
Mnafahamu wimbo wa maiti? “Nimekufa leo, kesho ni zamu yako!” Ukweli, watu wanakufa kila siku. Wengine wanakufa shauri ya uzee, wengine kwa ajali, wengine kwa kuuliwa na binadamu wenzao au wanyama wa porini, wengine kwa ugonjwa. Hakuna mtu anayajua atakufaje. Nadhani watu wangejua wangekaa kwa woga, wangeshinda wanalia na kutetemeka ovyo.
Nadhani ni vizuri kuwa sisi bindamu hatujui siku ambayo tumepangiwa kifo. Fikiria kama tungejua. Dunia ingekuaje?
Tuseme fulani anajua kuwa atakufa leo jioni saa mbili usiku. Basi ingekuwa hekaheka kuomba kupiga simu kwa watu na kuomba msamaha kwa watu aliyowakosea. Au angesema mi nakufa kleo ngoja nilipize kisasi kwa kumwua fulani na fulani. Mtu angeenda kuichoma moto nyumba ya mtu akijua kuwa hata akifungwa jela siku yake ya kufa ni karibu. Mtu asingehangaika na shule akisema haina faida maana atakufa siku fulani hivyo hiyo shule haitamsaidia na anapoteza muda. Asingeenda kazini, maana angesema nakufa siku fulani ngoja nifanye shughuli zangu binafsi.
Haya tuseme fulani anajua kuwa atakufa wiki ijayo Ijumaa saa tatu asubuhi. Basi anamaliza pesa kwenye credit card kwa kula laifu, na kuachia familia yake madeni tele. Huko anafanya ngono ovyo bila kujali magonjwa wala nini. Huenda angekunywa pombe kupita kiasi na kumaliza siku zake akiwa kwenye coma hospitalini! Wengine wangeenda kutapeli watu wakijua kuwa kifo kiko karibu hivyo hawana shida.
Wengine wangejua siku yao, basi ndo wangemaliza vitu walivyoanza halafu hawakumaliza kama vile kuandika vitabu, kushona gauni, wangemaliza kujenga nyumba zao, wangekazania kumpachika mtu mimba, wangeenda kwao kuona wazee na ndugu zao ambao hawajaona miaka mingi. Mtu angekaa na watoto wakae anawaambia kuwa anawapenda badala ya kushinda baa anakunywa pombe. Wangekuwa kanisani, miskitini, temple na sehemu zingine za dini wakitubu madhambi zao. Mtu kwenye foleni angeomba apishwe maana ni karibu saa yake ya kufa. Kwa kweli kama watu wangejua siku yao ya kufa ingekuwa pilika pilika.
Mungu aliumba kila kitu na sababu. Kwa kweli tunapita tu katika hii dunia. Mabibi na mababu zetu walitangulia na vizazi vijavyo vinafuata. Na ni maksudi alituumba kusudi tusijue siku ya kuondoka duniani. Hivyo kaeni mfikirie je, ningejua nitakufa lini ningefanya nini.