|
Mh. Zitto Kabwe akiongea na Mh. Samuel Sitta nje ya Karimjee Hall Miaka ya Nyuma |
Makala hii imeandikwa na Zitto Zuberi Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo
ALFAJIRI ya Novemba 7, 2016, tuliamka na kukutana na habari za kusikitisha ya kwamba mzee Samwel John Sitta, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametangulia mbele ya haki.
Mimi, kwa sababu ya heshima zangu kwake, nilikuwa nikimwita Babu. Ninafahamu kwamba alikuwa mgonjwa kwa kitambo kidogo akisumbuliwa na saratani ya tezi dume. Habari hizi zilisambaa kwa kasi kubwa kupitia mitandao ya kijamii.
Hatimaye taarifa rasmi ikatoka kuthibitisha habari hizo.
Sitta aliitumikia nchi yetu kwa muda mrefu na kwa uadilifu mkubwa sana. Sisi wengine pia kwa kiasi fulani kukua kwetu kisiasa kumetokana na utumishi wake uliotukuka kwa nchi yetu alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Babu yangu huyu ananigusa mimi binafsi moja kwa moja. Alikuwa mtu wangu wa karibu. Tukiwa bungeni akiniandikia kitu alikuwa akitumia neno hilo “babu” kwa mwandiko wake mzuri usiotoka kwenye kumbukumbu zangu kabisa.
Labda siku zijazo, ‘vi- note’ hivi vinaweza kuchapishwa pindi watafiti watakapokuwa wakiandika historia ya nchi yetu na Bunge letu.
Aliniapisha kiapo cha ubunge tarehe 29/12/2005. Maneno ambayo aliniambia baada ya kunikabidhi Kanuni za Bunge na Katiba ya Nchi niliyaandika kwenye daftari langu la kumbukumbu siku hiyohiyo jioni.
Baada ya kula kiapo cha Utii na cha Uaminifu, kawaida wabunge hupewa mkono na mwapishaji na kupewa nyaraka za kazi. Kwa upande wangu, Sitta alinikumbatia na kuniambia “ utakuwa kiongozi muhimu sana kwa nchi yetu. You have a bright future”.
Maneno haya hayajawahi kutoka katika kumbukumbu zangu na kila nikipata misukosuko yangu kisiasa huyakumbuka na wakati mwengine yeye mwenyewe alikuwa akinipigia na kunikumbusha na kunitia moyo. Babu alikuwa mlezi wa wanasiasa vijana.
Sitta pia naweza kusema amenilea kwa kunisomesha. Mwaka 1996 nilikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Galanos jijini Tanga nikisomea mchepuo wa Historia, Jiografia na Uchumi (HGE).
Hali ya hewa ya Tanga haikunipenda, hivyo nikawa naumwa umwa sana. Pia nilitaka kusoma Hesabu badala ya Historia.
Wakati wa likizo ya mwezi Disemba mwaka 1996, nilitoka Tanga nikaenda Dar es Salaam, Wizara ya Elimu kuomba uhamisho kwenda shule yenye Somo la Hesabu, kidato cha Tano na Sita.
Nikakataliwa. Lakini nikaambiwa kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari wakati ule, Alexander Ndeki, alisoma na Sitta. Kipindi hicho Sitta akiwa Mkurugenzi wa Investments Promotion Centre (IPC) kabla haijabadilishwa jina kuwa Tanzania Investments Centre (TIC).
Nikaenda ofisi za IPC mahala ambapo leo ni CRDB Tawi la Azikiwe. Nilipofika Katibu Muhtasi wake akaniuliza kama nina miadi na bosi wake, nikasema hapana. Akaniambia hawezi kukuona. Nikasisitiza sana na kumlilia dada yule aniruhusu dakika chache tu. Akaniruhusu.
Nilipofika Sitta aliniuliza shida zangu kwa heshima kubwa. Nikamwambia kwamba ninataka kuhama shule. Akaniomba matokeo yangu ya Kidato cha Nne, nikampa maana nilikuwa natembea nayo.
Alipoyasoma akaniambia, “ wewe hupaswi kuhangaika kutafuta shule maana kwa matokeo yako unaweza kusoma shule yeyote nchini ya chaguo lako”.
Akainua simu akampigia Ndeki. Kisha akaniandikia kikaratasi niende wizarani muda uleule. Nilipofika wizarani nikapewa uhamisho kwenda Shule ya Sekondari Mazengo.
Nilipotoka nje ya wizara, nikakutana na kijana mwengine anaomba uhamisho, yeye anatoka Mazengo anataka kwenda Tosamaganga, Iringa. Akaniambia, achana na Mazengo hakuna Mwalimu wa Uchumi na hali ya vyoo ni mbaya sana. Nikarudi kwa Mkurugenzi.
Mzee aliyenipa uhamisho aliponiona narudi na kumwambia sitaki Mazengo akachukua fomu zangu za uhamisho na akachukua ‘whiteout’ akafuta Mazengo na kuweka Tosamaganga huku akisema kwa hasira “ nyie watoto wa wakubwa bwana”.
Sikujali nikaenda zangu Tosa kusoma Uchumi, Jiografia na Hesabu (EGM). Tangu wakati huo, Sitta akaendelea kufuatilia maendeleo yangu shuleni hapo, kisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Taasisi ya InWent nchini Ujerumani.
Nilipotoka Ujerumani kusoma masomo ya Juu ya Biashara ya Kimataifa mwaka 2004, ilipaswa niwe na mradi wa kitaaluma. Nikachagua kuunganisha kampuni za Kijerumani na zile za Tanzania kwa kuandika mradi wa kuchukua wafanyabishiara 20 kutoka Tanzania na kuwaunganisha na wengine 20 kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya.
Ilibidi kupata Taasisi ya Tanzania kwa ajili mradi huo na Sitta akawa mstari wa mbele kuhakikisha mradi unafanikiwa na tukautekeleza kwa umakini kwa msaada wa afisa wa TIC aitwaye Phina Lyimo.
Mwaka mmoja baadaye, tukakutana na Sitta bungeni, yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki na mimi nikiwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini. Ulezi wake ukaendelea mpaka mauti yalipomkuta wiki hii. Nimempoteza Babu mlezi.
Sitta alikuwa mwana mageuzi (reformer) na kupitia uanamageuzi wake alifanya mabadiliko makubwa sana katika uendeshaji wa Shughuli za Bunge.
Sisi tuliohudumu kwenye Bunge la Tisa, tukimwita Spika wa Kasi na Viwango, tuliona wenyewe juhudi zake za kuliweka Bunge katika nafasi yake ya Kikatiba. Licha ya kuhakikisha kuwa maslahi ya wabunge yanakuwa yanayolingana na hadhi ya Bunge, alihakikisha pia kuwa Bunge linaisimamia Serikali sawasawa.
Haikuwa kazi rahisi sana kwani kulikuwa na mvutano mkubwa sana kati ya Spika Sitta na Waziri Mkuu, Edward Lowasa, katika kuleta mabadiliko hayo.
Tulikuwa tunaambiwa kuwa mvutano ule ulitokana na tetesi kwamba Sitta ndiye alipaswa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na hivyo kuwa na msuguano na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo.
Sio Sitta wala Lowasa ambaye alithibitisha ama kukanusha tetesi zile. Sitta ametangulia mbele ya haki, labda Lowasa ataweza kusemea hili siku za usoni.
Sitta alitumia fursa ya msuguano huo kufanya mabadiliko makubwa ya kanuni za Bunge na kutoa uhuru mpana wa mawazo ndani ya Bunge na kuhakikisha kuwa Taarifa za Kamati za Bunge na hususan Kamati za Usimamizi wa Serikali zinakuwa zinasomwa na kujadiliwa ndani ya Bunge kwa mujibu wa Kanuni.
Wakati wa Bunge la Nane, taarifa za CAG hazikuwahi kusomwa hata mara moja. Ni kutokana na mabadiliko haya ya kanuni ndipo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC ) ilianzishwa mwezi Machi, mwaka 2008. Nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati ile na kuingia kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo kipindi hicho tuliiona kama Kamati ya wabunge wazee.
Namna nilivyoingia kuwa Mwenyekiti wa POAC nayo ni hadithi nyengine ya namna ya malezi ya kiuongozi yaliyofanywa na Spika Sitta.
Sikuwa nimejaza fomu kuomba Kamati ya POAC. Wakati huo ulikuwa ni wakati wa vuguvugu la Buzwagi (Mkataba wa Madini uliosainiwa kwa siri na Waziri wa Nishati Hotelini nchini Uingereza ).
Nilikuwa mjini Bagamoyo kwenye kazi za Kamati ya Bomani nikiwa na Harrison Mwakyembe na Ezekiel Maige. Spika wa Bunge akanipigia simu, akaniambia “ Babu, kesho kuna uchaguzi wa Kamati za Bunge.
“Nimekuteua Kamati ya POAC ambayo ni kamati mpya itakayokuwa chini ya Kambi ya Upinzani. Najua hukuomba kuwa mjumbe wa kamati hii, lakini nahitaji damu changa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge.
“Naomba unikubalie na kesho uwepo Dar es Salaam kwa ajili ya uchaguzi na ugombee. Utashinda maana nimeshafanya kazi yangu”. Sikuwa na namna ya kukataa japo nilitaka sana kuendelea kuwa Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya Dk. Abdallah Kigoda, ama Kamati ya Nishati na Madini chini ya William Shelukindo.
Ombi la mzee ni amri. Nikawa Mwenyekiti wa POAC na kuwa mmoja wa washauri wakuu wa Spika wa Bunge. Kamati ya PAC ikawa chini ya John Cheyo na Kamati ya LAAC ikawa chini ya Dk. Willibrod Slaa. Ilikuwa ni Bunge lenye meno kwelikweli.
Sitta alikuwa mbabe. Ubabe wake ulimpelekea kufanya maamuzi ambayo wakati mwingine yalimweka kwenye matatizo na wananchi. Mfano mzuri ni suala la Hoja Binafsi ya Buzwagi na Hoja ya Wizi wa Fedha Benki Kuu ( EPA).
Mwanzoni, Spika alikuwa upande wa wabunge wenye hoja hiyo, mimi na Slaa kiasi cha kuziboresha hoja zile kwa kalamu yake mwenyewe. Wabunge wa chama chake hawakuwa wanapenda hoja hizi na hivyo Lowasa akamweka kwenye wakati mgumu sana wa kuegemea upande wa serikali.
Hoja ya Slaa akaitupa kuwa ‘ ni makaratasi ya kuokoteza’. Hoja yangu akaiingiza bungeni na akasimamia kusimamishwa kwangu Bunge.
Wananchi walimkasirikia sana. Siku moja usiku, nikiwa nyumbani kwa Freeman Mbowe Mikocheni, Samwel Sitta, akanipigia simu kulalamika kuwa wafuasi wangu wanamtukana kwa sms. Akaniambia niwakataze. Nilimkubalia tu, lakini sikuwa na uwezo huo.
Spika Samwel Sitta akawa ni Spika pekee wa nchi yetu aliyeshuhudia uundwaji wa Serikali mbili ndani ya miaka mitano ya Uspika wake. Mzee Msekwa yeye alikaa miaka 10 na Waziri Mkuu mmoja, ingawa mwaka 1993-1995 naye aliona mabadiliko ya Mwaziri Wakuu, kutoka John Malecela kwenda kwa Msuya.
Baada ya kujiuzulu kwa Lowasa, Sitta hakurudi nyuma tena. Aliendelea kuwa Spika wa viwango mpaka alipomaliza muda wake katika Bunge la Tisa.
Spika Sitta alikuwa mwepesi kuomba msamaha alipokosea.
Nakumbuka siku moja mwaka 2009 alimfukuza bungeni Cheyo kwa makosa ambayo mzee Cheyo hakufanya. Baadhi yetu tukakasirishwa na kitendo kile.
Nikaenda kumwona Sitta ofisini kumwuliza kulikoni amdhalilishe mwenzake namna ile. Akanieleza kuwa hakuwa sawa na atamwomba radhi Cheyo.
Tukiwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge, kwa ajenda zake za kawaida tu, Sitta akamwomba radhi Cheyo. Nikikumbuka kisa hiki nacheka sana maana Jaji Frederick Werema aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alicheka mpaka kuanguka chini. Sababu?
Sitta aliketi kwenye kiti chake, wenyeviti wote wa Kamati tukiwa tumetulia tuanze kikao. Mzee Sitta akasema “ John, naomba radhi kwa tukio lililotokea bungeni wiki iliyopita.
“Sijui nilikuwa nina nini siku hiyo, nadhani nilisumbuliwa na watu wanaopitapita jimboni kutaka kunitoa, nisamehe mzee mwenzangu”.
Baada ya maneno hayo ukumbi mzima ulitawaliwa na vicheko na Cheyo akamkubalia radhi yake huku naye akicheka na yakaishia hapo. Wazee hawa wawili wameandika pamoja kitabu “ Bunge lenye Meno”.
Nimwelezeje zaidi Babu? Nimwelezeje zaidi Spika huyu wa Kasi na Viwango? Mwanasiasa shupavu, jasiri, mwenye ngozi ngumu, mbabe, mnyenyekevu inapobidi na mwenye uthubutu.
Tangulia Babu. Tangulia Mtemi wa Unyanyembe Samwel John Sitta.
Raia Mwema