![]() |
| Logo ya Zanzibar Diaspora Association (ZADIA) |
Wanadiaspora wameelezea wasiwasi wao kuwa sheria mpya ya Makosa Ya Mtandao iliyoanza kufanya kazi tarehe mosi mwezi huu nchini Tanzania, huenda ikaishia Chumbe, imefahamika.
Hayo yamekuja kwenye kongamano maalum lililoandaliwa na Jumuiya Ya Wazanzibari Waishio nchini Marekani (ZADIA) kujadili Sheria Mpya ya Makosa Ya Mtandao na Athari zake Kisiasa.
Wageni rasmi katika kongamano hilo lililofanyika kwa njia ya simu walikua ni Mwandishi khabari Bi Salma Said, na Mwanadiplomasia mstaafu Bw. Muhammed Yussuf Mshamba.
Utata wa Kisheria:
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Bi Salma Said alisema kuwa sheria hii itakuwa na utata kutokana na jinsi ya mchakato mzima wa kuipitisha ulivyokwenda. "Sheria imepitishwa kimabavu, kwani wadau wote hawakushirikiswa, pia ilipitishwa wakati Wabunge wa upinzani wakiwa wametoka Bungeni" alifafanua Bi Salma na kuongeza kuwa Baraza la Wahariri Tanzania liliikataa sheria hiyo na kupitisha azimio la kumshauri rais Kikwete asiitie saini, lakini Mheshimiwa rais aliitia saini.
Kwa upande wake, Bwana Muhammed Yussuf Mshamba ambaye pia ni Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alielezea wasiwasi wake juu ya uwezekano wa sheria hiyo kutekelezeka kwa vile mfumo uliotumika kuiptisha haukukidhi haja.
Akizungumza katika kongamano hilo, Bwana Mshamba ambaye aliwahi kuwa mtia nia wa kuwania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM alisema "Sharia ile ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini Zanzibar hawakupata nafasi ya kuiangalia".
"Kwa mujibu wa kifungu cha 234 cha Katiba ya Zanzibar, sharia zote zinazopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambazo zinatakiwa kutumika Zanzibar na Bara, kwa mujibu wa kipengele kile ni lazima Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lipewe nafasi ya kuziangalia".
Alisema Bwana Mshamba na kuongeza kuwa, sheria ile ilipitishwa wakati Baraza la Wawakilishi limeshavunjwa na hakukuwa na njia ya kuliitisha angalau kwa kikao cha dharura ili kuweza kuijadili.


