Saturday, September 24, 2016

Hifadhi ya Ngorongoro katika Kashfa Mpya!

Hifadhi ya Ngorongoro katika Kashfa Mpya



SEP 22, 2016
by MWANDISHI WETU Raia Mwema

MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeingia katika kashfa kubwa ya kugawa eneo la msitu wa asili wa Olmoti lenye ukubwa wa ekari tano ndani ya hifadhi hiyo kwa kampuni ya Asilia ili kujenga jambi (campsite) kinyume cha sheria za mazingira na uhifadhi.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya NCAA na kuthibitishwa na vyanzo vya uhakika zimeeleza kuwa eneo la msitu huo lilimegwa kinyemela na maafisa wa shirika hilo na kulitoa kwa kampuni ya Asilia ambayo inamiliki mtandao wa hoteli kadhaa (lodges) katika hifadhi mbalimbali bila kufuata taratibu zinazotakiwa.
Msitu huo wa asili ambao huheshimiwa na wenyeji wa jamii ya wafugaji wa kimasai upo katika kijiji cha Olchniomelole kata ya Alailelai.
Ugawaji wa sehemu ya msitu huo ni mwendelezo wa menejimenti ya NCAA kugawa kiholela maeneo  ndani ya hifadhi kwa ajili ya ujenzi wa hoteli (lodges) na campsite hatua ambayo inahusishwa na ufisadi uliokithiri miongoni mwa watendaji wa NCAA.
Takwimu zinaonyesha kuwa hadi sasa ndani ya hifadhi hiyo kuna campsite 31 na hoteli tano kubwa zilizojengwa katika kingo za kreta ya Ngorongoro hatua inayolalamikiwa na wadau wa ndani na mashirika ya kimataifa kuwa ni hatari kwa ‘uhai’ wa kreta ya Ngorongoro.
Kutokana na ujenzi wa campsite hiyo ambao umelalamikiwa na wananchi wa kijiji wanaotishia kuichoma moto, Kamati ya Uhifadhi, Utalii, Maendeleo ya Jamii, Ekolojia na Mambo ya Kale ya Bodi ya NCAA inayoongozwa na Lucas  Seleli ilikutana na wananchi wa kijiji hicho Alhamis ya wiki iliyopita.
Mkutano wa hadhara
Akizungumza katika mkutano wa hadhara mbele ya kamati hiyo kusikiliza kero za wananchi hao kuhusu ujenzi wa campsite hiyo, Mwenyekiti wa kijiji hicho Kilembei ole Ngisilo alisema wananchi wanapinga ujenzi huo kwa kuwa hawakushirikishwa  wala kuarifiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Alisema wakati ujenzi huo unafanyika kampuni ya Asilia ilifyeka sehemu kubwa ya miti ya asili kwa malengo ya kusafisha eneo la ujenzi hivyo kuharibu mazingira na mandhari ya msitu huo.
“Pia magari makubwa ya kubeba malighafi za ujenzi yameharibu barabara tuliyojenga kwa nguvu zetu na magari hayo pia yamepita katika maeneo tofauti na kuharibu mazingira yote, wanyama hawapiti, watoto wetu na mifugo pia imeshindwa kupita eneo hilo kutokana na kuwa vumbi nyingi sana,” alidai na kuongeza; “Kama unavyowaona wananchi wana hasira sana walitaka kuichoma campsite hii lakini tumewasihi sana sisi kama viongozi kwa ajili ya kulinda heshima ya serikali yetu.”
Mwananchi mwingine Parmoyat ole Ngaikul ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kitongoji katika kijiji hicho alisema uharibifu wa mazingira uliofanyika katika eneo hilo hauwezi kuvumilika hata kidogo na kuwataka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuondoa haraka kambi hiyo.
“Sisi tumeishi ndani ya hifadhi hii kwa zaidi ya miaka 60 sasa, tunauheshimu msitu wa Olomot kwa sababu ni chanzo cha maji katika eneo letu na tumezuia kuingiza mifugo ndani ya msitu tunawashangaa NCAA wamethubutu vipi kugawa eneo la msitu huo kwa mwekezaji?”alihoji ole Ngaikul.
Habari zaidi kutoka NCAA zinafafanua kuwa ujenzi huo ni kinyume cha sheria kutokana na msingi kuwa haukuwa katika mpango wa maendeleo wa hifadhi wa General Management Plan (GMP) ambao hutoa dira ya muda mrefu ya hifadhi.
Akihitimisha mkutano Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Lucas Seleli, alikiri mbele ya wananchi kuwa ujenzi wa kambi hiyo ulikiuka sheria zinazosimamia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuongeza kuwa waliohusika wanaweza kuwajibishwa.



Seleli Akiri
Akizungumza na Raia Mwema kwa njia ya simu juzi, Lucas Selelii, alikiri kuwapo kwa mvutano huo. “Kamati ilifanya ziara ni kweli kuna malalamiko kuhusu ujenzi wa campsite hiyo kutoka kwa wananchi na tumewahoji watendaji wa NCAA pamoja na uongozi wa Asilia hivyo kamati inaandaa ripoti ambayo itawasilishwa katika kikao cha Bodi mwezi Oktoba mwaka huu,” alisema Selelii.
Selelii ambaye alikuwa Mbunge wa Nzega katika Bunge lililopita, aliongeza kuwa pamoja kuwasilisha taarifa hiyo kamati yake pia itatoa taarifa kwa Bodi kuhusu hali halisi ya uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali ndani ya hifadhi hiyo.
“Kwa ujumla ripoti yetu itazingatia jinsi hali ilivyo kwa sasa ndani ya hifadhi hii ambayo ni moja ya maeneo nyeti katika masuala uhifadhi nchini na kimataifa na imebeba taswira ya nchi yetu katika sekta ya utalii kimataifa,” alisema.
Mhifadhi afanya kikao
Habari zaidi kutoka ndani ya NCAA zinabainisha kuwa kutokana na sakata hilo, Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Ngorongoro,  Dk. Fredrick Manongi, alifanya kikao cha siri na baadhi ya viongozi kusafisha hali ya hewa.
Taarifa zinaonyesha kuwa kikao hicho kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Kijiji, Kilembei ole Ngisilo, Diwani wa Kata, Shutuk Kitamwasi; Mjumbe wa Bodi, Edward  Mwaura na Mzee wa kimila (Laigwanan) ambaye hata hivyo jina lake halikupatikana mara moja.
Wengine waliohudhura wametajwa kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji wilayani wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo, Wakuu wa Idara za Utalii na Uhifadhi wa NCAA.
Aidha imedaiwa kuwa katika kikao hicho Dk. Manongi  alijaribu kuwashawishi kuwa waache kufuatilia ujenzi huo na kuahidi kuwa NCAA itatoa fedha kurekebisha kasoro na athari za mazingira zilizotokea wakati wa ujenzi.
“Pia aliwaahidi viongozi hao watakuwa na mamlaka ya kutembelea kambi wakati wowote na kijiji kitapewa mgawo katika mapato yatakayokuwa yanapatikana kutoka kwa wageni watakaolala katika campsite hiyo,” kiliongeza chanzo chetu kutoka ndani ya kikao hicho.
Habari zaidi zimeongeza kuwa hatua hiyo ya Dk. Manongi imelenga kuficha makosa yaliyofanywa na mmoja wa maafisa wake, Asantaeli Melita, Msimamizi wa Idara ya Utalii (Principal  Tourism Officer) ambaye ndiye anayetuhumiwa kujichukulia mamlaka ya kugawa eneo hilo.
“Ni wazi kuwa kwa hatua hii ya kuitisha kikao cha siri Dk. Manongi anajaribu kumteteta Afisa (Melita) aliyehusika na ugawaji wa eneo hilo na pia taarifa za ndani zinadai kuwa ugawaji huo ulifanyika kwa maelekezo ya mhifadhi huyo,” kinadai chanzo chetu cha habari.
Aidha Dk. Manongi pia anatuhumiwa kuunda mtandao wake ndani ya taasisi hiyo huku akiwalinda wakuu wa idara wanaojihusisha na vitendo vya ufisadi ikiwemo matumizi mabaya ya fedha bila kuwachukulia hatua akitegemea zaidi uhusiano wake binafsi na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.
Akitoa mfano wa tuhuma za matumizi mabaya fedha mtoa habari wetu kutoka ndani ya NCAA alidai kuwa Dk. Manongi hadi sasa anamlinda mtumishi moja wa Idara Fedha (Jina linahifadhiwa) ambaye anatuhumiwa ‘kutumbua’ zaidi dola za Marekani 200,000 (sawa na mlioni 435) kati ya mwaka 2013/2015 bila kuchukuliwa hatua.
Juhudi za kumpata Dk. Manongi kwa ajili ya ufafanuzi kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwake hazikuweza kufanikiwa kutokana na simu yake kuita kwa muda mrefu bila majibu na huku Afisa Uhusiano wa NCAA, Vicent Mbirika, simu yake kutokuwa hewani kwa muda mrefu.
Hata hivyo Afisa anayetuhumiwa kuhusika kugawa eneo hilo Asantaeli Melita akizungumza na Raia Mwema alikanusha vikali akisema campsite hiyo ilikuwepo tangu mwaka 2004 katika eneo hilo.
“Kwanza itambulike kuwa mwenye mamlaka kuhusu ardhi ndani ya hifadhi ni NCAA na si wananchi, eneo hilo liligawiwa tangu mwaka 2004 na wala sikusuhika, hapa kuna kundi la wachochezi wanawapotosha wananchi tu,” alisema Melita na kuongeza; “Kwanza suala hilo limeisha jana (Jumamosi  iliyopita) baada ya kikao cha Mhifadhi na viongozi wa kijiji, Diwani, Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji, Wazee wa Kimila (Laigwanan) na tayari tofauti zilizojitokeza zimemalizika.”
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni hifadhi ya kipekee dunia ambayo hufanya mseto wa maisha kati ya binadamu na wanyama hivyo kuvuta watalii kutoka kila pembe ya dunia na huchukuliwa kama moja ya maajabu ya dunia.
Hata hivyo hifadhi inaelekea kuelemewa na shughuli nyingi za kibinadamu kutokana na kuongezeka kwa ujenzi wa hoteli na campsite hali ambayo inayochangia kuwapo kwa upungufu mkubwa wa maji pamoja na malisho kwa mifugo na wanyama.
Pia inakadiriwa kuwa ndani ya hifadhi hiyo kuna watu zaidi ya 80,000 pamoja na mifugo zaidi ya 120,000 na hali ambayo inahatarisha shughuli za hifadhi kiasi cha shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO mwaka 2008 kutahadharisha kuwa hifadhi inapoteza umaarufu wake kutokana na  uharibifu wa mazingira.
Mwisho
Chanzo Gazeti la Raia Mwema

No comments: