Kutoka ippmedia.com
Wakati umesalia mwaka mzima kufikia uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, imebainika kuwa ndani ya CCM vikao vya siri vyenye lengo la kuhakikisha kunakuwa na mgombea mwingine wa kumpiku rais aliyeko madarakani, Rais Jakaya Kikwete vimepamba moto.
Taarifa zilizolifikia gazeti zimefichua kuwa katika vikao hivyo, wahusika wanajadili namna ya kuhakikisha mtu wanayemtaka anapitishwa kuwania nafasi ya urais.
``Hivyo vikao vimeanza siku nyingi… wahusika wanavifanya kwa siri sana kwa sababu wanafahamu ni kinyume na taratibu za chama, lakini vipo na vimepamba moto hivi sasa, ``kimedai chanzo hicho.
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa CCM, Kapten John Chiligati alipoulizwa juu ya hilo, amesema katiba ya CCM inatoa haki ya kila mwanachama kuwania nafasi ya uongozi katika ngazi yoyote, na akasema kwa wale wanaokusudia kugombea urais kupitia chama hicho bado hawajavunja katiba ya chama.
Hata hivyo, akasema CCM ina utaratibu wa kumpa rais aliyeko madarakani kipindi cha pili cha kuongoza.
``Hao wanaokaa vikao vya siri wanapaswa kuongozwa na busara zao kuwa wanapoteza muda kwa sababu utaratibu wetu CCM wanaufahamu,`` akasema kabla ya kuongeza.
``Kwa mujibu wa katiba yetu kila mwanachama ana haki ya kugombea akitaka, lakini utaratibu wetu rais anapewa kipindi cha pili…kwa busara tu inapaswa wajue kuwa wanajisumbua,`` akasema Bw. Chiligati.
Amesisitiza kuwa wale wanaokomalia kukaa vikao vya kupitisha wagombea urais wanajisumbua na hawatafanikisha azma yao.
Amewafananisha watu hao na mtu mwenye paspoti na visa anayetaka kwenda London kwa miguu.
``Mtu akiwa na vitu hivyo anaruhusiwa kwenda Uingereza, lakini unapomuona anataka kwenda London kwa miguu, mwache tu maana akifika tu pale Namanga atakuwa hoi, hivyo mwanachama mwingine kuwania urais kupitia CCM mwakani ni vigumu kama kwenda London kwa miguu,`` akasisitiza Bw. Chiligati huku akiangusha kicheko.
Katika kinyang`anyiro cha mwaka 2005, Rais Kikwete alichuana na wana CCM kadhaa kabla ya kuibuka kidedea katika mchakato uliosisimua sana wa kumsaka mgombea ndani ya chama chake.
Baadhi yao ambao walikuwa na nia kama yake ya kumrithi Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ni pamoja na John Shibuda, Fredrick Sumaye, Balozi Ali Karume, Dk. Abdallah Kigoda, Balozi Patrick Chokala na wale waliochuana hadi kwenye ngwe ya mwisho ya tatu bora ambao ni Dk. Salim Ahmed Salim na Prof. Mark Mwandosya.
Akizungumzia sakata hilo la vikao vya siri na uhahali wake kisheria, mwanasiasa na Mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi amesema hakuna sheria inayomzuia mtu au kupanga muda wa kufanya kampeni za kuwania uongozi nchini.
Akasema mtu anaweza kuanza harakati za kuwania uongozi kwa muda mrefu kabla ya kutekeleza azma yake ya kujitosa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi.
``Kufanya kampeni za kuwania uongozi sio dhambi, hakuna sheria inayomkataza mtu wala kupanga muda wa kufanya kampeni, mtu anaweza kufanya kampeni hata kwa miaka miwili au mitatu kabla ya uchaguzi, ni haki ya kidemokrasia,`` akasema Dk. Mvungi.
Wakati hayo yakiendelea kuna taarifa kuwa tayari Umoja wa Vijana wa CCM wilayani Bukoba wametoa shilingi milioni moja kwa ajili ya Bw. Jakaya Kikwete kuchukua fomu ya kuwania urais mwakani, hali inayoonyesha tayari wamempitisha JK kama mgombea wa kiti hicho mwakani.
Kuhusu sakata la vikao vya siri ndani ya CCM, Dk. Mvungi amesema taarifa hizo alizipata muda mrefu, lakini akasema akaongeza kuwa vikao hivyo vimepamba moto kutokana na uchaguzi kukaribia.
``Hivyo vikao nimevisikia muda mrefu, lakini kwa sasa najua vimepamba moto, nadhani kwa vile uchaguzi unakaribia na wanataka kujiimarisha zaidi,`` akasema Dk. Mvungi.
Aidha amesema kuwa kuwepo kwa watu wanaotaka kutoa upinzani wa kuwania uongozi ndani ya chama ndivyo demokrasia inavyotaka na kuwa hatua hiyo haipaswi kupingwa.
Amesema katika harakati za kuwania uongozi, lazima kuwepo na kampeni za aina mbili ambazo ni zile za siri na zile za wazi.
Akifafanua zaidi, amesema mtu akitafuta kuungwa mkono na kundi la watu, lazima kwanza afanye kampeni zake kwa siri, na pale anapokuwa amewapata wanaomuunga mkono na kukubalika, ndipo kampeni hizo hugeuka na kuwa za wazi kwa ajili ya kupata wapiga kura wengi.
Hata hivyo, Dk. Mvungi amesema ikiwa vikao hivyo vinafanyika kwa maslahi ya watu binafsi litakuwa ni tatizo lingine ambalo litapaswa kushughulikiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour Party, TLP, Bw. Augustine Mrema naye amedai kuwa taarifa za kuwepo kwa vikao vya siri ndani ya CCM tayari amezipata.
Hata hivyo Mrema amesema taarifa alizonazo ni kwamba makundi hayo yanayofanya vikao vya siri yanajipanga zaidi kuwania urais mwaka 2015, ambapo wanaamini kuwa hawatakuwa na mpinzani aliyeko madarakani kwa vile rais wa sasa atakuwa amemaliza muda wake.
``Taarifa za kuwepo kwa vikao vya siri mimi ninazo, lakini ninavyojua hao wanaokaa vikao vya siri sasa wanajiandaa kwa ajili ya mwaka 2015, wanajua mwaka kesho hawamwezi Kikwete,`` akasema Bw. Mrema.
Aidha Bw. Mrema ameonya kuwa CCM ni wajanja ambao wanaweza kuonekana wakizozana au kupingana wakati fulani, lakini inapofika wakati wa kufanya maamuzi ya msingi wanapatana.
Amesema kwa sasa CCM imeshajengeka desturi ya kurithishana madaraka kwa kipindi cha miaka kumi, na hivyo sio rahisi hivi sasa akaibuka mwanachama akaweza kuwashawishi wamsimamishe mgombea mwingine, wakati aliyepo sasa hajamaliza muda wake wa miaka kumi ya kuongoza.
``Hawa CCM ni wajanja sana, wameshaamua kurithishana madaraka kwa muda wa miaka kumi, unaweza kuwaona wagombana sasa hivi, lakini ukifika wakati wa kufanya maamuzi wanakuwa kitu komoja,`` akasema Bw. Mrema.
Amedai kuwa kwa vile ameshashtukia mchezo wao, yeye (Mrema) na chama chake cha TLP wamegundua kuwa urais hivi sasa siyo dili, badala yake ameamua kugombea ubunge kwenye uchaguzi ujao.
``Tumegundua kuwa urais sasa siyo dili, bali dili ni ubunge ambao unakuwezesha kwenda kuwatetea wananchi bungeni, ndio maana chama changu kimenituma kwenda kugombea ubunge katika jimbo la Vunjo,`` akasema Bw. Mrema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment