Mh. Shy-Rose Bhanji |
Mimi
Shy-Rose Bhanji, Mbunge wa Afrika Mashariki-Tanzania, ninapinga vikali
na kwa nguvu zote shutuma zilizotolewa dhidi yangu kupitia mitandao
mbalimbali ya kijamii.
Shutuma hizi hazina ukweli wowote na
zinalenga, si kuniharibia, bali kuchafua sifa yangu na utendaji kazi
wangu katika Bunge la Afrika Mashariki.
Lengo kuu la shutuma hizo
ni kunivunja nguvu na ari ya kutetea maslahi ya nchi yangu na
Watanzania wenzangu kwani daima nimekuwa kikwazo na mwiba kwenye ajenda
zinazokiuka maslahi ya Tanzania.
Kwa mfano ardhi ya Tanzania
kugawiwa kwa wana Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kinyume na Sera ya
Tanzania. Nimekuwa miongoni mwa wabunge wa Tanzania tulio mbele katika
kulipinga suala hilo. Sishangai likinijengea uadui.
Isitoshe,
kwenye ajenda ya kumuondoa madarakani Spika wa EALA, Dk. Margaret Zziwa,
nilisimama kidete kwa kutounga mkono kwa sababu halikuwa na maslahi ya
Tanzania na yalikuwa kinyume na malengo ya ushirikiano wa Jumuiya nzima.
Hoja ya kumuondoa Spika ilikuwa ni sehemu ya ‘mchezo mchafu’ ya ajenda
ya siri ya kumweka kwenye nafasi hiyo mjumbe mwingine kwa maslahi ya
wachache.
Jaribio hili la kumuondoka Spika lilifanywa na
kushindikana mara tatu baada ya kukosa sahihi za kutosha kutoka
Tanzania, ikiwamo ya kwangu.
Baada ya kampeni ya kumwondoa Spika
kushindwa, wabunge kadhaa walikuwa wanasusia vikao vya Bunge wakati
wameshachukua posho za vikao. Kwa mfano kikao kilichofanyika hivi
karibuni hapa Dar es Salaam.
Malumbano ndio yamekuwa yakitawala
na kuinyima Bunge akidi ya kuendelea na ajenda za mtangamano. Huu ni
usaliti wa wazi kwa nchi zilizowachagua na kuwatuma katika Bunge la
EALA.
Ukijaribu kuwaasa kwamba mwenendo huo si sahihi, unageuka kuwa adui.
Na sasa wameamua kunitukana na kuzusha tuhuma kadhaa kupitia mitandao
ya kijamii ambako yote ni utunzi wa kisanii usiokuwa na chembe ya
ukweli, uhalali wala ushahidi.
Wahenga walisema ‘akutukanaye hakuchagulii tusi’. Walete ushahidi wa tuhuma zote dhidi yangu.
Kwa mfano, shutuma kwamba nililewa pombe ndani ya ndege, kuvunja chupa,
kufanya fujo na kufungwa pingu wakati wa safari ya Ubelgiji si kweli
hata kidogo.
Kama hizi tuhuma ni za kweli, kwanini hazikupelekwa polisi, serikalini au vyombo vingine vya sheria baada tu ya tukio?
Ijewe wamesubiri wiki mbili baada ya madai hayo ya tukio la kutunga
ndipo wajitokeze wakati wa kikao kinachoendelea mjini Kigali, Rwanda?
Kwanini wasubiri kikao cha Kigali ndipo uzushi huu utolewe?
Tuhuma kwamba nimewatukana marais wa nchi tatu hazina mashiko isipokuwa
kuhalalisha kampeni ya wale wanaonichafua na kuibua chuki kwa maraisi na
raia katika nchi za Kenya, Rwanda na Burundi.
Ninayo heshima
kubwa sana kwa marais wa nchi zote tano na raia wa nchi wanachama ambako
mara zote nimepokewa na kuishi kwa amani na upendo katika nchi hizo.
Naahidi kuedeleza heshima hii.
Hainiingii kichwani ni wapi
nilipoteza heshima hii isipokuwa kwa wale wasionitakia mema ambao
wamekusudia kufanikisha ajenda zao.
Shutuma zote dhidi yangu zimetengenezwa na watu ambao hatushabihiani katika hoja zetu na sishangai kwa hilo.
Mimi ni Mtanzania na ni Mbunge wa Tanzania. Hivyo nina wajibu wa
kulinda na kutetea maslahi ya Watanzania ili kuleta mtangamano wenye
uwiano sawa kwa nchi zote wanachama.
Ninaahidi nitaendelea
kuwatumikia Watanzania kwa nguvu zangu zote na kutoa ushirikiano kwa
wabunge wengine wa EALA kwa manufaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Nimeyasema haya nikiamini kuwa: “Uongo ukiachwa usemwe mara nyingi unaweza kuaminiwa kuwa ni ukweli.”
Umoja Wetu Ni Nguzo Yetu
Mungu ibariki Afrika Mashariki
Asanteni,
Shy-Rose Bhanji
Mbunge EALA
Shy-Rose Bhanji
Mbunge EALA
1 comment:
Sidhani kama hii ni njia sahihi ya kujibu tuhuma. Na ni akina nani wanakutuhumu, ni vizuri kulijua hili ili usije ukakuta unatoa nafasi kwa watu kuanza kufuatilia hata yale yaliyo nje ya hili.
Post a Comment