Saturday, April 08, 2017
Uzinduzi wa WASATU - Northampton, Uingereza
Na Freddy Macha
Jumuiya ya wasanii Watanzania Uingereza (WASATU) ilizunduliwa kwa vigelegele na muziki mjini Northampton , katikati ya Uingereza jumamosi iliyopita. Tafrija hiyo ndogo lakini iliyowakutanisha zaidi ya Watanzania mia moja na wenzao wa Kenya, Uganda, Kongo , Nigeria, Uingereza nk, ilihudhuriwa na Mheshimiwa Balozi Dk Asha Rose Migiro.
WASATU ilibuniwa mwaka jana kati ya wasanii wakiongozwa na mwanamuziki na mcheza sarakasi Fab Moses na promota wa vyakula vya Kitanzania, Bi Neema Kitilya. Asilimia 20 ya kipato cha onesho zilitolewa na WASATU kwa walio Northampton; kwa maafa ya mafuriko ya maji karibuni Tanzania.
Pichani: Watanzania na wasanii wenzao wakijimwaga ukumbi wa The Eastern District Social Club, Northampton
Tuesday, February 07, 2017
Sunday, November 13, 2016
Mafunzo Kwa Wasanii wa Filamu Mkoani Mwanza Yazaa Matunda
Saturday, June 25, 2016
Thursday, November 19, 2015
Mwanahabari Nashon Kenedy Awapa Siri Ya Mafanikio Wasanii wa Mwanza
Friday, September 05, 2014
Mtoto wa Baba wa Taifa na Viatglis Membe Kupanda Mlima Kilimanjaro Kuchangia Jukwaa la Sanaa
Afisa Habari wa shirika lisilo la kiserikali la Culture and Development East Africa (CDEA), Mandolin Kahindi akitambulisha viongozi wa CDEA kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) pamoja na dhumuni la kuitisha mkutano huo.
Na Mwandishi wetu
Madaraka Nyerere, Mtoto wa Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere, pamoja na Mwanamuziki Mzalendo Vitali Maembe wameteuliwa na shirika lisilo la kiserikali Culture and Development East Africa (CDEA) kuwa mabalozi wa kushiriki kampeni ya kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuhamasisha jamii kuchangia ujenzi wa jukwaa la sanaa na ubunifu jijini Dar es Salaam.
Kampeni hiyo ya kupanda Mlima Kilimanjaro imeandaliwa na CDEA kupitia njia ya kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia Septemba 7 hadi 13 mwaka huu ili kujenga jukwaa na sanaa na ubunifu litakalowapa fursa wasanii na vijana kukutana, kufikiri na kubuni kwa pamoja ambapo mawazo ya kisayansi yatakutana na sanaa na pia sanaa kukutana na taaluma nyinginezo nyingi.
Mkurugenzi Mtendaji wa CDEA, Ayeta Wangusa anasema “ili kufanikisha kampeni yetu ya mwaka mmoja tuliyoipa jina la ‘FUN FOR FUNDS’, tumeona ni vyema kupanda mlima Kilimanjaro kwa kumtumia Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya CDEA, Madaraka Nyerere pamoja na Vitalis Maembe ambaye ni mwanamuziki mzalendo”
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Culture and Development East Africa (CDEA), Ayeta Wangusa (wa pili kushoto) akielezea lengo la kuanzishwa kwa Jukwaa la sanaa na ubunifu ambalo vijana watapata fursa ya kukutana, kufikiri na kubuni kwa pamoja.
Wangusa anasema fedha zitakazopatikana kwenye kampeni hii maalumu zitatumika kusaidia uzalishaji wa kazi za ubunifu za njia mbalimbali za mawasiliano-bunifu, kuwekeza katika kuanzisha maabara ya Filamu(yaani film lab) na kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za Jukwaa la sanaa na ubunifu.
Kwa upande wake Madaraka Nyerere anasema, “Nimekuwa nikipanda Mlima Kilimanjaro mara kwa mara kwa lengo la kuchangia ujenzi wa shule na shughuli nyinginezo za maendeleo, hivyo mwaka huu nimeona nifanye jambo hili kuhamasisha uchangiaji wa jukwaa hili la sanaa na ubunifu kwa kushirikiana na CDEA”
Madaraka anawaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia katika kampeni hii ili kufanikisha kufikiwa kwa lengo lake. “Wadau watakaopenda kuunga mkono zoezi hili,wanaweza kutuma michango yao kwa njia zifuatazo: M-PESA: 0765544714, TIGOPESA: 0713160668 Au Benki: CRDB BANK PLC, Jina la Akaunti: CULTURE AND DEVELOPMENT EAST AFRICA TZS ACC: 0150210421400, USD ACC: 0252210421400, SWIFTCODE: CORUTZTZ”
Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi na Balozi wa kampeni ya "Fun For Funds", Madaraka Nyerere (wa tatu kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam dhumuni lake la kupanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuchangisha fedha za jukwaa la sanaa na ubunifu ili kukuza vipaji vya vijana kupitia mafunzo mbalimbali ya sanaa na kutoa muongozo wa jinsi ya kuanzisha wazo la ubunifu na kulikamilisha.
Na kuongeza pia vijana wataunganishwa na majukwaa mengine kama hili kwa nchi za Afrika Mashariki kama vile The Nest, PAWA 254 na Creative Garage yote ya Kenya na Africa Sanaa Kollective ya Uganda.
Kwa upande wake Mzee wa ‘Sumu ya Teja’, Vitali Maembe amesema pamoja na kuwa hii ni mara ya kwanza kupanda Mlima Kilimanjaro amefanya mazoezi ya kutosha kumuwezesha kufika kwenye kilele jambo ambalo ni ndoto yake kubwa kama mwanamapinduzi wa kimuziki.
Culture and Development East Africa (CDEA) ni shirika lisilo la kiserikali linalotoa huduma kwa wasanii, viongozi wa utamaduni, wajasiriamali, maafisa utamaduni na mipango miji. Pia hufanya kazi na Mashirika makubwa ya kimaendeleo, taasisi za kiraia na Elimu katika maendeleo ya utamaduni, mipango na utekelezaji kwa Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.
Balozi wa kampeni ya kuchangisha fedha, “FUN FOR FUNDS” mwanamuziki mzalendo mzee wa ‘Sumu ya Teja’ , Vitali Maembe akizungumza na waandishi wa habari ambapo amewataka wasanii wenzake kuungana kuwa kitu kimoja katika kukuza utamaduni wetu kwa kubadilishana uzoefu wa kazi zao bila choyo.
Mjumbe wa bodi ya shirika lisilo la kiserikali la Culture and Development East Africa (CDEA), Rose Haji Mwalimu akitoa rai kwa waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo (hawapo pichani) na kuwataka kutumia kalamu zao vizuri na kuhakikisha kampeni hii inafanikiwa.
Vitali Maembe akitoa vionjo vya wimbo wake Vuma.
Vitali Maembe akionyesha moja ya kazi zake za sanaa atakazoenda kuzitundika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro panapo majaliwa.
Picha ya pamoja baada ya mkutano na waandishi wa habari.
Saturday, July 19, 2014
Wema Sepetu 'Amlipua' vibaya Kajala -
![]() |
| Wema Sepetu (R) na Kajala |
Kutoka BONGO MOVIES. COM
Ikiwa ni siku chache zimepita baada ya mwigizaji Kajala kudai kuwa mrembo Wema Sepeteu ni Mnafiki, hatimaye Mwanadada Wema Sepetu , amemlipua aliyekuwa shosti wake, Kajala Masanja ‘K’ ambaye wiki iliyopita alimwita mnafiki, habari ambayo ilisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
Katika habari hiyo, Kajala alikaririwa akisema kwamba licha ya watu wengi kuamini wamepatana, hakuna ukweli kwani rafiki yake huyo ni mnafiki kufuatia kutomthamini na kutokuwa karibu naye kama zamani likiwemo suala la kumsifia mtu ambaye alikuwa na ugomvi na Kajala (Dacutee).
Akizungumza na mwanahabari wetu, Wema alisema alishangaa kuona Kajala anamwita mnafiki wakati hakuwahi kupatana naye tangu walipotofautiana kipindi cha nyuma kama alivyosema.
“Nashangaa Kajala ananiambia mimi ni mnafiki ‘ok fine’ na huo unafiki wangu unakuja pale nilipomu-wish Dacutee siku yake ya kuzaliwa, alitakaje eti? Yaani kwa kuwa yeye ana bifu la kumchukulia bwana’ke na mimi nijiingize kwenye bifu lao?
“Au tofauti zangu mimi na yeye, Aunty Ezekiel aingilie, itakuwa sahihi kweli kama wanavyofanya hao watu wake anaozurura nao siku hizi? Wanaingilia vitu ambavyo hawavijui kiundani wake? Nasema siyo sahihi kabisa mimi nitabaki kama Wema Sepetu na yeye atabaki kama Kajala Masanja na asifikirie kuwa nitakuja kuwa kama zamani na yeye halafu kama anamaindi kuhusiana na Dacutee mbona Petit Man ambaye ana uhusiano naye aliweka picha.
BOFYA HAPA KUSOMA HABARI KAMILI BONGO MOVIES.COM
Friday, December 21, 2012
Rais Kikwete Apongezwa na Wasanii Wakongwe Kwa Kuwajali
Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo Desemba 21, 2012 amepokea ujumbe wa wasanii wakongwe wa muziki wa dansi pamoja na filamu uliomtembelea Ikulu jijini Dar es salaaam kwa kuwajali wasanii wa aina zote na hata kuamua kutoa tuzo kwa wasanii ambapo mwaka huu amewatunuku Muhidin Maalim Gurumo na Hayati Marijani Rajabu.
PICHA NA IKULU
Wednesday, April 06, 2011
Wasanii na Wadau wa Filamu Tanzania Wapata Mkombozi wa Kweli
www.kasyome.bogspot.com+255 7141696655
Ukizungumzia tasnia ya filamu za Kitanzania kwa kuwataja wanaharakati au wadau wanaooiinua na kuipigania filamu, ni nadra sana kuacha kuwataja waigizaji maarufu, vikundi vyenye majina makubwa, taasisi, vyama au makampuni.
Steven Kanumba "The Great", Vincent Kigosi "The Greatest", Suzan Lewis "Natasha", Charles Magari "Mzee Magari", Blandina Chagula "Johari" na wengine wengi, ni miongoni mwa waigizaji ambao ni lazima uwataje kama ukitakiwa kuwataja waigizaji "wanaipiga tafu" tasnia ya filamu nchini.
Wadau wengine ni kwa mfano, makundi ya Mambo Hayo na The Spendid, yaliyotamba enzi zao na kuibua changamoto ambazo hadi sasa zinaonekana. Mengine ni Kaole Sanaa Group na Jakaya Arts Group.
Taasisi kama kituo cha Utamaduni cha Muungano wa Urusi na Tanzania (Russian - Tanzania Culture Center), taaisisi ya watu wa Ujerumani (Goethe Institute), Game 1st Quality, Steps Entertainment, BASATA, COSOTA na TAF.
Pamoja na wadau na wanaharakati mbalimbali, msanii bado hana mafanikio! bado ni omba omba! Wengi wenye maisha mazuri, si kutokana na filamu! Ni kutokana na background ya familia yake au kipato chake kingine nje ya filamu! wakiwa kwenye vyombo vya habari wanaficha ukweli ili wajikweze kwa kuwa wengi wao wanaingia kwenye taaluma ya filamu "kuuza sura"!
Mzalishaji, anaeumiza kichwa kutafuta mtaji na kuandaa bajeti ya filamu, uandaaji hadi kukamilika, bado hana sauti wala nguvu sokoni! Anafanya kazi kwa shinikizo la woga wa soko! Hana uhakika wa soko lake endapo atakuwa jeuri! kinachobaki ni kuweka mikono nyuma awapo mezeni ili filamu yake isambazwe! Haijalishi atalipwa kiasi gani!
Msambazaji, anatupiwa lawama za unyonyaji, Buguruni na Ubungo, filamu za elfu tano dukani, zinauzwa elfu moja moja! Muigizaji, ndugu jamaa na marafiki wanazinunua kwa wingi!
Mnunuzi wa mwisho bado anafuata mkumbo wa nguvu ya msambazaji bila kujali ubora filamu kuanzia kwa mtunzi wa hadithi, muigizaji, muongozaji, mpiga picha, mbamaji, mazingira na taaluma ya filamu yote! Ananunua filamu kwa mazoea ya majina na hadithi!
Idea For Action Tanzania (IFA Tanzania), mradi uliobuniwa kitaalamu, ni miongoni mwa wadau wa kweli na wa dhati kabisa katika kiwanda cha filamu za kitanzania.
Ni mradi wa kuibua na kuendeleza vipaji vya sanaa kwa kutoa elimu ya sanaa na ujasiriamali, bure, bila ada yoyote! Kila mdau wa sanaa anaalikwa kuhudhuria mafunzo.
Mafunzo haya yatolewayo kwa lugha anayoielewa kila mtanzania (Kiswahili) yanakwenda kwa muda wa miezi mitatu. Mlengwa anatakiwa kujiunga muda wowote na kuanza mafunzo baada ya kujaza fomu ya kujiunga. Hakuna umri, kabila, dini wala kiwango cha elimu kinachofaa kupata mafunzo isipokuwa yeyote mwenye mapenzi mema na sanaa na anayejua kusoma na kuandika, anapaswa kujiunga.
Baada ya kumaliza mafunzo, mwanafunzi anasimamiwa na wataalamu kufanya mafunzo kwa vitendo kwa vitendo ili kuthibitisha uelewa wake na kutunikiwa cheti cha awali cha kuhitimu.
Mwisho, mhitimu akipenda ataunganishwa na makampuni au taasisi wadau kufanya kazi kwa mkataba wa miaka miwili ili kuzidi kuapata uzoefu wa kazi ya sanaa na atabakiwa kuwa mwanachama wa mradi wa IFA Tanzania maisha yake yote kwa kushirikaina na mradi pale atakapohitajika, kuomba ushauri katika kuanzisha na kuendesha miradi mbali mbali ya sanaa na mambo mengine ya kimaendeleo.
Mradi huu ambao ni endelevu, umegawanywa katika vitengo vinne vya filamu, muziki, vichekesho na biashara. Tuzungumzie kitengo cha filamu. Ndani ya kitengo hiki, zinafundioshwa mada nane,saba ni taaluma ya filamu na moja na ujasirimalia wa filamu (Interprenuereship in Film Production)
Mada hizo saba ni Utunzi na Uandishi wa Hadithi (Screenwriting), Uigizaji na Upangaji wasanii (Acting and Casting), Upigaji wa picha (Cinematography), Ubunifu wa Sauti (Sound Designing), Ubunifu wa Uzalishaji (Production Design), Uongozaji/Uzalishaji/Masoko (Directin/Producing/Marketing) na Uhariri(Editing).
Malengo makubwa ya IFA Tanzania, kitengo cha filamu ni matatu. Kutoa taaluma ya filamu ili mnufaika aitambue filamu na kujitambua awapo ndani ya filamu.
Hilo mosi.
Pili, kutoa elimu ya ujasiriamali baada ya taaluma ili kugundua, kutambua na kutumia fursa mbalimbali zilizopo na kupata mafanikio kabla ya kumpelekea msambazaji!
Msambazaji awe mdau wa mwisho kwa mapato ya mzalishaji wa filamu za kitanzania! Tofauti na ilivyo sasa, ambapo mzalishaji ni lazima akampigie magoti msambazaji! Tena kwa kazi iliyomtoa jasho!
Tatu, ambalo ni kubwa zaidi, kuokoa utamaduni wetu. Uzalendo, haki na utaifa uwekwe mbele zaidi wakati elimu na burudani ikiimilishwa kitaalamu kama dhima kuu ya filamu ambayo ni kazi ya sanaa katika jamii.
Malengo ya mradi ni kumzalisha mtaalamu wa filamu mwenye mbinu za ujasiriamali ili atazame, azalishe au kushirikishwa katika filamu zinazozungumzia visa vya vita, magonjwa, upelelezi, tatizo la ukosefu wa ajira, njaa, afya, elimu n.k.
Iweje filamu za kitanzania ziwe na ujumbe wa kisa kimoja cha mapenzi pekee? Je, Je ni makosa kuzungumzia visa vingine? Utamaduni wetu wa sasa kwa vizazi vijavyo, utakuwaje? Tunaijenga Tanzania ijayo au tunaibomoa?
Tunasikitishwa sana na mfumo wa filamu zetu kiutendaji na kibiashara. Tunapoteza utamaduni kwa faida fulani fulani. Nani alaumiwe kati ya muigizaji, mzalishaji, msambazaji au mnunuzi wa mwisho?
Justin Kasyome, anaendelea, IFA Tanzania, ni mradi wa kizalendo, tunapigania utamduni wa mtanzania kwa kutengeneza faida inayokubalika katika mfumo mzuri kimasoko. Watanzania tujikomboe, elimu pekee ndio silaha yetu. Kwa pamoja tutshinda na kumwondoa adui yetu.
IFA Tanzania, inapatikana ndani ya majengo ya Chuo Cha Elimu Kuu Sanaa, eneo la Sinza Legho, barabara ya Shekilango, mkabala na Club ya Sun Cirro. Au kwa mtandao wa www.ifatanzania.blogspot.com
Friday, August 27, 2010
Hii Itasaidia Wasanii Tanzania Kweli?
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
USHIRIKI WA WASANII WASIOSAJILIWA KWENYE TUNZO NA MATUKIO YA SANAA NCHINI
Baada ya BASATA kusimamia na kuratibu uanzishwaji wa Mashirikisho manne ya Sanaa nchini ambayo ni Shirikisho la Sanaa Jongevu (Filamu), Shirikisho la Muziki Tanzania, Shirikisho la Sanaa za Maonyesho na Shirikisho la Sanaa za Ufundi kwa lengo la kuvipa nguvu vyama vya wasanii na kuvipa umoja kitaifa,Baraza linapeleka nguvu kwenye urasimishaji wa sekta ya sanaa ikiwa ni pamoja na wadau wote wanaojihusisha na sekta hiyo hususan wasanii.
Kwa mujibu wa Sheria na. 23 ya Bunge ya mwaka 1984, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepewa jukumu la kutambua na kusajili wadau wa Sanaa, kumbi zote za burudani Tanzania Bara na wasanii wote ikiwa ni pamoja na kutoa vibali vya kufanya shughuli za Sanaa.
Lengo ni kuzifanya shughuli za sanaa kufanyika katika mazingira rasmi na ya kufuata sheria za nchi pia kuwatambua wasanii wote nchini kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi yetu.Ikumbukwe kwamba, kufanya shughuli za sanaa bila kusajiliwa na kupewa kibali na BASATA ni kuvunja sheria za nchi na hivyo kustahili adhabu.
Faida za kurasimisha sekta ya sanaa hususan kwa wasanii
1. Kuendesha shughuli za sanaa kwa mujibu wa Sheria za nchi ili kuepuka usumbufu.
2. Kutambulika kwa shughuli ya msanii binafsi, kikundi, Chama nk. hivyo kufanya kazi kihalali.
3. BASATA kama shahidi wa Jamhuri hutoa utambulisho/uthibitisho kwa msanii, kikundi au chama halali mahali popote panapohitajika kwa mfano wakati wa kufungua akaunti benki, kupata VISA, pasi ya kusafiria, mikopo kwenye asasi za fedha, msaada au ushahidi mahakamani.
4. Ikihitajika kuweka ulinzi wa kisheria wa kazi za sanaa,kwa mfano wa Hakimiliki na Hakishiriki.
5. Kuingilia kati pale makubaliano/mikataba ya msanii, kikundi, chama nk. inapokiukwa na kuripotiwa katika Baraza.
6. Kushauri na kutoa mafunzo ya sanaa.
7. Kutafutiwa masoko na/au kuunganishwa na masoko, wasanii na fursa mbalimbali zinapojitokeza.
BASATA linawaagiza waandaaji wa matukio ya sanaa nchini (Tunzo za Sanaa/matamasha/maonyesho) kuhakikisha wanafanya kazi na wasanii waliosajiliwa tu na inapotokea kufanya vinginevyo basi muandaaji wa tukio husika na msanii atawajibika moja kwa moja.
BASATA linatoa hadi tarehe 31 Oktoba, 2010 kwa wasanii na wadau wote nchini kujisajili vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwazuia wasanii pia wadau wasiosajiliwa kushiriki tunzo/matamasha/Matukio ya Sanaa.
Ghonche Materego
KATIBU MTENDAJI, BASATA.
Thursday, March 18, 2010
Ray na Vincent Wanatafuta Waigizaji wa Kike Wapya!
03/18/2010
Kama unajihisi wewe ni mrembo basi kwa sasa tunatafuta wasanii wapya wa kike katika ofisi za RJ COMPANY zilizoko SINZA MORI. Lengo ni kuwapata wasanii wa kike ambao ni wapya katika tasnia ya filam nchini ili waje kushiriki katika filam mpya itakayoandaliwa na kampuni ya RJ. Umri ni kuanzia miaka 18 mpaka 28. Pia unaweza kutuma picha zako kabla hufika ofisini ili tuweze kukuona jinsi ilivyo.Muda wa ofisi ni saa 4 kamili asubuhi mpaka saa 12 jioni kwa siku za Jumatatu mpaka Ijumaa na siku za Jumamosi kuanzia saa 4 kamili asubuhi mpaka saa 8 mchana. HAKUNA GHARAMA ZOZOTE ZILE UTAKAZOLIPISHWA KWANI KAMPUNI INAJITOSHELEZA.
WASILIANA NA VINCENT aka RAY KUPITIA:Tel: +255 714 082729P.O. Box 11347
Email: vincentkigosi@gmail.com
Website: www.rjtanzania.com
*****************************************
Hapo napingana na Ray. Yaani watu zaidi ya miaka 28 hawawezi kuwa warembo? Angesema anatafuta kuanzia 18+. Katika sinema unahitaji waigizaji wa kila umri. Mambo ya vijana kujifanya wazee haipendezi. - Chemi














