Sunday, January 12, 2014

Mzee George Liundi Afariki Dunia

 Taarifa kutoka Tanzania, zinasema kuwa Mzee George Liundi, amefariki dunia leo.  Nakumbuka kazi aliyofanya wakati ule waliporuhusu vyama vingi Tanzania.  Yeye alikuwa Msajili.

Mungu ailaze roho yaka mahala pema mbinguni. Amen.

*****************************************
KWA HISANI YA KAKA MAGGID MJENGWA

TANZIA: NDUGU GEORGE LIUNDI AFARIKI DUNIA

Ndugu zangu,
Kama wengi wenu, nami nimepokea kwa masikitiko usiku huu, taarifa za kifo cha ghafla cha Ndugu George Liundi ambaye alikuwa Msajili wa kwanza kwa vyama vya siasa hapa nchini.

Kwa mujibu wa maelezo ya mwana wa marehemu, Taji Liundi, Ndugu Liundi amefariki leo mchana.

Mwezi Agosti mwaka jana, mara tu baadada ya Jaji Mutungi kuteuliwa kushika nafasi ya Ndugu John Tendwa kama msajili wa vyama, niliandika makala juu ya tukio hilo. Hii hapa chini ni sehemu ya makala hiyo iliyomhusu Ndugu George Liundi pia...

"Miaka 20 iliyopita nilipata bahati ya kukutana na Msajili wa kwanza wa Vyama Vya Siasa. Ni Bw. George Liundi. Ni mwaka 1993, ilikuwa ni katika mwaka wake wa kwanza kama Msajili. Nakumbuka vema, nikiwa kijana mdogo tu, George Liundi alinipokea kwenye ofisi zake pale Mtaa wa Shaaban Robert. Tulikunywa chai na kuongea kwa kirefu.

Sijui George Liundi yuko wapi siku hizi, hakika ningependa nikutane nae nimkumbushe juu ya mazungumzo yetu yale. Maana, baadhi ya changamoto za mfumo wa vyama vingi tulizoziongea na Bw. Liundi miaka 20 iliyopita ndio zinazoonekana sasa.

Nakumbuka Liundi alikuwa mtu muwazi sana. Alionyesha hata wakati huo, wasiwasi wake juu ya vyama kufichaficha mambo yao ya ndani na kuwa vingine vilikuwa ni kama NGO ya mtu au kikundi cha watu. Kwamba kulikuwa na tatizo la uwepo wa demokrasia ya ndani ya vyama- Intra party democracy.

Hata wakati ule, niliona kupitia mazungumzo yangu na Liundi, kuwa dhana ya kuwa Msajili wa Vyama ilionekana kwenye macho ya Chama Dola na jamii kwa ujumla kuwa ni kuwa mlezi wa vyama vinavyoanzishwa. Kwamba CCM ni chama kikongwe na hakikuhitaji ‘ kulelewa’ na Msajili.

Kwa wakati huo vyama vilivyosajiliwa havikuonekana kuwa na impact sana na hata kuwa tishio kwa CCM. Vingi vilikuwa kwenye ugomvi wa ndani kitu ambacho CCM kwa wakati huo haikuwa kabisa na tatizo hilo.

Nilichokipata kwenye mazungumzo yangu na Liundi miaka 20 iliyopita ni ukweli, kuwa hakukufanyika review ya kina juu ya katiba za vyama kabla ya kusajiliwa. Ndio maana, masuala kama haya ya vyama kuwa na vikosi au vikundi vyake vya ulinzi yalipaswa kupigwa marufuku na Msajili tangu wakati huo bila kujali kama CCM wana Green Guards." ( Raia Mwema)

Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi Ndugu George Liundi.

Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.


No comments: