Thursday, June 18, 2009

Ze Utamu Umetufundisha Nini?

Dr. Masangu Matondo Nzuzullima


ZE UTAMU IMETUFUNDISHA NINI?

Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima

Alhamisi tarehe 23/4/2009 rafiki yangu mmoja kutoka Dar es salaam alinitumia barua pepe ya kushangaza. Alikuwa analalamika kuhusu tovuti moja iliyokuwa ikiitwa Ze Utamu. Alisema kwamba tovuti hiyo mashuhuri sana ilikuwa ni tovuti ya hatari na ilikuwa imesababisha madhara makubwa katika jamii. Katika barua pepe hiyo alisema kwamba watu Dar es salaam walikuwa hawalali kwani hawakujua kama kesho yake wangejikuta wametamuishwa (kutundikwa katika Ze utamu) ama la. Kwa ujumla mambo hayakuwa shwari. Aliendelea kushangaa ni kwa nini serikali ilikuwa imeiachia tovuti kama hiyo kuendelea kuchafua amani na utangamano wa wanajamii.

Siku hiyo hiyo, gazeti la Majira lilikuwa na makala yenye kichwa cha habari "Waendesha mtandao Ze Utamu wasakwa, Ni baada ya kuwadhalilisha viongozi". Habari hizi pacha zilinitatanisha na kuniachia maswali mengi. Je, hii Ze Utamu ilikuwa ni tovuti ya aina gani na ilikuwa inaandika habari zipi mpaka kulisukuma jeshi la polisi kuacha shughuli zake muhimu za ulinzi wa raia na kuanza kuwasaka wamiliki wake? Niliikumbuka Jambo Forum ambayo nayo katika kilele chake ilileta kizaazaa mpaka wamiliki wake wakakamatwa na jeshi la polisi. Bila kupoteza muda nilikimbilia kwenye google na baada ya sekunde chache tu niliweza kuipata hiyo Ze Utamu. Nilichokiona kilinishangaza kwani sikujua kama Tanzania tulikuwa tumepiga hatua kubwa namna ile katika uhuru wa vyombo vya habari. Japo mitandao ya udaku imezoeleka sana katika nchi za Magharibi ambako kusema kweli hakuna mtu anayeshangazwa nayo tena, Ze Utamu kidogo ilikuwa tofauti. Hata huku kwa wazungu, sijawahi kuona mtandao ambao lengo lake ni kutukanana na kuchafuliana majina na hadhi. Kinyume na mitandao iliyotangulia kama vile Jambo Forum ambayo ilijikita zaidi kushambulia tabaka fulani la watu katika jamii, Ze Utamu yeye alikuwa hachagui tabaka la mtu wala nafasi na hadhi yake katika jamii – si matajiri, si masikini, si wanawake, si wanaume, si wazee, si vijana, si viongozi, si waongozwaji, si mafisadi, si wasafi – kila mtu alikuwa sawa mbele yake. Kinyume na nchi za Kimagharibi, mitandao na magazeti ya udaku huwa hayatiliwi maanani sana na wasomaji; na mara nyingi hakuna anayejihangaisha na kutaka kuthibitisha habari yanayoziandika. Gazeti la udaku la Globe kwa mfano limekuwa likiandika mara kwa mara habari zinazodai kwamba Obama ni shoga na kwamba aliwahi kuwa na mpenzi mwanamme wakati akiwa bado seneta (tazama www.matondo.blogspot.com). Kila mtu anajua kwamba habari hizi ni za uwongo na hakuna anayezijali wala kuzitilia maanani hapa Marekani. Hii ndiyo tofauti kubwa na nyumbani ambako watu bado wanadhani kwamba kila kitu kinachoandikwa katika magazeti au katika mtandao basi ni cha ukweli. Kama hili lingeeleweka, tovuti kama Ze Utamu isingeweza kuwa mashuhuri na kufikia hatua ya kuwanyima watu usingizi.

Ze Utamu ilikuwa nini?

Kimsingi, inavyoonekana Ze Utamu ilikuwa ni tovuti ambayo (kama walivyodai waendeshaji wake) ilikuwa na lengo la kurekebisha tabia za wanajamii wote bila kujali nafasi zao. Lengo lake kuu lilikuwa ni kupambana na ufisadi - ukiwemo ule wa ngono - na matendo yote machafu yaliyoonekana kukiuka maadili ya jamii yanayotendwa na mtu ye yote katika jamii bila kujali tabaka lake.

Kama tovuti hii ingemakinikia lengo lake hili, kwa hakika ingekuwa chombo makini na cha muhimu sana ambacho kingetoa mchango mkubwa katika kutetea maadili ya jamii ya Kitanzania wakati huu ambapo utandawazi unameza kila kitu kilicho chetu tena kwa kasi ya kutisha. Mitandao na magazeti ya aina hii wakati mwingine yamechangia kuibua kashfa nzito nzito za viongozi katika sehemu mbalimbali duniani. Kwa mfano, John Edwards - mgombea mwenza wa uraisi wa Marekani mwaka 2004 na mgombea uraisi mwaka 2008 kupitia chama cha Democrat alikumbwa na kashfa ya ngono ambayo iliibuliwa kwa mara ya kwanza na mtandao wa gazeti la udaku la National Enquirer. Mwaka juzi waziri mmoja kule Afrika ya Magharibi ilibidi ajiuzulu baada ya picha zake za ngono kuwekwa katika mtandao wa kurekebisha tabia kama Ze Utamu. Mifano hii inaonyesha kwamba mitandao kama hii inaweza kuwa na mchango fulani chanya katika jamii japo kusema kweli faida zake zinakinzwa na uhasi na migongano ambayo mitandao hii inaweza kusababisha katika jamii kama yetu ambako watu bado wanafikiri kwamba kila kitu kinachoandikwa katika mitandao au magazeti ni cha kweli.

Hata hivyo, Ze Utamu ilikuwa imeshalitelekeza jukumu la kurekebisha tabia za wanajamii, na badala yake iligeuka kuwa chuo kikuu cha matusi, majungu, fitina, udaku na husuda. Kama mtu ulimtongoza akakukataa, kama mtu ana maisha mazuri kukuzidi, kama mwenzio alikuzidi kete na kumchukua binti au mvulana uliyekuwa ukimtaka kwa muda mrefu, kama mtu anapendwa na watu kuliko wewe, kama .....basi ulichotakiwa kufanya ni kuitafuta picha yake (hata bila picha ni sawa tu) na kuituma kwa Ze Utamu. Fomyula ilikuwa rahisi sana: sema kwamba ni fisadi (wa ngono), anatembea na watu wengi kwa kujirahisi (unaweza kutaja majina machache), ana UKIMWI na anausambaza tena kwa makusudi, anachukua waume/wake za watu, anapenda vya bure (mteremko), anajiona sana kumbe hana lolote n.k. Halafu waombe "wadau" wamwage data. Na kweli data zingemwagwa na mara nyingi yalikuwa ni matusi ya kutisha ambayo yangeweza kukufanya ufiche uso wako kwa soni. Mara moja moja wadau wangeweza kusimama kidete na kumtetea huyo aliyetamuishwa wakidai kuwa kaonewa, ni mwanajamii makini asiye na ubaya na mtu n.k. Sifa moja ya Ze Utamu hata hivyo ilikuwa ni kwamba mtu ukishatamuishwa basi ulikuwa huachiwi hata utetewe/ujitetee vipi.

Kwa vile hakuna utafiti ambao umekwishafanywa na wanasosholojia au wanasaikolojia kujua hasa madhara ya kutamuishwa katika mitandao ya aina hii si ajabu mtandao huu tayari ulikuwa umeshaleta misukosuko ya kifamilia na kisaikolojia kwa wale ambao walishatamuishwa. Kutokana na matusi mazito yanayoporomoshwa hapo, bila kujali nafasi na tabaka la mtu aliyetamuishwa, watu wengi walianza kuhoji ulikokwenda undugu, umoja, amani, upendo na Utanzania wetu ambao Mwalimu Nyerere alituachia. Wengine walihoji ni kwa nini serikali ilikuwa imeufumbia macho mtandao wa aina hii kwa karibu miaka miwili mizima. Swali la msingi ambalo linaweza kuulizwa hapa ni hili: tumefikaje katika hatua hii ya kutamuishana – sisi Watanzania na Utanzania wetu? Jibu ni rahisi sana - UTANDAWAZI!

Utandawazi na Lengo Lake

Utandawazi ni joka la mdimu lenye vichwa vingi angamizi – vichwa vyenye kazi tofauti tofauti ambavyo lengo lake kuu la jumla hasa ni kuuangamiza utamaduni wetu na hivyo kutufanya tujidharau, tujidogoshe, tusijitambue na hatimaye tuweze kuendelea kutawalika, kunyonyeka na kudhulumika kirahisi zaidi.
Ni lazima ikumbukwe kwamba tapo la utandawazi tunalolishuhudia kwa sasa ni mojawapo tu ya matapo mengi ya utandawazi yaliyotangulia, matapo ambayo yalitukutanisha na wageni kutoka Ulaya na kwingineko. Mahusiano yetu na ulimwengu wa wageni hawa kutoka nje tangu mwanzo yamekuwa ya kihasama, kiunyonyaji na dhuluma – kuanzia enzi za biashara ya utumwa mpaka wakati huu tulio nao. Uzalendo, utu na Uafrika wetu ulikunguwazwa na kufishwa wakati wa biashara ya utumwa “tulipokubali” kugeuzwa bidhaa na kuuzwa kama nyanya au vitunguu sokoni. Ni wakati huu ambapo tulipondwapondwa kisaikolojia na kuaminishwa kwamba tulikuwa binadamu wa tabaka la chini ambao kamwe tusingeweza kuwekwa katika daraja moja na “mabwana” kutoka Ulaya na Uarabuni. Vita hivi vya kisaikolojia vilivyopiganwa kwa ujanja sana kupitia dini, sera za lugha na elimu dhidi yetu vilipiganwa kwa nguvu zaidi na “mabwana” wakati wa ukoloni. Ni wakati huu ambapo bara letu liliitwa bara la giza na tamaduni zetu zilizotukuza, kutulea huku zikishabihiana vyema na mazingira yetu ya asili zilibatizwa kuwa za kishenzi na kinyama. Ukoloni ulitazamwa na hata kutambulishwa kama mkakati wa “kutustaarabisha” na kututoa katika giza nene la kuabudu dini za “kishenzi”, kuongea lugha za kishamba na kukumbatia tamaduni zetu za kiwango cha chini. Lugha zetu ambazo kupitia kwazo fikra zetu na mtazamo wetu pamoja na nafasi yetu katika dunia hii vimefinyangwa ziliitwa duni, zikadumazwa na kunyimwa nafasi za matumizi katika sekta rasmi. Matokeo yake lugha zetu ambazo ndizo zinaamua sisi ni nani, nafasi yetu ni ipi katika ulimwengu huu na tunahusianaje na wengine katika mazingira yetu zilinyimwa “meno” na tangu hapo zimebakia kuwa lugha zisizo na mwelekeo wala matumaini. Kulingana na Ngugi wa Thiong’o, ukoloni na utumwa wetu wa kisaikolojia ulikamilika pale tulipokubali lugha zetu kuvishwa sanda na kutengwa na ulimwengu na mazingira yetu. Kuanzia hapo, tulikoma kuwa sisi na kuanzia wakati ule, sisi si sisi tena, hatujijui na hatujui kwamba hatujijui kuwa sisi ndisi. Tumekuwa watumwa wa fikra!
Japo kupatikana kwa uhuru wa bendera kuliwasha moto wa matumaini katika mioyo ya Waafrika, sasa ni wazi kwamba matumaini hayo yalikuwa yametiwa mubaalagha na ahadi za “kuutafuta kwanza uhuru wa kisiasa na uhuru mwingine ungefuata” tulizopewa na akina Kwame Nkrumah wetu zimeshindwa kutekelezeka. Lakini utumwa mbaya kabisa ni ule utumwa wa kisaikolojia - utumwa wa kimawazo uliomdogosha Mwafrika na kumfanya ajione kuwa yeye ni binadamu wa daraja la pili na utamaduni wake kuwa wa kizamani, usioendana na wakati na wa kishenzi. Mkakati mama ulioanzishwa na watawala wetu wakati wa biashara ya utumwa na kuendelezwa (wakati mwingine kwa nguvu) wakati wa ukoloni bado unaimarika siku hadi siku na bado umejikita barabara katika fikra zetu. Na baada ya miaka sitini ya uhuru bado tunaamini kwamba utamaduni wetu na hata lugha zetu ni za kishamba na hazifai kutumiwa katika sekta rasmi kama elimu na vyombo vya habari. Matokeo yake lugha zetu za jadi zimegeuka kuwa lugha za kuonewa haya na kizazi kipya hakitaki tena kuzizungumza. Ati bila lugha na utamaduni wetu wenyewe, sisi ni/tumekuwa/tutakuwa nani?
Kutokana na kutawaliwa kwetu kitamaduni, leo tunakazana sana kuiga utamaduni wa “mabwana” zetu wazungu. Kinashosikitisha zaidi ni ukweli kwamba mara nyingi uigaji wetu umegeuka kuwa mashindano ya kujidharau na tunaiga mpaka kuwazidi hao tunaojaribu kuwaiga. Mifano ni mingi kuthibitisha dai hili (mfano mashindano ya urembo yaliyozagaa kila mkoa, wilaya, mji, tarafa, kata, vitongoji na muda si mrefu pengine yataingia katika familia). Naona hata katika Ze Utamu tulifuata ruwaza (pattern) ile ile – kuiga mpaka kuwazidi tunaojaribu kuwaiga. Nadhani hata wazungu, pamoja na uhuru wao wa habari usio na kikomo, wanayo heshima kidogo kwa viongozi wao na hawawezi kuwa na tovuti mashuhuri ya kizushi ambayo inaweka picha za uongo (zilizofanyiwa photoshop) za viongozi wao wakiwa uchi na watu kuanza kuporomosha matusi mazito. Pamoja na kuishi Marekani kwa karibu miaka 10 sasa jambo hili lilinishangaza na kunisikitisha. Hata kama tovuti za aina hiyo zingekuwepo (au zipo), wenzetu hawa, kinyume na sisi ambao tunaparamia na kuiga mambo kwa pupa, wanajua kwamba huu ni upuuzi tu na hakuna mtu anauyetilia maanani.
“Kiinimacho” cha usawa, Undugu na Umoja
Swali kubwa nililojiuliza baada ya kuiona Ze Utamu ni hili: Moyo wa upendo, umoja, usawa, undugu na mshikamano ambao muasisi wa taifa letu Mwalimu Nyerere alijitahidi sana kuupandikiza mioyoni mwetu ulikuwa wapi? Chuki, uhasama na hasira ya “wadau” katika Ze Utamu ilikuwa ya kutisha na ilikuwa ni vigumu kuamini kwamba hawa walikuwa ni Watanzania waliobahatika kuwa na kiongozi mwanafalsafa, msomi na mwenye welewa mpana aliyepigana kufa na kupona kuangamiza ukabila, matabaka na kuhakikisha kwamba kila mtoto anapatiwa nafasi sawa ya elimu ambayo ndiyo mkakati mama wa ukombozi katika jamii. Je, upendo, usawa, amani, undugu na mshikamano vilivyokuwa vikihubiriwa sana miaka michache tu iliyopita vilikuwa vya kweli au vilikuwa kiinimacho tu kwa Watanzania? Hasira hii ya “wadau” – ambayo ilionekana waziwazi hasa kama mtu aliyetamuishwa alikuwa ni kiongozi, “fisadi” au mtu mashuhuri katika jamii – imetoka wapi? Inawezekana usawa, undugu na umoja vilivyokuwa vikihubiriwa sana vilikuwa ni viinimacho tu? Ati, hali halisi ikoje katika jamii? Ahadi zile za MwanaTANU na baadaye mwanaCCM bado zina ukweli wo wote? Ni kweli kwamba binadamu wote ni sawa au (kama wanyama wanavyogundua katika riwaya mashuhuri ya George Orwell ya Shamba la Wanyama) binadamu wote ni sawa lakini binadamu wengine ni sawa zaidi ya wengine?

Ze Utamu Imetufundisha nini? Tufanye nini?

Mbali na kuionyesha vyema tabia yetu tatanishi na ya kijinga ya kuiga mambo hadi kuwazidi hao tunaojaribu kuwaiga (na hivyo kuthibitisha zaidi utumwa wetu wa kisaikolojia na kitamaduni), Ze Utamu imetufundisha kwamba mambo si shwari katika jamii yetu na watu wana hasira; na kwamba upendo, amani, umoja na mshikamano uliokuwa ukihubiriwa sana ama vilikuwa ni kiinimacho tu au watu wameshtushwa na mfumuko wa matabaka na sasa wamechoka. Niliangalia maoni yaliyokuwa yakiwekwa na “wadau” baada ya mtu mashuhuri, kiongozi au “fisadi” kutamuishwa na niliweza kuiona hasira ya watu ikiwaka moto. Pengine matabaka ambayo tumeyaachia kufumuka kwa kasi ya risasi - ambapo tumewaruhusu watu wachache wajikusanyie “vijisenti” vyote na kuwaacha walio wengi wakiwa hawana kitu yameshatia sumu katika mioyo ya Watanzania na hasira kali inafukuta mumo kwa mumo kama volkeno iliyolala. Tusije tukaiachia volkeno hii iendelee kufukuta mumo kwa mumo kwani siku itakayoripuka Tanzania yetu itakuwa matatani.
Ze Utamu pia imetuonyesha tabia nyingine ambayo tunayo sisi Watanzania. Tunapenda sana kuongea na kupiga porojo na Mswahili hata kama hana hoja au mchango wa maana katika mjadala ni lazima achangie. Tazama kwa mfano mada mbalimbali makini katika blogu mashuhuri ya michuzi na utaona ninachokisema. Hata kama mada iliyoanzishwa ni nzuri, yenye manufaa na inayotaka mjadala hasa na hoja komavu, badala ya kutoa hoja na kujadili kwa heshima na hatimaye kukubali kutokubaliana kiungwana utakuta mara nyingi watu wataanza kubeza, kudharau na kumponda mtoa mada. Mfano mmoja ni mada ya hivi karibuni ya Profesa Mbele kuhusu safari za nje za Raisi Kikwete. Profesa Mbele kama vile Mtanzania ye yote anayo haki ya kutoa maoni yake na kwa vile hii ni topiki ya muhimu basi mtu ungetegemea hoja madhubuti za kuunga mkono ama kupinga. Badala yake hoja hutaziona na mahali pake ni mashambulizi na mengine ni yale wenyewe wanaita “personal attacks” Tabia hii inayokera na ambayo inaashiria uzembe wa kufikiri, kutafakari mambo kwa kina, kujenga hoja madhubuti na kuzitetea, kwa kiasi fulani inaakisi yale yaliyokuwa yakitokea kwenye Ze Utamu – kushambuliana na kudhalilishana. Kwa sisi Watanzania, tabia hii inatatanisha kwani kutokana na malezi yetu na falsafa yetu ya kitaifa tungetegemewa kuwa watu wenye upendo na masikilizano. Kuna chuki mioyoni mwetu na sijui kiini chake hasa ni nini!

Ninapoandika makala haya Ze Utamu haipo tena. Tusije basi tukakaa kitako, tukabweteka na kukenua meno tukidhani kwamba tumeshinda vita. Vita ndiyo tu kwanza vimeanza kwani inawezekana kabisa Ze Utamu wengine na pengine wabaya zaidi watazaliwa. Kwa vile sisi tunaiga kuzidi hao tuwaigao, tusubiri siku vipindi kama Jerry Springer, Maury na Cheaters vitakapofika kwetu. Sijui vitakuwa na sura gani. Tusije tukasahau kwamba adui yetu hasa ni utandawazi na hao “mabwana” zetu wanaotamani kututawala katika nyanja zote za maisha yetu milele na milele. Tufanyeje basi ili kuuokoa Utanzania, Uafrika na utu wetu? Kusema kweli si jambo rahisi na hakuna njia ya mkato. Kutokomeza utumwa wa kisaikolojia na kasumba ya kujidharau sisi pamoja na utamaduni wetu, kasumba iliyopandikizwa akilini mwetu kijanja kwa karne nyingi, kasumba inayotufanya tujione kuwa binadamu wa daraja la pili si kazi rahisi. Inabidi tuwe na mkakati mama wa kufufua utamaduni wetu na mahali pazuri pa kuanzia ni katika lugha zetu za kienyeji kwani kama asemavyo Ngugi wa Thiong’o katika kitabu chake cha Decolonizing the Mind lugha zetu ndizo nguzo hasa za utamaduni wetu na hatuwezi kuwa huru bila kuziheshimu lugha zetu na hivyo kuulinda utamaduni wetu. Wakati sasa umefika wa kuandaa sera makini inayotekelezeka kuhusu uhimizaji na uboreshaji wa lugha zetu - sera ambayo itazipa nafasi lugha zetu za kienyeji kutumika katika sekta rasmi kila inapowezekana. Mfumo wetu wa elimu urekebishwe na elimu tunayowapa vijana wetu ihusiane na mazingira yao. Ni lazima pia tupunguze tofauti za kitabaka kati ya wenye “vijisenti” na masikini walio wengi wanaoshindia mlo mmoja. Afya na mustakabali wa taifa letu unategemea ni kwa jinsi gani tutakavyofanikiwa katika kupunguza pengo kati ya matabaka haya kinzani. Si budi pia tuangalie upya dhana nzima ya maendeleo. Ati, tunaposema maendeleo tunamaanisha nini hasa? Ni lazima tuvumbue dhana mpya ya maendeleo – dhana yetu wenyewe kulingana na mazingira yetu. Yote kwa yote tukumbuke kwamba hivi ni vita vya kisaikolojia. Tukiweza kuwaaminisha vijana wetu kwamba kuongea Kisukuma, Kihaya au Kichaga kwa ufasaha ni jambo la kujivunia, kwamba siyo lazima kuvaa mitepesho kuashiria usasa, kwamba siyo lazima kujikondesha mpaka mbavu zichomoze kuwa mrembo, kwamba rangi nyeusi haina tofauti na rangi zingine na kamwe Mwafrika siyo kiumbe wa daraja la pili basi tutakuwa tumeanza kupiga hatua (japo za kitoto) katika safari yetu ndefu na ngumu ya kujitafuta na kujifahamu upya sisi ni nani na nafasi yetu katika dunia hii ya sasa ni ipi. Kizazi hiki cha dot com ni lazima kiandaliwe mkakati wa kuanza kukirudisha katika kiini cha Uafrika na Utanzania wake.

Waswahili wana msemo unaosema kwamba zimwi likujualo halikuli likakumaliza. Utandawazi ni zimwi lisilotujua – zimwi lililotuparura vibaya sana wakati wa utumwa, likafinyangafinyanga fikra zetu wakati wa ukoloni na sasa, baada ya miaka zaidi ya sitini ya uhuru, linatishia kuumeza kabisa utamaduni na usisi wetu. Kila siku tunapoamka ni lazima tujisaili: Utandawazi ambalo ni zimwi lisilotujua, linaweza kweli kutula lisitumalize? Je, tufanye nini?

4 comments:

Anonymous said...

Kama hao wahusika wa zeutamu wamenaswa, basi jambo la maana limetendeka. Hiyo site ilikuwa ya kudhalilisha watu tu, utakuta ulikuwa na rafiki yako ikisha mmegombana, basi siku ya pili yake unakuta picha yako imewekwa na kuandikwa maneno yote machafu yaliyokuwepo kwenye dunia. Mimi nimeingia kwenye huo mtandao mara moja tu na kuapa sitorudi tena na wala sijaona chochote cha kurekebisha tabia ya mtu bali kudhalilisha. Picha chafu sana sana ambazo hazifai kuwekwa public kwenye jamii yetu.

JOPO said...

if the people of UTAMU were caught, it show how conservative the society of Tanzania has been. we need to be liberal and open to criticism. The president photo was uploaded and he had the time in hell to go and close down the site,while he has people dieing, no electricity and economy which is still not diverse. he has alot to worry about other than UTAMU. i find it disgrace of the lack of freedom of speech in Tanzania and people have to be open and ask why and how. we see Iranian people wanting to be free, Tanzania need to be liberal and start top grow.

Anonymous said...

wewe jopo mpumbavu sana, i have a feeling that you were one of the zeutamu perpetuators....na unapotoa maneno kama haya be careful, u can end up in cell young man....ni rahisi kukutrace wewe na kukukamata mara moja, unajua uchunguzi na msako wa zeutamu owners and sympathisers bado unaendelea...wewe ndo utaeleza huyo zeutamu ni nani...angalia kijana, unaweza ingia matatizoni kwa vitu vya kipumbavu kama hivi....
Pia yawezekana hukuona picha ya rais ilikuwa ikoje, and if u are in full command of ur sense then i feel pitty for u...

Anonymous said...

Zeutamu ni mmoja kati ya mitandao ambayo tunaisubiri kwa hamu kwani ulikuwa na ukweli.zaidi haukujali mipaka ya uwezo wa mtu yoyote.tatizo ni Jamii ya watanzania hawapende ukweli na sikuzote wamejaa unafiki.Kuna mambo mengi sana ulikuwa huwezi yapata katika magazeti lakini ukayapata kwa ukeli na upana na picha madhuhuri katika zeutamu mtanao watu.Tanzania ni jamii ya wanafki na wanaendelea kutunza unafki kwa kuukatisha mtandao kwa kudaikuwa wamekamata.