TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu wanahabari,
Kwa muda sasa kumekuwepo na usambazaji wa
taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wakishirikiana na
baadhi ya vyombo vya habari zinazolenga kukejeli, kudhihaki, kukatisha tamaa,
kubeza na kudhoofisha jitihada zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi na Serikali
zake katika kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Kumekuwepo na makala zinazoandikwa na
magazeti mawili ya nje ambazo hutolewa kila baada ya miezi miwili na ambazo
zinapotosha na kuandika habari zisizo za kweli kuhusu Tanzania.
Pia, yapo magazeti mawili ya ndani ambayo
yamekuwa yakitoa makala mfululizo kwa kila wiki zinazolenga kumchafua
Mheshimiwa Rais na kuichafua taswira ya nchi yetu.
Tumesikitishwa na waandishi wa makala hizo
walioamua kujivua uzalendo na kushiriki mpango wa kuiharibu heshima na taswira
ya nchi yetu kwa maslahi ya maadui zetu wa nje na baadhi ya wanasiasa.
Tunafuatilia kujua nini kinawasukuma kufanya hivyo na kwa maslahi ya nani ilhali
sote ni Watanzania. Je ni tamaa ya madaraka tu au mengine? Hakuna anayepinga
ukosoaji bali unapaswa uwe ukosoaji wenye nia njema kwa nchi.
Ndugu wanahabari,
Mtakumbuka hivi karibuni aliyewahi kuwa
Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa tuhuma za ufisadi ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu
ya CHADEMA, Edward Lowassa, alisambaza taarifa kwa vyombo vya habari aliyoiita
ya tathmini ya mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015.
Katika taarifa yake hiyo, alidai kuwa alileta
msisimko mpya katika siasa za Tanzania, kwamba ameshirikiana na wenzake kuionyesha
nchi yetu maana ya demokrasia na kukosoa juhudi za serikali na wateule wa Rais.
Demokrasia kimsingi ni dhana inayohusisha
ushiriki na kuheshimu mawazo ya wengi katika kufikia uamuzi. Ikiwa maana halisi
ni hii, tunajiuliza ni ipi demokrasia aliyoionyesha Lowassa ambayo leo
anajisifu kuwa nayo?
-
Tulishuhudia akiwa mgombea urais wa chama ambacho hakijui,
hakushiriki kukijenga wala kutoa mchango wowote unaompa hadhi ya kupeperusha
bendera huku katiba na kanuni ya chama hicho
ikivunjwa. Kidemokrasia, anayepewa
fursa ya kupeperusha bendera ya chama chochote makini duniani ni kiongozi au
mwanachama aliyethibitika kwa imani na matendo, kuzielewa, kuzitekeleza,
kuzitetea falsafa, itikadi na malengo ya msingi ya chama hicho. Mgombea ni
taswira halisi na alama muhimu inayoakisi dhamira ya chama husika machoni kwa
wananchi.
-
Demokrasia ya kweli lazima ianzie ndani ya chama, ni demokrasia
ipi iliyotoa mamlaka kwa vyama vinavyounda UKAWA kuwanyima wanachama wao haki
ya kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera za vyama walivyoviasisi, kuvitetea,
kuvigharamia na walivyovitumikia kwa kuamua kumteua mgombea “MTUNGUO” (ambaye hajapimwa wala hajawahi
kuvipigania). Kitendo hicho cha kutowashirikisha wanachama na kuwanyima haki
yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kilidhihirisha usaliti wa hali ya
juu wa misingi ya demokrasia.
-
CHADEMA watuambie njia iliyotumika kuwapata wabunge wa viti
maalumu. Ni demokrasia gani inayotoa fursa kwa baadhi tu ya viongozi kuteua wabunge ambao wanakiwakilisha chama
chote. Ambapo kila kiongozi aliteua maswahiba zake na wengine kwa ugeni wao
ndani ya CHADEMA walikosa watu wanaowafahamu na kuamua kuwateua wanawake
maswahiba wao ndani ya CCM. Msingi wa kawaida wa kupata wabunge wa viti maalum
ukiacha kura za maoni, kigezo kingine muhimu ni mchango wa mgombea/mwanachama
huyo katika kukijenga na kukitumikia chama chake. Yaliyotokea kwa CHADEMA
kwenye wabunge wake wa viti maalum ni mapya kwenye ulimwengu wa demokrasia.
Inahitaji wataalamu wa sayansi ya siasa kufanya utafiti wa aina hii mpya ya
demokrasia.
Tulidhani baada ya mwaka mmoja kupita,
wenzetu hawa wangelikuwa wamejifanyia tathmini, kujikosoa, kujisahihisha na
hata kufanya uungwana wa kuwaomba radhi wanachama wao kwa uvunjifu mkubwa wa
misingi ya demokrasia, katiba na kanuni za vyama vyao.
Tunatoa wito kwa vyama vya siasa nchini
kutochukulia kwa wepesi masuala ya demokrasia na mabadiliko, yasiwe ni nyimbo
za kuburudisha au kutoa matumaini hewa kwa wanachama na wananchi. Kanuni
mojawapo ya demokrasia ndani ya vyama ni lazima ionekane katika muundo wake na
katika utekelezaji wa muundo huo.
Umefika wakati vyama vya siasa vinapaswa
kujifunza kuuza sera ili kujijenga na sio kusubiri matukio kwa ajili ya kupata
huruma ya wananchi. Tunasubiri kushuhudia na kusikia demokrasia
itakavyoendeshwa katika uchaguzi wa ndani wa vyama hivyo ambapo kuna taarifa
mmoja wa vigogo amefanikiwa kupata kiasi cha dola milioni 15 zitakazomsaidia
kupanga safu yake ya uongozi.
Katika kutimiza mpango huo, tayari yapo mawasiliano
ya mara kwa mara ya baadhi ya viongozi wakitoka Zanzibar na sehemu zingine za
nchi kuja Dar es Salaam, na imeonekana dhahiri mazungumzo yao kutowashirikisha
viongozi wenzao waandamizi kwani yanalenga kufanikisha mpango huo.
Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli,
ameendela kufanya juhudi kubwa katika kuijenga nchi kwa kuimarisha utendaji na
nidhamu ya utumishi serikalini, kukusanya mapato na kusimamia matumizi sahihi
ya fedha, kupambana na kuzuia mianya ya rushwa pamoja na kusimamia haki, usawa
na wajibu kwa raia. Mwenzetu anayaona haya kuwa ni kuufanya utumishi wa umma
kaa la moto.
Juhudi hizi na nyinginezo ikiwemo ununuzi wa
ndege mpya, ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, afya kwa kununua vitanda
vya wazazi, kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na nyinginezo hazipaswi kukatishwa tamaa kwa
maslahi ya wachache, ni vyema kuziunga mkono kwa maslahi ya taifa letu.
Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Rais
Dk. Magufuli madarakani, CCM inawaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono katika
dhamira yake safi ya kuwaondolea kero, kuboresha huduma za jamii na kuwaletea maendeleo
ya kiuchumi na kijamii.
KIDUMU CHAMA
CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;-
CHRISTOPHER
OLE SENDEKA
MJUMBE WA
NEC NA MSEMAJI WA CCM
28/10/2016.
No comments:
Post a Comment