Tuesday, November 10, 2009

IBUA FILMS STAR TANZANIA YAHAMIA MWANZA


Baada ya mchakato mzima wa kuibua vipaji vya wasanii chipukizi wa maigizo yaani IBUA Film Star Tanzania kuanzia Arusha, zoezi zima linahamia Mwanza katika Nyanza Shule ya msingi iliyopo Balewa Road tarehe 14 na 15 Novemba kabla ya kuhamia Dodoma.

Chipukizi waliofanikiwa kuiwakilisha mkoa wa Arusha ni pamoja na Salum Ahmed Shafii, Pauline Edward Munisi, Michael Elias Mrema, Mbara Meena na Enhard Haruna. Kutokana na mwamko mkubwa wa wasanii chipukizi, fomu za kujiunga na shindano la IBUA Film Star Tanzania zinaendelea kutolewa maeneo mbali mbali na mikoa husika. Hii ni kuwawezesha wasanii chipukizi kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wao ya kuendeleza vipaji vyao na kuviacha vikipotea kwa kukosa njia ya kuvikuza. Usaili wa mikoani utaandaliwa vipindi maalum na kuonyeshwa kupitia mojawapo ya runinga hapa nchini.

Taasisi ya YEC Production, inayojihusisha na kukuza na kuibua vipaji kwa vijana katika ulingo wa filamu nchini, imegundua njia pekee ya kuibua vipaji hivyo na kuviokoa visipotee kwa kuanzisha shindano maalum la kusaka vipaji. Washiriki wataonyeshwa kwenye runinga kupitia kipindi maalum ambapo watazamaji watahusishwa kumpata staa halisi wa filamu Tanzania.

Mbali na kuviendeleza vipaji vyao pia washiriki watapata mafunzo katika nyanja zote kuanzia za uandishi wa muongozo (scripting) hadi uigizaji bora na kuwawezesha kufikia malengo yao.

Vigezo vilivyotumika katika kumsaka msanii huyo chipukizi ni kuwa na umri wa miaka 16 ikiwa ni pamoja na uelewa. Hata kutokuonekana katika tamthilia au sinema ya aina fulani hapa nchini hicho pia ni kigezo kimojawapo ambacho ni kizuri, kwani vijana wanaochipukia ndiyo wanahitaji msaada mkubwa katika kuibuliwa vipaji, tofauti na wakongwe ambao tayari wamejitangaza.

YEC, imeahidi kuyaangalia matatizo yanayowakabili wasanii kwa kina na kuahidi kutoyarudia, kama yanavyofanywa na baadhi ya wasanii wakongwe, ndiyo maana wameamua kuingia mikataba ya mwaka mmoja na washindi watakaofika kumi bora, ili kuliepuka tatizo hilo.

Sambamba na mikataba hiyo kwa watakaofika kumi bora, pia watatoa nafasi ya kuwapeleka shule watakaoingia tano bora kwa ajili ya kujiendeleza mambo mbali mbali ya sanaa ambapo atakayeibuka kinara atapewa zawadi nyingine maalum.

Pia mchakato wa kuwapata washindi kumi hadi tano bora utaanzia kwenye 20 bora, ambapo watacheza filamu mbili huku majaji wakiangalia kipaji cha msanii mmoja baada ya mwingine na kuendelea kuchujwa hadi kupatikana mshindi.

Filamu watakayocheza zitakuwa katika mandhari ya mtanzania halisi, huku asilimia 60 ya mauzo ya kazi hizo yatakayopatikana zitakuwa kwa ajili ya wasanii wenyewe.

Kutokana na kuona umuhimu wa suala hilo, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) liliamua kutoa vibali halali vya kuendesha mchakato huo, ikiwa ni pamoja na kupewa baraka na chama cha hakimiliki Tanzania (COSOTA) ya kusimamia kazi hiyo.

Mikoa husika katika mchakato wa kwanza ni Arusha, Mbeya, Zanzibar, Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam lakini wigo wa mikoa utaongezeka mwaka hadi mwaka.

Jackline Wolper
Balozi IBUA Film Star Tanzania

No comments: