IJUE PIANO –
NA MANUFAA YAKE
Na Freddy Macha
KWA SIMU TOKA
LONDON- Mitaani na muziki wa Kizungu
Piano (au
kinanda) ni chombo mahsusi cha Wazungu.
Kitaaluma muziki
maana yake ni vitu vitatu : melodi (unayoisikia bila hata kujua maneno na
kuipigia uluzi), ridhimu (mapigo), na mpangilio wa sauti (“harmony”). Kipengele
cha tatu ndiyo kigumu zaidi....
Kati ya vyombo
muhimu vya kitengo cha utunzi na
upangaji (“harmony”) wa muziki ni Piano na Gitaa.
Ila Piano
inaongoza Uzunguni.
Ndiyo maana kila utakapokwenda, makanisani, mabaa, mashuleni, majumbani na
hata vituo vya usafiri hukosi Piano. Kihistoria, watunzi mashuhuri wa muziki
ulimwenguni wametumia Piano kupanga vibao vyao vilivyofahamika na kupendwa
miaka mingi zaidi.
Mifano michache ni George Gershwin (“Summertime”- 1934), Stevie Wonder (“Superstition”, 1973 ), Billy
Joel (“I love You Just the Way You are”-
1977) , Herbie Hancock (“Watermelon Man”, 1962), Paul McCartney ( “Nyimbo za
Beatles, “Let it Be”, “Long Winding
Road”, “Yesterday”, nk), Prince (”When Doves Cry”, 1984), Gill Scott Heron
(Mtunzi mashuhuri wa Mashairi aliyefariki 2011), na Alicia
Keys , binti , kijana anayewika sasa.
Hata wanamuziki
waimbaji walipiga piano, ingawa si sana hadharani. Prince, Michael Jackson,
James Brown, nk.
Afrika yetu
tunao marehem Fela Kuti na Abdullah Ibrahim (Afrika Kusini) anayeheshimika kama
mmoja wa wapiga piano wakubwa duniani wa Jazz. Watanzania marehemu Patrick
Balisidja na Kassim Magati (Sunburst) vile vile. Miaka yake ya mwisho
marehem Balisidja alipiga Piano akiwa na King Kiki.
Kimuziki Piano ni kama kamusi. Ni muhimu kuijua
kuelewa nini kinatendeka katika moyo, ngozi na mifupa ya muziki.
Kiafya upigaji Piano
huoanisha pande mbili za Ubongo na kuzuia kuchakaa kwake. Hivyo kwa Wazee na watu wa makamo ni kinga
maradhi ya kusinyaa na kulemaa Ubongo mathalan “Dementia” na “Alzheimer”...
Hii ni sababu mkono
mmoja hufanya tendo tofauti na mwingine,
unapotwanga Piano.
Kufuatana na
maelezo ya mwanasayansi wa Kimarekani, Roger Sperry (aliyeshinda tuzo la Nobel 1981)
upande wa kushoto wa Ubongo hufikiri, na kulia mambo ya hisia na utunzi. Bw Sperry alifikia
ugunduzi huo akifanya utafiti wa kiini cha Kifafa.
Ni vizuri pia kwa watoto wadogo na huwasaidia
kufanya vyema katika masomo yote. Ndiyo maana muziki na Sanaa (kijumla)
huzingatiwa sana mashuleni Uzunguni.
Mwafrika jifunze
Piano hata kama unaanza kuzeeka, itakufaa.
Na wasisitize wanao kufanya muziki na sanaa, utawajenga kiakili katika
hesabu na sayansi pia.
No comments:
Post a Comment