Saturday, December 26, 2009

CCM UK na Mwaka Mpya

Na mimi nasema CCM Juu, Juu, Juu Zaidi!

*******************************************************************
Ndugu Wana CCM na Watanzania wenzangu.

Kwa niaba ya CCM Tawi la UK napenda kuwatumieni Salaam njema za Krismasi 2009 na kheri ya Mwaka Mpya 2010. Msimu huu wa Krismasi 2009 umetukuta katika hali ya hewa yenye mvua,theluji na barafu nyingi zikiathiri miundo mbinu na makutano ya kijamii. Aidha vichocheo-uchumi bado havijamaliza mgogoro wa kiuchumi ulioathiri na kufumua bei ya vyakula;gharama za huduma ya makazi;gharama za usafiri na upungufu mkubwa na ukosefu wa kazi hapa UK. Matatizo haya yameikumba dunia nzima.

Nyumbani Tanzania, wachache wetu walizipokea changamoto hizi na kuzitafsiri katika medani za kisiasa. Ni jambo la msingi wanajamii kutekeleza haki yao ya kidemokrasia na ni busara pia kutambua juhudi zinazofanywa na watumishi katika sekta za umma na binafsi.

Serikali ya Awamu ya Nne imeendelea kwa kasi nzuri kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM iliyokubalika na wananchi wengi zaidi katika kuleta maendeleo kwa Taifa zima. Kwa kuwa mwaka 2010 ni kipindi cha Uchaguzi, tutajifunza katika Taarifa ya Serikali kuhusu mafanikio ya utekelezaji, uanzishwaji au/na marekebisho ya mipango endelevu ya miradi ya maendeleo katika nyanja mbalimbali zenye maslahi kwa Taifa ndani na nje ya nchi.

Tutashuhudia kuwa Watanzania wa makundi na jinsia zote hususan vijana, wanawake, walemavu, wazazi na wazee wetu, na wadau waishio ughaibuni wamenufaika au wanatarajia kunufaika na mipango hiyo endelevu. Aidha maeneo yote ya kiuchumi yamelengwa yakijumuisha Kilimo(kilimo kwanza); Elimu(ongezeko la wanafunzi-jinsia zote na la kitaasisi kwa ngazi zote); Madini na Nishati(marekebisho ya mikataba inayokidhi haja za Taifa dhidi ya sheria banifu za kimataifa); Afya(kasi usambazaji wa huduma umma/binafsi kwa kata na vijiji); Sheria na Usalama wa Raia(uhuru wa vyombo vya sheria kuwajibika na ongezeko la nguvu kazi); Fedha(ongezeko la huduma na sheria angalizi na rekebisho) pia Serikali kuanza kushughulikia sheria za Uraia wa Nchi Mbili na mashauri mengineyo.

Ni kweli kwamba katika maeneo haya bado kuna mianya inayo hitaji marekebisho kwa ushirikiano wa taasisi za umma na binafsi na pia wananchi kwa ujumla kuanzia sasa na kuelekea miaka mitano mingine ya Awamu ya Nne. Ndugu Watanzania wenzangu, tusibaki nyuma tukilalamika bila sisi kutekeleza wajibu wetu ipasavyo. Huo ndio UHURU wa kweli. Tusikosoe kwa Hisia tu bali Tusahihishane kwa ufasaha ili tufikie ufanisi maridhawa.

Uchaguzi ujao ni wetu wote. Lazima tushiriki. Kwa kupiga, kupigiwa au kuelimisha ndugu, jamaa na marafiki kushiriki kupiga KURA kutatuongezea haki na wajibu kwa Taifa letu. CCM inapinga Rushwa kwani ni Adui wa haki. Tafadhali usimshauri mtu kuandaa, kutoa au kupokea Rushwa wakati wote na hasa wa Uchaguzi.

Tutumie ratiba ya vikao vyetu vizuri kuanzia kwenye mashina yetu ili tujadili kwa makini kero zinazotusibu hapa Ughaibuni na Tanzania. Viongozi wetu watafikisha hoja katika vikao vya juu kwa ajili ya ufumbuzi. Nawashukuru kwa ushirikiano wa dhati kwa mwaka 2009. Mwaka ujao 2010 CCM inahitaji zaidi ushirikiano wenu. Mungu awabariki.

MAPINDUZI DAIMA
MAINA ANG'IELA OWINO
Mwenyekiti wa CCM Tawi la UK.
TEMBELEA www.ccmlondonuk.org.

No comments: