Thursday, October 01, 2009

Swine Flu (H1N1) Nchini Tanzania - Taarifa!


Taarifa Maalum Kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu hali ya ugonjwa wa Mafua Makali ya Nguruwe (Influenza A H1N1), Ikiwa ni taarifa ya tatu kutolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii tangu ugonjwa huu uingie hapa nchini.

Ugonjwa huu kwa mara ya kwanza ulitokea katika nchi ya Mexico mwanzoni mwa mwezi wa Aprili 2009. Hadi hivi sasa nchi 24 katika bara la Afrika zimethibitisha kuwa na ugonjwa huo, zikiwa na jumla ya wagonjwa 8,187 na vifo 41.

Nchi inayoongoza kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa katika bara la Afrika ni Afrika ya Kusini ambayo ina jumla ya wagonjwa 7,606 na vifo 31. Hadi kufikia tarehe 30/09/2009 idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huu hapa nchini ni 170.
Kati ya wagonjwa hao 151 ni kutoka mkoa wa Dar es salaam, 15 kutoka Wilaya ya Mbulu mkoa wa Manyara, na 4 kutoka mkoa wa Mara. Wengi wa wagonjwa hao walikwishatibiwa na kupona na kwa sasa hivi wagonjwa waliolazwa ni 15 ambao wapo wilayani Mbulu.

Vile vile, kati ya wagonjwa hao 170, kuna Watanzania 80. Hii inaonyesha kwamba, maambukizi ya ugonjwa huu yameanza kuingia kwenye jamii yetu. Aidha, hali ya sasa ya ugonjwa inaonyesha kuwa maambukizi yametokea katika shule mbalimbali za mkoa wa Dar es salaam. Sababu kubwa ni kwamba, virusi vya ugonjwa huu huenea kwa haraka kwenye mikusanyiko ya watoto, kundi ambalo limethibitishwa kisayansi kuwa katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya Ugonjwa huo.

Idadi ya shule zilizothibitishwa kuwa na ugonjwa huu mpaka sasa, zilizoko katika mkoa wa Dar es salaam ni 9. Shule hizo ni pamoja na International School of Tanganyika, Delhi Primary School, Little Scholar, French Primary School, Dar es salaam International School, Msasani Peninsular Primary School, Feza Girls Secondary School, Makongo Secondary school na Litlle Deau Mont.

Wagonjwa wengi waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huu hapa nchini hawakuwa na dalili kali za ugonjwa huo, na walipona kati ya siku 3 hadi 5 baada ya kupatiwa matibabu. Wizara imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na ugonjwa huo ambapo: ·

Imeimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa huu, katika viwanja vya ndege, mipakani pamoja na bandari.
· Imeimarisha Ufuatiliaji na Utambuzi wa ugonjwa huu katika hospitali za rufaa, mikoa na wilaya na kuunda kamati za wataalamu za kitaifa, mikoa na wilaya ili kupambana na ugonjwa huu

· Pia mafunzo yametolewa kwa watumishi wa afya katika hospitali za rufaa, mikoa pamoja na kamati za afya za wilaya kuhusiana na ugonjwa huu.

· Wizara imepeleka vifaa kinga katika hospitali zote za rufaa na mikoa pamoja na dawa (Tamiflu) dozi 1000 kwenye hospitali zote za rufaa, mikoa na wilaya.

· Wizara ilitembelea na kufanya majadiliano na uongozi wa hospitali binafsi za mkoa wa Dar es salaam, na imezipatia mafunzo pamoja na dawa za ugonjwa huu.

· Huduma za upimaji pamoja na dawa zinatolewa bila malipo.

· Wizara kwa kushirikiana na uongozi wa mganga mkuu wa jiji la Dar es salaam pamoja na manispaa zake imeimarisha ufuatiliaji katika shule zote zilizoathirika na ugonjwa huu, ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu mashuleni.

· Wizara imesambaza vipeperushi na imeendelea kutoa elimu ya afya kuhusu ugonjwa huo kupitia njia mbalimbali za mawasiliano kama vile televisheni, radio pamoja na magazeti.

TAHADHARI
Wizara inapenda kuufahamisha Umma kuwa, ugonjwa huu hauambukizwi kwa kula nyama ya nguruwe. Njia kuu ya maambukizi ni kwa njia ya hewa iwapo mgonjwa atakohoa au kupiga chafya bila kufunika pua au mdomo, au kwa kugusa sehemu zenye virusi hivyo na kujigusa mdomomi au puani.


HITIMISHO
Kwa kuzingatia hali hiyo, Wizara inapenda kuwaelekeza wananchi KUNAWA MIKONO VIZURI KWA SABUNI NA MAJI MARA KWA MARA na pia KUZUIA MDOMO NA PUA KWA KITAMBAA AU KARATASI LAINI (TISSUE PAPER) WAKATI WA KUKOHOA AU KUPIGA CHAFYA. Pia, wananchi wanashauriwa kutoa taarifa haraka kwenye kituo chochote cha matibabu, mara wanapoona dalili za ugonjwa huu.

Blandina S. J. Nyoni
Katibu Mkuu
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii

2 comments:

John Mwaipopo said...

Mungu wa ajabu sana. anajua kubalansisha mambo. we angalia aina ya hizo shule zilizothibitika kuwa na homa ya kitimoto. ni zile zile za midterm watoto wanaenda uingereza. huyo wa makongo mmmh sijui. hivi homa hiyo ingekuwa tandale kwa mtogole ama mwembeyanga kuna wa kupona kweli hapo. hao walibainika kuumwa kaugonjwa haka ndio wanaopelekwa shule na magari binafsi. hakuna contamination ya hewa kama katika daladala za mbagala na gongo la mboto.

juu ya yote ni kuwa homa hiyo haipatikani kwa kutafuna kamnyama ketu mashuhuri na maridhawa. Mungu alijua tu tusingesikia na kama tungesikia ingekuwa baadya ya wengi kuteketea. si mnajua tunaotumia ni wengi (najua mnajua namaanisha nini).

Anonymous said...

Mungu Atunusuru!