TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za pole Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange kufuatia kifo cha Meja Jenerali Anatory Ruta Kamazima (Mstaafu) aliyefariki jana tarehe 25 Septemba, 2012 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Nimepokea kwa mshituko na huzuni nyingi habari za kifo cha Meja Jenerali Kamazima, ni pigo kubwa sana kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Taifa kwa ujumla” Rais amesema katika salamu hizo.
Mchana wa leo Rais ameitembelea familia ya marehemu nyumbani kwao Tegeta kuwafariji wafiwa.
Marehemu alizaliwa mwaka 1946 katika kijiji cha Maruku, Mkoani Kagera. Alijiunga na Jeshi mwaka 1967, mara baada ya kuhitimu Chuo Kikuu mwaka 1966.
Marehemu Kamazima amesoma kozi mbalimbali za kijeshi hapa nchini na nchi za China, India, Uingereza na Misri na kulitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika ngazi mbalimbali ambapo mwaka 1989, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Kuzuia Rushwa Tanzania, hadi alipostaafu Juni 2003.
Rais amemuelezea marehemu Kamazima kama mzalendo na mtu aliyeipenda na kuitumikia nchi yake kwa weledi mkubwa, uaminifu na moyo mmoja.
“Nimemfahamu Marehemu kwa miaka yote ya utumishi wake jeshini na serikalini kama mzalendo, muaminifu na mwenye moyo wa kulinda nchi yake wakati wote” amesema “Marehemu Kamazima alikua mtu wa kutumainiwa sana katika nchi yetu na kamwe hatutamsahau kwa utumishi wake uliotukuka”.
“Tutamkumbuka na kumuenzi siku zote, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote na tunamuombea mapumziko mema Marehemu Kamazima. Amina”. Rais ameongeza.
Marehemu ameacha mjane, watoto na wajukuu.
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu.
DAR ES SALAAM
26 Septemba, 2012
*************************************************************************
Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akitoa pole kwa mjane na ndugu wa wa Meja Jenerali Mstaafu Anatoli Kamazima leo nyumbani kwa marehemu Tegeta, Dar es salaam. Marehemu Kamazima, ambaye amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumatano ya Tarehe 26 Septemba, 2012 utokana na mshtuko wa moyo, alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU.
Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Brigedia Jenerali Mstaafu Tindamanyire, ndugu wa hayati Meja Jenerali Mstaafu Anatoli Kamazima, leo nyumbani kwa marehemu Tegeta, Dar es salaam. Kulia kwa Rais ni Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange na Mnadhimu Mkuu Luteni Jenerali Samwel Albert Ndomba. Marehemu Kamazima, ambaye amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumatano ya Tarehe 26 Septemba, 2012 utokana na mshtuko wa moyo, alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU.
PICHA NA IKULU
No comments:
Post a Comment