Showing posts with label Wanafunzi. Show all posts
Showing posts with label Wanafunzi. Show all posts

Saturday, November 02, 2019

Leah Mwamoto Awaonya Wazazi wa Kilolo Wanaokatisha Masomo ya Wanafunzi

Mjumbe wa halmashauri Kuu (CCM) Mkoa wa Iringa, Leah Mwamoto akiongea na wazazi wa shule ya sekondari ya Mlafu iliyopo katika wilaya ya Kilolo mkoani Iringa
 Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mlafu iliyopo katika wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wakicheza nyimbo mbele ya mgeni Rasmi

NA FREDY MGUNDA,KILOLO

Mjumbe wa halmashauri Kuu (CCM) Mkoa wa Iringa, Leah Mwamoto amewaonya wazazi wanaokatisha masomo watoto kuwa serikali itawachukulia hatua kali pindi watakapobainika kufanya kosa hilo.

Mwamoto ameongea hayo katika mahafali ya kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Mlafu iliyopo katika kijiji cha Mlafu wilayani Kilolo alipomuwakilisha mbunge wa jimbo la Kilolo Venance Mwamoto.

Akiwaonya wazazi katika mahafali hayo Mwamoto amewaeleza wazazi juu ya mazingira mabaya wanayoyakuta watoto wanaokwenda kufanya kazi za ndani katika miji mikubwa.

Hata hivyo amewaomba watendaji wa kata kuendelea kuwafutilia watoto ili kuwaepusha kujiingiza katika mazingira hatarishi yatakayoharibu ndoto zao.

Aidha Mwamoto amepongeza uongozi wa shule ya sekondari Mlafu kwa matokeo mazuri pamoja na mbunge wa jimbo la Kilolo, Mhe Venance Mwamoto kuchangia bati 180 na mifuko 100 ya saruji kwa ujenzi wa zahanati kijiji cha Mlafu.

Awali akisoma taarifa fupi ya shule mwalimu mkuu wa shule hiyo Emmanuel Mbangwa ameomba wadau kujitokeza kuboresha mazingira katika shule hiyo hususani kujenga nyumba za walimu na mabweni.

Nae diwani Mlafu Isidory Kiyenge amewataka wazazi wa kata hiyo pamoja na wadau kuwa tayari kuchangia katika sekta ya elimu ili kuongeza mazingira ya ufaulu.

Kayenge amewataka wanafunzi kujiandaa kwa mitihani ya kidato cha nne huku alito ahadi ya kuwaandalia chakula wakati wa mitihani.

Monday, September 06, 2010

MFUMO WETU WA ELIMU NA CHANGAMOTO ZAKE!

Ubungo mwaka 1980. Mwanafunzi wa Chuo Kikuu alienda kunywa pombe kwenye baa fulani. Wakati ule wanafunzi wa UDSM walikuwa na hela shauri ya posho zao kutoka serikalini. Jamaa alilewa. Akaanza kuongea kimombo/kiingereza. Alipigwa na wananchi wenye hasira kwa vile jamaa eti alikuwa na KASUMBA!

Wadau waliosoma Tanzania tangu miaka ya sabini katikati waliposema kuwa eti Shule za msingi zifundishwe kwa kiswahili halafu sekondari na kuendelea ziwe English wtakubaliana na mada huu.

Na mimi siku zote nasema maana ya shule ya msingi ni nini? Si ndo msingi? Sasa kama huna msingi mzuri si utapata shida baadaye. Katika jumuiya ya Afrika Mashariki sisi waTanzania ndo tuna matatizo ya kuongea na kuandika kiingereza shauri ya kukosa msingi mzuri wa Kiingereza shuleni.

Fikiria watoto wanafundishwa kiingerea na watu ambao hawana msingi wa lugha, yaani lugha yao ni broken. Kuna dada moja ambaye nilisoma naye Tabora Girls alikuwa ancheka akisema, "Chemi, si unakumbuka English ilivyokuwa taabu kwangu, basi mimi ndio mwalimu wa English katika shule ya sekondari fulani! Si maajabu hayo" Maajabu ndo yeye eti alijua kiingerza kuliko wengine.

Hata hapa USA unakuta mTanzania ana Masters/Ph.D lakikni anakosa kazi ya maana kwa vile hajui kuongea kiingereza vizuri. WaKenya na WaGanda hawana shida hiyo. Naukumbuka miaka ya 90 mwanzo nilienda kwenye kijiji fulani huko Uganda. Wau masjini watoto wamevaa nguo zilizochanika hlafu mavumbi matupu lakini walikuwa wanajua kiingereza kizuri.

Nashukuru kuwa sasa Tanzania wameruhusu shule za msingi za kiingereza kwa muda, lakini ni za kulipia (private). Lakini ni wakina nana wanafaidi? Ndo matokeo ya KASUMBA.

Mwaka 1993 (?)...mara baada ya kuruhusu vyama vingi, Chifu Abdallah Fundikira alihubiria umati mkubwa wa wananchi huko Jangwani. Chama chake ilikuwa UMD. Alisema, "Mwalimu Nyerere alikuwa anaongea Kiingera kizuri sana...The Queen's English, halafui alitaka nyie msiongee!" (Nilikuwa mwandishi wa habari Daily News wakati huu, na iliandika hiyo kwatika original copy, lakini ilifutwa kabla ya kuchapishwa!)



***********************************************************************



Imeandikwa na Malkiory William Matiya

Waswahili walisema, mkunje samaki angali mbichi. Wataalamu na watafiti katika fani mbali mbali wanatuambia kuwa hali/tabia ya mtu mzima kwa kiwango kikubwa ni matokeo ya mazingira ya makuzi/malezi yake ya utotoni. Mfano tabia kama vile ukatili, ukimya, woga, wasiwasi, hasira, okorofi, furaha, upendo, kujiamini n.k. ukubwani ni baadhi tu ya matokeo hayo.

Kama hivyo ndivyo basi, nadhani utakubaliana nami kuwa tunahitaji mfumo dhabiti na bora wa kujifunza/ufundishaji katika ngazi ya elimu ya awali/kindergarten na msingi. Ni dhahiri kuwa tendo la kijifunza linakuwa limekamilika pale ambapo mabadiliko ya kudumu ya kitabia yanapoanza kujitokeza kwa walengwa ambao ni wanafunzi. Hivyo basi, inatubidi tukubali ukweli kuwa mabadiliko chanya ya kitabia yatatokana na ufundishaji/uelimishaji chanya pia.

Mtoto wa kitanzania anapoanza elimu ya msingi hufundishwa masomo yote kwa lugha ya kiswahili isipokuwa somo moja tu la kiingereza kwa miaka yote saba ya elimu yake ya msingi. Baada ya hapo mambo hubadilika ghafla pale mwanafunzi anapoanza elimu ya sekondari, kwani masomo yote huwafundishwa kwa kiengereza isipokuwa somo la kiswahili.

Tatizo hili huchangia kwa kiwango kikubwa kupunguza kasi, ari na uwezo wa mwanafunzi kujifunza, kwasababu mwanafunzi hujifunza mambo mageni kwa lugha ya kigeni kwa maana ya kiingereza. Hali hii kwa mtizamo wangu inachangia kuzorotesha na kupunguza ufanisi wa wanafunzi wetu kilugha katika ngazi zote.

Zaidi ya yote, mfumo wetu wa elimu katika ngazi zote haujaandaliwa katika misingi ya kumwezesha mwanafunzi kujifunza kwa vitendo. Pamoja na shule zetu kuwa na ukosefu wa vifaa vya kufundishia kwa vitendo, lakini pia ubunifu miongoni mwa walimu ni jambo jingine.

Mfano, wakati wa kufundisha somo la umeme kwa wanafunzi washule ya msingi, hapa si lazima kuwa na umeme, maana shule nyingi za vijijini hazina umeme, badala yake walimu wanaweza kutumia betri ya gari kuzalisha umeme na mwanga.


Madhalani, wakati wa kufundisha somo la uzazi wa mimea, hapa walimu wanapaswa kuandaa bustani ya majaribio, ambapo wanafunzi watapata fursa ya kuona jinsi mimea inavyoweza kuzaliana kwa vitendo.

Na kama kama ni wakati wa kufundisha somo linalohusiana na mifumo mbali mbali kama vile mfumo wa chakula, mfumo wa hewa, mfumo wa uzazi, mfumo wa neva, mfumo wa fahamu n.k hapa walimu wahusika wanaweza kumchinja chura au panya ili waweza kuonyesha kwa vitendo.

Ili kukabiliana na changomoto hizi ningependa kuishauri serikali kupitia wizara ya elimu na mafunzo kama ifutatavyo. Kwanza, kubadili mfumo wa mitaala yetu ambayo tumeirithi toka enzi za mkoloni. Jambo la msingi hapa ni kubadilisha lugha ya ufundishaji toka ngazi ya chini ya elimu hadi elimu ya juu, yaani kutoka shule ya vidudu hadi chuo kikuu.

Kama ni kiswahili basi iwe ni kiswahili toka mwanzo hadi mwisho na kama ni kiingereza basi iwe ni kiingereza toka mwanzo mpaka mwisho. Pili mitaala ibuniwe kwa lengo la kumwezesha mwanafunzi kujifunza kwa vitendo zaidi tofauti na hali ya ufundishaji wa sasa uliojikita zaidi kwenye nadharia.

Hakika kama serikali inakusudia kuwekeza kwenye ubora wa elimu basi ni lazima walimu wa stashahada/diploma na wale wa shahada/degree nao wapewe jukumu la kufundisha katika shule za msingi.

Jambo hili linaweza kuwa na ugumu wake katika utekelezaji endapo mazingira ya kufanyia kazi kwa walimu hayataboreshwa, hii ikiwa ni pamoja nyumba nzuri za kuishi walimu, huduma kama vile umeme, maji, internet, minara ya simu na TV. Upatikanaji wa huduma hizi unaweza kuwafanya walimu kudumu katika mazingira yao ya kufanyia kazi.

Iwapo jambo hili litazingatiwa basi ubora wa elimu yetu utaongezeka, na hata uwezekano wa kubadili mitaala yetu kuwa katika lugha ya kiingereza toka shule ya vidudu/ kindergarten hadi chuo kikuu utafanikiwa.

Mwisho, tukumbuke kwamba uimara wa nyumba kwa kiasi kubwa hutegemea MSINGI! Bila kusahau usemi kuwa, utavuna ulichopanda.


--
Malkiory William Matiya

Mnaweza kutembelea blogu yake: http://www.malkiory-matiya.blogspot.com/