Na Freddy Macha
Kwa ufupi:
            
Desturi ya kula inayozagaa nchini kote hususan majiani ni ile iitwayo ‘fast food’ huku Majuu. Ilianzia Marekani.
Tumalizie mada yetu leo iliyoanza wiki tatu zilizopita.
Kitakwimu idadi ya vijana Tanzania ni kubwa zaidi 
ya wazee, nchi zilizoendelea walipitisha miaka 70 ni wengi sababu ya 
ubora wa maisha. Lakini hapo hapo Uzunguni yapo ‘mabaya’ yanayostahili 
kuangaliwa.
Azma ya kutamani ‘maendeleo ya haraka haraka’ bila
 simile imeanza kuchangia aina ya maradhi ya kisasa. Zamani kisukari, 
ugonjwa wa moyo au kupoteza nguvu za mapenzi yalikuwa magonjwa ya wazee,
 walakin leo yanawakaba na kuwasepetua vijana.
Katika makala mbili zilizopita tumejadili namna 
taratibu nzima ya maisha, siasa- uchumi, elimu na utambuzi 
yanavyochangia adha hii. Mathalani kama hulali saa nane kwa siku, 
unaharibu akili, sura, tabia na afya yako.
Kipindi cha miaka 30 iliyopita. kumekuwa na tatizo
 la Wazungu, hata weusi waliozaliwa huku Majuu, kupungukiwa mbegu za 
uzazi. Ndoa nyingi zinavunjika. Tatizo hili linaloitwa “low sperm count”
 au kwa wanawake ‘infertility problems’, limefanyiwa utafiti sana. 
Mathalan nchini Marekani, imethibitishwa kuwa kutozaa husababishwa na 
udhaifu wa mayai ukihusisha wote, wanawake na wanaume. Asilimia 30 
wanaume na asilimia 30 wanawake wana tatizo hilo.
Sababu zilizotolewa ni pamoja na kurithi hali 
hiyo, kutokula vyakula asilia, maradhi ya zinaa, uchovu kutokana na kazi
 na maisha ya kasi sana (“stress”). Tatizo hili lilifikia kilele miaka 
ya 1980 ambapo wenyeji walipendelea zaidi ndoa na sisi tunaotoka nchi za
 joto au zinazoendelea.
Kwa nini?
Aina ya maisha (Afrika, Asia na Marekani ya 
Kusini) ni tofauti na ya Uzunguni. Joto, kutokimbiakimbia ovyo 
(“stress”), vyakula na hewa safi asilia isiyoathiriwa na moshi, pia 
mashine za kisasa ni baadhi ya mambo yaliyochangia mbegu, haiba na tabia
 zetu kimapenzi kuwa bora.
Hivi sasa Wazungu wamegundua kula vyakula asilia 
(“organic food”) na kufanya mazoezi hustawisha siha ya mapenzi na ngono.
 Miaka 15 iliyopita vuguvugu la maisha ya siha, limetanda kiasi ambacho 
maduka yamejazana vyakula asilia vinavyonunuliwa nchi maskini. Mathalan 
hivi karibuni nilikuwa nakwenda duka moja hapa London kununua nyama ya 
nyati wa Zimbabwe.
Kwa nini Wazungu wanalipia zaidi vyakula asilia ?
Hapo! Wamegundua njia waliyokuwa wakiipitia baada 
ya maendeleo ya mashine yaliyoanza karne ya 18 na kufikia kilele karne 
ya 20 inawaharibia afya na maisha. Sisi tumejaza vitu hivyo, lakini 
hatuvithamini.
Mwaka 1976 wakati nilipoanza kazi Gazeti la Uhuru,
 tulikuwa tukila katika vibanda na magenge ya Mama Ntilie. Enzi hizo 
ubwabwa kwa maharage na ndizi mbivu vilikuwa sehemu mahsusi ya mlo wa 
mchana. Mwisho wa juma tulipotoka dansini au disko, kando ya barabara 
yalikaangwa mayai (macho ya ng’ombe) kwa nyanya na vitunguu.
Nilikuwa na rafiki yangu mwanahabari (marehemu) mpigapicha, Awadh Shebe, akiishi Kariakoo. Kila mchana siku za Jumamosi tuliingia Mnazi Mmoja kupata “fruti” yaani bilauri za mseto wa matunda. Leo kinachotiliwa mkazo ni vinywaji vya “kisasa” kama Cocacola, Mirinda kwa “chips” kavu baada ya kazi. Mafuta ya hizo “chips” huwa yameshapikia hata wiki nzima bila kubadilishwa. Sawa kweli?
Desturi ya kula inayozagaa nchini kote hususan majiani ni ile iitwayo ‘fast food’ huku Majuu. Ilianzia Marekani.
Huko ndiko walikojenga maduka na migahawa maarufu 
ya MacDonalds. Wamarekani haohao wanasemwa hawajui kupika, hawali 
vyakula asilia. Wanakumbwa na maradhi ya unene na moyo. Haya ndiyo mambo
 yanayoingia kwetu Afrika. Tena kwa haraka sana.
Je, wangapi leo tunapika nyumbani?
Ni vijana wangapi wanajua kupika msosi ukalika?
Tunakimbilia nyama na ndizi choma tu. Kula nyama 
choma siyo vibaya hata kidogo. Ubaya imegeuzwa chakula kikuu. Waafrika 
tunapenda nyama. Twazila kila siku. Nyama nzuri ndiyo. Lakini 
yanatuponza. Afrika Magharibi na ya Kati wamefikia kula nyama mwitu : 
panya, nyani na popo! Matokeo ndiyo hiyo Ebola inayoangamiza watu Guinea
 sasa hivi.
La pili ni ulevi.
Wiki ya jana vyombo vya habari Uzunguni 
vilitangaza matokeo ya utafiti wa Shirika la ‘Slimming World’ 
linaloangalia matatizo ya unene kwa walevi 2,000, hapa Uingereza. 
Kawaida mwanaume anatakiwa asizidishe bia tatu kwa siku, yaani kipimo 
cha vitengo (“units”), kumi. Ikizidi, mwili hubadilika na kuharibika. 
Wanawake wanashauriwa vitengo vinane, yaani glasi 2 za mvinyo kama bia 
mbili. Ulevi unapokiuka vitengo hivyo, mtu hutaka kula zaidi.
Utafiti ulisema, tabia ya kilevi ni kutaka kula ‘chochote kile’ kiwe kibaya au kizuri, kujaza tumbo baada ya kulewa.
Matokeo ni nini? Kutapika, vitambi, ushuzi, unene, harufu mbaya ya mdomo na mwili na mambo kama hayo.
Utafiti wa pili ulichunguza wazee wenye umri wa 
zaidi ya miaka 60. Ukadadavua kuwa kadri umri unavyokwenda, ndivyo 
ubongo husinyaa na kupungua uwezo, hii husababisha kusahau, kutofanya 
mambo sawasawa-yaani ‘dementia’ kwa lugha ya kitaalamu. Utafiti 
ukashauri kuwa, mazoezi ya viungo kama kutembea (dakika 20 hadi 45 kwa 
siku), kuogelea, kukimbia na kadhalika kwa watu wa makamo kuimarisha 
bongo zetu.
Je, yanaathiri vipi vijana?
Vijana leo, (Uzunguni na nyumbani) wanaonyesha dalili za kuwa na
 matatizo yanayostahili kuwapata wazee. Kwa kuwa bangi ni rahisi 
kupandisha nishai kuliko pombe (aghali) vijana huanza kuivuta wakiwa 
wadogo sana. Bangi na dawa za kulevya, humfanya mtumiaji kutojali 
wakati, kujisikia mzito, mvivu na mwenye usingizi, moyo kukimbia na 
kadhalika. Bangi inasababisha pia maradhi ya akili (‘schizophrenia’). 
Ukishazoea sana bangi unakuwa sugu; unataka “kali zaidi.” Unatafuta 
(‘cocaine’), sindano za ‘heroin’, na kadhalika. Ushetani huu huathiri 
mzunguko wa damu, jambo linalochangia kupungua nguvu za kufanya mapenzi.
Mwisho, tuangalie ulimbukeni.
Neno hili limetokana na “limbua” au “kulimbuka” 
yaani mara ya kwanza, kama ua linalochanua. Ulimbukeni ulioenea Tanzania
 na Afrika unatokana na azma ya kujaribu kupambana na hali duni ya 
maisha. Kijana anayekua sasa hivi anahitaji uongozi thabiti. Je, ikiwa 
uongozi bora haupo tutafanyaje? Itabidi tuyakubali maneno ya mwanamuziki
 wa Kispanyola Manu Chao aliyefanya mahojiano hapa London mwaka 2007 
akadai: “Hatuhitaji viongozi. Kila mmoja wetu ahitaji kuwa kiongozi.” 
Siyo kuvuta bangi na ushetani. Siyo kuwa wavivu. Bali kujituma. 
Kujielewa sisi nani. Kuipenda nchi yetu; kuipigania. Kujisomea na 
kujipenda zaidi.



2 comments:
Endeleeni kula hambuga na chipsi! Ohooo!
Aibu kweli unaende kitandani na puuuu, jamaa kalegea hataki kuamka!
Post a Comment