TAMWA kutoa elimu kupambana na ulevi Kupindukia
![]() |
| Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka akisisitiza jambo katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo. |
KITUO
cha Usuluhishi (CRC) kinachofanya kazi chini ya Chama cha Wanahabari
Wanawakecha (TAMWA) kimejipanga kutoa elimu kwa jamii kuhakikisha
kinapambana na matumizi ya pombe kupindukia kwa jamii suala ambalo
limezidisha vitendo vya ukatili wa jinsia unaofanywa na watumiaji pombe
kupindukia.
Akizungumza na
wahariri wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa
TAMWA, Valerie Msoka alisema utafiti uliofanywa na Shirika la IOGT
International unaonesha kuwa kiwango cha unywaji pombe jijini Dar es
Salaam ni asilimia 47.6 kwa wanaume na asilimia 29 kwa wanawake huku
ikibainika kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya vitendo vya ukatili na
matumizi ya pombe kupita kiasi.
Bi. Soka
alisema takwimu zinaonesha kuwa wanawake ambao waume zao wanalewa mara
kwa mara wengi wao wanakumbana na ukatili unaohusisha vipigo, kuumizwa
na ukatili wa kingono kwa asilimia 77, huku kiwango cha ukatili kwa
wanawake ambao waume ama wenzi wao hawanywi pombe ni asilimia 33.
"...Utafiti
uliofanywa na shirika la IOGT International unaonyesha kwamba kiwango
cha unywaji pombe katika jiji la Dar es Salaam ni asilimia 47.6 kwa
wanaume na asilimia 29 kwa wanawake...lakini takwimu kutokana na utafiti
wa Demographia na Afya Tanzania (TDHS) 2010...unaonesha wanawake ambao
waume zao wanalewa mara kwa mara wengi wao wanakumbana na ukatili
unaohusisha kipigo/kuumizwa na ukatili wa kingono kwa asilimia 77,"
alisema.
Aidha
aliviomba vyombo vya habari kushirikiana na TAMWA kutoa elimu kwa jamii
kupunguza matumizi ya pombe kupindukia kwani licha ya ukatili huo
familia pia zimekuwa zikiathirika kiuchumi juu ya matumizi ya pombe huku
baadhi ya watoto wakikosa huduma za msingi kutoka kwa baadhi ya wazazi
ambao ni walevi kupindukia.
Alisema TAMWA
inatekeleza mradi wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana
unaosababishwa na pombe huku lengo kuu ikiwa ni kuhakikisha maisha ya
wanawake na watoto yanaboreshwa kwa kuimarisha sheria na kupunguza
ukatili wa kijinsia unaosababishwa na unywaji wa pombe kupindukia.
Hata
hivyo alisema tayari chama hicho kimeanza kufanya utafiti mwingine
katika Wilaya ya Kinondoni kuangalia madhara yanayotokana na unywaji wa
pombe kupindukia ili kuangalia hali halisi ya matumizi ya pombe eneo
hilo na madhara ambayo yamekuwa yakitokana na matumizi hayo.
Alisema
malengo mengine ya mradi ni pamoja na kuboresha maisha ya wanawake na
watoto kwa kuimarisha sheria na kupunguza ukatili wa kijinsia
unaosababishwa na unywaji wa pombe katika wilaya ya Kinondoni na pia
kujenga uelewa miongoni mwa jamii juu ya madhara yatokanayo na unywaji
wa pombe kupindukia.
Mkurugenzi
huyo Mtendaji wa TAMWA aliongeza kuwa mapambano hayo pia yatasaidia,
kukabiliana na matumizi ya pombe na kutoa taarifa kwa vyombo husika
kuhusu ukatili dhidi ya wanawake unaotokana na matumizi ya pombe, ikiwa
ni pamoja na kujenga uwezo wa jamii kukabiliana na ukatili
unaosababishwa na unywaji wa pombe dhidi ya wanawake na watoto.


