Showing posts with label Manda. Show all posts
Showing posts with label Manda. Show all posts

Thursday, January 02, 2020

Tanzia - Bibi Jeredina Paulo Suka Haule

Ninasikitika kutangaza kifo cha ndugu yangu, Bibi Jeredina Paulo Suka Haule, kilichotekea, Janauri 1, 2020, huko kijijini, Ilela, Manda, Tanzania. Alikuwa mama Mzazi wa Stephen Challe na Burton Challe.

Bibi Suka amekwisha lazwa katika nyumba yake ya milele. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema mbinguni. Amen.





Bibi Jeredina Paulo Suka Haule
October 28, 1928 to January 1, 2020

Mimi na Bibi Suka (mwenye ndoo)  kijijini Ilela mwaka 2009

Bibi Suka na baadhi ya wajukuu wake mwaka 2014

Misa ya Kumwombea Bibi Suka Kanisa Anglikana Ilela



Saturday, May 02, 2015

Asanteni Wadau - Msiba wa Dr. Aleck H. Che-Mponda (1935-2015)


Wadau, asanteni sana kwa salamu za pole, rambirambi, simu, sms nk.  Baba amezikwa kijijini kwao, Ilela, Manda, Tanzania siku ya jumatano tarehe 8, Apriil 2015.   Aliugua  ugonjwa wa Saratani (Prostate Cancer).

Mwenyezi Mungu Ailaze Roho ya Dr. Aleck H. Che-Mponda (1935-2015) mahala pema mbinguni. Amen.

Saturday, April 16, 2011

Muganda - Ngoma ya Bila Jasho

Leo nawapeleka kwetu, Manda (mkoa wa Iringa) mfaidi Ngoma ya kwetu. Ni Muganda aka. Ngoma ya bila Jasho!

Thursday, November 12, 2009

Bandari ya Kyela

Meli MV Songea (Meli Kubwa)

Wadau, Ziwa Nyasa ni kubwa mno. Ni kama bahari. Ina mawimbi makali kama bahari. Nilitoka Dar es Salaam na basi, hadi Kyela. Nililala gesti (Pattaya Centre Hole) na asubuhi tuliondoka kuelekea bandarini. Kuna bandari mbili huko Kyela. Hii bandari tuliyoenda ni nje ya mji wa Kyela. Ukitaka kwenda Lupingu, Manda, Mbamba Bay na sehemu kadhaa unapanda meli hapo. Hiyo Meli inaendeshawa na Tanzania Railways.

Siku tuliyoondoka, Oktoba 29, 2009, ndo meli kubwa MV Songea ilikuwa inarudishwa katika huduma. Walikuwa wanaifanyia matengenezao ya mwisho mwisho. Walisema meli itaondoka saa 7 mchana, lakini iliondoka saa 11 jioni. Swahili Time kweli kweli. La sivyo ingebidi tupande meli ndogo MV Iringa kesho yake.

Muda wote huo wasafiri pale bandarini waliishia kuchomwa na jua kali. Yaani kali kuliko hata Dar es Salaam. Kulikuwa na akina mama na watoto wao wengi tu pale. Kivuli hakuna. Kulikuwa na vimiti, na pia kajumba. Hiyo jumba walisema inafunguliwa tu, kama kuna wasafiri wanaolala pale kungojea meli, mfano inachelewa kuondoka. Ofisi ya kuuza tiketi ni kontena.

Kundi la akina mama waliamua kwenda kupeleka watoto wao kuoga pale kwenye beach. Mimi mwenyewe nilitia miguu kwenye maji ili kupooza ile joto. Ajabu, polisi fulani mwenye cheo ndogo sana alitokea na kuwafukuza wale wakina mama na watoto wao pale kwenye maji. Halafu alikuwa anatukana matusi ya nguoni, ila watu wamsikie huko kavaa magwanda yake. Sijui alijiona mtu mkubwa sana kwa kitendo chake.

Ningeomba serikali waweke angalau kibanda chenye kivuli pale, bandari ili watu wasichomwe na jua.

Kuna akina Mama Ntilie pale, na wanapikaga dagaa safi sana!
Jua lina zama. Ziwa Nyasa imetulia.
Bado tuko Kyela

Chai kwa Mama Ntilie. Ndizi, dagaa na soda.




Vibanda Vya Mama Ntiliel. Nilipata wali/dagaa/maharage safi sana pale kwa shs. 1,200/-.



Bandari ya Kyela

Hao wazungu ni wanafunzi wa udaktari huko Muhimbili. Wanatoka Ujerumani. Walikuwa wanafanya backpacking. Tulisafiri nao kwenye meli, walikuwa wanaenda Mbamba Bay. Mmoja wao aligombezwa kwa kupiga picha ya meli, MV Songea.

Tuesday, November 10, 2009

Chemi Kijijini Ilela, Manda

Kaburi la marehemu bibi yangu, Gandula Mary Makatochi. Alifariki 1977 nikiwa mwanafunzi wa Form One, Zanaki Girls Sec.

Manda saa za jioni, mnaona Ziwa Nyasa


Muhogo ni chakula kikuu huko Manda. Hivi sasa kuna ukame. Nashangaa kwenye picha naona kijani kijani, lakini nilivyokuwa huko kila kitu kilikuwa 'brown' shauri ya kukosa mvua! Ugali wa muhogo na dagaa wa Ziwa Nyasa tamu sana.

Nilionana na ndugu wengine sana huko Ilela. Wengi walinikumbuka kwa vile nilikuwa mtundu sana nuikiwa mdogo.

Kaburi la Marehemu baba mdogo, Prof. Crispin Hauli huko Ilela. Alipofariki mwaka 2001 alikuwa mbunge wa Ludewa na pia Naibu Waziri wa Fedha.


Njia kati ya Nsungu na Ilela, Manda Mnaona mlima wa Manda. Inaitwa Mt. Likolombola. (wadau naomba mnisaidie jina sahihi)


Ndugu huko Ilela Manda (Mama Nsumuka)

Niko na Ndugu wengine

Mimi na Bibi Mburuma, siyo bibi yangu lakini ni ndugu wa karibu.
Sara binti wa ndugu yangu Cassian ananisalimia
Niko na Happy, mtoto wa ndugu yangu Mama Rose

Ilela, Manda

Kijiji waliokaa mabibi na mababu zangu ni Ilela, Manda. Sehemu kubwa ya hicho kijiji kiko chini ya maji ya Ziwa Nyasa. Kijiji nilichojua nikiwa mtoto iko chini ya maji unayaoona pichani. Yaani hii beach unayoona ndo ilikuwa milima ya enzi zile. Nilikaa kwenye kiti nje ya tulipofikia na kutazama yale maji na kutoa machozi. Kijiji kilimezwa mwaka 1974. Natamani marine archeologists waende huko wachunguze hiyo eneo. Kumbe kuna Tsunami Afrika, tena kwenye ziwa! Na tulipokuwa kwenye meli kuelekea kijijini nilionja hasira ya Ziwa Nyasa, mawimbi makali kama bahari!

Marehemu bibi yangu, Gandula, kabla ya kufariki alisimulia hivi.... Walikuwa kijijini wanafanya shughuli zao. Ghafla wakaona zinga la wimbi la inakuja, walikimbia mlimani. Kijiji karibu chote kikamezwa. Maajabu hakuna aliyekufa wakati huo. Nyumba za wanavijiji, nyumba za mkoloni, miti, mibuyu, shule, makaburi, kila kitu kilimezwa na ziwa!

Wanasema kuna Mzee fulani, Mzee Kwiyanja, aliwaambia miaka mingi, hameni hapo Ilela, maana kijiji kitamezwa. Bibi alisema kuwa walikuwa wanamcheka yule Mzee na kumwona mwendawazimu. Yeye alihama na kujenga mlimani. Baada ya tukio wakamwona yule mzee kama mtume (prophet).

Kuna sehemu ya Ilela imebaki. Na nilipoenda kutembea nilikutana na wanavijiji wengi walionikumbuka hasa kwa ajili ya utundu wangu nikiwa mdogo. Picha zaidi za Ilela zinakuja.

Bandari ya Manda

Ukitoka bandarini kuelekea kijijini unakutana na huo mbuyu mkubwa. Niliuliza vijana wenye mgahawa hapo historia ya huo mbuyu, wakasema ni mbuyu tu. Nahisi ina miaka kama mia 500 au zaidi. Lazima imeona mengi. Ingeweza kusema! Manda, ilikuwa makao makuu ya Nyasaland enzi za Mjerumani. Walipaita, Wiedhaven au Wiedhafen.


Hiyo ni gofu la bandari ya zamani.
Meli ndo inapiga nanga hapo usiku sana kwenye giza. Manda hakuna umeme. Tulifika saa nane ya usiku, lakini kulikuwa na mba la mwezi safi sana. Ziwa Nyasa ni kubwa kama bahari.

Monday, November 09, 2009

Kivutio cha Watalii kijijini Manda


Wadau, hii kaburi ni la Mjerumani aliyekufa huko Manda mwaka 1904. Alizaliwa 1879. Maandishi yalikuwa kwa kijerumani hivyo sikuelewa vizuri wanasema nini. Nasikia wazungu wakifika kijijini ni lazima wafike huko kuona kaburi. Ni njiani kwenda kanisa la St. Thomas, huko Nsungu. Pia watu huko wanaamini kuwa wajerumani wameacha dhahabu tele huko kijijini. Kila siku watu wanachimba huko kuzitafuta!
Stori inaendea hivi, Mwingereza alipovamia, wajerumani walitia dhahabu yao kwenye sanduku. Waafrika wawili walipewa kazi la kubeba hiyo sanduku. Waliambiwa wachimbe shimo kubwa la kuficha hiyo sanduku. Baada ya kuchimba hilo shimo, waliingiza sanduku. Wajerumani waliwapiga risasi hao waafrika wawili na kuwazika humo humo kwenye shimo na hilo sanduku la dhahabu. Walihofia watasema wameficha wapi hiyo dhahabu. Kuna watu ambao wanaamini kuwa wajerumani wameacha ishara kadhaa kuonyesha walipozika ila sanduku.
Picha zingine zitabandikwa kesho jioni.