzinduzi wa
kampeni za CCM na kuipiga vijembe CHADEMA, chama hicho jana kilijibu
mapigo kupitia kwa Mbunge wa Msoma Mjini, Vincent Nyerere, ambaye ni
Naibu Meneja wa Kampeni wa CHADEMA.
Akizungumza katika mikutano ya kampeni maeneo mbalimbali, mbunge huyo
alishusha tuhuma nzito juu ya kile alichokiita ‘utata’ wa kifo cha
Mwalimu Nyerere huku akihusisha na maamuzi ya Mkapa kung’ang’ania
Mwalimu aende kutibiwa Uingereza baada ya kuanza kumkosoa juu ya sera
za ubinafsishaji.
Nyerere ambaye ni mmoja wa wanafamilia wa hayati Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere, akiwa amekulia katika familia hiyo, aliwaambia
wananchi wa maeneo hayo kuwa umefika wakati sasa Mkapa atoke hadharani
afafanue alikuwa na nia gani kumlazimisha Mwalimu Nyerere akatibiwe
Uingereza wakati mwenyewe alikuwa amekataa, akisema kuwa ugonjwa
uliokuwa unamsumbua tayari ulikuwa unajulikana na daktari wake,
Profesa David Mwakyusa, alikuwa tayari akimhudumia vizuri bila tatizo.
“Jana katika hotuba yake ametumia muda mwingi sana kuisema CHADEMA na
akanisema mimi kwa jina moja kwa moja, sasa ‘kanibipu’ na mimi
nimeamua kumpigia, tunamtaka kama anaweza arudi hapa Arumeru, aje
ajibu maswali ya msingi juu ya ufisadi unaomwandama. Alianza kwa kuuza
mashirika ya umma, akauza viwanda, ukienda leo miji mikubwa kama Dar
es Salaam na kwingineko, vijana wengi wamegeuka kuwa waokota makopo
kwa sababu hakuna ajira, viwanda viliuawa wakati wa Mkapa.
“Kwa kupitia sera yake ya ubinafsishaji akauza kila kitu, akauza
viwanda, wawekezaji walionunua nao wakafanya ufisadi wamegeuza viwanda
hivyo kuwa maghala ya kutunzia vitu vyao, viwanda ambavyo vingeweza
kuajiri vijana Watanzania vikauzwa kiholela kwa bei ya kutupa, vingine
wakajiuzia wao wenyewe. Misingi iliyowekwa na Mwalimu yote ikabomolewa
badala ya wao kujenga nyumba juu ya misingi hiyo.
“Mashirika yaliyokuwa yakifanya kazi vizuri au ambayo yalihitaji
usimamizi tu mzuri ili yafanye vizuri yakauzwa kiholela, yakauzwa
kifisadi, tena mkumbuke alianza kwa kuuza benki. Mwalimu kuona hivyo
akashtuka, akaanza kumhoji na kumkosoa hadharani juu ya sera yake
hiyo, jamaa (Mkapa) kuona hivyo akaona huu sasa ni usumbufu, akaanza
kumshawishi Mwalimu aende akatibiwe Uingereza, Mwalimu alikataa kabisa
akisema kuwa ugonjwa unaomsumbua tayari daktari wake anamhudumia
vema,” alisema Nyerere na kuongeza:
“Mwalimu alikuwa akihoji inakuwaje reli inakufa, yeye amekazana tu na
ubinafsishaji, Mwalimu akahoji inakuwaje anatoza kodi kibao na kutunza
pesa, kumbe Mkapa tayari alikuwa anaandaa pesa za EPA ambazo baadaye
ndizo mlizisikia kupitia kashfa maarufu ya mabilioni ya EPA. Mkapa
akamng’ang’ania Mwalimua akatibiwe Uingereza, akasema naye ni mmoja wa
wanafamilia yetu, basi tukakubali, lakini mnajua kuwa Mwalimu
alikwenda anatembea akarudi amenyamaza ndani ya jeneza?
“Sasa Mkapa atuambie ukweli juu ya hili, aje ajibu maswali yote haya,
nitakuja na vigongo vingine, lazima tupambane na ufisadi hadi mwisho.
Ilifikia mahali hata taarifa za ugonjwa akawa anatoa yeye Mkapa, oooh
mara Mwalimu amepatwa na mkanda wa jeshi, mara oooh leo imekuwa hivi,
badala ya daktari wake. Baada ya Mwalimu kufariki dunia, wakamwambia
yule daktari wake agombee ubunge watampatia uwaziri, ndivyo
ilivyotokea,” alisema Nyerere.
Aliongeza kusema kuwa pamoja na uhakika wa maisha yake baada ya
kustaafu ambapo anagharimiwa kila kitu kwa kodi za Watanzania, bado
Rais Mkapa alijimilikisha mgodi wa Kiwira ambao baada ya kelele nyingi
za nguvu za umma, zikiongozwa na CHADEMA bungeni na nje ya Bunge,
hatimaye umerudishwa kwa umma.
Alimtaka Rais Mkapa kujibu tuhuma juu ya ufisadi katika ununuaji wa
ndege, wakati tayari serikali ilikuwa na ndege nyingine mbili, moja
ikinunuliwa wakati wa Mwalimu na ina uhakika wa kufanya kazi kwa miaka
100 iwapo ingefanyiwa matengenezo kadiri inavyotakiwa.
Pia akamtaka kujibu hoja za Watanzania juu ya ufisadi wa rada, ambao
hata Waingereza wanaupigia kelele, baada ya yeye na wenzake serikalini
kufanya ‘dili’ kujinufaisha wao badala ya kuongoza wananchi.
Nyerere aliongeza tuhuma kwa Mkapa akisema kuwa pia anatakiwa kujibu
hoja juu ya mauaji ya Zanzibar ya mwaka 2001, ambapo kwa mara ya
kwanza Tanzania mbali ya serikali kuua raia wake kwa risasi,
ilizalisha wakimbizi kwenda nchi za Kenya na Somalia.
Akifafanua tuhuma za ufisadi dhidi ya Rais Mkapa, mbunge huyo alisema
kuwa kama Mkapa anataka kueleweka mbele ya Watanzania wenye uchungu na
nchi yao, anatakiwa kujibu hoja za msingi juu ya tuhuma hizo za
ufisadi zinazomwandama tangu akiwa madarakani hadi anastaafu.
Mbunge huyo ambaye alikuwa akihutubia mamia ya wakazi wa maeneo ya
Lenguruki, Poli, Sing’isia na Nkoaranga, alisema kuwa rais huyo
mstaafu anapaswa kuwa mmoja wa watu wa mwisho kusimama mbele za watu
kwani hali inayolikabili taifa kwa sasa, ikiwamo ufisadi uliotapakaa
ndani ya chama chake na serikali ya CCM, iliasisiwa tangu wakati wa
utawala wake, kwa kuanzia na sera za ubinafsishaji zilizoua misingi ya
viwanda iliyowekwa na Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wake, mgombea wa CHADEMA Joshua Nassari, alisema kuwa
amegombea kwa nia ya kubeba ‘mizigo’ ya wana wa Arumeru kwani
anaitambua, hivyo yuko tayari kuibeba kwenda nayo bungeni Dodoma na
katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru, kuwasemea na kuiwajibisha
serikali ili iwajibike kwa wananchi.
Joshua alionekana kuwagusa wananchi wa maeneo hayo pale alipokuwa
akizungumzia kero za kila eneo husika, kama vile ardhi, maji, afya na
elimu na namna ambavyo wanaweza kushirikiana pamoja na mbunge wao
katika kuyatatua, iwapo watamchagua yeye ambaye amezaliwa na kukulia
katika maeneo hayo na yuko tayari kuwatumikia akiwa anaishi katika
maeneo ambayo wanaishi wao pia.
Aliwataka watu wa Meru wasidanganyike na maneno ya Mkapa kuwa
atakwenda kumshauri Rais Jakaya Kikwete ashughulikie matatizo ya ardhi
katika wilaya hiyo, kwani alishindwa kufanya hivyo wakati akiwa na
mamlaka ya urais, hawezi kuifanya kazi hiyo kwa sasa kwani rais ana
hiari ya kukubali au kukataa ushauri wa mtu yeyote kwa mujibu wa
katiba yetu mbovu.
“Kwa mujibu wa katiba yetu mbovu ambayo tunataka tuiandike upya, rais
halazimiki kuchukua ushauri wa mtu yeyote, hivyo Kikwete anaweza
kukataa ushauri wake huyo Mkapa, aje ajibu hoja hapa kwa nini
alishindwa kutatua matatizo ya ardhi kwa watu wa Arumeru wakati akiwa
madarakani?” alihoji Nyerere.
CHANZO: Tanzania Daima 14 Machi 2012
10 comments:
jamani mnafanya makosa makubwa sana kwa kuhoji hoja ya vincent nyerere.
kwanza jambo linaloibuliwa sasa si ukosefu wa adabu kwa mkapa. ipo hoja ya maana kuwa ilikuwaje mtu mwenye afya karibu na mzima kaondoka anatembea na ghafula katika kipindi cha siku nne au tano akawa mahututi na kurejeshwa kwenye jeneza?
pili ipo hoja ya yerere na mkapa kudiffer kuhusu ubinafsishaji siyo siri. nyerere aliquestion busara ya kubinafsisha mashirika na makampuni yaliyokuwa yanajiendesha na akahoji uuzwaji wa nbc na ghafla akapelekwa nje kutibiwa.
tatu hii ni mara ya kwanza mtu kutoka familia ya nyerere anahoji utaratibu uliofuatwa kwenye matibabu ya mwalimu - very interesting na hatupaswi kusema ni utovu wa nidhamu kwa sababu kuna hoja inaibuliwa kazi yetu ni kutafakari.
nne mkapa akiwa mwanasiasa anapaswa kujibu hoja zote zinazoelekezwa kwake siyo tu kuishia kusema "ni uongo, uongo na uongo mtupu" bila kusema ukweli ni upi. alijibinafsishia kiwira haipingiki hiyo, alipewa mkopo na nbc wakati inabinafsishwa na akarudisha ndani ya miezi bila kueleza alipataje fedha za kulipa au alifanya biashara gani ikulu ndipo akalipa kama si hongo ni nini?
hapa tusiseme kuna utovu wa nidhamu badala yake tumsifu aliyeibuwa hoja zinazojadilika. fulstop.
Kwa mwafrika, hakuna kifo kisichokuwa na mkono wa mtu! Hata Nyerere alisingiziwa kuwa alimuua Sokoine kuhofia nguvu zake na kuwaasa waTz kuamini kuwa Sokoine kafa kwa ajali!
Ina maana walim KOLIMBA Mwalimu?
Kila jambo na wakati wake. Kuna wakati wa kunyamaza na wakati wa kusema. Yule dada Mmarekani aliyefanya mapenzi na rais wa Marekani alikaa miaka yote hadi sasa wakati ulipofika na kuandika kitabu. Kuna wakati wa siri na wakati wa siri kutobolewa. Kusema sasa hakuondoi uhalali wa jambo. Hata watoto wanaolawitiwa na viongozi wa dini hunyamaza hadi wakati wa kufichua siri unapofika. Kwa hiyo mimi simlaumu kijana kuwa na hasira kwa jinsi alivyosemwa. Vita haichagui ndio maana wakati enzi za zamani mtu aliyeoa karibuni haruhisiwa kwenda vitani maana mshali hauchagui mtu. Vivyo hivyo nchi kama Marekani hawawezi kumpeleka mtoto mmoja kwenye famila kwenda vitani maana wanajua hiyo siri kwamba risasi haisemi kuwa huyo ni mwana wa pekee. Ndio wakasema vita havina macho!
Hivi kumhusisha Mkapa na kifo cha Nyerere au kutaja madhambi yake kutaisaidia vipi Chadema kushinda Arumeru? Naona Chadema wamemshupalia Mkapa bila kueleza watawafanyia nini watu wa Arumeru endapo mgombea wao atachaguliwa.
Hivi CCM ilikosa kabisa mtu wa kufungua Kampeni zao....?
Mara nyingi hawa vijana wananishangaza sana. Mshangao mkubwa hasa unakuja unapoona wale ambao kihalisia wamefaidi matunda ya nchi hii, walioona jinsi ndugu zao walisaidiwa kwa jasho la watanzania, wale waliolelewa katika misingi ya Uzalendo na Utaifa wanaanza kukengeuka. Mtizamo wangu ni kwamba hawafai (kwa lugha ya kiungwana tu). Tuhuma kama hii ni nzito kwa kijana aliyelelewa katika misingi ya kitaifa hangestahili kuyasema haya. Ni kwa vile alikuwa huenda mtoto mchanga hakujua kilichokuwa kikiendelea. Kwake tukio la kifo Baba wa Taifa ilikuwa kama hadithi ya mtoto mmoja aliyekwenda kwenye msiba wa jirani yao, alimkuta mtoto wa marehemu akiwa na wali, alipomuomba naye apatiwe wali yule mtoto wa marehemu akakataa ndipo yule mtoto akamwambia hivi " Na mimi baba yangu akifa nitakunyima wali".
Mtoto katika mfano huu kimsingi hakujua maana ya tukio lile alichoona ni wali tu. Huyu kaona Ubunge tu wa ARUMERU wala hakujua kilichotokea na sidhani kama kwa matamshi haya ana haja ya kujua kilichoendelea.
Kwetu kuna methali kwamba "Mchuzi usiofaa kulia viazi haufai hata kumpa mbwa".Kama watu wenyewe ni wa aina hii hii tu, hapana hata uongozi wa nyumba kumi hawafai. Mkapa aliyeweka juhudi kubwa za kukusanya kodi wakati anashika uongozi tulikuwa tunakusanya Shs: 28.00 Bil kwa mwezi hadi wakati anang'atuka kwenye uongozi tulikuwa tunakusanya zaidi ya shs: 180.00 Bil.
Wakati anachukua nchi ilikuwa haikopesheki lakini akarejesha heshima na tukaanza kukopesheka. Hata hivyo kwa busara ya kawaida sioni sababu ya Mkapa kujibu upuuzi huu. Mimi nawasamehe pia.
Mdau wa Mchuzi Usiofaa umepitwa nawakati,maovu ya Mkapa ulimwengu mzima unajua.Kukusanya kodi Mamilioni na kuzitumia[kuzifisadi]hesabu hiyo haina kichwa wala miguu.Mashirika aliyoyauza,mashamba,mabemki na mauaji ya Mgodi wa Geita nk ni Ufisadi ni kwa vile Bongo kuna kulindana ukweli Mkapa anastahiki Kushitakiwa kama vile Chiluba wa Zambia.Kumbuka hakuna mtu aliye juu ya Sheria.Wakati umefika wa kubadilisha Katiba Mbovu iliyopitwa na Wakati.
Jamani siasa za Tanzania zimekuwa very complex katika miaka ya karibuni. Vincent Nyerere amemshambulia vibaya sana Benjamin Mkapa na by extension CCM. Lakini asichoelewa Vincent ni ukweli kwamba baadhi ya viongozi wa ngazi za juu Chadema wamepakatwa na mafisadi ndani ya CCM na ndio maana huwezi kuwasikia hata siku moja wakiwasema vibaya watu hawa hadharani.
Huyu jamaa jiona lake ni Vincent Kiboko. Huu "uNyerere" amechipachiuka tu.
Post a Comment