Saturday, November 23, 2013

Teteeni nchi badala ya kuiponda kwenye mablogu - Rais Kikwete awaambia Watanzania

Teteeni nchi badala ya kuiponda kwenye mablogu, Rais Kikwete awaambia Watanzania

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

  • Teteeni nchi badala ya kuiponda kwenye mablogu, Rais Kikwete awaambia Watanzania 

Watanzania waishio nje Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema wajibu mkuu wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni kuisemea vizuri, kuihangaikia na kuitetea nchi badala ya kushinda kwenye mablogu wakiiponda, kuibeza na kulalamika.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kuishi kwa Watanzania nje ya nchi kutaonekana jambo la maana zaidi ikiwa watatumia rasilimali na fursa wanazozipata ugenini kusaidia kubadilisha hali na maisha ya ndugu zao waliobakia Tanzania.

Rais Kikwete pia amewaonya Watanzania hao wasije kuchanganyikiwa na kujichanganya wenyewe kwa kuiga tamaduni za kigeni kupita kiasi. 


Rais Kikwete alikuwa anazungumza na Watanzania waishio nchini Poland usiku wa jana, Alhamisi, Novemba 21, 2013, kwenye Hoteli ya Bristol mjini Warsaw ambako alifikia wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku nne katika Poland.

Aliwaambia Watanzania hao na familia zao: “Matumaini na matarajio yetu sisi tuliobakia nyumbani ni kwamba mtaisemea vizuri nchi yetu, mtaitetea nchi yenu, mtaihangaikia nchi na kuleta faida nyumbani. Ni jambo haliingii akilini kuwa baadhi yenu mnaweza kuishi hapa na kazi yenu ikawa ni kushinda kwenye mablogu mkilaumu nchi yenu wenyewe. Nchi mbaya,
viongozi hawafai..mnapata faida gani. Mnazo nchi ngapi?”

Aliongeza Rais Kikwete: “Kuhangaikia nchi yetu ni wajibu wenu ambao hamwezi kuukwepa. Matumaini yetu ni kwamba asukuma mbele maslahi ya nchi yenu, mtatetea ustawi wa nchi yenu na ndugu zenu. Fursa zilizoko hapa mnazijua wenyewe, sisi hatuzijui. Nyie ndio mnaishi hapa, sisi tuko mbali na hatuwezi sisi kutegemewa na kutarajiwa tufanye
mambo ya hapa ambayo hatuyajui.”

Alisisitiza Rais Kikwete: “Mbona kazi za ma-Ngo’s mnazifanya vizuri bila kusukumwa ama kushawishiwa lakini kazi za kusaidia ndugu zenu hamfanyi? Kama hata hamwezi kusaidia ndugu zenu mnachangia nini nchi yenu?”
Rais amesema kuwa kwa Watanzania waishio nje kuonekana wanajali na kutetea nchi yao kutasaidia kujenga hoja ya msingi kuhusu umuhimu wa kuanzishwa kwa uraia pacha (dual citizenship) ambao Watanzania waishio nje wanaulilia. “Mnaweza kuhalalisha hoja ya uraia pacha kwa kuwa watu wenye faida kwa nchi.”

Kuhusu ombi lao la uraia pacha, Rais Kikwete amesema kuwa ni wajibu wa Watanzania waishio nje kuongeza kasi ya kuchangia mjadala kuhusu suala hilo ili likubaliwe kuingizwa kwenye Katiba Mpya.

“Rasimu ya kwanza ya Katiba ililikataa jambo hilo kwa sababu hili ni jambo lisilokuwa na ushabiki na upenzi mwingi nyumbani. Ujumbe wangu kwenu ni jipangeni vizuri kutetea hoja yenu hii. Saidieni mjadala wa jambo hilo badala ya
kushinda kwenye mablogu mkijadili siasa na hivyo kusahau yenye maslahi kwenu.”

Kuhusu kuiga tamaduni za nchi nyingine na kusahau za nyumbani, Rais Kikwete aliwaambia kuwa inaelekea kuwa baadhi wachache wanaoishi nje ya nchi, wamejichanganya na kuchanganyikiwa kiasi cha kusahau mambo ya kwao.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo baada ya mmoja wa Watanzania kudai kuwa suala zima la mahari limepitwa na wakati na kuwa kutoa mahari ni sawa ni kuwauza watoto wa kike.

Rais ambaye alionyesha kushangazwa na kauli hiyo, alijibu: “Msiige mambo ya kigeni kiasi cha kuanza kuchanganyikiwa.”

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

22 Novemba, 2013

3 comments:

Anonymous said...

Hapa Rais wetu kasema vizuri-tuitangaze vema nchi yetu. Hakikamuhimu kila mmoja wetu aipende nchi yetu kwa moyo wote.
Lakini pia kulinda heshima ya nchi yetu katika uso wa mataifa watawala wetu wawe waangalifu kuhakikisha kuwa kiwango cha uvunjaji wa haki za binadamu nchini kinadhibitiwa, maana matukio hayo kwa mfano Dr Sengondo Mvungi, Mhadhiri wa wa sheria Chuo Kikuu kuuwawa kikatili kwa mapanga, Daudi Mwangosi kuuwawa na polisi mchana kweupe, matukio hayo yanasambaa kama moto wa nyika katika zama hizi ya mawasiliano huru na hivyo kuiweka nchi yetu katika kundi la nchi chache ovu duniani.

Anonymous said...

Rushwa.
Ufisadi
Kutetea maovu ya wakubwa.

Hata tukiwa wazalendo kiasi gani ni vigumu kutetea mambo haya na mengine.

Ni mambo ambayo hayakubaliki!

AMINA said...

ni kweli watu siku hizi wamepoteza uzalendo kabisa karibu tuzungumze pia www.chatguest.com