HISTORIA YA CCM TANGU TANU NA ASP
Imetolewa
na Idara ya Itikadi na Uenezi kwa ajili ya Semina za Halmashauri Kuu za
Taifa, Mikoa na Wilaya. Inapatikana pia katika kitabu cha Sera za
Msingi za CCM
Makao Makuu ya CCM
Dodoma, 2004
HISTORIA YA CCM TANGU TANU NA ASP
1.0 UTANGULIZI:
Maelezo ya awali
Chama
cha Mapinduzi (CCM) kilizaliwa tarehe 5 Februari, 1977 kutokana na
kuvunjwa kwa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na
Afro-Shirazi Party (ASP).
Tendo hilo la
kihistoria lilikuwa ni la kuendeleza utamaduni uliokuwa umeanza huko
nyuma wa kuunganisha nguvu kwa lengo la kujiimarisha katika mapambano.
Kwa mfano, ASP kwa upande wa Zanzibar ilitokana na kuungana kwa African
Association (AA) na Shirazi Association (SA), tendo ambalo liliunganisha
nguvu za wanyonge katika mapambano ya kuundoa usultani na utawala wa
kikoloni wa Kiingereza. Kwa upande wa Tanzania Bara, TANU ilitokana na
kujibadilisha kwa Tanganyika African Association (TAA) kutoka jumuiya ya
kutetea maslahi ya kijamii na kuwa chama cha siasa.
Kupatikana
kwa uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Desemba, 1961 na ule wa Zanzibar
kupitia Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964, kulifanya TANU na ASP viwe
vimekamilisha jukumu la ukombozi wa nchi hizi kutoka makucha ya ukoloni
mkongwe na usultani. Hata hivyo, vyama vya siasa hivi viliendelea
kukabiliwa na majukumu ya kuendeleza mapambano ya ukombozi katika Afrika
na kote duniani; kujenga Tanganyika na Zanzibar huru kiuchumi na
kijamii na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa,
Katika
mazingira ya ubeberu duniani wakati huo na hali ya unyonge wa mataifa
haya machanga, yakielewa kuwa ‘umoja ni nguvu’, Tanganyika na Zanzibar
zilibaini umuhimu wa muungano, hivyo ziliamua kuungana tarehe 26 Aprili,
1964. Muungano huo ndio uliowezesha kuzaliwa kwa Tanzania. Chini ya
Muungano huo, Tanzania iliendelea kuwa na vyama vya siasa viwili, yaani
TANU na ASP katika mazingira ya chama kimoja cha siasa. Vyama hivi
vilitambua fika kwamba vinahitaji chombo madhubuti cha uongozi katika
kutekeleza majukumu yake ya ukombozi kwa ukamilifu hivyo uamuzi
ulifanywa rasmi wa kuvunja TANU na ASP na kuundwa kwa Chama Cha
Mapinduzi tarehe 5 Februari, 1977.
Katiba ya
CCM, katika Azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa wa Pamoja wa TANU na ASP
tarehe 21 January, 1977, inaeleza kuwa, (uk. 2-3), “...kwa kauli moja
tunaamua na kutamka rasmi kuvunjwa kwa Tanganyika African Union(TANU) na
Afro-Shirazi Party (ASP) ifikapo tarehe 5 Februari, 1977 na wakati
huohuo kuundwa kwa Chama kipya cha pekee na chenye uwezo wa mwisho
katika mambo yote kwa mujibu wa Katiba.”
Muungano
wa TANU na ASP ndio uliowezesha CCM kuwa Chama chenye nguvu, imara na
madhubuti, hivyo kuwa Chama cha siasa pekee chenye uwezo wa hali ya juu
wa kuwaunganisha Watanzania. Aidha, CCM kimeweza kuwaongoza wananchi
katika mapambano ya kitaifa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kufuatana na
mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza ndani na nje ya nchi.CCM
kimeendelea kupewa dhamana na wananchi ya kuunda serikali na kukamata
dola tangu 1977 chini ya mfumo wa demokrasia ya chama kimoja hadi sasa
katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, kufuatia mageuzi
yaliyoidhinishwa na marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Tanzania Juni
1992.
1.2 Umuhimu wa kuielewa historia ya CCM na Vyama vilivyokitangulia
Historia
ya CCM tangu TANU na ASP ina umuhimu wa pekee katika Taifa letu katika
kuelewa tulikotoka, tulipo hivi sasa na tunakoelekea. Historia ya nchi
yetu haiwezi kukamilika bila ya historia ya vyama hivi vya ukombozi.
Historia hutoa mafunzo na ni mwelekezaji pia, kwa hiyo ni wajibu wa
Watanzania, hasa wanachama wa CCM kujifunza kutokana na historia yetu.
Kazi kubwa na ya msingi inayofanyika katika kujifunza historia hiyo, ni
kurithisha dhamira ya kujituma na kudumisha uhuru wa nchi yetu. Hivyo,
ili kuendelea kukijenga Chama, na kuimarisha uwezo wa kuendelea kukamata
dola barabara kwa namna endelevu, hapana budi ihakikishwe kuwa historia
ya CCM inabeba pia jukumu la msingi la kusaidia:-
Kujua Chama kilikotoka, mahali kilipo na kinakoelekea katika misingi ya sera, itikadi, malengo na wanachama.
Kuunganisha wanachama na kuwaweka pamoja kiimani, kiitikadi na kiutendaji.
Wanachama kujitambua, kutambua wajibu na majukumu yao na kujenga moyo wa kujiamini na kujithamini.
Kuinua
kiwango cha ushiriki wa wanachama wa CCM na wananchi katika kubuni na
kutekeleza mkakati na mbinu sahihi za kutetea na kuendeleza Chama na
taifa kufuatana na hali ya wakati na mahali.
Kuweka misingi ya kufanya tathmini na hivyo kuwa na uhakika katika kufanya maamuzi.
Kupanda mbegu bora za upendo, uzalendo na uchungu wa kweli kwa uhai wa CCM na taifa kwa ujumla.
Kuwa na majibu sahihi wakati wote kwa hoja mbalimbali zinazotolewa kuhusu Chama Cha Mapinduzi na taifa kwa ujumla.
Kuweka msingi wa kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine maadili ya msingi wa uhai wa CCM.
Kuhifadhi
kuweka na kueneza kumbukumbu sahihi ya historia ya Chama, nchi, mchango
wa Waasisi na wanachama na kuhakikisha wapotoshaji hawapati fursa ya
kueneza uongo.
1.3 CHIMBUKO LA HISTORIA YA CCM
Pamoja
na kwamba Chama Cha Mapinduzi kuwa kilizaliwa rasmi tarehe 5 Februari,
1977, chimbuko lake linaanzia miaka mingi kabla, sambamba na historia ya
uhai wa taifa la Tanzania. Mizizi ya historia ya CCM imo ndani ya
harakati za kukataa ukoloni na usultani, zilizofanywa na wananchi wa
Tanzania. Wahenga wetu kwa pamoja tangu enzi, walionyesha wazi kukataa
kwao kutawaliwa. Historia ya Tanzania inao utajiri wa mifano mingi ya
harakati hizo japokuwa zilijengwa katika misingi ya ukoo na ujirani,
katika wilaya na mikoa mbalimbali hata kabla ya kuundwa kwa vyama vya
TANU na ASP.
Wananchi hao waliotutangulia
walikataa kunyonywa, kupuuzwa, kubaguliwa, kutawaliwa, kunyanyaswa na
kugawanywa katika misingi ya rangi, kabila, dini, jinsia, nk. Utu na
uhuru wao ulikuwa na thamani kubwa sana. Hivyo waliamua kupambana dhidi
ya udhalimu huo. Baadhi ya mifano ya jitihada za mapambano ya awali ni
Vita ya Majimaji huko Umatumbi na maeneo ya kusini, Mbiru huko Upare,
Waluguru, Wameru, Wahehe na mengineyo huko Unguja, Pemba, Kanda ya Ziwa
na katika jamii za wafugaji. Ari, utashi, uzalendo na dhamira ya kweli
ya kutaka kujitawala vilivyojidhihirisha katika harakati hizo,
viliotesha mizizi iliyoshikilia uhai wa vyama vya TANU na ASP.
2.0 TANU NA HARAKATI ZA KUPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA
2.1 TANU ilizaliwa katika mazingira yaliyoandaliwa na Tanganyika African Association (TAA):
TAA
iliundwa 1948 kufuatia tukio la kutengana kwa African Association (AA)
ya Tanganyika na Zanzibar. AA ilizaliwa Dar es Salaam 1927 chini ya
uongozi wa Cecil Matola akiwa Rais na Kleist P. Sykes akiwa Katibu.
Malengo ya AA yalikuwa ni kupigania haki, maslahi na umoja wa Waafrika.
AA ilikuwa na matawi yake makuu Dodoma na Zanzibar. Aidha, AA ilifungua
matawi katika miji iliyokuwa makao makuu ya wilaya.
Katiba
ya TAA ilitamka wazi kwamba Chama hicho hakikuwa na malengo ya kisiasa.
Mwaka 1953 yalifanyika mabadiliko ya uongozi katika TAA. Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere alichaguliwa kuwa Rais wa TAA. Chini ya uongozi mpya,
Katiba ya TAA ilionekana kwamba isingeweza kukidhi malengo ya kisiasa.
Mwalimu alipewa jukumu la kuandaa Katiba mpya ya TAA ambayo ingezingatia
malengo ya kisiasa. Baada ya uandaaji wa Katiba hiyo kukamilika, haja
ya kubadili jina ilionekana dhahiri na majina mengi yalipendekezwa
likiwemo la TANU. Nafasi ya TAA ilichukuliwa na TANU iliyozaliwa tarehe 7
Julai, 1954. TANU ilirithi matawi ya TAA, wanachama na viongozi wa TAA
katika maeneo mengi.
Waasisi wa TANU ambao walihudhuria na kushiriki katika Mkutano wa kuzaliwa kwa TANU walikuwa 17:
Mwalimu J.K. Nyerere – Rais wa TAA/TANU
Geremano Pacha – Jimbo la Magharibi
Joseph Kimalando – Jimbo la Kaskazini
Japhet Kirilo – Jimbo la Kaskazini
C.O. Milinga – Jimbo la Mashariki
Abubakari llanga – Jimbo la Ziwa
L.B. Makaranga – Jimbo la Ziwa
Saadani A. Kandoro – Jimbo la Ziwa
Suleman M. Kitwara – Jimbo la Ziwa
Kisung’uta Gabara – Jimbo la Ziwa
Tewa Said Tewa – Jimbo la Mashariki
Dossa A. Aziz – Jimbo la Mashariki
Abdu Sykes – Jimbo la Mashariki
Patrick Kunambi – Jimbo la Mashariki
Joseph K. Bantu – Jimbo la Mashariki
Ally Sykes – Jimbo la Mashariki
John Rupia – Jimbo la Mashariki
TANU ilizaliwa baada ya Vita ya Pili ya Dunia:
Katika
vita ya Pili ya Dunia (1939 – 1945), Watanganyika walishiriki wakiwa
askari upande wa Waingereza. Katika kushiriki huko, baadhi yao
walipigana vita nchi za nje, kwa mfano, India, Burma, Madagascar n.k.
Wakiwa huko vitani walipata fursa ya kubadilishana mawazo ya kisiasa na
askari wenzao waliokutana nao katika uwanja wa vita.
Baadhi
ya askari hao wa Tanganyika waliporejea kutoka vitani walikuja na fikra
mpya za ukombozi wa Mwafrika. Fikra hizi mpya zilioana na zile za Kituo
cha Wasomi wa Kiafrika waliokuwa London. Kituo hicho kilijishughulisha
sana na suala la ukombozi wa Mwafrika kupitia midahalo.
TANU ilizaliwa katika mazingira ya vyama vya ushirika:
Katika
miaka 1950, wakulima walikwishajiunga na kuanzisha vyama vya kuuza
mazao yao ya biashara ili waweze kupata bei nzuri kwa kupunguza gharama
ya mtu wa kati ambaye alikuwa ni mfanyabiashara wa Kiasia. Baadhi ya
Vyama vya Ushirika vilivyokuwepo kabla ya TANU ni:-
Kilimanjaro Co-operative Union Ltd (1933)
Ngoni – Matengo Co-operative Union Ltd. (1936)
Rungwe African Co-operative Union Ltd. (1949)
Bukoba Co-operative Union Ltd. (1950)
Lake Province Native Growers Association.
Kwa
kuwepo vyama vya ushirika, ujumbe wa TANU kuwafikia wananchi
ulirahisishwa. Wanachama wa vyama vya ushirika walijiunga na TANU.
Wanachama na viongozi wa vyama vya ushirika waliunga mkono TANU katika
madai yake ya kudai uhuru. Baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika
walichaguliwa kuwa viongozi wa TANU katika ngazi ya Taifa. Kwa mfano:-
Ndugu Nsilo Swai
Sir George Kahama
Ndugu Jeremiah Kasambala
Balozi Paul Bomani
Ndugu John Mhavile.
TANU
nayo iliunga mkono vyama vya ushirika katika madai yake ya bei nzuri ya
mazao yao na kuondoa ushuru wa kahawa uliokuwa unatozwa na Serikali
Kuu. Aidha, TANU ilihimiza na kuwahamasisha wananchi kuanzisha na
kuimarisha vyama vya ushirika. Kazi hii ya kuhimiza na kuhamasisha
wananchi kujiunga na ushirika iliendelea kufanywa na TANU hata baada ya
Tanganyika kupata uhuru wake.
Baada ya Uhuru,
TANU iliuona ushirika kuwa ni chombo cha kuleta maendeleo hivyo wananchi
walihimizwa kuanzisha ushirika katika maeneo ambayo hayakuwa na vyama
vya ushirika. Hali hii inaendelea hadi hivi sasa ambapo katika mfumo wa
uchumi wa Soko, CCM inauona ushirika kuwa ni chombo cha kumwezesha
mwananchi kiuchumi katika kumiliki na kuendesha uchumi wa Taifa lake
TANU ilizaliwa katika mazingira ya vyama vya wafanyakazi:
Lengo kuu la Vyama vya Wafanyakazi lilikuwa ni kutetea maslahi ya wafanyakazi. Baadhi ya vyama vya wafanyakazi ni:-
Chama cha Wafanyakazi Serikalini (1929)
Chama cha Makuli (1937)
Chama cha Wapishi na Madobi (1939)
Chama cha Wapishi na Watumishi wa Ndani
Chama cha Madereva
Chama cha Walimu
Chama cha Wafanyakazi wa Reli
Chama cha Wafanyakazi Mashambani
Chama cha Wafanyakazi Viwandani.
Vyama
vya Wafanyakazi viliunda Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
(Tanganyika Federation of Labour –TFL) tarehe 10 Oktoba, 1955.
Wafanyakazi kupitia vyama vyao walikuwa na madai yafuatayo:-
nyongeza ya mshahara
mapumziko ya mchana siku ya kazi
umri wa kustaafu na
kuondoa ubaguzi katika ajira na huduma za jamii.
Vyama
vya wafayakazi vilisaidia kuvunja ukabila na hivyo kuwa chanzo cha
umoja. Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi lilisaidia kueneza TANU kwa
njia zifuatazo:-
Kila Chama cha Wafanyakazi
chini ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TFL) kilitakiwa
kuwashawishi na kuwahimiza wanachama wake kujiunga na TANU.
Kila mwanachama wa TANU aliyekuwa mwanachama wa Chama cha Wafanyakazi alitakiwa kulipa mchango wake wa kila mwezi kwa TANU.
Vyama vya Wafanyakazi, wakati mwingine kupitia TFL, viliweza kusaidia TANU kifedha fedha hizo zilitokana na michango ya hiari.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi lilisaidia sana kuleta mwamko wa kisiasa miongoni mwa wafanyakazi.
Vyama vya Wafanyakazi vilifanya yote hayo kwa kuelewa kwamba uhuru ndio ungekuwa suluhisho la kweli la matatizo yao.
Kama
ilivyokuwa kwa vyama vya ushirika, baadhi ya viongozi wa vyama vya
wafanyakazi walichaguliwa kuwa viongozi wa TANU. Mwaka 1958, Katibu Mkuu
wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Mzee Rashid Mfaume Kawawa,
alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU. Toka
wakati huo hadi hivi sasa, Mzee Kawawa amekuwa na uongozi uliotukuka
katika TANU/CCM.
Kwa upande wake, TANU iliunga
mkono madai ya vyama vya wafanyakazi na migomo ya wafanyakazi. Katika
historia ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, mgomo wa wafanyakazi wa
Shamba la Mazinde huko Tanga na mgomo wa wafanyakazi wa Kiwanda cha Bia
Dar es Salaam ni miongoni mwa migomo maarufu.
Shamba
la Mazinde lilikuwa mali ya bepari mmoja wa Kiingereza, mwanachama
mashuhuri wa United Tanganyika Party (UTP) aliyewahi kushiriki katika
kugombea na kushindwa na mgombea wa TANU katika Uchaguzi Mkuu wa Baraza
la Kutunga Sheria mwaka 1958. Wafanyakazi katika Shamba la Mazinde
walijiunga na Chama cha Wafanyakazi Mashambani (Tanganyika Plantation
Workers’ Union – TPWU) ambacho kilikuwa kimeshirikishwa katika
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi. Mmiliki wa Shamba la Mazinde
alikuwa na tabia ya kuwafukuza wafanyakazi walioonyesha kupinga UTP na
walioamua kujiunga na Chama cha Wafanyakazi Mashambani. Katika harakati
za kuwaunga mkono wenzao waliofukuzwa, wafanyakazi wote elfu tatu
(3,000) waliamua kugoma na matokeo yake wote walifukuzwa kazi.
Jitihada
za TFL kusuluhisha mgogoro huo kati ya Mwajiri na wafanyakazi
zilishindikana. TFL na TANU kwa pamoja viliunga mkono mgomo wa
wafanyakazi wa Shamba la Mazinde. TANU kupitia Mwalimu Nyerere ilitoa
wito kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga kuwahifadhi wafanyakazi waliofukuzwa
kazi. Wananchi waliitikia wito wa TANU na kuwapokea na kuishi nao.
Aidha, TFL na TANU vilitoa wito kwa wananchi kususia shamba la Mazinde.
Wafanyakazi hao hawakurejea kazini hata baada ya mmiliki kuwataka
kufanya hivyo. Matokeo yake ni kwamba mmiliki huyu wa Shamba la Mazinde
hakuchukua muda akafilisika na akarejea kwao Uingereza.
Huu
ulikuwa ni ushindi wa TANU na TFL. TANU ilitambuliwa na wafanyakazi
mashambani na iliendelea kuimarika. Kwa kuwa ngome ya UTP, na baadaye
African National Congress (ANC) ilikuwa huko Tanga pigo hili
lilisababisha kifo cha UTP na kuzorota kwa ANC.
Kuhusu
mgomo wa Kiwanda cha Bia Dar es Salaam, mgomo ulianza Aprili hadi Juni,
1958. Mgomo uliwashirikisha wafanyakazi wapatao mia tatu (300).
Wafanyakazi walikuwa wanadai nyongeza ya mshahara. Wafanyakazi wote
waliogoma walifukuzwa kazi na mwajiri.
Katika kuonyesha mshikamano na wafanyakazi katika mgomo huu wa Kiwanda cha Bia, TANU ilichukua hatua zifuatazo:-
Ilitoa wito kwa nchi nzima kususia pombe zote za kigeni;
Iliwaomba wananchi wa Dar es Salaam kuwasaidia wagomaji kwa kuwachangia chakula na fedha;
Iliwaomba wananchi wenye nyumba Ilala kuwapokea wagomaji katika nyumba zao pasipo kuwatoza kodi ya nyumba.
Kama kawaida yao, wananchi waliitika wito na maombi ya TANU. Kwa kupitia migomo TANU ilizidi kuimarika miongoni mwa wafanyakazi.
2.5 TANU ilizaliwa katika mazingira ya kero na adha za wananchi kutoka Serikali ya Kikoloni:
Malalamiko hayo ya wananchi yalijidhihirisha katika maeneo yafuatayo:-
Upinzani huko Upare dhidi ya ulipaji kodi kulingana na mapato (Mbiru);
Wahehe kukataa kuogesha ng’ombe wao;
Waluguru kupinga juhudi za kuhifadhi mapori na kulima matuta;
Wafugaji (Wasukuma) kupinga kodi ya ng’ombe na kupunguza idadi ya ng’ombe, kumi kwa kila mia;
Wameru wapatao 3,000 walipinga kunyang’anywa ardhi yao na Serikali ya Kikoloni na kuwapa walowezi.
TANU ilitumia kero hizo za wananchi katika kuwaunganisha wananchi na kuwaelekeza namna ya kutafuta haki zao.
Kuhusu ardhi ya Wameru, Katika mkutano wake wa kwanza, TANU ilitoa tamko lifuatalo:-
“Mkutano
huu unasikitika sana juu ya mambo yaliyofanywa na Serikali ya nchi hii
huko Meru. Mkutano unakubali kwamba Serikali inayo mamlaka kuchukua
ardhi ya raia hata kwa lazima ili ardhi hiyo iwe faida ya watu wote kama
vile kupitisha reli, barabara, kujenga hospitali, shule au kutumia kwa
jambo lingine la manufaa kwa wote. Lakini Serikali haina mamlaka
kuchukua ardhi ya raia ili ardhi ile wapewe raia wengine waitumie kwa
faida yao wenyewe … Mkutano huu unataka Serikali iwarudishie Wameru
ardhi yao ama kuwalipa fidia kwa hasara walizopata kubwa, kwa kufukuzwa
kama mahabusu, kama Baraza la Umoja wa Mataifa lilivyokubaliana.”
(Historia ya Chama cha TANU 1954 hadi 1977, uk 36).
2.6 Kuenea kwa TANU na Kupata Ushindi:
Dhumuni
la kwanza la TANU mwaka 1954 lilikuwa ni kuwatayarisha Watanganyika
kujitawala na kujitahidi kwa bidii mpaka Tanganyika imepata uhuru na
inajitawala. TANU ilibaini kwamba lengo lake kuu ni kupigania uhuru wa
Tanganyika na silaha yake kubwa ni umoja hasa umoja wa Waafrika. Kwa
mnasaba huo, TANU iliacha mlango wake wazi kwa Waafrika bila ya kujali
kabila, dini, rangi, jinsia na majimbo yao. Toka mwanzo, msingi huu
uliifanya TANU kuwa chama cha umma. Hata hivyo uamuzi wa kukifanya Chama
cha TANU kuwa wazi kwa Waafrika tu ulikuwa ni uamuzi wa kimkakati tu.
Haikukusudiwa kukifanya Chama hicho kuwa cha kibaguzi na kwa hakika
kiliendelea kushirikiana na kuwaenzi Waasia na Wazungu walioafiki imani
na madhumuni ya TANU.Miongoni mwa Waasia na Wazungu waliokuwa na mtazamo
wa kizalendo katika shughuli za kisiasa ni Amir Jamal, Al-Noor Kassim,
Derek Bryceson, Babra Johnson na Leader Stirling. Baada ya uhuru (1962),
Waasia na Wazungu waliruhusiwa kuwa wanachama wa TANU.
Katika harakati za kuitangaza TANU, njia mbali mbali zilitumika:-
TANU ilifungua matawi katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu.
TANU ilitumia mikutano ya hadhara katika kufikisha ujumbe wake kwa wananchi.
TANU ilitumia mikutano ya ndani ya wanachama.
TANU ilitumia vyombo vya habari, hususan magazeti, kama vile Sauti ya TANU, Habari za TANU na Mwafrika.
2.7 Jumuiya za TANU za Umoja wa Wanawake, Umoja wa Vijana na Wazazi zilifanya kazi kubwa katika kukieneza na kukiimarisha Chama.
TANU
ilianzisha rasmi mwaka 1955 sehemu ya Wanawake wa TANU. Chama
kilitambua kwamba mapambano ya kudai uhuru yasingeweza kufanikiwa bila
ya kulitumia jeshi kubwa la Wanawake. Chama kilimpata Bibi Titi Mohamed
na kumpa jukumu la kuwakusanya wanawake ili washiriki katika mapambano
ya kudai uhuru. Sehemu ya Wanawake ilipewa majukumu yafuatayo:-
Kupata wanachama wa TANU wengi;
Kueneza Chama hasa vijijini kwa moyo wa kujitolea;
Kuona kwamba viongozi wa Chama wako salama/ulinzi wa viongozi na
Kukipatia Chama fedha kutokana na shughuli halali mbali mbali.
Katiba
ya TANU ya mwaka 1954, sehemu ya sita, ilitoa nafasi kwa vijana kuunda
umoja wao ili waweze kushiriki kwa ukamilifu katika mapambano ya kudai
uhuru. Umoja wa Vijana ulikuwa na majukumu yafuatayo:
Kuwaandaa vijana katika uongozi;
Kuwahimiza vijana kujitolea kufanya kazi za TANU;
Kutekeleza shabaha za TANU;
Kuunda makundi ya starehe na maendeleo miongoni mwa wanachama kama vile, elimu, biashara na michezo;
Kukusanya habari na kufuatilia mwenendo wa kisiasa nchini;
Kushirikiana na vyama vingine vya vijana visivyo na upinzani kwa TANU.
2.8 TANU ilivyopambana na kuvishinda vikwazo na hila za Mkoloni
Jumuiya
ya Wazazi (Tanganyika Parent’s Association – TAPA) iliundwa mwaka 1955
chini ya Ndugu Lawi Sijaona. TAPA ilikuwa ndiye mtekelezaji mkuu wa
Azimio la Mkutano Mkuu wa Tabora lililohusu upanuzi wa elimu. Katika
kutekeleza jukumu lake, TAPA ilifungua shule za msingi na sekondari
nyingi nchini na kuendesha kisomo cha Watu Wazima. Huu ulikuwa mkakati
wa makusudi wa kuwaandaa wananchi kushika madaraka baada ya uhuru.
Jinsi TANU ilivyozidi kuimarika ndivyo hivyo ilivyopambana na vikwazo na hila za Mkoloni:
Serikali
ya Kikoloni ilipitisha Sheria mwaka 1953 ya kuwakataza watumishi wa
Serikali wa mataifa yote kujiunga na vyama vya siasa. Aidha, Tangazo la
Serikali Namba 2 la 1954 lilifafanua kuwa hata Sukuma Union kilikuwa ni
Chama cha Siasa. Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 6 la 1954,
maafisa wote wa Serikali waliokuwa wanachama wa TANU na waliotaka
kuendelea na utumishi serikalini walitakiwa kujiuzulu mara moja. Aidha,
Sheria ya vyama vya siasa, 1954, ilitaka kila tawi la TANU lisajiliwe
kabla ya kuandikishwa kisheria. Sheria hii iliiwezesha serikali ya
mkoloni kusajili au kutokusajili tawi lo lote la TANU.
Mara
tu baada ya TANU kuundwa, Rais wake Mwalimu Nyerere alitakiwa na
Serikali ya Kikoloni achague moja kati ya mambo mawili ama kuendelea
kuiongoza TANU au kujiuzulu uongozi wa TANU na kuendelea na kazi yake ya
ualimu katika Shule ya Sekondari Pugu. Mwalimu aliamua kuendelea
kuihudumia TANU hivyo akalazimika kujiuzulu kazi ya ualimu. Bila shaka,
Serikali ya Kikoloni ilidhani kwamba Mwalimu asingejiuzulu ualimu.
Katika suala hili, uamuzi wa Mwalimu haukuwa rahisi hasa kwa kuzingatia
kwamba kazi ya ualimu ndio alikuwa ameisomea, riziki yake na ya familia
ilitokana na ualimu na kwamba kuitumikia TANU wakati huo ilikuwa ni
kupambana na Serikali ya Kikoloni na hii ilikuwa ni hatari kubwa. Kwa
kujiuzulu ualimu, Mwalimu alipata nafasi kubwa zaidi ya kuihudumia TANU.
Mwalimu
Nyerere mwaka 1958 alishitakiwa na Serikali ya Kikoloni kwa kosa la
kuwakashifu District Commissioners wa Songea, Geita na Musoma. Kwamba
kashfa hiyo aliifanya kwa kupitia makala aliyoiandika kupitia Gazeti la
“Sauti ya TANU” Toleo Namba 29 la tarehe 27 Mei, 1958. Katika kesi hii
iliyosikilizwa na Mahakama ya Dar es Salaam, Mwalimu alihukumiwa faini
ya shs. 3,000/= (shilingi elfu tatu) au kifungo cha miezi 6. Mwalimu
alilipiwa faini hiyo na TANU.
Serikali ya
kikoloni pia ilijitahidi kadri ilivyoweza kuwatumia baadhi ya machifu
kuwa chombo cha kuzuia uenezaji wa TANU. Machifu walipewa madaraka
makubwa zaidi na zaidi ili wajisikie kuwa ni sehemu ya utawala na kwamba
TANU ilikuwa na lengo la kuwakosesha maslahi yao. Mwaka 1957, Serikali
ya kikoloni iliunda Baraza la Machifu wa Tanganyika (Territorial
Convention of Chiefs). Kwa kuwatumia machifu, Serikali ya kikoloni
ilitegemea kuwagawa Watanganyika kwa misingi ya ukabila ili kuweza
kuwatawala wananchi kwa urahisi zaidi. Aidha, Serikali ya kikoloni
ilikuwa na lengo la kuwagonganisha machifu na viongozi wa TANU.
Serikali
ya kikoloni ilihimiza kuundwa kwa United Tanganyika Party (UTP) ndani
ya Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1956. UTP ilikuwa ni chombo na Sauti
ya Serikali ya kikoloni kwa sababu zifuatazo:-
Uongozi wa UTP uliundwa na Wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria,
“Tanganyika Unofficial Members Organization (TUMO)”
Wajumbe hao waliteuliwa na Gavana na hivyo hawangeweza kupingana na siasa ya Serikali ya Kikoloni.
Licha
ya hila na vikwazo vya mkoloni, TANU ilijikuta ina mtihani mgumu wa
kuamua kushiriki ama kutokushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza mwaka
1958. Akifungua kikao cha kwanza cha Baraza la Kutunga Sheria mwaka
1956, Gavana Edward Twining alitangaza kuwa Serikali ilikuwa na mpango
wa kufanya Uchaguzi Mkuu wa kwanza mnamo 1958. Sharti moja kubwa la
uchaguzi huo lilikuwa kwamba kila mpiga kura apige kura tatu: moja kwa
Mzungu, moja kwa Mwasia na moja kwa Mwafrika.
Suala
hili la kura ya Mseto lilijadiliwa kwa undani katika Mkutano Mkuu wa
TANU uliofanyika Tabora mwaka 1958 na kuhudhuriwa na Wajumbe 300 kutoka
sehemu zote za Tanzania Bara. Ili kupata nafasi nzuri ya kujadili agenda
hii, Mwalimu Nyerere aliomba asiwe Mwenyekiti wa kikao hicho, nafasi
yake ilichukuliwa na Mwalimu Kihere kutoka Tanga.
Mwalimu
Nyerere aliweza kuushawishi Mkutano kukubali kushiriki katika Uchaguzi
Mkuu wa kwanza mwaka 1958. Hoja za Mwalimu zilikuwa ni kwamba kama TANU
isingeshiriki, ingekuwa imeshindwa kwani isingekuwa na wawakilishi
katika Baraza la Kutunga Sheria. Kujitoa katika uchaguzi huo kungekuwa
na maana ya kujitoa katika uwanja wa mapambano ambao sasa ungemilikiwa
na UTP. Uamuzi wa TANU kushiriki katika uchaguzi huo ulikuwa ni wa
busara kwani wagombea wote waliosimamishwa kwa tiketi ya TANU walishinda
na hivyo TANU kunyakua viti vyote vya wajumbe wa kuchaguliwa wa Baraza
la Kutunga Sheria.
Matokeo ya kukubali kura ya
mseto, aliyekuwa Katibu Mwenezi wa TANU, Ndugu Zuberi Mtemvu aliamua
kuachana na TANU na kuanzisha African National Congress (ANC) mwaka
1958. Hata hivyo toka kuanzishwa kwake hadi kifo chake, ANC haikupata
hata kiti kimoja katika Baraza la Kutunga Sheria. Aidha, Ndugu Mtemvu
alibwagwa kwa kishindo na Mwalimu Nyerere katika kugombea Urais wa
Jamhuri ya Tanganyika mwaka 1962.
Uchaguzi Mkuu
wa pili ulifanyika mwaka 1960. Katika uchaguzi huo, TANU ilijikuta
imefanikiwa kupitisha wagombea wake 58 bila ya kupingwa. Kati ya
wagombea hao 58 waliopita bila kupingwa, 8 walikuwa Wazungu, 11 Waasia
na 39 Waafrika. Tarehe 30 Agosti, 1960 ulifanyika uchaguzi katika sehemu
nyingine ambako kulikuwa na zaidi ya mgombea mmoja katika jimbo la
uchaguzi. Wagombea viti wote jumla walikuwa 25 kati ya hao 11
walisimamishwa na TANU na walishinda isipokuwa mmoja tu wa kiti cha
Mbulu, Chifu Amri Dodo aliyeshindwa na Herman E. Sarwatt ambaye alikuwa
mgombea binafsi. Hata hivyo, Sarwatt alikuwa ni mwanachama wa TANU.
Pamoja
na vikwazo hivi Msimamo sahihi usioyumba uongozi bora umoja mshikamano
ari na dhamira ya wananchi ya kutaka kujitawala vilikuwa chachu
iliyosababisha TANU kupata ushindi wa kishindo na kutokana na ushindi
huo, Gavana Richard Turnbull alimwomba Rais wa TANU, Mwalimu Nyerere
kuunda Baraza la Mawaziri ambalo lilikuwa na jukumu la kuongoza nchi kwa
jumla na kumshauri Gavana. Serikali ya Madaraka iliundwa na kuapishwa
tarehe 3 Septemba, 1960. Tanganyika ilipata Serikali ya Ndani tarehe 1
Mei, 1961 na uhuru kamili tarehe 9 Desemba, 1961 na Mwalimu Nyerere kuwa
Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika huru.
2.9 Siri ya ushindi wa TANU
Uhuru
wa Tanganyika ulipatikana katika kipindi cha miaka saba tu ya kudai
uhuru. Kipindi hiki ni kifupi. Siri ya TANU ya ushindi ilitokana pamoja
na mambo yafuatayo:-
Tanganyika ilikuwa chini
ya Udhamini wa Umoja wa Mataifa tofauti na nchi kama Kenya, Uganda,
Zambia na Malawi zilizokuwa makoloni moja kwa moja chini ya Serikali ya
Kiingereza iliyokuwa na sauti ya mwisho. Chini ya udhamini huo watawala
wa Kiingereza, walipaswa kuitawala nchi hii kwa mujibu wa masharti ya
Umoja wa Mataifa kuhusu makoloni ya udhamini.
Nafasi
ya Jamhuri ya Kisovieti (Urusi) (ilikuwa miongoni mwa mataifa manne
makubwa) katika Umoja wa Mataifa ilisaidia kutoa msukumo kwa Umoja huo
katika kufanikisha juhudi za TANU za kudai uhuru wa Tanganyika. Aidha,
Urusi ilikuwa ni Mjumbe wa Baraza la Udhamini. Msimamo wa Urusi kuhusu
makoloni ulikuwa thabiti kwamba makoloni yana haki ya kujitawala. Uhuru
wa India, Pakistani na Ghana ulisaidia kutoa msukumo kwa makoloni
kujipatia uhuru.
Lugha ya Kiswahili ilisaidia
sana katika kuharakisha maendeleo ya siasa. Kiswahili kilisaidia
kuwaunganisha wananchi na hasa kilirahisisha kazi ya viongozi wa TANU.
Viongozi hao hawakuhitaji wakalimani wakati wa kuwahutubia wananchi
katika mikutano ya hadhara. Lugha ya Kiswahili ilisaidia na inaendelea
kusaidia katika kuleta umoja na mshikamano wa kitaifa.
Katika
Tanganyika hapakuwepo na mtengano wa kijamii wenye nguvu. Tanganyika
ilikuwa na makabila yapatayo 120 lakini kihistoria hapakuwa na utawala
wa kikabila wa kugandamiza kabila lingine.
Tanganyika
ilikuwa na walowezi wachache ikilinganishwa na nchi kama Kenya. Katika
makoloni mengi uhuru wa wananchi ulicheleweshwa kutokana na siasa za
walowezi ambazo msingi wake ni uchumi hodhi.
Umoja
wa Vijana na Umoja wa Wanawake chini ya TANU, walitoa msukumo mkubwa
katika kudai uhuru. Vikundi hivyo vilijawa na ari na moyo wa
kimapinduzi; vilifanya kazi ya kujitolea usiku na mchana.
Vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya Ushirika viliweza kuwabana vilivyo Wakoloni kwa njia ya migomo na ususiaji wa bidhaa.
Uongozi
bora wa TANU, hususan uongozi wa Mwalimu Nyerere. Uongozi bora wa TANU
ndio uliokipa Chama msimamo thabiti na kuwafanya wananchi kuwa na imani
kubwa na TANU.
Aidha TANU iliweza kushinda changamoto katika sura ya hila na vikwazo kadhaa na kupata mafanikio kama vile:-
3.0 ASP NA HARAKATI ZA MAPAMBANO DHIDI YA UKOLONI WA KIINGEREZA NA USULTANI WA KIARABU
Mazingira ambamo ASP ilizaliwa:
ASP
ilizaliwa katika mazingira yaliyokwisha andaliwa kisiasa na African
Association (AA) na Shirazi Association (SA); vyama ambavyo vilikuwa
nusu vya siasa na nusu vya kupigania maslahi ya Watumishi wa Kiafrika
kazini. Katika mazingira hayo, waafrika na Washirazi walielewa kwamba:-
Adui wa Waafrika ni ukoloni wa Kiingereza na umwinnyi wa Kiarabu ukiongozwa na Sultani.
Umoja miongoni mwa Waafrika ni muhimu ili kujipatia uhuru wa kisiasa.
Ukoloni wa Kiingereza ulikuwa na nia ya kutoa uhuru kwa Waarabu wa Oman ambao walichukuliwa kwamba ndio wenye nchi.
Aidha,
ASP ilizaliwa katika mazingira yaliyokuwa yamejaa manung’uniko dhidi ya
ukoloni wa Kiingereza na ubwanyenye/umwinyi wa Kiarabu.
Miongoni mwa manung’uniko hayo ni:-
Kutokuwepo na demokrasia ya kweli katika utawala wa kikoloni.
Kutokuwepo na wawakilishi wa Waafrika katika baraza la Kutunga Sheria kuanzia mwaka 1926 hadi 1946
Ubaguzi katika kazi na huduma za jamii, hususan elimu na afya.
Ardhi ilikuwa inamilikiwa na kusimamiwa na Waarabu. Waafrika walikuwa manokoa katika mashamba ya Waarabu.
Sheria ya Serikali ya Kikoloni ya mwaka 1953 iliwazuia wafanyakazi Serikalini wasishiriki katika shughuli za kisiasa.
ASP
ilizaliwa baada ya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) au HIZBU kuwa
imeundwa mwaka 1955. HIZBU ndicho chama kilichotoa upinzani mkubwa kwa
ASP.
ASP ilizaliwa
baada ya Vita Kuu ya Pili. Uingereza ilitoka vitani ikiwa maskini ajabu
ikilinganishwa na kipindi kabla ya vita na haikuwezekana tena kuendelea
kushikilia makoloni yake. Marekani ilizuka katika vita ikiwa Taifa lenye
nguvu zaidi kuliko mataifa yote ya Ulaya Magharibi.
ASP
ilizaliwa baada ya vyama vya siasa vingine kuwa vimeibuka katika nchi
nyingine za Afrika hasa TANU ambayo ilikuwa na mahusiano ya karibu na
ASP. Hata kabla ya ASP, kulikuwa na uhusiano wa kihistoria uliojengeka
tangu kuanzishwa kwa AA Tanzania Bara na Zanzibar na vile vile
kuendeleza ushirikiano huo kupitia TAA na AA ya Zanzibar. Hata wakati wa
kuunganisha AA na SA na kuunda ASP, Rais wa TANU Mwalimu Nyerere
alihudhuria Mkutano huo.
Kuzaliwa na Kuimarika kwa ASP:
Wazo
la kuunganisha nguvu za Waafrika liliwasilishwa kwenye Mkutano wa
Pamoja wa African Association (AA) na Shirazi Association (SA)
uliofanyika tarehe 5 Februari, 1957. Mkutano huo ulikubaliana
kuunganisha AA na SA na kuanzisha Afro-Shirazi Party (ASP). Sheikh Abeid
Amani Karume alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa ASP na Sheikh Thabit
Kombo alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu.
Waasisi wa ASP waliohudhuria Mkutano huo na kupitisha uamuzi wa kuunganiisha AA na SA ni:-
African Association (AA): Shirazi Association (SA):
1. Sheikh Abeid Amani Karume 1. Sheikh Thabiti Kombo
2. Sheikh Mtoro Rehani 2. Sheikh Muhidini Ali Omar
3. Sheikh Ibrahim Saadallah 3. Sheikh Ali Ameir
4. Sheikh Mtumwa Borafia 4. Sheikh Ameir Tajo
5. Sheikh Bakari Jabu 5. Sheikh Ali Khamis
6. Sheikh Rajab Swedi 6. Sheikh Mdungi Ussi
7. Sheikh Saleh Juma 7. Sheikh Haji Khatibu
9. Sheikh Abdullah Kasism Hanga 8. Sheikh Othman Sharif
9. Sheikh Ali Juma Seif
10. Sheikh Mzee Salehe Mapete.
Chimbuko
la kuunganisha AA na SA lilitokana na Tangazo la Serikali ya Kikoloni
kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Kwanza wa kuwachagua Wajumbe 6 kati ya 12 wa
kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria Zanzibar (Legislative Council –
LEGCO). Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Julai, 1957. wajumbe 6 wengine
walitakiwa kuteuliwa na Sultani. Bila ya kuungana isingekuwa rahisi kwa
AA na SA kupata viti katika Baraza la Kutunga Sheria hasa kwa kuzingatia
kwamba Waarabu walikwishaunda Chama chao cha siasa Novemba, 1955. Licha
ya ASP kutaka kushiriki na kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa Julai, 1957
lengo kuu la ASP lilikuwa ni kudai uhuru kamili wa Zanzibar kutoka kwa
Wakoloni wa Kiingereza na utawala wa kidhalimu wa Kisultani.
Msimamo
wa ASP ulikuwa kwamba Zanzibar ni nchi ya Kiafrika na hivyo uhuru wa
Zanzibar usingeweza kukamilika kama Usultani wa Kiarabu usingeondoka.
Msimamo huu ulikuwa tofauti kabisa na ule wa HIZBU ambao ulitaka uhuru
wa Zanzaibar akabidhiwe Sultani.
Licha ya lengo kuu la kisiasa la kuleta uhuru, ASP pia ilikuwa na malengo ya kiuchumi na kijamii. Miongoni mwa malengo hayo ni:-
Kugawa upya ardhi ili imilikiwe na wengi badala ya wachache tu;
Kutoa elimu bure kwa wote;
Kueneza huduma za afya;
Kuwapatia wananchi makazi bora;
Kuondoa dhuluma mbali mbali na;
Kujenga ujamaa na ushirika.
Uchaguzi Mkuu wa Kwanza Julai, 1957:
Katika
uchaguzi huo, ASP ilipata viti 5 kati ya 6. Kiti hicho kimoja cha Stone
Town kilichukuliwa na mgombea wa Muslim Association ambacho kilikuwa
Chama cha Wahindi wasiokuwa Hindu. Ingawa HIZBU ilisimamisha wagombea
katika majimbo yote 6 ya uchaguzi, hawakupata kiti hata kimoja.
Baada
ya uchaguzi huo, Zanzibar ilitawaliwa na vituko. Serikali ya kikoloni
ilimteua Ali Muhsin Barwani kuwa Waziri. Huyu alikuwa Rais wa ZNP
(HIZBU) aliyeangushwa na Abeid Amani Karume kwa kura 3,328 dhidi ya kura
918 katika Jimbo la Ng’ambo. ASP iliwasilisha malalamiko yake kwa
Balozi Mkazi wa Kiingereza dhidi ya uteuzi huo lakini malalamiko hayo
yalipuuzwa. Hii ikiwa ni kielelezo cha upendeleo aliokuwa nao Balozi
Mkazi wa Kiingereza kwa Waarabu chini ya ZNP.
Mwaka
1959 Sultan Khalifa bin Haroub alipata nafasi ya kutembelea Uingereza,
mwanae Seyyid Abdulla ndiye akawa Sultani wa muda na wakati huo
akajiunga na ZNP. Mwanae Sultan kujiunga katika Chama cha siasa ilikuwa
ni mbinu ya kuwakandamiza Waafrika.
Sultani
na Balozi Mkazi wa Kiingereza walijitahidi kwa nguvu zao zote
kuiangusha ASP. Balozi Mkazi wa Kiingereza aliwaita Washirazi na
kuwashawishi kuanzisha Chama chao wakati Sultani naye aliwashawishi
Washirazi wajitoe katika ASP. Baadhi yao walishawishika. Kwa mfano,
Ameir Tajo alikwenda kinyume na matakwa na maadili ya ASP kwa kumweleza
Balozi Mkazi wa Kiingereza kwamba Zanzibar ipatiwe uhuru wake baada ya
miaka 10. Kamati Kuu ya ASP ilihitaji uhuru wa Zanzibar upatikane mwaka
1960. ASP ilimfukuza Ameir Tajo uanachama na uongozi. Aidha, Sheikh
Mohammed Shamte na Sheikh Ali Sharif Mussa walijiondoa kutoka ASP baada
ya Sheikh Ameir Tajo kufukuzwa.
Zanzibar
and Pemba People’s Party (ZPPP) ilizaliwa mwishoni mwa mwaka 1959. ZPPP
ilianzishwa na wanachama wa ASP waliofukuzwa na kujiondoa kutoka ASP.
Rais wa ZPPP alikuwa Sheikh Mohammed Shamte. Miongoni mwa viongozi
mashuhuri wa ASP waliounda ZPPP ni pamoja na Sheikh Ameir Tajo aliyekuwa
Mjumbe wa Kamati Kuu ya ASP na Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria akiwa
Mwakilishi wa Unguja Kusini na Sheikh Ali Shariff Mussa ambaye pia
alikuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria akiwakilisha Pemba Kaskazini.
Ikumbukwe pia kwamba Sheikh Mohammed Shamte alikuwa akiwakilisha Pemba
Kusini katika Baraza la Kutunga Sheria. Kwa hiyo kuondoka kwa hao
Wajumbe 3 kulikuwa na maana ya ASP kubakia na Wajumbe 2 katika
Baraza
la Kutunga Sheria. Wajumbe hao wawili ni Sheikh Abeid Amani Karume
akiwakilisha Jimbo la Ng’ambo na mwakilishi wa Unguja Kaskazini, Sheikh
Daud Mahmoud.
Kitendo
cha kuzaliwa ZPPP kilifurahisha sana HIZBU na Balozi Mkazi wa
Kiingereza. Katika furaha hiyo, Balozi alitoa nafasi kwa Rais wa ZPPP,
Sheikh Mohammed Shamte kwenda kutembelea Uingereza na Marekani.
Ziara ya Ian Macleod, Waziri wa Makoloni:
Ian
Macleod alitembelea Zanzibar Desemba 1959 na alifanya mazungumzo na
viongozi wa ASP, ZNP na ZPPP. Katika mazungumzo hayo, Macleod alikubali
mambo mawili:-
(a) Tume iteuliwe kuchunguza Katiba (maendeleo ya kikatiba)
(b) Uchaguzi Mkuu wa pili uliokuwa umepangwa kufanyika Julai, 1960 uahirishwe hadi hapo Tume itakapokuwa imetoa mapendekezo yake.
Tume
ya Hilary Blood iliteuliwa na kupata nafasi ya kusikiliza maoni ya
viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa Jumuiya. Kama kawaida ya
Tume, mapendekezo yalitolewa.
Mapendekezo ya Tume ya Sir Hilary Blood:-
(1) Sultan asijihusishe na mambo yoyote ya siasa kwa maana ya kujiunga na chama cha siasa au kusaidia chama cho chote cha siasa.
(2) Kuhusu
muundo mpya wa Baraza la Kutunga Sheria, ilipendekezwa kwamba liwe na
wajumbe 21 wa kuchaguliwa na 8 wa kuteuliwa. Aidha, ilipendekezwa kwamba
Baraza jipya liwe na Spika badala ya kuongozwa na Balozi Mkazi wa
Kiingereza.
(3) Baada
ya uchaguzi mkuu, Zanzibar iwe na mfumo wa Wizara chini ya Waziri Mkuu
asiyekuwa na mamlaka ya mwisho. Balozi Mkazi wa Kiingereza ndiye
angekuwa na mamlaka ya mwisho.
(4) Pawepo na upande wa Upinzani katika Baraza la Kutunga Sheria na Kiongozi wa Upinzani apangiwe mshahara kamili.
(5) Zanzibar kufanya mipango ya kujiunga katika mazungumzo ya shirikisho la Nchi za Afrika Mashariki.
Uchaguzi Mkuu wa Pili Januari, 1961:
ASP,
ZNP na ZPPP walishiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Pili uliofanyika
Januari, 1961. Tangazo la tarehe 16 Januari, 1961 lililotolewa na Balozi
Mkazi wa Kiingereza lilieleza wazi kwamba chama cho chote kitakachopata
viti zaidi katika uchaguzi mkuu wa pili ndicho kitakachounda Serikali.
Katika uchaguzi huo, majimbo ya uchaguzi yalikuwa 22 yaani majimbo 13
Zanzibar na majimbo 9 Pemba.
Matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa ifuatavyo:-
ASP – viti 10 (viti 2 Pemba na 8 Unguja)
ZNP – viti 9 ( viti 4 Pemba na 5 Unguja)
ZPPP – viti 3 (viti 3 Pemba na 0 Unguja).
Kwa
mujibu wa matokeo hayo, mshindi alikuwa ni ASP. Hata hivyo, matokeo
hayo yalibadilika baada ya Wajumbe 2 wa ZPPP Sheikh Mohammed Shamte na
Sheikh Bakari Mohammed Bakari kuamua kujiunga na ZNP na Mjumbe mmoja
Sheikh Ali Shariff Mussa kujiunga na ASP.
Kwa
kuzingatia kwamba ASP na ZNP walikuwa na viti sawa katika Baraza la
Kutunga sheria, uamuzi ulifikiwa wa kuunda Serikali ya Mseto ambayo
ilitakiwa kudumu kwa muda wa miezi sita.
Uchaguzi Mkuu wa Tatu Juni, 1961:
Katika
uchaguzi huo, majimbo ya uchaguzi yaliongezwa toka 22 hadi 23. Jimbo
jipya la uchaguzi lilikuwa Mtambile, Pemba Kusini ambapo ZPPP ilikuwa na
nguvu. ASP, ZNP, ZPPP vilishiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Tatu. Hata
hivyo,
ZNP
na ZPPP walikuwa na makubaliano kwamba anaposimamishwa mgombea wa ZNP
asisimamishwe mgombea wa ZPPP na kinyume chake. ASP ilisimamisha
wagombea wake katika majimbo yote 23 ya uchaguzi.
Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Tatu uliofanyika tarehe 1 Juni, 1961:
ASP – viti 10 (Unguja 8 na Pemba 2)
ZNP – viti 10 (Unguja 5 na Pemba 5)
ZPPP – viti 3 ( Unguja 0 na Pemba 3)
Kuhusu
kura, waliojiandikisha kupiga kura ni 94,218 na waliopiga kura ni
90,595 sawa na asilimia 96.15. ASP ilipata asilimia 49.9 ya kura zote
zilizopigwa, ZNP asilimia 35.0, ZPPP asilimia 13.7 na kura
zilizoharibika zilikuwa asilimia 1.4
Matokeo
haya yanaonyesha kwamba ZNP na ZPPP kwa pamoja walipata viti 13 na ASP
viti 10. Balozi Mkazi wa Kiingereza alimwomba Sheikh Ali Muhsin Barwani,
Rais wa ZNP kuunda Serikali ya madaraka ambaye pia alitoa nafasi hiyo
kwa Sheikh Mohammed Shamte, Rais wa ZPPP kuwa Waziri Mkuu.
Uchaguzi Mkuu wa Tatu ulitawaliwa na vurugu:-
Baadhi ya wapiga kura walipiga kura mara mbili.
Katika baadhi ya masanduku kura zilitumbukizwa kabla ya upigaji kura.
Siku
ya uchaguzi tarehe 1 Juni, 1961 kulikuwa na fujo iliyosababisha
mapigano kati ya wafuasi wa ASP na ZNP. Inakisiwa kwamba watu wapatao
400 walijeruhiwa na 68 walikufa. Machafuko hayo yalipamba moto zaidi
tarehe 2 Juni , 1961 baada ya taarifa kuwafikia wanachama wa ASP kuwa
Serikali ya Madaraka ilikuwa imeundwa na ZNP pamoja na ZPPP. Vikosi vya
kuzuia fujo kutoka Kenya na Tanzania Bara ilibidi viende Zanzibar kuzuia
fujo.
Mkutano
wa kwanza wa Katiba ulifanyika London Machi, 1962. ASP iliongozwa na
Mzee Karume na Othman Shariff wakati ZNP na ZPPP iliongozwa na Ali
Muhsin Barwani (ZNP) na Mohammed Shamte (ZPPP). Baada ya Mkutano huo,
Umma Party chini ya Abdurahaman Mohammed Babu ilizaliwa. Umma party
ilikuwa na fikra za kimapinduzi, hususan fikra za kikomunisti. Babu
alijitoa ZNP na hili lilikuwa ni pigo kwa chama hicho.
Uchaguzi Mkuu wa Nne Julai, 1963:
Majimbo
ya uchaguzi yaliongezwa toka 23 hadi 31 yaani majimbo 17 Unguja na
Majimbo 14 Pemba. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Zanzibar, watu
wazima wote (miaka 18 na kuendelea) waliruhusiwa kupiga kura bila ya
vikwazo vya kisomo na kipato. Uchaguzi ulifanyika chini ya ulinzi wa
majeshi ya Kiingereza yaliyochukua sura ya mazoezi ya kivita kuliko
uchaguzi.
Matokeo ya uchaguzi huo:-
ASP – viti 13 (Unguja 11 na Pemba 2)
ZNP – viti 12 (Unguja 6 na Pemba 6)
ZPPP – viti 6 (Unguja 0 na Pemba 6)
Kuhusu
kura, ASP ilipata kura 87,085 sawa na asilimia 54.21; ZNP na ZPPP kwa
pamoja zilipata kura 73,559 sawa na asilimia 45.79 ya kura zote halali
zilizopigwa.
Kwa matokeo hayo, Sheikh Mohammed
Shamte alitakiwa na Balozi Mkazi wa Kiingereza Kuunda Serikali ya Ndani
tarehe 17 Julai, 1963. Mkutano wa Pili wa Katiba ulifanyika London
kuanzia tarehe 20 hadi 24 Septemba, 1963 na Zanzibar ilipewa uhuru wake
wa bandia tarehe 10 Desemba, 1963 kwa mujibu wa makubaliano ya Lancaster
House – London.
Mapinduzi:
Mara
baada ya uhuru, ASP ilianza maandalizi ya kufanya Mapinduzi. Kamati ya
Mapinduzi ya watu 14 iliteuliwa na Mzee Karume na kupewa jukumu la
kuandaa na kuendesha mapinduzi. Wajumbe wa Kamati hiyo walikuwa:
(1) Seif Bakari
(2) Said Washoto
(3) Abdalla Natepe
(4) Khamis Hemed
(5) Said Idi Bavuai
(6) Yussuf Himid
(7) Pili Khamis
(8) Mohammed Abdalla
(9) Hafidh Suleiman
(10) Hamid Ameir
(11) Ramadhani Haji
(12) Khamis Darwesh
(13) Mohammed Mfaranyaki
(14) John Okello
Kamati
hii ya watu 14 ilifanikisha Mapinduzi Matukufu tarehe 12 Januari, 1964
na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ikatangazwa. Tarehe 26 Aprili, 1964
Zanzibar na Tanganyika ziliungana rasmi na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Baada ya mapinduzi, Serikali ya Mapinzudi Zanzibar ilichukua hatua zifuatazo:-
Kuanzisha mfumo wa Chama kimoja cha Siasa;
Kutaifisha ardhi na wananchi kugawiwa ekari tatu tatu kutokana na mashamba makubwa yaliyokuwa yakimilikiwa na makabaila;
Kupiga marufuku ubaguzi wa aina zote;
Kujenga majumba ya wazee;
Kuanzisha na kuendeleza mradi wa nyumba za kuishi;
Kutoa elimu bure na matibabu bure;
Kupiga marufuku rehani;
Kuchoma moto maringisha (rickshaws) ambayo ni aina ya mikokoteni ya raha iliyotumika kuwasafirisha mabwanyenye na watalii.
4.0 CHAMA CHA MAPINDUZI
Kuzaliwa kwa CCM
Katika
Mkutano Mkuu wa Pamoja wa TANU na ASP uliofanyika tarehe 22 Septemba,
1975 Rais wa TANU, Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba Tanzania ni nchi
yenye Chama kimoja;
“Lakini kwa sababu kuna
vyama viwili TANU na ASP, Katiba inazungumza juu ya Chama kimoja, hicho
Chama kimoja kwa kweli ni vyama viwili … Siasa ya TANU na ASP ni moja
yaani Ujamaa na Kujitegemea. Midhali Katiba ya Tanzania ni ya Chama
kimoja, Katiba hiyo inataka hicho Chama chenye Siasa ya Ujamaa na
Kujitegemea kishike hatamu na uongozi wa nchi”. (Tathmini ya Miaka 20 ya
CCM, uk. 3-4).
Kwa
msisitizo huo, Mwalimu alipendekeza kuunganishwa kwa TANU na ASP na
kuundwa kwa chama kipya. Pendekezo hilo liliwasilishwa kwa wanachama wa
TANU na ASP ili kujadili na kutoa maoni yao. Matokeo ya maoni ya
wanachama ni kwamba zaidi ya asilimia 90 ya wanachama walikubaliana na
pendekezo la Mwalimu Nyerere. Baada ya kupokea matokeo ya maoni ya
wanachama wao, Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU na ile ya ASP,
zilikutana na kufanya kikao cha pamoja Oktoba, 1976. Katika mkutano huo
iliteuliwa Tume ya Watu 20 iliyopewa jukumu la kutayarisha Katiba ya
Chama kipya. Mwenyekiti wa Tume hiyo alikuwa Sheikh Thabit Kombo na
Katibu wake alikuwa Ndugu Pius Msekwa.
Wajumbe wa Tume ya Watu 20 ya kuandaa Katiba ya CCM:-
Kutoka ASP: Kutoka TANU:
1. Sheikh Thabiti Kombo 1. Ndugu Peter A. Kisumo
2. Ndugu Ali Mzee 2. Ndugu Pius Msekwa
3. Ndugu A.S. Natepe 3. Ndugu Daudi N. Mwakawago
4. Ndugu Seif Bakari 4. Ndugu Kingunge Ngombale-Mwiru
5. Ndugu Hamisi Hemed 5. Ndugu Jackson Kaaya
6. Ndugu Rajab Kheri 6. Ndugu Peter S.Siyovelwa
7. Ndugu Asia Amour 7. Ndugu Nicodemus M. Banduka
8. Ndugu Hassan N. Moyo 8. Ndugu Lawi N. Sijaona
9. Ndugu Juma Salum 9. Ndugu Beatrice P. Mhango
10. Ndugu Hamdan Muhiddin 10. Ndugu Basheikh A. Mikidadi
Mkutano Mkuu wa Pamoja wa vyama vya ASP na TANU uliofanyika tarehe 21 Januari, 1977 uliazimia ifuatavyo:-
“Sisi
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa pamoja wa TANU na ASP tuliokutana
leo tarehe 21 Januati, 1977 mjini Dar es Salaam, chini ya uongozi wa
pamoja wa Mwalimu Julius K. Nyerere, Rais wa TANU na Ndugu Aboud Jumbe,
Rais wa ASP, kwa kauli moja tunaamua na kutamka rasmi kuvunjwa kwa
Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shirazi Party (ASP)
ifikapo tarehe 5 Februari , 1977 na wakati huo huo kuundwa kwa Chama
kipya cha pekee na chenye uwezo wa mwisho katika mambo yote kwa mujibu
wa Katiba” (Katiba ya CCM).
Aidha, Azimio hilo lilisisitiza kwamba:
“Chama
tunachokiunda tunataka kiwe chombo madhubuti katika muundo wake na hasa
katika fikra zake na vitendo vyake vya kimapinduzi vya kufutilia mbali
aina zote za unyonyaji nchini …” (Katiba ya CCM)
Mkutano
Mkuu huo wa pamoja ulipitisha pia Katiba ya CCM na kumchagua Mwalimu
Nyerere kuwa Mwenyekiti wa CCM, Sheikh Aboud Jumbe kuwa Makamu
Mwenyekiti wa CCM na Ndugu Pius Msekwa kuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM.
Azma
ya CCM ilikuwa ni kuendeleza mazuri yote ya TANU na ASP na kuyaacha
mabaya. Miongoni mwa mazuri yaliyoendelezwa na CCM ni pamoja na:-
Kuendelea kuimarisha uhuru wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kudumisha Mapinduzi ya Zanzibar.
Kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.
Kuendelea kutekeleza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Kuendelea
kupanua na kuimarisha demokrasia ndani ya Chama na nchini ikiwa ni
pamoja na kufungua milango ya demokrasia Zanzibar. Katiba ya CCM
iliwataka wanachama wake Zanzibar kuwa na viongozi wengi wa kuchaguliwa
badala ya uteuzi kama ilivyokuwa chini ya ASP. Kwa kupitia Katiba ya
Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, wananchi wa
Zanzibar walipata fursa ya kwanza ya kuwachagua Wabunge wao. Aidha, kwa
kupitia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979, Baraza la Wawakilishi
liliundwa mwaka 1980 na Wawakilishi kupatikana kwa njia ya kura ya siri.
CCM katika kipindi cha Mageuzi:
CCM
kama ilivyokuwa kwa TANU na ASP, kimeendelea kuongoza nchi yetu hata
chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa uliorejeshwa rasmi tarehe 1
Julai, 1992. Changamoto inayoikabili CCM ni kuendelea kuwa chombo cha
uongozi katika mazingira haya ya mfumo wa vyama vingi vya siasa na
mazingira ya utandawazi bila ya kuwepo Baba wa Taifa.
Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere alifariki dunia tarehe 14 Oktoba, 1999 Jijini
London katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas. Kifo cha Baba wa Taifa
kilikuwa ni pigo kubwa kwa CCM na Taifa letu. Kwa Watanzania, Mwalimu ni
maarufu kwa sababu yeye ndiye mwanzilishi wa Taifa letu, ni mwanzilishi
wa TANU hadi kuleta uhuru; Mwalimu na Mzee Abeid Amani Karume ndio
walioasisi Muungano; Mwalimu na Mzee Aboud Jumbe ndio walioasisi CCM;
Mwalimu ndiye aliyelijenga na kutuachia Taifa lenye umoja, udugu na
mshikamano. Afrika itamkumbuka kama kiongozi shupavu na aliyejitolea
mhanga kwa ajili ya ukombozi wa Afrika. Dunia itamkumbuka Mwalimu kama
mtetezi wa wanyonge wa dunia, hasa wa nchi za Kusini. La msingi katika
kumkumbuka ni kuendeleza yote mema aliyotuachia.
Chini
ya mfumo wa Vyama vingi vya siasa CCM kimeweza kufanya mageuzi makubwa
ya kisiasa kiuchumi na kijamii. Mageuzi ya kiuchumi yanaendelea kwa
mafanikio makubwa kupitia Ubinafsishaji na mkakati wa Uwezeshaji chini
ya mkakati mkuu wa modenaizesheni. Mageuzi ya kisiasa yameibua
kuanzishwa kwa vyama 16 vya siasa vilivyosajiliwa. Hata hivyo CCM
kimeweza kujiimarisha kisiasa na kiuhalali kupitia ushindi wa chaguzi
kuu za 1995 na 2000. Ilani ya Uchaguzi ya 2000 inaendelea kutekelezwa
kwa mafanikio makubwa. Mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 2003 kasi ya
kukua kwa uchumi wa Tanzania umefikia asilimia 6.5 licha ya hali ya
majanga kama vile ukimwi na ukame yanayotishia mafanikio hayo. Kasi hii
ni ya juu katika nchi za SADC kwa kipindi hicho.
Aidha
CCM inaendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa ikiwa ni
pamoja na kuhakikisha mfumo wa vyama vingi hauwi sababu ya chuki na
msambaratiko wa umoja wa kitaifa, amani na mshikamano. Katika msimamo
huo CCM imeweza kufikia MUAFAKA na CUF, hatua ambayo imetoa fursa kwa
Zanzibar kurejesha hali ya amani, utulivu na mashirikiano, hivyo kuweza
kupiga hatua kubwa ya maendeleo.
5.0 HITIMISHO:
5.1
Tunajifunza nini kutokana na historia ya TANU na ASP? Historia ya TANU
na ASP inaonyesha kwamba Chama chetu wakati wote kimekuwa na sifa
zifuatazo:
kuimarisha umoja;
kujenga utaifa na uzalendo;
kupanua demokrasia ndani ya chama;
kubadilika mara kwa mara kifikra na kimuundo kulingana na wakati;
pamoja na kutambua na kushughulikia matatizo ya wananchi.
CCM
kinayo nafasi nzuri ya kujifunza mambo mengi mazuri kutokana na
historia ya TANU na ASP. Katika kipindi kinachotukabili inabidi CCM
kikabiliane na changamoto mbalimbali kwa kutumia mafunzo si tu
yatokanayo na historia ya TANU na ASP, bali pia kwa kuzingatia uzoefu
wake hadi sasa. Changamoto ya utandawazi na majukumu ya kisiasa,
kiuchumi kiutamaduni na kijamii hayana majibu katika historia peke yake.
Mada zinazofuata zinatoa fursa ya kutafakari mustakabali, mbinu na
mikakati ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo mbele ya CCM
ili kiendelee kushinda na kuendelea kuwa Chama Tawala kinachokidhi
matakwa ya Watanzania.