Tuna furaha
kuwatangazia wakereketwa wote wa
Kiswahili duniani, walioko barani Afrika
na kwengineko pia, kuhusu kuundwa kwa
Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili
Duniani(CHAUKIDU). Chama hiki kitakuwa na makao yake makuu katika mji
anamoishi na kufanya kazi Rais wa chama, na kwa sasa ni katika Chuo Kikuu cha
Wisconsin-Madison, Marekani. Madhumuni makuu ya Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili
Duniani (CHAUKIDU) ni: Kuwajumuisha pamoja waendelezaji wa Kiswahili duniani
kote kwa lengo la kuchochea kasi ya malengo mahususi yafuatayo:
1.Kukuza
Kiswahili
katika nyanja zote ambamo lugha hii inatumika au inaweza kutumika na kuongeza
ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa maarifa ya aina zote,
uandishi/utangazaji wa habari, uandishi wa vitabu, uchapishaji vitabu na
majarida, utayarishaji wa safari za mafunzo katika Afrika ya Mashariki na Kati,
nk.
2.Kusambaza
habari na matokeo ya utafiti kwa kutumia kijarida, jarida, na teknolojia ya mtandao wa
kompyuta juu ya vipengele mbalimbali vya Kiswahili na masuala yanayohusiana na
Kiswahili.
3.Kujumuisha
pamoja wanachama kwa ajili ya kubadilishana mawazo na tajiriba zao katika masuala
mbalimbali yanayohusu Kiswahili (k.v. uboreshaji wa ufundishaji, utangazaji,
utafiti, uandishi, nk.) kwa njia ya mkutano wa kila mwaka, warsha au semina au
kongamano maalumu, na hata kwa njia ya mtandao.
4.Kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kujivunia, kuendeleza, na
kuheshimu Kiswahili.
5.Kushauri ama
kushinikiza
serikali za nchi ambamo Kiswahili kinazungumzwa kutambua thamani iliyobebwa na
maliasili hii ili kuunda sera muafaka za kukiendeleza kadri ya uwezo wake kwa
manufaa ya maendeleo ya serikali na watu wake kijamii, kisiasa, kiuchumi,
kiutamaduni, n.k.
. Chama hiki
kimeundwa baada ya miaka mingi ya miito, matayarisho, na majadiliano mbalimbali
baina ya wakereketwa kutoka pembe mbalimbali
duniani ambao wote kwa jumla walidhamiria kuwepo chama ambacho
kitashirikiana na vyama vingine vya Kiswahili na asasi nyingine mbalimabli
kukisukuma mbele Kiswahili kipate hadhi na ukuzaji muafaka ndani na nje ya
Afrika.
Chama hiki
cha CHAUKIDU kimebuniwa na kuzinduliwa baada ya katiba kupitishwa kwenye kikao
maalum kilichofanyika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison mnamo Aprili 26, 2012. Wanachama watarajiwa ni pamoja na walimu,
watafiti, wanafunzi, waandishi wa habari, wasanii, waandishi wa vitabu,
wachapishaji, maafisa utalii, taasisi, n.k .Tayari Bodi ya Uongozi imechaguliwa na imeshaanza kutekeleza
hatua za mwanzo za urasimu kuhusiana na chama.
Bodi imewachagua Dkt.Ken Walibora kuwa Rais wa CHAIUKIDU, Dkt. Leonard
Muaka, Mkurugenzi, Bi Zeinab Iddi, mhariri, na Bi Judith Namayengo,
katibu. Washiriki wote wa Bodi ya
Uongozi ni kama wafuatao:
1. Bi. Zeinab Iddi (Chuo Kikuu cha
Taifa, Zanzibar)
2. Bw. David Kyeu (Chuo Kikuu cha
Wisconsin-Madison)
3. Dkt. Clara Momanyi (Chuo Kikuu
cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki)
4. Dkt. Lioba Moshi (Chuo Kikuu
cha Georgia)
5. Dkt. Leonard Muaka (Chuo Kikuu
cha Winston Salem)
6. Dkt. Samuel Kamau Mukoma (Chuo
Kikuu cha San Francisco)
7. Bi. Judith Mayanja (Chuo Kikuu
cha Wisconsin- Madison)
8. Prof. F.M.K. Senkoro (Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam)
9. Dkt. Ken Walibora Waliaula
(Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison)
Bodi ya Uongozi inawashukuru waasisi
wa chama kama vile Dkt. Katrina Thompson, Dkt. Mahiri Mwita, Dkt. Charles
Bwenge, Bwana Deo Tungaraza na Dkt. Alwiya Omar na wengineo ambao wamejitolea
kwa hali na mali na kujikusuru vilivyo katika kupanga mikakati ya kuundwa kwa chama hiki. Kwa niaba ya
wanachama wote, waliomo chamani na
watarajiwa, tunafurahi sana kuhusishwa na tukio hilo la kihistoria hatuna budi kutangaza kujitolea kwetu
kutekeleza majukumu ya chama kwa mujibu wa katiba ya chama na kwa kuzingatia
matarajio na maslahi ya wanachama wote.
Ni matamanio yetu kwamba kwa ushirikiano wa wote wanaohusika na watakaohusika,
CHAUKIDU, kitatoa mchango wake mkubwa katika ukuzaji wa Kiswahili barani Afrika
na kwengineko duniani.
Dkt. Ken Walibora Waliaula, Rais wa CHAUKIDU
Profesa
Mwandimizi katika Idara ya Fasihi na Lugha za Kiafrika
Chuo Kikuu cha
Wisconsin-Madison
Baruapepe:
waliaula@wisc.edu
Simu: 608-262-8983
4 comments:
Duuh, hii imekaa vyema,jamani tusaidie hili ili lugha yetu iwe miongoni mwa lugha za kimataifa, ...maana moja ya kitu kinachopunguza nguvu ya elimu hasa huku kwetu ni lugha....
Kumbuka mtoto ana lugha yake ya asili, anatakiwa ajifunze kiswahili na bado ili aonekane kasoma anatakiwa akijue kiingilishi...kazi kweli kweli
Kujiunga unafanyaje nataka sana na niko huku kwa Obama
ni suala zuri sana,je kujiunga unafanyaje mimi ni Igira,Frank E.mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es salaam
chama kikubwa kama hiki kina undwa wakati sisi walengwa hatujui,basi si wote hata sisi wasomi wa lugha hii,kingine kwa nini makao makuu ya chama hiki yawe marekani wakati lugha hii ni ya taifa la Tanzania?kuna mambo hapa hayaendi sawa,tunaomba udhibitisho wa swala hili sisi kama wenye lugha hii
Post a Comment