Saturday, March 18, 2017
Dk. Ryoba Awaona Waanidshi wa Habari wa Uhuru Leo
Saturday, May 03, 2014
Waandishi wa Habari Msikubali Kutumiwa
Baadhi ya waandishi wa habari na wadau kutoka asasi mbalimbali nchini wakifanya usajili kwenye kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini Arusha.(Picha na Zainul Mzige).
Na Waandishi Wetu, Arusha
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuyapa uzito matukio yanayowatokea waandishi wa habari na kuyapigia kelele kwa nguvu zote ili kuyakomesha.
Kibanda aliyasema hayo jana mjini Arusha katika kongamano lililoandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani na kuongeza kwamba wakati umefika kwa waandishi wa habari kuondoa tofauti zao na kuungana pamoja kuongeza nguvu waliyonayo kukabiliana na ukatili unaoendelea dhidi ya waandishi wa habari katika miaka ya hivi karibuni.
“Baadhi ya wahariri huwa hawayaandiki madhila yanayowasibu waandishi wa habari na kuyapa uzito unaostahili aidha kwa huyapuuzia au kudharau kwa kuwa hayawahusu moja kwa moja,” alisema Kibanda.
Aliongeza kwa kusema kuwa vyombo vya habari mara nyingi vimekuwa vikinyooshewa vidole na kulaumiwa kwa kutokufanya kazi kwa uadilifu jambo ambalo linatafsiriwa kuwa ni la uonevu, vinatumiwa vibaya na hakuna anayesimama kuvitetea kutokana na mchango wake mkubwa katika jamii.
Afisa Mipango Kitengo cha Mawasiliano, Habari na Tehama UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph, akiwasilisha mada kuhusu mchango wa uhuru wa vyombo vya habari katika utawala bora, kukuza uwezo na kupunguza umaskini kongamano la waandishi wa habari lilioandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanayofanyika jijini Arusha.
“Kwa sasa tasnia hii iko kwenye wakati mgumu sana kwani hata marais wa nchi mbalimbali mfano Uganda, Kenya hata Marekani wanakinzana na vyombo vya habari kwa madai kuwa kauli zao zinapotoshwa, laikini ukweli ni kwamba ni vyema kauli hizo za viongozi zikachunguzwa kwa undani zaidi ili kuelewa iwapo zina uwajibikaji ndani yake,” alisema Kibanda.
Kibanda aliongeza kuwa wakati umefika sasa kwa waandishi kutambua kuwa kuna ajenda za siri zilizojificha dhidi ya uteswaji wa waandhishi wa habari hivyo yasidharauliwe, yafanyiwe kazi kwa kina ili kuelewa kiini cha tatizo kwa kupata ufumbuzi.
Kwa upande wake mwandishi mkongwe na aliyetunukiwa tuzo ya maisha mwaka 2012 na Baraza la Habari Hamza Kasongo alisema vyombo vya habari vina nguvu kubwa katika kushawishi hivyo vitumie nguvu hiyo kama muhimili wa nne wa nchi katika kuzikabili changamoto zilizopo.
“Kuwe na mtandao unaoeleweka wa mawasaliano kati ya waandishi wa habari nchini ili kuhakikisha kuwa matatizo yaliyopo yanatatuliwa bila woga na kwa ujasiri kwa lengo la kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa,” alisema Kasongo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Sheria , Bw. James Jesse, akitoa mada kuhusu umuhimu wa sheria katika kulinda haki ya uhuru wa kujieleza kwa kila mtu wakati wa kongamano la waandishi wa habari lilioandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani yanayofikia kilele leo jijini Arusha.
Mwanahabari mwingine mkongwe Dokta Samwilu Mwaffisi aliyetoa mada ya Maadili ya Uandishi wa Habari alisema kuwa kuna haja ya waandishi kuzingatia uhuru wa habari walionao kwa kuzingatia maadili yanayowaongoza ili kuboresha heshima waliyonayo katika jamii kwa kuandika ukweli na uhakika, bila upendeleo, kutoa fursa ya kujitetea na kukubali kuomba radhi pale unapokosea.
“Kuandika habari zenye kuzingatia maadili kunapunguza manung’uniko, mashauri na kuongeza heshima ya chombo cha habari na mwanahabari mwenyewe,”
Akizungumzia suala la ufanisi, Rais wa Vilabu vya Waandishi wa Habari, Kenneth Simbaya, aliwaasa waandishi wa habari kusimamia ukweli katika kazi zao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea jambo ambalo litakawaweka huru zaidi katika utekelezaji wa shughuli zao za uandishi wa habari.
Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na umoja wa asasi mbalimbali chini ya uenyekiti wa MISA TANZANIA unafikia kilele chake tarehe 3 Mei kwa kuzindua majarida mbalimbali, matamko kutoka asasi mbalimbali na kuhitimishwa kwa tafrija ya chakula cha jioni chini ya mgeni rasmi Jaji Mstaafu Mheshimiwa Mark Bomani.
Mwanahabari Mkongwe kutoka Chuo Kikuu Huria, Dokta Samwilu Mwaffisi (kulia) akiwasilisha mada ya Maadili ya Uandishi wa Habari kwenye kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini Arusha. Kushoto ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Iringa, Bw. Simon Berege.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, akitoa maoni yake wakati wa kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini Arusha.
Pichani juu na chini ni baadhi ya waandishi wa habari wakongwe, mabalozi na wanahabari washiriki katika kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini Arusha.
Mwandishi wa Habari Chokonozi, Bw. Fredrick Katulanda, akielezea madhila mbalimbali yaliyomsibu katika utekelezaji wake wa kuandika habari za uchambuzi.
Mwanahabari Mkongwe Bi. Leila Sheikh akichangia mada ya Mchango wa Uhuru Wa Vyombo Vya Habari Katika Utawala Bora, Kukuza Uwezo Na Kupunguza Umaskini wakati wa kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini Arusha.
Mmiliki wa Gazeti tando la Mjengwa na Kituo cha Redio Kwanza Jamii, Bw. Maggid Mjengwa akielezea jinsi Intaneti inavyoweza kuunganisha mtandao wa Redio.
Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania (COMNETA) na Mkurugenzi wa kituo cha mawasiliano Sengerema, Bw. Felician Ncheye akichangia mada.
Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Mama Rose Haji Mwalimu, (kushoto) akiwa na baadhi ya washiriki wa Kongamamo hilo.
Rais wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Bw. Kenneth Simbaya, akishiriki kwenye kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini Arusha.
Picha juu na chini Baadhi ya washiriki wakichangia maoni yao kwenye kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini Arusha.
Kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 likiendelea.
Mwanakamati wa maandilizi ya maadhimisho ya Kongamano la Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 2014, Usia Nkhoma Ledama wa Kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda nje ya ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa AICC jijini Arusha.
Monday, March 18, 2013
Utekaji watu Tanzania: Baada ya Kibanda Nani Atafuata?
Wadau, hivi karibuni yametokea matendo ambayo hatjuazaoea kusikia Tanzania. Waandishi wa Habari, Viongozi wa Dini kutekwa, kuteswa na kuuawa! Gazeti la Mwanachi inachambua.
************************
Kutoka Gazeti la Mwananchi
Posted Jumatatu, Marchi18 2013
Kwa ufupi
Ni matukio ambayo yameacha maswali mengi zaidi ya majibu, huku wengine katika jamii wakisaka mchawi. Polisi na hata vyama vya kijamii, kila mmoja akiibuka na msimamo wake. Hata hivyo, si rahisi kusema ni lini jibu litapatikana!
Padri Auawa Zanzibar kwa Risasi
Tukio lingine ambalo lilishtua wengi ni la kuawa kwa Padri Evarist Mushi, Paroko wa Parokia ya Minara Miwili , Zanzibar. Yeye, aliuawa kwa kupigwa risasi kichwani na kufa papo hapo na watu wasiojulikana asubuhi akielekea kanisani.
Msemaji wa Polisi Zanzibar, Inspekta Mohamed Mhina alithibitisha tukio hilo huku akisisitiza kuwa uchunguzi wa kina zaidi ungefanyika kuhakikisha waliofanya hilo wanachukuliwa hatua.
Mwingine Apigwa Risasi
Awali, Kabla ya kuuawa padri Mushi, padri mwingine, Ambrose Mkenda naye alipigwa risasi na watu wasiofahamika kwenye lango la nyumba yake maeneo ya Kitomondo mjini Zanzibar, ambako ndiko makazi yake yalipo akiwa ndani ya gari aliyokuwa akiendesha pekee yake.
Hali yake siyo nzuri kwani risasi aliyopigwa imemdhuru maeneo ya mdomoni na hadi sasa bado hajaweza kuwa imara. Waliompiga risasi padri huyo inasemekana ni watu waliokuwa kwenye pikipiki, ambao walimvamia akisubiria afunguliwe geti kuingia nyumbani kwake.
Katibu wa Mufti Amwagiwa Tindikali
Pia Zanzibar ilikumbwa na tukio la linalofanana na matukio hayo kwani kiongozi mwingine wa dini aliingia kwenye msukosuko.
Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, alimwagiwa tindikali na watu wasiyojulikana huko Magogoni Msumbiji Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Yussuf Ilembo, alisema Sheikh Soraga alimwagiwa tindikali majira ya alfajiri alipokuwa akifanya mazoezi ya viungo.
Ni kwamba wakati akifanya mazoezi, alimuona mtu akifanya mazoezi akielekea mbele yake na baada ya kukutana uso kwa uso alimmwagia tindikali na kumjeruhi sehemu za usoni na kifua kabla ya mtu huyo kutoweka.
Dk Stephen Ulimboka
Kiongozi wa jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Stephen Ulimboka, saa sita usiku alitekwa, kupigwa na watu watatu wenye silaha na kisha kutupwa maeneo ya mabwepande ambapo aliokotwa na kupelekwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) jijini Dar es Salaam.
Wengi wanahoji sababu ya kutekwa Dk Ulimboka, hasa kutokana na ukweli kwamba si mfanyabiashara…Nani alimteka kwa lipi? Ni swali lisilo na jibu.
Dk Ulimboka aliwahi kuwaambia waandishi wa habari na baadaye akasisitiza kauli hiyo kupitia wanasheria wake, Oktoba 2012, kuwa aliyehusika na mipango ya kutekwa na kuteswa kwake ni Ofisa wa Ikulu. Kama ni kweli, je, ofisa huyo alitumwa au alijituma ? Na je, aliwahi kuhojiwa polisi ili Ikulu ijisafishe kutoka katika madai haya ya Dk Ulimboka?
Waandishi wa Habari Wauawa
Baadhi ya waandishi wa habari waliouawa katika mazingira ya utata ni pamoja na wa Kituo cha Redio Kwizera wilayani Kakonko mkoani Kigoma, Issa Ngumba (45) ambaye aliuawa kwa kunyongwa na kisha kupigwa risasi mkono wa kushoto.
Mwili wake ulipatikana katika pori la Mlima Kajuluheta Kijiji cha Muhange, wilayani humo asubuhi baada ya wananchi kufanya msako wa siku tatu mfululizo bila mafanikio.
Lakini, pia vitendo kama hivyo vinawakuta wenye ulemavu wa ngozi ambao wengi wameathirika , lakini waliohukumiwa kunyongwa tangu mwaka juzi mpaka sasa hawajanyongwa.
Richard Masatu Auawa
Richard Masatu aliuawa Agosti 2011. Yeye, alikuwa Mkurugenzi wa gazeti la KASI MPYA, alifia Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure mjini Mwanza, akipatiwa matibabu. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa marehemu alifariki kutokana na majeraha ya kushambuliwa na watu wasiojulikana.
Friday, April 13, 2012
Baraza la Habari Tanzania Yaja Juu! - Kifo Cha Steven Kanumba
KAMATI ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) leo mchana imetangaza imesikitishwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili uliojitokeza hivi karibuni kwa baadhi ya vyombo vya Habari ambavyo wakati vikiripoti kuhusu kifo cha Msanii Steven Charles Kanumba, vimemhukumu msichana Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu, kuwa amemuua msanii huyo.
Ukiukwaji huo umejitokeza hasa baada ya msichana huyo kufikishwa Mahakamani, ambapo baadhi ya magazeti yanayoheshimika katika jamii jana Alhamisi, Aprili 12, 2012 yaliandika vichwa vikubwa vilivyosomeka: Lulu Kortini kwa kumuua Kanumba na Lulu Kizimbani kwa mauaji ya Kanumba.
Kwa mujibu wa sheria na maadili ya Uandishi wa Habari mtu yeyote anayekamatwa kwa tuhuma yoyote ile ni mtuhumiwa mpaka atiwe hatiani na mahakama.
Kanuni hii ya siku nyingi katika fani ya uandishi wa habari inafahamika na waandishi na wahariri wote wanaoheshimu kazi yao.
Baraza pia limeshatoa matamko mara kadhaa kuwakumbusha wanahabari kujiepusha na uandishi wa habari au vichwa vya habari vinavyohukumu.
Baraza linafahamu fika kuwa kesi zilizoko Mahakamani ni kivutio kwa umaa kutaka kujua kinachoendelea ili kuona haki ikitendeka na pia wanahabari wana haki ya kujua na kuripoti yanayojiri huko na katika vyombo vingine vya sheria.
Lakini lazima ifahamike kuwa wakati wakitumia fursa na haki hiyo Wanahabari wanapaswa kuzingatia kanuni, miongozo na sheria zinazolinda haki za msingi zxa watuhumiwa na uhuru wa Mahakama.
Ni wazi kuwa vichwa vya habari vilivyoitajwa hapo juu vimeliingilia uhuru wa Mahakama kwa kuchapisha habari ambazo zinaonekana kushawishi au kushinikiza uamuzi wa Mahakama.
Wanahabari ni lazima watambue kuwa kuna taratibu na makubaliano ya kijamii juu ya namna gani taarifa zinavyopaswa kuripotiwa ili kutowadhuru watu wengine.
Hivyo basi , Baraza la Habari Tanzania linapenda kuwakumbusha tena wahariri kuhakikisha kuwa wanafanya kazi yao kwa kuzingatia maadili na weledi katika kuripoti mkasa huu unaogusa hisia za watu.
Imesainiwa na
Jaji Thomas B. Mihayo
Mwenyekiti
Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania.


























