Nimepata kwa E-Mail:
WAZIRI Mkuu Mstaafu Mhe. Fredrick Sumaye,ameiangukia serikali na kuomba
msaada baada ya wananchi kuchukua sheria mkononi na kuvamia eneo lake
la ekari 33 lililopo Mabwepande katika Manispaa ya Kinondoni nje kidogo
ya jiji la Dar es salaam. Serikali imemuahikikishia Mhe. Sumaye kuwa
haina mpango wa kumkandamiza mtu mnyonge wala tajiri hivyo itahakikiha
inatoa haki kwa kila mmoja baada ya wiki mbili kwa kua imesikiliza pande
zote mbili katika mgogoro huo.
Akizungumza katika kikao cha
pamoja kati ya wananchi wa kitongoji cha Kimondo mtaa wa mji mpya Kata
ya Mabwepande na Mhe.Sumaye Dar es Salaam leo asubuhi, Mkuu waWilaya ya
Kinondoni Paul Makonda alisema ili kumaliza mgogoro huo ambao Waziri
Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye ameiomba serikali kuingilia kati ni lazima
busara kutumika. Alizitaka pande hizo mbili kuiachia serikali kwa wiki
mbili ili kutafuta njia bora ya kumaliza tatizo hilo huku wananchi
wakitakiwa kuache kuendelea na ujenzi na kugaiana maeneo katika shamba
hilo.
“Serikali ya Rais Magufuli ni sikivu na ndio maana ilikuwa
tayari kumsikiliza Waziri Mkuu wetu Mstaafu Sumaye na kusikiliza
wananchi ili kutenda haki tunatambua migogoro ya ardhi ilivyokuwa na
athari kwa jamii hatuna mpango wa kumkandamiza tajiri wala
mnyonge,”alisema. Alisema katika eneo hilo anajua jinsi wananchi
walivyotumia nguvu katika kuwekeza ujenzi na rasilimali zao lakini kwa
sasa wasitishe shughuli hizo na kuendelea kugawana maeneo na Sumaye pia
kuacha uwekezaji ili kutafuta suluhu.
Zipo njia nyingi
tutazitumia kumaliza mgogoro huu ikiwemo kufuata sheria kwa kuangalia
iwapo mzee wetu alikiuka taratibu kweli za kumiliki ardhi kama
ilivyodaiwa na wananchi hatua gani serikali tuchukue,”alisema. Alisema
pia wanaweza kukaa na Sumaye na kuzungumza naye ili kukubali hasara kwa
kutoa eneo kidogo na kuwapatia wananchi hao ambao hawana makazi au
Manispaa kutafuta eneo mbadala na kuwauzia kwa bei nafuu.
Alizitaka pande hizo mbili kutambua umuhimu wa kulinda amani katika
mgogoro huo kwa changamoto zilizopo kutatuliwa bila kutumia
nguvu.Makonda pia aliagiza serikali ya kijiji kufanya utambuzi wa
wananchi hao wenye makazi katika shamba la Sumaye. Awali katika mkutano
huo Mhe. Sumaye alimueleza Mhe. Makonda jinsi serikali ilivyo na kazi
ngumu ya kushughulikia migogoro ya ardhi na kuomba kutumia busara zake
kumpatia eneo hilo analomiliki kihalali.
“Mheshimiwa Mkuu wa
Wilaya kama nilivyokueleza awali serikali yetu inakazi ngumu sana hasa
kutokana na viongozi wa chini kutokuwa wasikivu na wakweli eneo hili
namiliki kihalali nina nyaraka zote na ninalipia kila mwaka na nilikuwa
katika mpango wa kutafuta wafadhili ili kuliendeleza kwa kujenga Chuo
Kikuu,”alisema. Alisema yeye na familia yake waliuziwa eneo hilo toka
mwaka 1997 na anaamini serikali itatenda haki.
Diwani wa kata
hiyo Suzan Masawe alisema anauthibitisho kuwa eneo hilo lilikuwa pori na
Sumaye alilitelekeza kwa muda mrefu na kusababisha uhalifu ikiwemo
wanawake kubakwa,mali za wizi kufichwa na uhalifu mbalimbali. Alisema
kutokana na hatua hiyo walimtafuta Sumaye lakini hakuwa na ushirikiano
kwakuwa hata alipofanya uwekezaji kwa kuchimba kisima cha maji alikataa
kuwapa wananchi .
Suzan alisema kutokana na hasira za wananchi
hao kwa kukosa huduma za kijamii kwa muda mrefu ikiwemo eneo hilo
kutokuwa na shule,Zahanati wala kituo cha polisi waliamua kuvamia na
kujigaia maeneo. Mmoja wa wananchi hao Athuman Mnubi alikiri kweli
hawana umiliki halali wa eneo hilo na katika hatua ya kutafuta makazi
walivamia msitu huo uliotelekezwa na Sumaye.
Alisema wanaamini
kutokana na ahadi ya serikali ya Rais Magufuli katika kupora maeneo
yaliyotelekezwa na wawekezaji watasaidiwa. WAKATI huo huo Makonda
alisimamisha na kukamata baadhi ya malori ya kokoto na mchanga,
wafanyakazi na Mwekezaji wa kigeni kutoka India Sules Waljan wanaochimba
mchanga,kokoto na kifusi katika eneo la Mabwepande. Hatua hiyo imekuja
baada ya kuona uharibifu mkubwa wa mazingira na alipowahoji wafanyakazi
na Mwekezaji huyo kama wanavibali walisema hawana.
Makonda
amewafikisha watuhumiwa hao kituo cha polisi cha Wazo Hill ili kutoa
maelezo ya kina na kusema kuwa serikali inatumia gharama kubwa kwa
uhalibifu huo wa mazingira ambao pia unafanywa katika vyanzo vya maji na
matengenezo ya madaraja yanayoharibiwa ni makubwa.
No comments:
Post a Comment