PRESS RELEASE
Ndugu
Zitto ziarani Ulaya
Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Naibu Kiongozi wa
Upinzani Bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini ndugu Zitto Zuberi Kabwe ameanza
ziara ya kikazi nchini Ujerumani ambapo atahudhuria na kuhutubia Mkutano mkubwa
wa masuala ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Africa. Mkutano huo
“Economic Conference: Commitment to Africa Initiative” utafanyika Jijini Berlin
kuanzia tarehe 9 – 11 Desemba 2012 na umeandaliwa na Wizara ya Ushirikiano wa
Kimaendeleo ya Serikali ya Ujerumani.
Katika ufunguzi wa Mkutano huo ndugu Zitto atatoa
mada kuhusu mgongano wa maslahi kati ya Kampuni binafsi na Jamii ambapo
ataongelea suala zima la makampuni makubwa ya kimataifa yanavyonyonya
rasilimali za Afrika bila kuwajibika kulipa kodi na kuendeleza jamii
zinazozunguka shughuli zao. Atazungumzia pia mitaji kiduchu inayokuja Afrika na
fedha nyingi inayotoroshwa Afrika kupitia rushwa, ukwepaji kodi na wizi wa
rasilimali. Afrika inapoteza zaidi ya dola za kimarekani 583 bilioni kila mwaka
kutokana na utoroshaji wa fedha unaofanywa na makampuni ya kimataifa kwa
kushirikiana na baadhi ya viongozi wa Afrika. Hata hivyo Afrika inapokea
takribani dola za Kimarekani 80 bilioni tu kwa mwaka kutokana na Uwekezaji
(FDI) na Misaada (foreign Aid). Tanzania ni moja ya nchi inayopokea misaada
mingi kutoka nje na moja ya nchi ambayo rasilimali zake zinatoroshwa na baadhi
ya viongozi wake kutorosha fedha na kuzihifadhi kwenye mabenki ya Ulaya kama
Uswiss.
Mnamo tarehe 11 Desemba ndugu Zitto atakuwa kwenye
jukwaa moja na Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani kuzungumzia namna bora ya
kushirikiana kati ya Ujerumani na nchi za Kiafrika. Miongoni mwa mapendekezo ya
Zitto ni kuondokana na mfumo wa sasa wa ushirikiano wa misaada na badala yake
kuwe na ushirikiano wa kujengeana uwezo ili kila nchi iweze kuhimili maendeleo
yake yenyewe.
Katika ziara hii Zitto atakutana na Mawaziri Wakuu
wa majimbo ya Nord Rhein Westphalen jimbo ambalo limefanikiwa sana katika vita
dhidi ya ukwepaji kodi unaotokana na raia wa Ujerumani kuficha fedha kwenye
mabenki ya Uswiss na wa jimbo la Lower Saxony kwa ajili ya mazungumzo kuhusu
ukarabati wa Meli ya Liemba na kujenga mahusiano kati ya Mkoa huu na Mkoa wa
Kigoma pia kati ya mji wa PapenBurg na Manispaa ya Kigoma.
Zitto anatarajiwa kutembelea baadhi ya nchi
nyingine za Ulaya na kukutana na watu mbalimbali katika kuimarisha mtandao wa
kimataifa dhidi ya utoroshaji wa fedha kutoka Afrika (illicit money transfer).
Pia atakutana na watu binafsi wenye ujuzi na weledi katika masuala haya ya
kupambana na watoroshaji wa fedha. Zitto anataraji kurudi nchini mnamo tarehe
16 Desemba 2012. Kwa namna itaakavyowezekana umma utapewa taarifa kuhusu ziara
hii kupitia akaunti ya twitter na facebook ya ndugu Zitto. Pia mada zote
atakazowasilisha zitawekwa kwenye blogu ya zittokabwe.com
kila itakapowezekana.
Waziri Kivuli wa Fedha na Naibu Kiongozi wa
Upinzani Bungeni anawatakia Watanzania wote kila la kheri katika Sikukuu ya
Uhuru wa Tanzania Bara. Utu, Uzalendo, Uadilifu na Uwajibikaji ni silaha muhimu
sana za kujenga Taifa lenye heshima na jamii ya watu wenye fursa za kuendeleza
maisha yao kwa haki na amani. Tutimize wajibu wetu katika kuijenga Tanzania
tuitakayo kwa ajili yetu na kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Imetolewa na Ofisi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini
8 Desemba 2012, Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment