Friday, September 05, 2014

Mtoto wa Baba wa Taifa na Viatglis Membe Kupanda Mlima Kilimanjaro Kuchangia Jukwaa la Sanaa

DSC_0009

Afisa Habari wa shirika lisilo la kiserikali la Culture and Development East Africa (CDEA), Mandolin Kahindi akitambulisha viongozi wa CDEA kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) pamoja na dhumuni la kuitisha mkutano huo.

Na Mwandishi wetu

Madaraka Nyerere, Mtoto wa Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere, pamoja na Mwanamuziki Mzalendo Vitali Maembe wameteuliwa na shirika lisilo la kiserikali Culture and Development East Africa (CDEA) kuwa mabalozi wa kushiriki kampeni ya kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuhamasisha jamii kuchangia ujenzi wa jukwaa la sanaa na ubunifu jijini Dar es Salaam.

Kampeni hiyo ya kupanda Mlima Kilimanjaro imeandaliwa na CDEA kupitia njia ya kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia Septemba 7 hadi 13 mwaka huu ili kujenga jukwaa na sanaa na ubunifu litakalowapa fursa wasanii na vijana kukutana, kufikiri na kubuni kwa pamoja ambapo mawazo ya kisayansi yatakutana na sanaa na pia sanaa kukutana na taaluma nyinginezo nyingi.

Mkurugenzi Mtendaji wa CDEA, Ayeta Wangusa anasema “ili kufanikisha kampeni yetu ya mwaka mmoja tuliyoipa jina la ‘FUN FOR FUNDS’, tumeona ni vyema kupanda mlima Kilimanjaro kwa kumtumia Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya CDEA, Madaraka Nyerere pamoja na Vitalis Maembe ambaye ni mwanamuziki mzalendo”

DSC_0090

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Culture and Development East Africa (CDEA), Ayeta Wangusa (wa pili kushoto) akielezea lengo la kuanzishwa kwa Jukwaa la sanaa na ubunifu ambalo vijana watapata fursa ya kukutana, kufikiri na kubuni kwa pamoja.

Wangusa anasema fedha zitakazopatikana kwenye kampeni hii maalumu zitatumika kusaidia uzalishaji wa kazi za ubunifu za njia mbalimbali za mawasiliano-bunifu, kuwekeza katika kuanzisha maabara ya Filamu(yaani film lab) na kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za Jukwaa la sanaa na ubunifu.

Kwa upande wake Madaraka Nyerere anasema, “Nimekuwa nikipanda Mlima Kilimanjaro mara kwa mara kwa lengo la kuchangia ujenzi wa shule na shughuli nyinginezo za maendeleo, hivyo mwaka huu nimeona nifanye jambo hili kuhamasisha uchangiaji wa jukwaa hili la sanaa na ubunifu kwa kushirikiana na CDEA”

Madaraka anawaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia katika kampeni hii ili kufanikisha kufikiwa kwa lengo lake. “Wadau watakaopenda kuunga mkono zoezi hili,wanaweza kutuma michango yao kwa njia zifuatazo: M-PESA: 0765544714, TIGOPESA: 0713160668 Au Benki: CRDB BANK PLC, Jina la Akaunti: CULTURE AND DEVELOPMENT EAST AFRICA TZS ACC: 0150210421400, USD ACC: 0252210421400, SWIFTCODE: CORUTZTZ”

DSC_0045

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi na Balozi wa kampeni ya "Fun For Funds", Madaraka Nyerere (wa tatu kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam dhumuni lake la kupanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuchangisha fedha za jukwaa la sanaa na ubunifu ili kukuza vipaji vya vijana kupitia mafunzo mbalimbali ya sanaa na kutoa muongozo wa jinsi ya kuanzisha wazo la ubunifu na kulikamilisha.

Na kuongeza pia vijana wataunganishwa na majukwaa mengine kama hili kwa nchi za Afrika Mashariki kama vile The Nest, PAWA 254 na Creative Garage yote ya Kenya na Africa Sanaa Kollective ya Uganda.

Kwa upande wake Mzee wa ‘Sumu ya Teja’, Vitali Maembe amesema pamoja na kuwa hii ni mara ya kwanza kupanda Mlima Kilimanjaro amefanya mazoezi ya kutosha kumuwezesha kufika kwenye kilele jambo ambalo ni ndoto yake kubwa kama mwanamapinduzi wa kimuziki.

Culture and Development East Africa (CDEA) ni shirika lisilo la kiserikali linalotoa huduma kwa wasanii, viongozi wa utamaduni, wajasiriamali, maafisa utamaduni na mipango miji. Pia hufanya kazi na Mashirika makubwa ya kimaendeleo, taasisi za kiraia na Elimu katika maendeleo ya utamaduni, mipango na utekelezaji kwa Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

DSC_0067

Balozi wa kampeni ya kuchangisha fedha, “FUN FOR FUNDS” mwanamuziki mzalendo mzee wa ‘Sumu ya Teja’ , Vitali Maembe akizungumza na waandishi wa habari ambapo amewataka wasanii wenzake kuungana kuwa kitu kimoja katika kukuza utamaduni wetu kwa kubadilishana uzoefu wa kazi zao bila choyo.

DSC_0104

Mjumbe wa bodi ya shirika lisilo la kiserikali la Culture and Development East Africa (CDEA), Rose Haji Mwalimu akitoa rai kwa waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo (hawapo pichani) na kuwataka kutumia kalamu zao vizuri na kuhakikisha kampeni hii inafanikiwa.

DSC_0113

Vitali Maembe akitoa vionjo vya wimbo wake Vuma.

DSC_0121

Vitali Maembe akionyesha moja ya kazi zake za sanaa atakazoenda kuzitundika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro panapo majaliwa.

DSC_0146

Picha ya pamoja baada ya mkutano na waandishi wa habari.

No comments: