Mke Wa Rais Mama Salma Kikwete Atunukuniwa Tuzo ya MDGs nchini Marekani
Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA,
Mama Salma Kikwete akipokea tuzo ya Millenium Development Goals, Women
Progress Awards,2013, kutoka kwa Ms Jennie Yeung , Rais wa Shirika la
Sun Zhong Shan Foundation lililo chini ya United Nations Education,
Science, Cultural and Health Advancement Foundation
la nchini Marekani. Mama Salma alipokea tuzo hiyo baada ya kutimiza
baadhi ya malengo ya Millenia katika masuala ya ukimwi, elimu kwa watoto
waliokosa fursa na kuwawezesha wanawake kiuchumi nchini Tanzania.
Kulia ni Katibu wa WAMA, Ndugu Daud Nassib na kushoto ni Dr. Judy
Kuriansky, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani.
*******************
Na Anna Nkinda – New York
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo ya Malengo ya Maendeleo
ya Milinia ya mwaka 2013 kwa wanawake na Shirika la Voices of African
Mothers (VAM) la nchini Marekani kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya
kusaidia jamii wakiwemo wanawake na watoto.
Sherehe ya
kukabidhi tuzo hizo zimefanyika jana katika ukumbi wa mikutano uliopo
makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) amekabidiwa tuzo hiyo kutokana na uongozi wake madhubuti,
mafanikio na mchango wake na kujitoa kwake kuwasaidia wanawake na watoto
wa Tanzania.
Akikabidhi tuzo hizo Nana – Fosu Randall ambaye
ni Rais na mwanzilishi wa shirika hilo alisema kuwa tathimini
ilitofanyika kwa mwaka 2012 juu ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia
wametambua kwamba malengo matatu yamefikiwa nchini Tanzania kabla ya
muda uliowekwa wa kikomo wa mwaka 2015.
Alisema kuwa wake wa
Marais wa Afrika wanamajukumu mbalimbali katika nchi zao ili kufikia
Malengo hayo, Taasisi ya VAM imekuwa ikifanya tathimini juu ya hatua
zilizofikiwa na Taasisi za wake wa Marais kupitia taarifa za mwaka na
zingine zinazowasilishwa.
“Wanawake hawa wanastahili kutuzwa
kwani wamefanya kazi kubwa pamoja na kufanya shughuli zao katika
mazingira yenye changamoto nyingi ukilinganisha na wenzao katika nchi
zingine.
Hafla ya tuzo hizi siyo tu inasherehekea mafanikio ya
wake wa marais wa Afrika bali pia inawahamasisha na kuwatia moyo wakati
huu ambapo mwaka 2015 unakaribia”, alisema .
Alimalizia kwa
kusema kuwa mara nyingi vyombo vya habari vimekuwa vikiandika habari
zisizokuwa sahihi kutokana na kazi zinazofanywa na wake wa marais lakini
vinasahau kuandika mambo mazuri na kazi kubwa wanayoifanya ya
kuwasaidia wananchi na kuviomba vyombo hivyo kubadilika na kuthamini
kazi kubwa wanayoifanya.
Akiongea mara baada ya kukabidhiwa
tuzo hiyo Mama Kikwete alishukuru kwa tuzo aliyopewa na kusema kuwa
Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimepiga hatua kubwa sana katika kufikia
malengo ya milinia kwani vifo vya watoto vimepungua kwa asilimia 45 na
49 kwa watoto wachanga.
Alisema kuwa haya ni mafanikio makubwa
sana japokuwa lengo ni kuondoa kabisa vifo ambavyo vinatokana na sababu
ambazo zinazuilika na katika malengo mengine maambukizi ya Virusi vya
Ukimwi (VVU) yanaendelea kupungua kutoka asilimia 5.7 kwa mwaka 2004
hadi asilimia 5.1 kwa mwaka 2011.
Mama Kikwete alisema, “Elimu
ya msingi inatolewa bure kwa watoto wote walio na umri unaostahili na
hatua kubwa imepigwa katika kupunguza ugonjwa wa maralia na vifo vya
akina mama vinavyotokana na tatizo la uzazi”
Kwa upande wa
harakati za kumkomboa mtoto wa kike alisema kuwa ni lazima ziendelee na
zizingatie changamoto mpya za mazingira mapya kwani unapompatia elimu
unampunguzia changamoto za ujinsia na kumpatia huduma ya afya ikiwemo
uzazi wa mpango, unamuwezesha kushiriki zaidi shughuli za maendeleo ya
kiuchumi, unasaidia familia yake na jamii kuweza kuendelea.
Kwa
upande wake Dk. Judy Kuriansky ambaye ni mwakilishi wa Asasi zisizo za
Kiserikali zilizo chini ya UN alisema kuwa wake wa marais wanafanya kazi
kubwa ya kuisaidia jamii hivyo basi ni jukumu la kila mmoja kuwaunga
mkono na kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kutimiza malengo ya
maendeleo ya milinia.
Dk. Kuriansky alisema kuwa ili kufikia
malengo ya milinia inatakiwa kuimarisha miundombinu iliyopo jambo ambalo
litasababisha kuifikia jamii kwa ukaribu zaidi na kuweza kutatua
changamoto zinazowakabili.
Tuzo hizo zimetolewa kwa mara ya
kwanza na shirika hilo kwa kushirikiana na Taasisi ya The reed for Hope
(RFHF) na Bethesda Counsel kwa wake wa marais wa Afrika akiwemo Mke wa
Rais wa Burundi Mama Dk. Denice Nkurunziza, Mke wa Rais wa Equatorial
Guinea Mama Mintou Doucoure Epse Traore na Mke wa Rais wa Mali Mama
Dk. Malika Issoufou.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment