Saturday, November 08, 2014

Basi la Happy Nation yapata Ajali Mbeya!


 Natoa pole kwa waliojeruhwa!

****************************************************



Basi lenye namba T281 ARR mali ya Happy Nation likiwa limepinduka eneo la Meta Igurusi kilometa 54 kutoka Mbeya

Picha na Maelezo Kutoka MBEYA YETU BLOG:



Watu 37 wamenusurika kifo baada ya basi la abiria lenye namba za usajili T 281 ARR aina ya Scania linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Dar es Salaam linalomilikiwa na Kampuni  ya Happy Nation kuacha njia na kupinduka eneo la Meta Kata ya Igurusi wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi amesema ajali hiyo imetokea leo majira ya saa moja asubuhi  basi hilo likitokea Mbeya baada ya kupasuka gurudumu la mbele kulia kisha kupoteza uelekeo  na baadaye kumgonga mpanda baiskeli na kupinduka.



Msangi amesema baada ya ajali hiyo Dereva wa basi hilo aliyefahamika kwa jina moja la Shabani alikimbia ambapo Jeshi la Polisi linafanya juhudi za kumtafuta ili kueleza sababu za ajali hiyo.



Aidha Msangi amesema katika ajali hiyo kulikuwa na majeruhi 37 wanaume 26 wanawake 10 na mtoto mmoja wa kiume.



Baada ya ajali hiyo majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya Chimala ambapo mjeruhi 10 bado wamelazwa na wanne wamekimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi.



Kwa mujibu wa Daktari Mkuu Mahenge wa Hospitali ya Chimala amesema kuwa waliolazwa Hospitalini hapo ni wanaume sita na wanawake wanne na walohamishiwa Rufaa ni wanaume wanne.



Daktari Mahenge amesema kuwa hali za majeruhi 10 walipo Chimala hali zao zinaendelea vema ingawa wanakabiliwa na upungufu wa damu na wameomba msaada katika kitengo cha benki ya Damu salama Mbeya.



Hata hivyo baadhi ya abiria wamelalamikia mwendo kasi wa basi hilo kwani baada ya kutoka kituo kikuu cha Mabasi lilianza kwenda kwa mwendo wa kasi na mara kadhaa walikuwa wakimuonya Dereva lakini alikuwa akikaidi.



Pia walikuwa wakifukazana na mabasi mengine yaliyotokea Mbeya kuelekea Jijini Dar es Salaam hali iliyosababisha basi hilo kupasuka gurudumu la kulia likiwa katika mwendo kasi na kona kali kisha kupinduka.



Wakati huo huo Kamanda Ahmed Msangi amesema  watu wawili wamefariki dunia wilayani Mbozi baada ya roli la mizigo kugongana uso kwa uso na gari linalomilikwa na NSSF.


Msangi amesema bado majina ya waliofariki hayajapatikana na kwamba Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Serikali Mbozi.

KWA PICHA ZAIDI BOFYA HAPA:

No comments: