Wednesday, September 02, 2009

Watoto Wafungwa Jela!

Nauliza, Je, huu ni uungwana? Viongozi wako wapi?

*********************************************************************
Kutoka Michuzi Jr. Blog:

Watoto wafungwa jela ili kumfurahisha mwekezaji

Tuesday, September 1, 2009

MWANAFUNZI wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Mariwanda B, Juma Sylvester (16), alipaswa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka jana. Badala yake, yeye na wenzake wawili Hurushi Wambu (16) na Ndamo Wambu (16) wakafunga mwaka 2008 wakiwa jela.

Watoto hao ambao wana umri chini ya miaka 18, wako jela ya watu wazima wakitumikia kifungo cha miaka mitatu kwa kosa la kuingiza mifugo katika eneo la mwekezaji kampuni ya Grumet wilayani Bunda mkoani Mara.

Vijana hao walitiwa hatiani Agosti 4 mwaka jana, katika mahakama ya wilaya ya Bunda na hakimu wa wilaya hiyo, Richard Maganga baada ya kukiri kosa la kulisha ng’ombe katika eneo hilo lililokodishwa kwa shughuli za uwindaji na uhifadhi kwa kampuni ya Grumet.

Sylvester au Gujoru Girabi, Wambu na Wambu wanatimiza mwaka mmoja gerezani huku mwenzao mmoja Juma Nyakire (15) akipumua baaada ya Mahakama Kuu kanda ya Mwanza kumfutia kesi iliyokuwa inamkabili kama hiyo, Agosti 5 mwaka huu.

Nyakire mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Kunzugu wilayani Bunda mkoani Mara pia alifungwa miaka mitatu Januari 2 mwaka huu, katika kesi namba 381/2008 kwa kuingiza mifugo eneo la hifadhi huku watoto wenzake wenye kesi namba 212/2008 na 282/2008 wakiendelea kusota jela.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mariwanda B, David Barijera anasema kufungwa kwa mwanafunzi wake, Juma Silivesta kumemfanya ashindwe kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka jana.

"Kijana huyu alikuwa tayari kapewa namba ya mtihani ambayo ni PS/090/137/013 lakini hakufanya na alikuwa kati ya wanafunzi bora, lakini hiki kitendo cha kufungwa mwanafunzi wetu kimetusikitisha sana," anasema Barijera.

Unaweza usiamini unaposoma taarifa hii lakini hii ni hali halisi ambayo serikali ya awamu ya nne imelifikisha taifa hili. Sasa wawekezaji, kama alivyosema Mbunge ya Jimbo la Kyela Dk. Harrison Mwakyembe wanaonewa aibu na Serikali kama wakwe hata pale inapodhihirika wazi wamekosea .

Wakati taarifa ya matukio haya ikitolewa kwa wanasheria wa kituo cha haki na binaadamu (LHRC) mkoani Arusha , wakili wa shirika la kutetea wafugaji Pingos Forum na waandishi wa habari ilikuwa vigumu kuamini lakini baadaye yote yaliyoelezwa yalithibitika kuwa ni ukweli.

Watoto wadogo watatu, ambao walipaswa kulindwa na sheria zilizopo, wanatumikia kifungo huku kampuni ya Grumet ikiendelea na shughuli zake za kuvuna wanyama pori katika pori hilo la akiba ya Grumet.

Baada ya kuvuna wanyama pori, mwekezaji huvilipa vijiji saba vya wilayani Bunda jumla ya Sh 1.8milioni kila mwaka. Vijiji hivyo ni vile vinavyopakana na pori la akiba la Grumet.Mwenyekiti wa kijiji cha Mariwanda, Samson Kisung'uda anasema wakati watoto wao wanafungwa hawaoni manufaa ya mwekezaji huyu kwani hata hizo Sh 1.8milioni huwa hawazipati kwa wakati."Hadi sasa mwezi Agosti hajatupa hizo fedha.

Bajeti ya kijiji tayari imepita, mwaka jana alitoa mwezi wa 11 baada ya kulalamika sana serikalini na mwaka 2004 hakutoa kabisa hatujui nchi hii inakwenda wapi?"anahoji Kisung'uda.
Awali eneo hilo lenye mgogoro, katika mpango wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji, lilitengwa kama eneo la malisho, lakini hivi karibuni liliingizwa kinyemela katika eneo la pori la akiba la Grumet jambo ambalo linawafanya wafugaji wa kijiji hicho kukosa eneo la malisho.

"Katika hili eneo Mto Rubana unapita na miaka yote tumekuwa tukipeleka mifugo kunywa maji sasa baada ya mipaka ya pori kuingizwa hadi sehemu ya kijiji ndio sababu kila mara wafugaji na wananchi wanakamatwa kwa madai ya kuingiza mifugo kwenye pori," analalamika Kisung'uda.
Eneo hilo ndiko walikoshikwa watoto hao wanaotumikia kifungo na akina mama wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara wakienda kuchukua kuni za kupikia.

Kutokana na matukio hayo kijiji kimechoka. Mwenyekiti huyo anasema hawaoni manufaa ya mwekezaji huyo kwani serikali imeficha mkataba wake. Wanaitaka serikali iuweke wazi mkataba huo na ieleweke wazi kiasi cha fedha anazotoa kwa vijiji saba vinavyozunguka eneo alilokodishiwa na serikali ni za kisheria au msaada tu.

Diwani wa kata ya Hunyali, Sumera Kiharata ambaye vijiji vyake vinne vinapakana na mwekezaji huyo, anasema hata yeye kama diwani na mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Bunda hajui mkataba na mwekezaji huyo na serikali unasemaje.

"Hapa tuna mgogoro wa muda mrefu na jambo hili la kukamatwa watoto na kunyanyaswa wananchi tumelifikisha hadi vikao vya chama na serikali lakini inaonekana hakuna ufumbuzi kwani hata halmashauri ya wilaya haijui mkataba wa mwekezaji na serikali," anasema Kiharata.
Pamoja na malalamiko ya viongozi hao wa kata na kijiji, mkuu wa wilaya ya Bunda, Chiku Gawallawa anasema mwekezaji huyo, licha ya kuchelewesha fedha za vijiji na kukamata watoto, ana manufaa makubwa katika wilaya hiyo.

"Ni kweli kuna ucheleweshaji wa fedha, hilo tutalisukuma lakini huyu mwekezaji ni muhimu sana kwa wilaya nzima na hizo fedha za mwaka 2004 ambazo hawakupata vijiji zilitumika katika miradi mingine ya maendeleo," anasema Gallawa.

Kuhusu watoto waliokamatwa, Gallawa anasema walikubali kutumika kama ngao, pale wafugaji wanapovamia eneo la mwekezaji na kuingiza mifugo kwa kisingizio cha kufuata maji Mto Rubana.
"Ni kweli kuna watoto walishikwa kwa kuingiza mifugo eneo la pori la akiba la Grumet siku hiyo wananchi wengi walijitokeza kutaka kufanya vurugu na ili kujilinda waliwatanguliza mbele watoto kama ngao. Ila nadhani watoto walikwishaachiwa," anasema mkuu huyo wa wilaya bila kuwa na uhakika juu ya mahali waliko watoto hao.

Migogoro, mkuu huyo wa wilaya anakiri kwamba imekuwa mingi katika wilaya hiyo kutokana na kuwepo wafugaji ambao ni wahamiaji haramu, hatua ambayo inalazimisha kuendesha operesheni ya kuwaondoa wafugaji hao.

Anasema mifugo mingi imevamia wilaya hiyo hatua ambayo inasababisha kukosekana kwa eneo la malisho hadi kufikia wananchi kung’ang’ania kuchungia mifugo eneo la pori la akiba la Grumet.
Mkuu wa wilaya inaelekea hajui kitu maana taarifa yake hiyo inapingana na taarifa ya meneja wa pori la akiba la Grumet, Mathias Rwegasira anayesema wilaya hiyo inayozungukwa na mapori ya akiba na hifadhi ya taifa ya Serengeti, inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa malisho ya mifugo.

Anasema tangu pori hilo lilipotangazwa rasmi mwaka 1994 kumekuwa na migogoro ya mipaka hasa katika kijiji cha Mariwanda kutokana na wananchi kudai kuna eneo lao la asili na malisho limeingizwa katika eneo la pori la akiba.

"Huwa wanakuja ofisini wanaomba kibali kwenda katika eneo hilo ili kufanya mambo yao ya asili na tumekuwa tukiwapa kibali lakini tatizo kubwa ni kuingiza mifugo," anasema Rwegasira.
Meneja huyo anasema kampuni ya Grumet ina mkataba na serikali kuwinda kitalii na kuhifadhi eneo la ukubwa wa hekta za mraba 400 katika pori la Grumet na nyingine 500 pori la Ikirongo huku eneo la Ikoma sasa kumeanzishwa hifadhi za jamii (Wildlife Management Area-WMA).
Wananchi wa Bunda ambao wanaishi katika vijiji vinavyopakana na mwekezaji, wanasema wao hawapingi uwekezaji ila mazingira ambayo serikali inayaweka kwa kuwakumbatia sana hata wawekezaji wanapokiuka sheria ndicho wanacholalamikia.

Hata hivyo, Rwegasira anakiri kuwepo malalamiko ya wananchi juu ya mwekezaji huyo, lakini anasema miaka ya hivi karibuni wamejitahidi sana kuyapunguza kwani awali askari wa mwekezaji walikuwa wakilalamikiwa sana.“Hata kamati ya bunge ilifika hapa na kuulizia masuala haya ila tunajitahidi kuyashughulikia na sasa matatizo yanapungua kwani awali askari wa mwekezaji walijipa madaraka makubwa na hivyo kusuguana na wananchi," anasema.

Kuhusu kukamatwa na kufungwa watoto watatu, Rwegasira anasema yeye hana taarifa hizo japo kuwa alikiri kuwahi kusikia malalamiko alipotembelea vijiji vinavyozunguka pori hilo.Wakati Gallawa na Rwegasira hawajui hatima ya watoto hao, Mkuu wa gereza la kilimo la Serengeti, Deogratius Rwanga anakiri gereza lake kuwa na watoto wawili kati ya hao watatu na siku hiyo walikuwa wameondoka asubuhi kwenda machungani.

"Ni kweli tuna hao vijana hapa ila muda huu wapo machungaji," anasema Rwanga. Hii ndiyo hali halisi ya wilaya ya Bunda ambayo inaacha maswali mengi ni kipi kipaumbele cha serikali kati ya wananchi wake na wawekezaji.

*Mwandishi wa makala haya mwenye makazi yake mkoa wa Arusha anapatikana 0754296503 Email mussasiwa@gmail.com

********************************************************
Jamani naomba habari hizi muzifwatilie kwa kina na tujue mwisho na hatima ya watoto hao walio jela. Tunasema vijana Taifa la Kesho, sasa tukiwaweka vijana jela ndio watakuwa Taifa la Kesho kweli?
Habari zenu jamani, habari hii nimeipata kutoka Mwananchi unaweza kusoma kupitia
http://www.mwananchi.co.tz/newsre.asp?id=14280# naomba uweke na watanzania waone kinachoendelea huko Bunda

3 comments:

Anonymous said...

Waachiwe mara moja! Wameonewa!

Anonymous said...

Hiyo ndo bongoland ambapo penye udhia inapenyezwa rupia kumaliza mambo yote. Serikali inakumbatia hao waoitwa wawekezaji kwa kuwa viongozi wa serikali wanafaidika kwa kupata bakshishi hivyo kwao manufaa binafsi ni bora kuliko manufaa ya taifa. Kwanza kwa sheria za Tanzania si haki kwa watoto kufungwa katika jela za watu wazima hata kama wamedhibitika kufanya makosa. Niliwahi kusoma maandishi kwenye lori moja kuwa "Duniani sheria, haki mbinguni". Inawezekana kuna ukweli katika maandishi hayo.

Nachelea kusema kuwa nchi inaporomoka kwa kasi kuelekea kwenye vurugu...ni suala la muda tu.

John Mwaipopo said...

Kwa mlio ughaibuni the other kid was beamed on tv after release. he is really affected psychologically.