MAENDELEO YA KILIMO TANZANIA-WAWEKEZAJI WAKUMBUSHWA-
HAKUNA VIZUIZI ...
Imeandaliwa kwa ushirikiano wa Urban Pulse na Freddy
Macha
Wawekezaji wamehimizwa kutosikiliza propaganda za
uongo kuhusu uporaji ardhi Tanzania na kuendeleza miradi ya kilimo nchini.
Akiongea katika
mkutano wa wafanyabiashara na viongozi wa taasisi, mashirika na
makampuni mbalimbali ya ukulima na mazao
Uingereza na Tanzania, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza alisisitiza
serikali iko tayari kumsaidia yeyote anayetaka kuchangia idara hii muhimu ya
uchumi.
Waziri wa Kilimo Mh. Christopher Chiza |
Waziri Chiza
aliyewasili London Jumatatu, kwa
ziara ya kiserikali ya siku tano akiongoza msafara wa wanataaluma wa kilimo, alikuwa akijibu swali lililoulizwa
mara kadhaa kuhusu ugawaji ardhi Tanzania.
Alifafanua: “ Lipo gazeti moja lilisema serikali
imechukua hekta milioni tatu. Si kweli. Ardhi
iliyoshakaguliwa katika miaka miwili iliyopita si zaidi ya hekta 4,000.
Habari hizi zimesababisha Tanzania kuondolewa katika kundi la nchi za kuwekeza
kilimo. Hata wafanyakazi wa mashirika
yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanatangaza uongo huu ambao ni marudio tu ya mambo
yasiyo kweli yaliyoshazushwa zamani. Tafadhali njooni muongee na sisi wizarani
na serikalini au taasisi zinazoaminika
kama SAGCOT. Tutawaambia ukweli na kufanya nanyi kazi.”
Mkutano husika ulifanyika ukumbi wa Reform Club
mtaa wa Pall Mall, London, na kuhusisha wafanyabiashara wenye shughuli za kilimo
Tanzania, makampuni makubwa yanayojishughulisha
bara Asia, Afrika na Uingereza, mathalan duka maarufu la Sainsburys.
Kati ya wazungumzaji wakuu alikuwa Balozi wetu, Uingereza, Mhe Peter Kallaghe
aliyesisitiza sera ya Tanzania kuendeleza mahusiano ya kibiashara badala ya
kutegemea sana misaada ya kigeni; Rachel Turner
mkurugenzi wa tawi la Mashariki na Afrika ya kati, idara ya serikali ya
Uingereza ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID); Afisa Mtendaji Mkuu wa kituo cha mpango
maalum wa uendelezaji kilimo ukanda wa Kusini Tanzania ( SAGCOT), Geoffrey
Kirenga na Profesa Peter Mahamudu Msolla, Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Katika hotuba yake Waziri Chiza alifafanua
malengo matatu muhimu kuhusu ziara hii, yaani kuendeleza fursa ya kibiashara na
uwezekaji, kujifunza teknolojia zinazohitajika na kuwaeleza wakulima na
wafanyabiashara mambo takikana.
Msisitizo wa uwekezaji kupitia sekta binafsi
ulitolewa mfano mzuri na Bwana Carter Coleman, Afisa Mtendaji wa Agrica linaloongoza mradi wa kuendeleza
hifadhi, misitu na kilimo bora Afrika Mashariki.
Coleman ambaye amekuwa na mahusiano ya karibu na
Tanzania toka 1987 alieleza baadhi ya shida zinazokabili kilimo kwa kusisitiza
kuwa “ kilimo Afrika ni aghali kuliko sehemu nyingine zote duniani.”
Alitaja baadhi ya matatizo makuu kuwa kupatikana
kwa umeme, ghala na hifadhi za mazao, matengenezo ya vifaa kama trekta, maradhi
ya mimea na kujua mbegu zipi zitumike wapi na vipi.
“Kutokana na hayo kitengo cha uwekezaji na
biashara ya binafsi ni muhimu sana kuendeleza kilimo Afrika,” alikumbusha.
Mheshimiwa Waziri Chiza anatazamiwa kukutana na
Watanzania leo Jumatano katika ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania London, uliomtayarishaji
mkuu wa safari hii nzima.
Balozi Mh. Kallaghe Akihutubia Mkutano |
No comments:
Post a Comment