Sunday, May 19, 2013

Rais Obama kutua Tanzania


President Barack Obama

 Kutoka Gazeti la Mwananchi

Rais wa Marekani Barack Obama ambaye anatarajiwa kudhuru Tanzania siku za hivi karibuni 
Kwa ufupi;
Akizungumza na Mwananchi Jumapili Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni mchumi kitaaluma, amesema kuwa ujio wa Rais Obama unaweza kuleta neema hasa kama atakuwa ameambatana na wataalamu wa masuala ya maendeleo.

Hii itakuwa ziara ya pili ya Rais Obama katika Bara la Afrika.
Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa ujio wa Rais Barack Obama wa Marekani nchini, ni fursa nyingine kwa Tanzania kukuza uchumi na kuimarisha uwekezaji.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni mchumi kitaaluma, amesema kuwa ujio wa Rais Obama unaweza kuleta neema hasa kama atakuwa ameambatana na wataalamu wa masuala ya maendeleo.

Hii itakuwa ziara ya pili ya Rais Obama katika Bara la Afrika.
Ziara yake ya kwanza aliifanya wakati wa awamu yake ya kwanza madarakani, wakati ziara ya safari hii ni kipindi chake cha lala salama.

Rais Obama alianza rasmi awamu yake ya kwanza kama Rais wa Taifa kubwa, Januari 20, 2009, wakati ng’we yake ya mwisho ilianza Januari 21, 2013.

Rais Obama anatarajiwa kufanya ziara hiyo mwishoni mwa Juni mwaka huu, ambapo Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi za mwanzo za Afrika Mashariki kutembelewa na kiongozi huyo.
Ziara ya Rais Obama inafanyika baada ya ziara ya Rais Xi Jiping wa China aliyeitembelea Tanzania Machi 28, mwaka huu, ambapo Tanzania ilikuwa nchi yake ya kwanza kuitembelea kwa Afrika tangu achaguliwe kuwa rais, Machi 14, 2013.

Akizungumzia ziara hiyo tarajiwa, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni mchumi, alisema amani, utulivu na uimara wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kwa kulinganisha na nchi nyingine za jirani, vimechangia kuwapo kwa ziara hiyo.
Profesa Lipumba alisema pia ugunduzi wa rasilimali za asili kama vile gesi, mafuta na madini ya urani ni sababu nyingine iliyomfanya Rais huyo kuja nchini.

Hivyo aliwashauri viongozi wa Serikali kujipanga kwa ajili ya kufungua mlango huo mwingine wa uchumi na uwekezaji.

Alisema pamoja na hali hiyo pia kuna mambo ambayo yanaweza kuchafua taswira ya nchi kama vile ubovu wa miundombinu ya barabara, msongamano wa magari barabarani na msongamano wa meli bandarini wakati zikisubiri kushusha mizigo.

Jumatano ya wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry alitangaza mbele ya wajumbe wa Kamati ya Ushirikiano kati ya Marekani na Afrika, kwamba Rais Obama hivi karibuni atafanya ziara Afrika.

Ingawa Kerry hakutoa maelezo zaidi ya nchi gani za Afrika ambazo Rais Obama atazitembelea, lakini baadhi ya vyombo vya habari vya Nigeria vilieleza kiongozi huyo atafanya ziara Tanzania, Rwanda na Nigeria.

Kiongozi wa kwanza wa Afrika kukutana na Rais Obama tangu awe Rais wa Marekani, alikuwa Rais Jakaya Kikwete aliyekutana naye Mei 2009, Washington, Marekani.

Kwa nini ni Tanzania na Rwanda
“Kenya asingeweza kwenda kutokana na suala la Rais na Makamu wake kutuhumiwa kuhusika katika mauaji ya kimbari yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu 2007/2008, kwani msimamo wa Marekani ni kutaka wahusika wa vitendo vile wakamatwe na kufikishwa mahakamani. Hivyo kwake kuwatembelea watuhumiwa asingeeleweka,” alisema Profesa Lipumba.

Alibainisha kuwa Rwanda ina uhusiano wa karibu na Marekani na pengine suala la mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) litachukua nafasi.

Kulingana na taarifa za Ikulu ya Marekani, Rais Obama alikuwa amepanga muda wake mwingi wa awamu ya pili ya uongozi wake kujihusisha na masuala ya Afrika.

1 comment:

Mbele said...

Katika mstari wa kwanza, makala inasema Rais Obama ataidhuru Tanzania. Hii inamaanisha atailetea madhara. Neno sahihi lingekuwa ataizuru.