Saturday, September 10, 2016

UNESCO Yazindua Ripoti ya Ufuatliaji wa Elimu Duniani (GEM) 2016

 Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Bi. Zulmira Rodriguez akimkabidhi mgeni rasmi, Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bw. Nicholaus Bureta, sanduku la Ripoti ya Ufuatiliaji wa Elimu Duniani 2016 (GEM).
 Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya siku ya kisomo, Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bw. Nicholaus Bureta akigawa Ripoti ya Ufuatiliaji wa Elimu Duniani 2016 (GEM) kwa baadhi ya wafanyakazi wa wizara yake.


Na Mwandishi wetu
Katika kutambua umuhimu wa kusoma na kuandika Tanzania na mataifa mengine duniani zimeungana kwa pamoja kuadhimisha siku ya Kisomo Duniani ambayo huadhimishwa kila Septemba, 8 ya kila mwaka ambapo pamoja na maadhimisho hayo pia iliambatana na Uzinduzi wa Ripoti ya Ufuatiliaji wa Elimu Duniani (GEM).

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Bi. Zulmira Rodriguez alisema kuwa dhumuni la UNESCO kuweka siku hii ya Septemba 8 kila mwaka kuwa siku ya kisomo kimataifa ili kuziunganisha jamii zote za kimataifa duniani kuweka na kuendeleza nguvu na juhudi kwa watu kujua kusoma na kuandika ili kuleta maendeleo katika jamii mbalimbali.

“Kauli mbiu hii inatufungulia milango ya uelewa juu ya malengo na mafanikio ya miongo mitano iliyopita ambayo yaliwekwa ya kutaka kila mtu anajua kusoma,” alisema Bi. Rodrieguez na kuongeza.

“Tunataka kujua ni changamoto gani zinazoikabili sekta ya elimu katika kusoma na kuandika na tunataka kufahamu namna ya kukabiliana na changamoto hizo ili kufikia malengo ambayo UNESCO iliyakusudia kufikiwa ya kila mmoja awe anajua kusoma.”

Kwa upande wa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bw. Nicholaus Bureta ambaye alimuwakilisha Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo alisema serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imejizatiti kuondoa tabaka la wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa vijana na watu wazima kwa kujenga uwiano sawa wa utoaji wa elimu kwa watu wote.

“Wizara imejipanga vizuri, na lengo kubwa la wizara ni kuhakikisha tunakuwa na mtanzania aliye elimika na aliye na stadi, maarifa na uwezo wa kutumia elimu aliyoipata,” alifafanua Bureta.

Vile vile Bw. Bureta amesema kwa sasa wizara ipo kwenye mpango wa kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) ambao unaanzia chini kwa wanafunzi wa awali mpaka shule za msingi.

Katika mpango huo walimu wamekuwa wakipata mafunzo mbalimbali ya namna ya kumuwezesha mwanafunzi kujua Kusoma Kuandika na Kuhesabu katika ngazi ya elimu ya awali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, Basilina Levira amesema kwamba kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, asilimia 78 ya vijana na watu wazima ndio waliokuwa wakijua kusoma na kuandika.

Akaongeza kuwa mwaka 2015 idadi hiyo ya wanaojua kusoma na kuandika ilishuka na kufikia asilimia 77 ambapo ilipelekea wizara hiyo kutoka na mikakati inayokusudia kuondoa kabisa tabaka la watu wasiojua kusoma na kuandika nchini.

Aidha, Basilina amesema kuwa Serikali ilipitisha sheria ya vyumba vya madarasa ya shule zote nchini kutumika kufundishia vijana na watu wazima ambao hawajui kusoma na kuandika muda wa jioni baada ya wanafunzi wa kawaida wanapomaliza masomo yao.

Amefafanua kwa kusema kuwa, wizara imeandaa programu ambayo iko kwenye mfumo wa Televisheni na picha za video (DVD) yenye masomo 65 ya kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu, ambapo kwa kutumia programu hiyo mwanafunzi anaweza kujua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa muda wa miezi 4 mpaka 6.
Mafunzo hayo kwa njia ya Televisheni na Picha za Video tayari yameanza kutumika kwa wilaya za Ilemela, Dodoma Manispaa, Songea Manispaa, Bagamoyo, Mkuranga, Temeke, Ilala na Kinondoni, ambapo asilimia 65 ya vijana na watu wazima wasiojua kusoma na kuandika wamejitokeza kujiunga na Elimu hiyo huku idadi kubwa ikiwa ni ya wanawake.

Siku ya Kisomo Duniani huadhimishwa Duniani kote kila ifikapo Septemba, 8 ya kila ya mwaka, ambapo mwaka huu 2016 maadhimisho hayo yametimiza miaka 50 tangu yalipoanza kuadhimishwa mwaka 1966.

Kauli mbiu ya siku ya kisomo duniani kwa mwaka huu ni ‘Tunasoma yaliyopita, Tunaandika yajayo, Elimu endelevu’ ambayo kwa lugha ya kiingereza ni ‘Reading the future, Writing the past’.

No comments: